Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 9/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Gharama Kubwa ya Uhalifu
  • Watawa Wahalifu
  • Glavu Zenye Matundu
  • Kukabiliana na Walaghai Shupavu
  • Matatizo ya Afya ya Brazili
  • Uhaba wa Viungo
  • Jirani Mwenye Gharama
  • Nguvafarasi Mwaminifu
  • Yenye Tamaa ya Metali Nzito
  • “Kupika—Na Kupumua kwa Uzito—Na Gesi”
  • Mitindo-Maisha Yenye Kudhuru Afya—Inagharimu Kadiri Gani?
    Amkeni!—1997
  • Je! Wanadamu Wanaweza Kuleta Amani na Usalama Wenye Kudumu?
    Amani na Usalama wa Kweli—Wewe Unaweza Kuupataje?
  • Farasi Wanaocheza Dansi Baharini
    Amkeni!—2004
  • Je, Sayansi Itamaliza Magonjwa?
    Amkeni!—2007
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 9/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Gharama Kubwa ya Uhalifu

Idara ya Sheria yakadiria kwamba vitendo vya uhalifu vipatavyo 94,000 hufanywa Marekani kila siku. Uhalifu huo hugharimu wananchi wa Marekani kiasi gani? Kulingana na mchanganuzi wa mambo ya uchumi Ed Rubenstein, gharama za moja kwa moja—kutia ndani kupoteza mali ya binafsi, kama vile magari, pesa, na vito—zakaribia dola bilioni 20 kwa mwaka. Hata hivyo, kuongezea hiyo, kuna gharama zinazohusika na idara za kutekeleza sheria, mahakama, magereza, na mifumo ya kuachilia wafungwa chini ya masharti. Hilo huongeza gharama hiyo kuwa karibu dola bilioni 100. Vilevile, kwa kuwa wahasiriwa wa uhalifu mara nyingi hupatwa na vipindi vya hofu, fadhaiko, au kushuka moyo, wengi hukabiliana na hisia hizi zisizofaa kwa kutokwenda kazini. Basi, upotezo wa faida kazini hufanya kwa urahisi “gharama zote za wahasiriwa wa uhalifu” kufikia kati ya “dola bilioni 250 na 500 kila mwaka,” asema Rubenstein.

Watawa Wahalifu

Katika Thailand mtawa mpya wa Dini ya Buddha mwenye uraibu wa dawa za amphetamines amekiri kwamba alimbaka na kumuua kimakusudi mtalii mmoja Mwingereza mwenye umri wa miaka 23, laripoti World Press Review. Hata hivyo, uhalifu huo ni mojawapo tu “kashfa nyingi” ambazo zimekumba makasisi wa Dini ya Buddha majuzi. “Kwa kuongezea idadi yenye kuongezeka ya matendo ya uhalifu, pupa ya mali inafisidi Dini ya Buddha.” Kwa njia gani? “Kuuza hirizi za bahati-nzuri ni biashara kubwa kwa baadhi ya watawa, ambao hupelekwa kwa magari makubwa.” Tokeo ni kwamba “imani ya watu kwa makasisi wa Dini ya Buddha ambao zamani waliheshimiwa sana inapingwa.” Gazeti hilo pia lilisema kwamba katika jitihada za kukomesha “matumizi mabaya ya dawa za kulevya” miongoni mwa watawa, “makao ya watawa yamefungua vituo vya kuwasaidia kuacha uraibu.”

Glavu Zenye Matundu

Jozi moja ya glavu za lateksi huenda isitoshe kukinga wenye kuivaa dhidi ya virusi HIV au mchochota wa ini, laripoti New Scientist. Huo ulikuwa mkataa uliofikiwa na watafiti katika Chuo cha Kitiba cha Wisconsin walipogundua kwamba “glavu moja kati ya kila glavu tatu hupitisha virusi vinavyotoshana na virusi HIV au virusi vya mchochota wa ini.” Jordan Fink, mkuu wa idara ya mizio ya chuo hicho kikuu, alianza kuchunguza glavu za lateksi baada ya madaktari na wauguzi kulalamika kwamba walikuwa wanapatwa na mizio katika 1992. Huo ulikuwa ndio mwaka ambao serikali ya Marekani ilianza kutaka wafanyakazi wa kitiba kuvaa glavu za mpira ikiwa kuna uwezekano wa kugusa damu ya mgonjwa au umajimaji wa mwili. Kulingana na Fink, wafanyakazi wa kiafya ambao wana mikato au mikwaruzo fulani kwenye ngozi wapaswa kufikiria kuvaa zaidi ya jozi moja ya glavu, lasema gazeti hilo. Hata hivyo, wafanyakazi wa kitiba wasio na mkwaruzo wowote kwenye ngozi wasiwe na wasiwasi isivyofaa. “Ngozi isiyo na mkwaruzo ni kinga nzuri,” asema Fink.

