Kuutazama Ulimwengu
Kirusi HIV cha India
Wanasayansi kwenye Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa UKIMWI katika Pune, India, kwa kushirikiana na kikundi cha watafiti chenye kuongozwa na Dakt. Max Essex, wa Taasisi ya UKIMWI ya Harvard, wamegundua aina ya kirusi HIV ambayo imeenea zaidi India. Kirusi hicho ni HIV-1C, kinachoaminiwa kuwa hupitishwa kwa urahisi mara tano hadi kumi kuliko HIV-1B, ambacho kimeenea Ulaya na Amerika. Kulingana na Indian Express, Dakt. Essex alisema kwamba kiwango cha mweneo wa HIV katika India kinaelekea kuwa cha juu kuliko sehemu nyingi za ulimwengu. Mwanasayansi Dakt. V. Ramalingaswami alisema kwamba kati ya dawa chache za chanjo zinazoonekana kuweza kuzuia UKIMWI, hakuna hata moja ambayo inaweza kuzuia HIV-1C.
Kitulizo kwa Ukame wa Zimbabwe
Katika miaka ya majuzi, Mashahidi wa Yehova mara nyingi wameandaa kitulizo katika maeneo yaliyopatwa na misiba. Roho yao ya Kikristo hasa huhitajika katika nchi zinazoendelea kama Zimbabwe, ambako ukame umeathiri maeneo mengi ya nchi. Kwa upendo, kiasi kikubwa cha chakula na nguo kilitolewa kikiwa mchango kwa ajili ya jitihada hiyo, na ofisi ya tawi ya Watch Tower Society katika Zimbabwe kwa mafanikio iligawanya vitu hivyo kwa Mashahidi na marafiki wao katika maeneo ya mbali ya nchi hiyo. Kwa kuongezea chakula na nguo, Mashahidi wa Zimbabwe walitoa dola 7,500 (za Marekani), na Watch Tower Society ikatumia kiasi kingine cha dola 20,500 ili kutimiza utume wao wa kutoa kitulizo. Sosaiti na Mashahidi walioathiriwa walishukuru sana kwa upendo mwingi ulioonyeshwa na ndugu zao Wakristo.
Asili Moja?
Kulingana na International Herald Tribune la Paris, makala moja katika jarida la Kiyesuiti lenye mamlaka nyingi La Civiltà Cattolica yasisitiza kwamba “huenda Mungu alisema kupitia vitabu tofauti-tofauti kama vile Koran cha Waislamu, Vedas na Bhagavad-Gita cha Wahindu na maandiko matakatifu ya Tao ya China na Shinto ya Japani.” Makala hiyo yapendekeza kwamba vitabu hivyo na maandishi mengine ya kidini “si fasihi au falsafa tu, bali ni ‘ufunuo’—Mungu akisema kupitia mwanadamu.” Kwa sababu makala za jarida hilo hukaguliwa kwa njia isiyo rasmi na wakaguzi wa Vatikani, maswali yamezushwa kama maoni haya ni maoni binafsi ya papa juu ya suala hilo. Gazeti Tribune lilionelea kwamba katika kitabu chake Crossing the Threshold of Hope, John Paul 2 alisema kwamba kanisa lilikuwa likitafuta katika dini nyinginezo jambo ambalo ni la asili moja na mafundisho ya kanisa.
Moto wa Miaka 100 Wazimwa
Zaidi ya miaka 100 iliyopita, makaa-mawe ambayo hayakuwa yamechimbwa katika China yalishika moto, nayo yameendelea kuchomeka hadi majuzi. Moto huo ulienea kwa kilometa sita hivi za mraba na kuchoma tani 300,000 za makaa-mawe kila mwaka. Jitihada za kuuzima moto huo mkubwa zimeshindwa kwa miaka mingi. Hata hivyo inaripotiwa kwamba zima-moto hatimaye wamefaulu kuuzima moto huo. Ili kuuzima moto huo, zima-moto walitumia vilipukaji ili kuchimba mashimo ambayo wao waliyajazia mchanga, mawe, na kumwagia moto maji.
Msongo wa Juu wa Damu na Usahaulifu
“Uchunguzi mpya mmoja waonyesha kwamba wanaume wa makamo wenye msongo wa juu wa damu wanaelekea kupatwa na hitilafu ya kumbukumbu, uamuzi, na ya kukaza akili wafikiapo tu miaka yao ya mwisho-mwisho ya 70,” laripoti Psychology Today. Watafiti wamepata kwamba kwa ongezeko la kipimo kumi katika kila msongo wa damu unaotokana na pigo la moyo uwezekano wa upungufu wa utendaji wa ubongo huongezeka kwa asilimia 9. “Twajua kwamba msongo wa juu wa damu unahusika na mshtuko wa akili na maradhi ya moyo,” asema Dakt. Lenore Launer, mkurugenzi wa uchunguzi huo, akiongezea kwamba: “Hiyo ni sababu nyingine ya kupunguza msongo wa juu wa damu.”
Pengo la Mawasiliano
Gazeti la habari The Courier-Mail la Brisbane, Australia, laripoti kwamba uchunguzi wa hivi majuzi ulipata kwamba wanafunzi matineja wa shule za sekondari huzungumza kwa uzito mara chache sana na baba zao, au hawazungumzi kamwe mambo mazito. Uchunguzi huo ulionyesha kwamba matineja wengi hutumia chini ya dakika 15 kwa siku wakiongea na baba zao, lakini wao hutumia muda wa saa moja kwa siku wakizungumza na mama zao. Ni mara chache sana wazazi walisema na watoto wao kuhusu maadili au kuchunguza ni programu zipi za televisheni au video wanazotazama. Mazungumzo yoyote kati ya wana na baba yalielekea kuwa juu ya mambo ya juu-juu kama vile magari na michezo. Mawasiliano na mama mara nyingi yalihusu marafiki, shule, na mipango ya kijamii na ni mara chache yalihusu mambo mazito. Mara nyingi mawasiliano kati ya baba na binti yalikuwa tu kutaniana au kufanyiana mizaha.
