Dini Yajiunga
MNAMO Septemba 1, 1939, Ujerumani ilivamia Poland, ikianzisha Vita ya Ulimwengu 2. Majuma matatu baadaye The New York Times lilikuwa na kichwa: “Askari Wajerumani Wachochewa na Makanisa.”[1] Je, kweli makanisa ya Kijerumani yaliunga mkono vita vya Hitler?
Friedrich Heer, profesa wa Katoliki ya Kiroma wa historia katika Chuo Kikuu cha Vienna, alikubali kwamba makanisa yalitenda hivyo: “Ni kweli zilizo wazi kabisa katika historia ya Ujerumani kwamba, Msalaba na Swastika zilikuja kuwa karibu sana, mpaka utawala wa swastika ukapiga mbiu ya ushindi kutoka kwenye vinara vya makathedro ya Ujerumani, bendera za swastika zilitokea kwenye altare, na wanatheolojia Wakatoliki na Waprotestanti, mapasta, wanakanisa na wanasiasa walikaribisha muungano huo na Hitler.”[2]
Hakika, viongozi wa kanisa waliunga mkono kabisa jitihada za Hitler za vita, kama profesa wa Katoliki ya Kiroma Gordon Zahn alivyoandika: “Mkatoliki Mjerumani yeyote aliyetafuta mwongozo na mwelekezo wa kiroho kutoka kwa viongozi wake wa kidini kuhusu utumishi katika vita vya Hitler alipata majibu yaleyale ambayo angepata kutoka kwa mtawala huyo wa Nazi mwenyewe.”[3]
Dini Zawa Upande Ule Mwingine
Lakini makanisa yaliyokuwa katika nchi zilizopinga Ujerumani yalikuwa yakisema nini? The New York Times la Desemba 29, 1966 liliripoti: “Kwa wakati uliopita mabaraza ya viongozi Wakatoliki wenyeji karibu kila wakati yaliunga mkono vita vya mataifa yao, wakibariki vikosi vya vita na kutoa sala nyingi kwa ajili ya ushindi, ilhali kikundi kingine cha maaskofu upande ule mwingine kilisali peupe kwa tokeo kinyume.”[4]
Je, huu uungaji mkono wa majeshi yaliyopingana ulifanywa kwa ukubali wa Vatikani? Fikiria hili: Mnamo Desemba 8, 1939, miezi mitatu tu baada ya kufyatuka kwa Vita ya Ulimwengu a 2, Papa Pius 12 alitoa barua rasmi kwa makasisi Asperis Commoti Anxietatibus. Barua hiyo iliandikiwa makasisi katika majeshi ya mataifa yaliyopigana, na iliwahimiza wote waliokuwa katika pande zote mbili kuwa na imani katika maaskofu wao wa jeshi. Barua hiyo iliwashauri makasisi wa jeshi “wanapopigania bendera za nchi yao wapiganie Kanisa pia.”[5]
Dini mara nyingi hutoa mwongozo mkali katika kutayarisha mataifa kwa vita. “Hata katika makanisa yetu tumeweka bendera za vita,” akakubali Harry Emerson Fosdick aliyekufa, kasisi Mprotestanti.[6] Na kuhusu vita ya ulimwengu ya kwanza, amiri mkuu wa majeshi Mwingereza Frank P. Crozier alisema: “Makanisa ya Kikristo ndio wachochezi wa umwagaji damu walio hodari zaidi tulio nao, nasi tuliwatumia kikamili.”[7]
Hata hivyo, hiyo ilikuwa rekodi ya dini kwa wakati uliopita. Ni nini fungu layo la karibuni kuhusiana na vita katika jamhuri za ile iliyokuwa Yugoslavia, ambapo watu walio wengi ni ama Wakatoliki wa Kiroma au Waorthodoksi?
