Kuutazama Ulimwengu
Ugunduzi wa Kiakiolojia
Kwa muda mrefu waakiolojia walifikiri kwamba hakuna uvumbuzi wa maana uliosalia kufanywa katika Bonde la Wafalme la Misri baada ya kupata ziara lenye kujaa hazina la Mfalme Tutankhamen katika 1922. Lakini ziara jipya limepatikana ambalo huenda likawa kubwa kupita yote na lililo tata zaidi katika hilo bonde. Kukiwa na angalau vyumba 67 na sehemu ya chini ambayo yadhaniwa huenda ikazidisha hiyo idadi kufikia zaidi ya 100, yaonekana lilijengwa na Ramses 2 likiwa mahali pa kuzika wana wake. Ramses 2 alitawala kwa miaka 66 katika karne ya 13 K.W.K. na alikuwa na watoto zaidi ya 100, kutia ndani wana 52. Maziara ya wawili wa hao wana, tayari yalikuwa yamepatikana. Yafikiriwa kwamba wale wengine walizikwa katika ziara hili jipya lililopatikana, mahali ambapo wana wanne, kutia ndani kifungua mimba chake, Amen-hir-khopshef, yamepatikana. Jambo hili limewatatanisha wasomi wa kidini kwa sababu wengine wamedadisi kwamba Ramses 2 alikuwa farao wa Misri wakati wa Kutoka kwa Waisraeli. Hata hivyo, wasomi wengine wameweka wakati wa Kutoka kuwa 1513 K.W.K.
“Biashara Hatari”
“Kiasili, kuchimba migodi ni kazi hatari,” laonelea WeekendStar la Johannesburg, “na ambayo ni muhimu kwa uchumi wa nchi.” Jinsi kuchimba migodi kulivyo hatari kulionyeshwa Mei wakati gari moja la chini ya ardhi lenye tani 12 katika moja ya migodi katika Afrika Kusini “lilivunja zaidi ya vidude vitatu vya usalama kabla ya kutumbukia kwenye shimo lenye kina cha meta 2 103 na kuvunja-vunja lifti,” ambayo ilikuwa na wachimba migodi 104. Hakuna mmoja aliyeokoka. “Kwa kusikitisha, misiba kama hiyo imekuwa ya kawaida katika Afrika Kusini,” likasema WeekendStar. “Katika miaka ya kwanza 93 ya karne hii wafanyakazi zaidi ya 69 000 waliuawa na zaidi ya milioni moja wakajeruhiwa ndani ya migodi yetu.”
Muhula wa Vita na Msukosuko
“Baadhi ya wanahistoria wanaamini kwamba karne ya 20 itaonekana kuwa kipindi cha ukatili usio na kifani,” likaonelea The New York Times. “Kwa kuongezeka, kipindi cha miaka 75 kutoka 1914 hadi 1989, chenye kutia ndani vita viwili vya ulimwengu na vita baridi, chaonekana na wanahistoria kuwa, muhula maalumu na cha kipekee, wakati uliojitenga ambao katika huo sehemu kubwa ya ulimwengu ilikuwa ikipigana vita, ikipata nafuu kutoka vitani ama kujitayarisha kwa vita.” Makala fulani katika The Washington Post yakubali: “Vita vyetu vya karne ya 20 vimekuwa ‘vita kamili’ dhidi ya wanajeshi na raia pia,” ikasema. “Majeruhi, kutia ndani maangamizi ya jamii nzima-nzima ya Wayahudi, wapimwa kwa makumi ya mamilioni. Vita vya ujahili vya karne zilizopita kwa ulinganifu vilikuwa vidogo na visivyotokeza kamwe.” Miamko ya raia imeongezea hayo machinjo. Ni wangapi wamekufa? “Vile ‘vifo vingi sana’ tangu 1914, kwa kadirio fulani la Zbigniew Brzezinski, vimejumlisha milioni 197, ‘ulingano wa zaidi ya mtu mmoja katika watu kumi ya jumla ya watu ulimwenguni katika 1900,’” lasema Post. Laongezea kwamba ni “uhakika ulio bayana kwamba uuaji wa kiharamia na kiholela-holela umeshika kikiki desturi za karne hii” na kwamba “kufikia sasa hakuna mfumo wa kisiasa au kiuchumi katika karne hii ambao umetuliza au kuridhisha mamilioni yasiyotulia.”