Aksidenti za Magari —Kwa Nini?
Uchunguzi mmoja uliotangazwa na wizara ya uchukuzi ya Brazili ulionyesha kwamba karibu asilimia 90 za aksidenti za magari hutukia kwa sababu ya makosa ya madereva au kwa sababu ya uzembe. Kulingana na ripoti hiyo, madereva mara nyingi hujitumaini kupita kiasi wanapoendesha katika halihewa nzuri au kwenye barabara zilizonyooka. Ripoti hiyo pia ilifunua kwamba aksidenti za magari zilizosababishwa na hali mbaya ya barabara na kasoro za magari husababisha vifo 25,000 na kujeruhi watu 350,000 kila mwaka Brazili.
Kupora Bahari-Kuu
“Katika hekaheka za kupata dawa mpya ziwezazo kuleta faida kubwa, ‘watafuta viumbe viwezavyo kuleta faida ya kibiashara’ wanaofanyia kazi makampuni ya kutengeneza madawa wanachukua viumbe vingi katika bahari-kuu bila kufikiria matokeo,” lasema New Scientist. Kulingana na Mary Garson, mwanasayansi wa biolojia na kemia wa bahari kwenye Chuo Kikuu cha Queensland, Australia, asilimia 98 ya viumbe vinavyotolewa baharini hutupwa bila kuchunguzwa vizuri. Kwa kielelezo, kilo 450 za kiluwiluwi acorn na kilo 2,400 za sifongo zilitokeza tu sehemu ya milioni 35 za miligramu moja kwa ajili ya kitu fulani cha kuzuia kansa, kilo 1,600 za kitungulemaji zilitokeza sehemu ya milioni 350 za miligramu 10 za peptidi ambayo hutumika kutibu melanoma, na kilo 847 za maini ya mkunga moray zilihitajika kutoa sehemu ya milioni 12 za miligramu 0.35 za ciguatoxin za uchunguzi. “Hatuwezi kuondoa tu kiasi kikubwa cha kiumbe fulani kutoka bahari-kuu—hata kiwe chenye manufaa kivipi—ila tu kama tuna hakika ya kwamba hatukiangamizi,” asema Garson.
Sayari Yagunduliwa Kiaksidenti
Sayari ndogo iligunduliwa majuzi na mwastronomia asiye mtaalamu George Sallit wa Bradfield, kijiji kimoja kilichoko Uingereza, akitumia darubini-upeo katika kibanda cha bustani yake. “Ilikuwa aksidenti tu,” yeye alikiri. “Niliipiga picha na nilipoichunguza nikatambua kwamba hiyo ilikuwa sayari fulani iliyokuwa imesonga polepole kwenye mfululizo wa picha.” Sallit One, kama sayari hiyo mpya inavyoitwa sasa, ina kipenyo cha kilometa 30 tu na iko umbali wa kilometa zipatazo milioni 600 kutoka duniani. Mzunguko wayo huipeleka kati ya Mihiri na Sumbula. Darubini-upeo iliyotumiwa ina kioo chenye ukubwa wa sentimeta 30, na kuongozwa na kompyuta ya dola 7,000 (za Marekani) lakini inayotumia programu za kompyuta zilizokusudiwa kutumiwa katika darubini-upeo ya Hubble, laripoti The Times la London. Huenda kuna maelfu ya sayari kama hizo ndogo-ndogo, au asteoridi, katika mfumo wetu wa jua.
Mshangao kwa Wakulima wa Mpunga
Kwa miaka mingi wakulima wa mpunga katika Asia wamenyunyizia mazao yao dawa nyingi mapema katika msimu ili kuua mabuu ya nondo wenye kuviringa majani, ambao humaliza majani ya mpunga. Hata hivyo, majaribio ya majuzi yameonyesha kwamba mipunga inaweza kupoteza nusu ya majani yayo bila kuathiri kiasi cha mchele itakachotoa. Wakulima wengine wa Vietnam walisadikishwa waache kunyunyizia mipunga dawa mapema katika msimu—ambayo ni asilimia 30 hadi 50 ya dawa za visumbufu ambazo wakulima wa Asia hutumia—nao walipata kwamba mazao hayakuathiriwa kamwe.
Dini na Siasa Zakataliwa
Kulingana na gazeti la habari The Australian, “tineja wa kawaida wa Australia” hapendezwi sana na siasa au dini. Uamuzi huo wategemea uchunguzi uliofanyiwa wanafunzi wenye umri wa kati ya miaka 13 hadi 16, ambao ulijumlishwa na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sydney Dakt. Jennifer Bowes. Matangulizi ya vijana yalikuwa hivi kwa mfuatano wa yanayopendwa zaidi: “kuwa na marafiki wa karibu, kupata elimu nzuri, kuwa na kazi salama, kusitawisha vipawa vyangu, kuwa karibu na familia yetu, kuhifadhi dunia kwa ajili ya vizazi vijavyo, kulinda wanyama, kuwa na nyumba nzuri, kusafiri nchi nyinginezo, kuchuma pesa nyingi, kujaribu kukomesha uchafuzi, kufunga ndoa, kuwasaidia wale wasiojiweza, kusaidia nchi yangu, kufanya jambo la kufaa jamii, kuwa na mamlaka juu ya watu fulani.” Mambo yasiyo ya maana zaidi kati ya mambo 18 yaliyoorodheshwa yalikuwa “kufuata kanuni za dini yetu” na “kuwa mwanasiasa mtendaji.”