Daraka la Dini
Kichwa katika Asiaweek la Oktoba 20, 1993, kilitangaza hivi: “Bosnia Ni Kitovu Hususa cha Vurumai za Kidini.”[8] Kichwa cha maelezo katika San Antonio Express-News la Juni 13, 1993, kilipiga mbiu hivi: “Wakuu wa Kidini Wapaswa Kumaliza Ole za Wabosnia.” Makala hiyo ilisema hivi: “Dini za Katoliki ya Kiroma, Orthodoksi ya Mashariki na Waislamu . . . haziwezi kuepuka daraka la yale yanayotokea. Si kwa wakati huu, ulimwengu unapotazama habari kila usiku. Vita ni yao. . . . Ile kanuni ya kwamba viongozi wa kidini wana daraka la vita ni wazi. Kule tu kujifanya kwao eti ni watakatifu kwaichachisha. Kwa kubariki upande mmoja dhidi ya ule mwingine wao hufanya hivyo.”[9]
Kwa mfano, kwa nini kuna uhasama mkubwa kati ya washiriki wa Kanisa Katoliki ya Kiroma na Makanisa Orthodoksi ya Mashariki? Mapapa, maaskofu wakuu, na viongozi wengine wa kanisa wana daraka. Tangu mtengano wa mwisho kati ya dini hizi katika mwaka wa 1054, viongozi wa kanisa wamekuza uhasama na vita kati ya washiriki wao. Gazeti la Montenegro Pobeda, la Septemba 20, 1991, lilielekeza kwenye mtengano huo wa kidini na matokeo yake katika makala kuhusu lile pigano la majuzi. Chini ya kichwa “Wauaji kwa Jina la Mungu,” makala hiyo ilieleza hivi:
“Si suala la siasa kati ya Tudjman [rais Mkroatia] na Milošević [kiongozi Mserbia] bali ni vita ya kidini. Inapaswa kutajwa kwamba tayari miaka elfu moja imepita tangu Papa aamue kukomesha dini ya Orthodoksi wakiwa washindani wake. . . . Katika 1054 . . . Papa alitangaza Kanisa Orthodoksi kuwa na daraka la mtengano huo. . . . Katika 1900 kongamano la kwanza la Katoliki lilieleza kwa wazi mipango ya machinjo makubwa dhidi ya Orthodoksi kwa karne hii ya 20. Mpango [huu] unatukia sasa.”[10]
Hata hivyo, vurumai ya majuzi siyo kielelezo cha kwanza cha ugomvi wa kidini katika karne hii. Miaka 50 iliyopita, katika Vita ya Ulimwengu 2, Wakatoliki wa Kiroma walijaribu kuondoa Kanisa Orthodoksi katika eneo hilo. Kwa msaada wa papa, chama cha utaifa cha Wakroatia kiitwacho Ustashi kilikuja kutawala lile jimbo huru la Wakroatia. The New Encyclopædia Britannica yaripoti kwamba sheria hiyo iliyoidhinishwa na Vatikani ilitia ndani “mazoea ya kutenda ukatili usio wa kawaida, uliohusisha mauaji ya mamia ya maelfu ya Waserbia na Wayahudi.”[11]
Katika kitabu The Yugoslav Auschwitz and the Vatican, si kwamba tu mauaji haya mengi yameandikwa humo—zaidi ya 800,000 kwa ujumla, na zaidi ya 200,000 walioko kwenye kambi ya mateso katika Jasenovac pekee—bali pia ujihusisho wa Vatikani umeandikwa.[12]
Kwa upande ule mwingine, Kanisa Orthodoksi limesaidia Waserbia katika kupigana kwao. Kwa hakika, kiongozi mmoja Mserbia wa kikundi cha jeshi alinukuliwa akisema: ‘Askofu ni kamanda wangu.’[13]