Kukabiliana na Walaghai Shupavu

Baada ya kutumia miaka 17 akiwa ripota wa ununuzi kwa ajili ya stesheni ya televisheni ya kwao katika Boston, Massachusetts, Paula Lyons ameorodhesha orodha ya njia za kushinda “ujanja wenye udanganyifu na udumifu wa walaghai shupavu.” Kulingana na makala moja katika Ladies’ Home Journal, madokezo ya Lyons yatia ndani: Usifanye biashara kupitia simu na mtu usiyemjua. Usiweke mali zako katika kile usichokielewa. Usilipe chochote ili upate zawadi ya “bure.” Usitumaini sana uhakikisho wa kwamba utarudishiwa pesa zako usiporidhika. Epuka kutoa upaji kwa mashirika ya kufadhili usiyoyajua. Usinunue kamwe gari ambalo limetumiwa kabla ya kukaguliwa kwanza na mekanika anayejitegemea. “Huenda sheria hizi zikaonekana kuwa za kikale,” asema Lyons, lakini “hizo zaweza kukulinda na baadhi ya mazoea ya ufisadi yaliyo katika biashara.”

Matatizo ya Afya ya Brazili

Mkurugenzi wa kituo cha kitaifa cha Brazili cha mweneo na udhibiti wa maradhi, Dakt. Eduardo Levcovitz, alilalamika hivi: “Kwa kusikitisha watu wetu wanaugua matatizo ya afya ya Nchi Zilizositawi kiviwanda na maradhi yawezayo kuepukwa ya Nchi Zinazoendelea.” Akinukuliwa katika The Medical Post, Dakt. Levcovitz ataja baadhi ya visababishi vikubwa vya matatizo ya afya miongoni mwa Wabrazili. Kwanza katika orodha ni maradhi ya moyo, kansa, na maradhi ya upumuaji. Kisha yafuatiwa na kifo kutokana na uhalifu wenye jeuri na aksidenti. Yenye kufuatia maradhi ya “Nchi Zilizositawi” ni maradhi ya kuambukiza yatokanayo na hali mbaya za kuishi. “Inakadiriwa kwamba nusu ya idadi ya watu wa Brazili huugua aina fulani ya maambukizo ya vimelea,” lasema The Medical Post. Malaria pekee hukumba Wabrazili wapatao 500,000 kila mwaka. Maradhi mengine ya kawaida ya vimelea yapatikanayo Brazili ni maradhi ya Chagas, kichocho, safura, vidonda vya kusedeka, na matende.

Uhaba wa Viungo

Katika 1994 “idadi ya watu waliohitaji kupachikwa viungo” Marekani “ilishinda idadi ya wenye kutoa viungo kwa karibu thuluthi moja,” lasema The Journal of the American Medical Association. Tangu 1988 hadi 1994, idadi ya watu wenye kupokea mipachiko iliongezeka kwa asilimia 49, huku idadi ya wenye kutoa viungo ikiongezeka kwa asilimia 37 pekee. Huku uhitaji wa viungo ukishinda ugavi, wengine walio wagonjwa mahututi wamekufa wakingoja kiungo kipatikane. Likieleza juu ya jambo hilo gumu, gazeti New Scientist lasema: “Kadiri mipachiko iwavyo ya kawaida zaidi, ndivyo watu wengi zaidi huongezeka kwenye orodha.” Hivyo ripoti hiyo yataja kwamba “mipachiko ya viungo imehasiriwa na ufanisi wayo yenyewe.”