Uchunguzi wa Afya Ulimwenguni
Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), katika uchunguzi walo wa kwanza wa kila mwaka wa afya tufeni, laripoti kwamba karibu asilimia 40 ya watu ulimwenguni—zaidi ya watu bilioni mbili—ni wagonjwa wakati wowote ule. Mengi ya maradhi na magonjwa si lazima yatukie na yaweza kuzuiwa, wao wasema. Umaskini ndio kisababishi kikubwa kupita zote, kwani zaidi ya nusu ya watu bilioni 5.6 ulimwenguni hawapati dawa zilizo muhimu zaidi, thuluthi ya watoto wao hawana lishe bora, na hali ya zaidi ya moja kwa tano ya watu ulimwenguni, ni duni au ni maskini wasioweza kuzuia au kutibu yoyote ya magonjwa yao. Maradhi yenye kufisha zaidi—maradhi ya moyo, mshtuko wa akili, maradhi ya mapafu, kifua kikuu, malaria, na maambukizo ya mfumo wa kupumua, pamoja na kuhara kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano—huua mamilioni ya watu kila mwaka. Hata hivyo, hiyo ripoti yaonelea kwamba katika miaka 25 iliyopita, matarajio ya kiwango cha kuishi yameongezeka hadi miaka 65 kutoka 61. “Kwa mamilioni mengi ya watu ambao kumudu kila siku ni balaa, matarajio ya kiwango cha kuishi maisha marefu yaonekana kuwa ni kama adhabu bali si thawabu,” alisema Dakt. Hiroshi Nakajima, mkurugenzi-mkuu wa WHO.
Maoni Tofauti-Tofauti Kuhusu Har–Magedoni
Dini katika Japani zimechochewa kutoa maoni yazo kuhusu Har–Magedoni baada ya dini ya Aum Shinrikyo kuvuta uangalifu wa umma kuhusiana na shambulizi la gesi aina ya sarin katika kituo cha gari-moshi cha Tokyo katika Machi lililoua watu. “Kwa miaka, kiongozi wa madhehebu Shoko Asahara . . . ametoa unabii kwamba ulimwengu ungeona Har–Magedoni,” laripoti The Daily Yomiuri. Ingawa Aum kwa msingi ni ya Kibuddha, vikundi viwili vya Kibuddha vilisema kwamba “dhana ya Har–Magedoni haikujulikana katika Dini ya Buddha,” laripoti Mainichi Daily News. “Vikundi viwili vya dini mashuhuri za Kikristo vilivyochunguzwa . . . vilitupilia mbali itikadi ya AUM kwamba Har–Magedoni iko karibu sana. Kikundi cha Katoliki kilisema hiyo itikadi haijulikani kwa Wakatoliki, huku kikundi cha Protestanti kilisema kwamba hiyo madhehebu haikupaswa kutumia neno ‘Har–Magedoni’ kwa sababu ‘neno la Kibiblia lilitumiwa mahali pasipofaa.’ Unification Church lilitaarifu kwamba ‘mbinu za kueneza mambo za kidini ambazo huchochea hofu ya ujumla hazifai,’ na kikundi cha Shinyoen kilitaarifu kwamba ikiwa maoni mengine yalazimishwa kwa ukali mno watu huhisi kutishwa.” Yaonekana, mwanzilishi wa Aum alitilia shaka unabii wake mwenyewe. Kiongozi mmoja wa cheo cha juu wa madhehebu hiyo alinukuliwa akisema hivi: “Nadhani mradi wa sarin ulianzishwa ili kwamba unabii wa kiongozi huyo uje kuwa kweli.”
Dini na Uponyaji
Uchunguzi fulani wa wagonjwa 232 wazee-wazee waliofanyiwa upasuaji wa moyo umeonyesha kwamba wagonjwa “walioweza kupata nguvu na faraja katika mtazamo wao wa kidini walikuwa na kiwango cha kuokoka upasuaji mara tatu zaidi kuliko wale ambao hawakupata kitulizo katika imani ya kidini,” lasema International Herald Tribune la Paris. Ingawa utafiti wa awali ulionyesha faida za kiafya za kuwa na uhusiano wa karibu pamoja na utegemezo kutoka kwa marafiki na familia, huu ulikuwa uchunguzi wa kwanza “kuonyesha faida ya kiafya yenye nguvu kama hiyo itokanayo na imani ya kidini miongoni mwa wagonjwa walio wagonjwa sana,” likasema Tribune. Mkurugenzi wa utafiti, Dakt. Thomas Oxman, alionelea hivi: “Yaonekana kwamba kuweza kustahimili hali hatari, zenye kutisha uhai—kuwa na imani kwamba kuna maana kubwa zaidi au msukumo—kwasaidia kitiba.”