Ni nini kingaliweza kufanywa ili kusimamisha mauaji hayo, ambayo katika Bosnia na Herzegovina pekee yaliacha watu wapatao 150,000 au wamekufa ama wamepotea?[14] Fred Schmidt alitangaza katika San Antonio Express-News ya kwamba Baraza la Usalama la UM lapasa kupitisha “azimio rasmi likitoa wito kwa papa, askofu wa Constantinople, na [viongozi wengine] wa makanisa ya Katoliki, Orthodoksi ya Mashariki, na ya Waislamu walio na uenyeji katika eneo hilo la Bosnia-Herzegovina waagize sasa hivi kwamba kuraruana kama mbwa kukomeshwe mara moja na wakutane ili waamue jinsi washiriki wa dini zao wanavyoweza kukubali kuishi pamoja kama majirani na washiriki wa dini zile nyingine.”[9]
Kwa kupatana na hilo, maelezo kwenye Scottsdale, Arizona, Progress Tribune yalimalizia ya kwamba vita hiyo “huenda imalizwe ikiwa viongozi wa kidini huko watajizatiti kuisimamisha.” Makala hiyo ilidokeza ya kwamba wao wafanye hivyo “kwa kumwondoa mara moja kanisani mshiriki yeyote anayethubutu kurusha makombora katika Sarajevo.”[15]
Hakuna Kani ya Kuleta Amani
Hata hivyo, kwa kufululiza mapapa wamekataa kuwaondoa katika ushirika wahalifu walio wabaya zaidi kivita, hata Wakatoliki wenzao wasihipo kutekelezwa kwa tendo kama hilo. Kwa kielelezo, Catholic Telegraph-Register la Cincinnati, Ohio, Marekani, chini ya kichwa “Akuzwa Akiwa Mkatoliki Lakini Akiuka Imani Yasema Kebo kwa Papa,” liliripoti hivi: “Ombi limetolewa kwa Pius 12 ya kwamba Reichsfuehrer Adolph Hitler aondolewe katika ushirika. . . . ‘Adolph Hitler,’ [hiyo kebo] ilisomeka kwa sehemu, ‘alizaliwa na wazazi Wakatoliki, alibatizwa kama Mkatoliki, na alilelewa na kuelimishwa akiwa hivyo.’”[16] Hata hivyo Hitler hakuwahi kuondolewa katika ushirika.
Fikiria pia, hali katika sehemu za Afrika ambapo vita vya jeuri vimechacha. Maaskofu 15 Wa Katoliki ya Kiroma kutoka mataifa ya Kiafrika ya Burundi, Rwanda, Tanzania, Uganda, na Zaire walikiri ya kwamba, kujapokuwa kuwepo kwa “Wakristo” wengi waliobatizwa katika eneo hilo, “mizozano ya kindani imeongoza kwenye machinjo makubwa, uharibifu na kuondoa watu kwa nguvu.” Maaskofu hao walikubali ya kwamba kiini cha tatizo hilo “ni kwamba imani ya Kikristo haijapenya vizuri njia ya kufikiri ya watu hao.”[17]
National Catholic Reporter la Aprili 8, 1994, lilisema “papa . . . alihisi ‘uchungu mwingi sana’ kwa ripoti mpya za mizozano katika taifa dogo sana la Kiafrika [la Burundi], ambalo wakaaji walo ni Wakatoliki hasa.”[18] Papa alisema kwamba katika Rwanda, ambapo karibu asilimia 70 ya idadi ya watu ni Wakatoliki, “hata Wakatoliki wana daraka” la mauaji hayo.[19] Naam, Wakatoliki katika pande zote mbili wamechinjana, kama vile wamefanya katika vita visivyohesabika vya wakati uliopita. Na, kama vile tumeona, dini zingine zimefanya vivyo hivyo.
Hivyo basi tufikie mkataa kwamba dini zote hujiunga katika vita? Je, kuna dini iliyo kani halisi ya kuleta amani?
[Picha katika ukurasa wa 5]
Hitler, ambaye hapa aonekana pamoja na papa nuncio Basallo di Torregrossa, hakuwahi kuondolewa katika ushirika
[Hisani]
Bundesarchiv Koblenz