Miamba Inayoruka
JE, UMEPATA kuona nyota yenye kuruka ikiwaka kuvuka anga wakati wa usiku usio na mawingu? Huenda utaona moja karibuni. Kulingana na wanasayansi fataki hizi za asili hufuatia njia zazo kuvuka anga za dunia mara zipatazo 200,000,000 kila siku!
Hizo ni nini? Ni vipande vya mawe au kimetali tu vinavyoitwa meteoroidi ambazo huwaka kwa halijoto ya juu mno zinapoingia katika angahewa la dunia. Mstari mwangavu wa nuru ambavyo hufuatia kuvuka anga kama inavyoonekana kutoka duniani huitwa meteori.
Meteoroidi nyingi huungua kabisa kabla ya kufika duniani, lakini nyingine huokoka joto kali mno na kufika kwenye uso wa dunia. Hizi huitwa meteoroiti. Wanasayansi fulani hukadiria kwamba kila siku tani zipatazo 1,000 za mwamba huu wenye kuruka huangushwa duniani.a
Ni mara chache sana mipasuko hii huwa hatari kwa binadamu, hasa kwa sababu ya saizi ndogo kwa kulinganishwa ya miamba hii yenye kuruka. Kwa hakika, meteori nyingi husababishwa na meteoriti zisizo kubwa kuliko punje ya mchanga. (Ona sanduku, “Miamba Kutoka Anga za Nje”.) Lakini namna gani maelfu ya miamba mikubwa zaidi irukayo katika anga za juu? Chukua, kwa mfano, mmoja uitwao Ceres, ambao una kipenyo cha kilometa 1,000! Na kuna miamba mingine 30 ijulikanayo yenye kipenyo kikubwa zaidi ya kilometa 190. Miamba hii mikubwa zaidi kwa hakika ni sayari ndogo. Wanasayansi huziita asteroidi.
Namna gani ikiwa moja ya hizi asteroidi ingedunda kwa kishindo duniani? Tisho hili liwezalo kutokea ndiyo sababu moja inayofanya wanasayansi wachunguze asteroidi. Ingawa asteroidi nyingi huzunguka katika eneo kati ya Mihiri na Sumbula, nyingine zilionwa na waastronomia hasa zikivuka mzunguko wa dunia. Tisho la mgongano latiwa mkazo na kuwako kwa kreta kubwa mno kama vile Kreta ya Meteori (iitwayo pia Barringer Crater) karibu na Flagstaff, Arizona, Marekani. Moja ya dhana za kutoweka kwa wanyama aina ya dinosaur ni kwamba mgongano mkubwa sana ulibadili angahewa na kutumbukiza dunia katika kipindi kirefu cha halihewa baridi ambayo dinosaurs hawangeweza kukiokoka.
Mgongano kama huo wa kimsiba leo yaelekea ungeharibu wanadamu wote. Hata hivyo, Biblia huonyesha kwamba “wenye haki watairithi nchi, nao watakaa humo milele.”—Zaburi 37:29.
[Maelezo ya Chini]
a Makadirio hutofautiana.
[Sanduku katika ukurasa wa 23]
Tufe-Moto Kwenye Ukanda wa Vidio
Meteoroiti fulani huwa nyangavu na kubwa isivyo kawaida. Hizo huitwa tufe-moto. Mnamo Oktoba 9, 1992, tufe-moto lililoonyeshwa katika picha iliyo juu lilipita kuvuka angahewa za majimbo kadhaa ya Marekani. Hilo tufe-moto lilionwa kwanza West Virginia na lilionekana kwa mweneo wa bara wa kilometa 700. Kipande kimoja, chenye uzani wa kilogramu 12, kilitua juu ya gari lililoegeshwa katika Peekskill, New York.
Kilicho cha kipekee kuhusu tukio hili ni kwamba kwa sababu ya pembe-mkwaruzo ambayo meteoroidi hiyo iliingia katika angahewa, tufe-moto jangavu lilitokezwa ambalo lilibaki kwa zaidi ya sekunde 40. Hili liliwezesha fursa ya kipekee ya kurekodi katika vidio kutoka angalau pembe 14 tofauti-tofauti. Kulingana na gazeti Nature, “hizi ndizo picha za kwanza zenye kusonga za matufe-moto ambayo kwayo meteoriti imepatikana tena.”