Huduma ya Barua ya Polepole Mno
Wowote waliopata kuwa na sababu ya kulaumu huduma za posta za polepole wanaweza kujifariji kwa kisa cha mume na mke kutoka Vicenza, Italia. Akiwa amefungwa katika kambi za mateso za Nazi kaskazini mwa Ulaya katika 1944, mume Mwitalia alimwandikia mkeye hivi: “Usiwe na shaka ikiwa habari kutoka kwangu huchukua muda mrefu kukufikia.” “Yaelekea lilikuwa ono la kimbele,” lasema gazeti la habari la La Repubblica, kwani huo ujumbe uliwasili miaka 51 baadaye. Mume na mke, sasa wakiwa katika miaka yao ya 80, walipatwa na mshangao wenye furaha barua hiyo ilipowasili nao walifanyia marafiki zao karamu ndogo ili kutia kusherehekea hiyo pindi. Njia iliyopitia hiyo barua kabla ya kuwasili hatimaye haijulikani.
Tokeo la Mchezo wa VR
Mchezo wa VR (Virtual Reality) “huenda ukafikia thuluthi moja ya ununuzi wa michezo ya nyumbani ya vidio kufikia mwishoni mwa hii karne,” yadai ripoti moja katika gazeti la habari la The Globe and Mail la Kanada. Katika michezo kama hiyo wachezaji huvalia kofia ambayo hutia ndani vitoa sauti vya masikioni na kiwambo cha kuonyesha mambo mbele ya kila jicho. Glovu zenye waya humwezesha mchezaji kupitisha ishara za mwendo na kuingia katika ulimwengu wenye kutendeshwa na kompyuta. Lakini pamoja na michoro halisi ya michezo hiyo pia kuna ripoti za “ugonjwa wa utatanikaji” huenda kwa sababu ya utofautiano wa wakati kadiri taswira zifanyizwazo na kompyuta ziitikiavyo miendo ya mwili. Matokeo ya baadaye hutia ndani kuvurugika akili, kuchafuka moyo, kuumwa na kichwa, mkazo wa macho, matatizo ya kupatanisha utendaji mwilini, na kurudiwa ghafula na kumbukumbu za awali. “Watazamaji watabiri kwamba kwa sababu ya visa vingi vya ugonjwa wa utatanikaji, ni karibuni tu na mmoja ataumia na VR itapelekwa mahakamani,” lasema The Globe. Hiyo ripoti yadokeza kwamba mpaka wakati uigizaji utazidishwa kufikia mwendo wa maitikio ya watu, “masimulizi kidogo ya maisha halisi, mwendo uliopungua kidogo, yasiyoigiza sana na mipaka ya wakati kwenye mashine huenda kukasaidia.”
Mashine ya Kutumbukiza Pesa kwa Ajili ya Mifano ya Kidini
Katika nchi ambazo kidesturi ni za Kikatoliki, mifano ya kidini ni mojapo ya ishara zenye kuonekana zaidi za “ujitoaji maarufu wa watakatifu wakuu na walinzi wa mahali patakatifu,” likaonelea gazeti la habari la kila siku la Kiitalia La Repubblica. Sasa, ufundi umeanzishwa kwenye hiyo biashara yenye kunawiri ya vifaa hivi vya kidini. Mashine fulani ya kutumbukiza pesa kwa ajili ya sanamu, yenye maandishi “kwa sanamu ya kujionyesha yenyewe,” huonyesha moja kwa moja sanamu za kidini inapotumbukizwa sarafu za kipekee. “Huo mfumo wa kujihudumia utahakikisha busara katika kuchagua, utaondoa milolongo, na utahakikisha kwamba wote wanaweza kupata mifano ya kidini,” likasema hilo gazeti.