Kumpa Muumba Sifa
“MAUA yako kwa ajili ya urembo, na matunda kwa ajili ya kutumiwa. Lakini mengi ya matunda ni marembo. Baba yetu wa kimbingu hupenda kuambatanisha urembo na kile chenye manufaa.” Nukuu hili halitokani na kitabu cha kidini. Ni kutoka kitabu cha sayansi chenye kichwa The Child’s Book of Nature. Kilichoandikwa katika 1887, mtungaji wacho, Worthington Hooker, M.D. (Daktari wa Kitiba), alinuia hicho kitabu kitumiwe katika familia na katika shule ili kufunza watoto.
Mtindo wa uandishi wa kitabu hiki watoa uthibitisho wa itikadi ya mtungaji na kicho kwa Muumba. Dakt. Hooker aandika zaidi hivi: “Unamna wa ladha zenye kupendeza katika matunda ya duniani ni mwingi mno, kama utakavyoona ukifikiria mengi kadiri uwezavyo. Huu ni uthibitisho ulioje wa wema mwingi wa Mungu! Yeye haturidhishi katika vitu vichache tu, bali katika vitu vingi. Vitu vyenye kupendeza vya ulimwengu huu yaelekea havina mwisho katika unamna wavyo. Ni ajabu kama nini kwamba mtu yeyote anaweza kujua yote haya, na kuishi siku baada ya siku bila shukrani kwa Mfanyi wake!”
Wakati The Child’s Book of Nature kilipotangazwa kwa mara ya kwanza, nadharia za Darwin zilikuwa zimesambazwa kwa mapana kwa yapata miongo mitatu. Hata hivyo, kitabu cha Dakt. Hooker chaonyesha kwamba hata mwishoni mwa karne ya 19, kitabu kingeweza kumpa Mungu sifa hadharani, badala ya nasibu, kwa sababu ya maajabu ya asili.—Linganisha Isaya 40:26.