Hilo tufe-moto lilivunjika kwa angalau vipande 70, ambavyo vyaonekana katika baadhi ya kanda za vidio vikiwa vitupe vyenye kuwaka. Ingawa ni meteoriti moja tu kutoka tukio hili ambayo imepatikana, wanasayansi wanaamini kwamba kipande kimoja au vingine huenda vilipenyeza angahewa la dunia na kudunda kwa kishindo barani. Ni hivyo tu ambavyo huenda vilibaki kutoka kwa meteoridi kubwa mno ambayo mbeleni ilikuwa na uzani wa tani 20.
[Sanduku katika ukurasa wa 24]
Miamba Kutoka Anga za Nje
Asteroidi: Inayoitwa pia planetoidi au sayari ndogo. Sayari hizi ndogo mno husafiri katika mzunguko kuzunguka jua. Nyingi zina maumbo yasiyo ya kawaida ambayo yanaweza kuonyesha kwamba ni vipande vya vitu vilivyokuwa vikubwa wakati mmoja.
Meteoroidi: Kipande kidogo kadiri fulani cha kimetali au kijiwe kinachoelea katika anga za juu au kuanguka kupitia angahewa. Wanasayansi fulani hufikiri kwamba meteoroidi nyingi ni vipande vitokavyo katika asteroidi vinavyotokezwa na mgongano au na masazo ya miamba kutoka kometi zilizotoweka.
Meteori: Wakati meteoroidi zinapopenya angahewa la dunia, msuguano wa hewa hutokeza joto jingi mno na nuru nyangavu. Mchirizo huu wa gesi moto zenye kuwaka huonekana kwa muda ukiwa mstari wa nuru katika anga. Huo mstari wa nuru huitwa meteori. Wengi huuita nyota yenye kuruka au nyota inayoanguka. Meteori nyingi huonekana mara ya kwanza zinapokuwa kilometa 100 hivi juu ya uso wa dunia.
Meteoriti: Nyakati fulani meteoroidi ni kubwa sana hivi kwamba haiungui kabisa inapoingia ndani ya angahewa, nayo hudunda duniani kwa kishindo. Meteoroiti ndilo jina la meteoroidi kama hiyo. Nyingine zaweza kuwa kubwa sana na nzito. Meteoroiti moja katika Namibia, Afrika, ina uzani wa zaidi ya tani 60. Meteoroiti nyingine kubwa zenye uzani wa tani 15 au zaidi zimepatikana katika Greenland, Mexico, na Marekani.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 24]
Ida na Mtoto Mwezi Wayo
KILIPOKUWA kikipiga picha asteroidi iitwayo Ida, chombo cha anga za juu cha Galileo, ikiwa njiani kuelekea Sumbula, ilifanya uvumbuzi usiotarajiwa—tukio la kwanza kuandikwa la mwezi ukizunguka asteroidi. Kama ilivyoripotiwa katika Sky and Telescope, wanasayansi wanakadiria kwamba mwezi huu wenye umbo la yai, unaoitwa Dactyl, una ukubwa wa kilometa 1.6 kwa 1.2. Mzunguko wao ni kilometa 100 hivi kutoka katikati mwa asteroidi Ida, ambayo ina ukubwa wa kilometa 56 kwa 21. Rangi zazo infrared hudokeza kwamba zote mbili Ida na mwezi wayo mdogo ni sehemu ya makundi ya asteroidi ya Koronis, ambayo hufikiriwa kuwa vipande vya mwamba mmoja mkubwa ulio peke yao ambao ulivunjwavunjwa kwa mgongano katika anga za juu.
[Hisani]
Picha ya NASA/JPL
[Picha katika ukurasa wa 25]
Kreta ya Meteori, karibu na Flagstaff, Arizona, Marekani ina kipenyo cha meta 1,200 na kina cha meta 200
[Hisani]
Picha na D. J. Roddy na K. Zeller, U.S. Geological Survey
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]
Sara Eichmiller Ruck