Jirani Mwenye Gharama

Wakati wenye nyumba wanapouza nyumba zao nchini Uingereza, wao wanawajibika kisheria kufunua mambo madogo-madogo ya mizozo ya wakati uliopita ambayo imepata kutukia kati yao na majirani wao, laripoti The Sunday Times la London. Mjane mmoja mwenye umri wa miaka 80 aliyekosa kuwaarifu wanunuzi wa nyumba yake kwamba mara mbili alikuwa amelalamikia wenye mamlaka wa huko kuhusu jirani mwenye makelele alishtakiwa kwa mafanikio kwa kutosema mambo hayo. Sasa yeye anakabiliwa na ufilisi baada ya hukumu ya kutozwa dola 45,000. Hao wenyeji wapya waliishi katika nyumba hiyo kwa miaka sita, lakini walipata kwamba ilikuwa vigumu sana kuishi na jirani yao na hawakuwa na la kufanya ila kuiuza hiyo nyumba, waliiambia mahakama. Ili kuepuka matatizo kama hayo, wanunuzi wengine wamegeukia kuajiri wapelelezi wa kujitegemea ili kuchunguza mwenendo wa wale watakaokuwa majirani wao. Uchunguzi wa kijuu-juu waweza kugharimu kiasi kidogo kama dola 75, lakini wanunuzi wengine wako tayari kulipa dola 1,500 kwa uchunguzi wa kina zaidi.

Nguvafarasi Mwaminifu

Mtaalamu wa wanyama wa Oxford Amanda Vincent amegundua kwamba inaonekana nguvafarasi hudumisha uaminifu kwa mwenzi wake maishani mwote. Akichunguza spishi Hippocampus whitei mwenye urefu wa sentimeta 10 katika pwani ya Australia, Dakt. Vincent alishangaa kuona uaminifu wa namna hiyo miongoni mwa samaki, lataja The Times la London. Ilionwa kwamba kila asubuhi mume humngoja mwenzi wake mahali palipopangwa tayari. Wakutanapo, hao nguvafarasi hubadilika rangi na kucheza. Kutokeza wazao ni ushirikiano wa wote wawili. Wa kike hutaga mayai yake na kuyaweka katika pochi ya kipekee katika mkia wa yule wa kiume. Kisha wa kiume huyatungisha, nayo mayai hayo hubaki katika pochi hiyo hadi wakati wa kuzaliwa. Mwenzi mmoja akifa, nguvafarasi anayebaki atajifunganisha tu na nguvafarasi mwingine asiye na mwenzi. Kwa kuhuzunisha, kuokoka kwa viumbe hivyo vyenye kupendeza kumo hatarini, kwa kuwa mamilioni hushikwa kila mwaka kwa ajili ya matangi ya samaki au kwa ajili ya kutumiwa katika dawa za kienyeji za Asia.

Yenye Tamaa ya Metali Nzito

Metali nzito kama vile nikeli, risasi, zinki, na kadimi, zinapochafua udongo, ardhi huwa hatari na isiyoweza kutumika. Njia za sasa za kuziondoa zahitaji kuondolewa kwa udongo wa juu na kuutupa katika mashimo yaliyochimbwa au kuondoa udongo uliochafuliwa na kuuwekea asidi zenye nguvu ambazo huondoa metali zenye kukwamia udongo. Hata hivyo, njia hizo za kuondoa metali ni ghali sana. Sasa wanasayansi wanajifunza njia ya gharama nafuu zaidi na iliyo safi zaidi ya kusuluhisha tatizo hilo. Inaitwa phytoremediation (suluhisho la mimea). Utaratibu huo wahusisha kutumia mimea ambayo hufyonza metali nzito kutoka kwa udongo na kusafirisha metali kwenye majani, mashina, na sehemu nyinginezo za mmea zilizopo juu ya ardhi. Mara tu metali nzito zinapoondolewa ardhini, mimea inaweza kusagwa na metali zenye thamani zaidi kurejelezwa, lasema gazeti Science.

“Kupika—Na Kupumua kwa Uzito—Na Gesi”

Likitumia kichwa hicho, Science News liliripoti kwamba watafiti wa Uingereza wamepata kwamba “wanawake ambao hupika kwa gesi wana mwelekeo wa angalau mara mbili kupatwa na matatizo ya kupumua, kukosa pumzi, na dalili nyinginezo za ugonjwa wa pumu kuliko wale ambao hutumia majiko na tanuu za umeme.” Huo uchunguzi, uliofanywa katika Hospitali ya St. Thomas katika London, wasema kwamba dalili hizo zilidumu hata wakati mapepeo yalipotumiwa. Na ingawa wanaume kwa wanawake walishiriki katika uchunguzi huo, “athari hizo zilipatikana katika wanawake pekee—labda kwa sababu wao hutumia muda mwingi zaidi jikoni.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki