Mitindo-Maisha Yenye Kudhuru Afya—Inagharimu Kadiri Gani?
“UGONJWA ni bwana-mkubwa wa kila mtu,” yasema methali moja ya lugha ya Denmark. Mtu yeyote ambaye amesedeka atakubali upesi kwamba huyu “bwana-mkubwa” anaweza kuwa mkatili! Lakini, huenda ukashangaa kujua kwamba mara nyingi ugonjwa ni mgeni-mwalikwa badala ya kuwa bwana-mkubwa. Vitovu vya Kudhibiti na Kuzuia Maradhi vya Marekani vyasema kwamba asilimia 30 ya siku ambazo wagonjwa hulala hospitalini hutokana na maradhi na majeraha ambayo yanaweza kuepukwa. Kisababishi? Mitindo-maisha yenye kudhuru afya na iliyo hatari. Ebu fikiria mifano fulani.
KUVUTA SIGARETI. Ira, mwenye umri wa miaka 53, ana ugonjwa wa kupumua kwa shida—ambao umesababishwa na kuvuta sigareti kwa karibu miongo minne. Ili kutibu ugonjwa wake, yeye huhitaji daima oksijeni ya chupa, ambayo hugharimu dola 400 hivi kila mwezi. Katika 1994 hali yake ilifanya alazwe hospitalini kwa siku tisa na kugharimu dola 18,000, na kufanya jumla ya gharama ya kutibu Ira mwaka huo izidi dola 20,000. Na bado, Ira haoni umuhimu wa kuacha kuvuta sigareti. “Nina tamaa ya ajabu sana,” yeye asema.
Kisa cha Ira si cha kipekee. Japo hatari zijulikanazo wazi za kuvuta sigareti, ulimwenguni pote watu huvuta sigareti zipatazo bilioni 15 kila siku. Katika Marekani, gharama za kutibu maradhi yanayohusika na kuvuta sigareti imekadiriwa kuwa dola bilioni 50. Hiyo yamaanisha kwamba katika 1993, kwa wastani, kwa kila pakiti ya sigareti iliyonunuliwa, karibu dola 2.06 zilitumiwa kugharimia matibabu yaliyohusu kuvuta sigareti.
Mtoto azaliwapo, gharama za kitiba zinazohusika na kuvuta sigareti zaweza kuanza kurundamana. Kwa kutaja mfano mmoja tu, uchunguzi mmoja Marekani ulipata kwamba watoto wazaliwao na akina mama ambao huvuta sigareti wana uwezekano wa mara mbili wa kupatwa na mipasuko ya midomo au ya kaakaa, tatizo ambalo laweza kuhitaji upasuaji hadi mara nne kabla ya mtoto kufikia umri wa miaka miwili. Gharama ya wastani ya maisha yote ya kutibu tatizo hilo na gharama zihusikazo nalo ni dola 100,000 kwa kila mtu. Bila shaka, hakuna kiasi cha fedha kiwezacho kulipia fadhaiko la kihisia-moyo la kuzaliwa na ulemavu.
Watu fulani husema kwamba gharama ya juu sana ya kutibu madhara ya kuvuta sigareti husawazishwa na jambo la kwamba wavutaji wengi wa sigareti hawaishi muda mrefu wa kuweza kupata Malipo ya Uzeeni. Lakini, kama jarida The New England Journal of Medicine lisemavyo, “huo ni uamuzi ambao umezusha ubishi; isitoshe, wengi wangekubali kwamba vifo vya mapema vinavyotokana na kuvuta sigareti si njia nzuri ya kudhibiti gharama za juu za matibabu.”
MATUMIZI MABAYA YA KILEO. Matumizi mabaya ya kileo yamehusianishwa na matatizo kadhaa ya afya, kutia ndani kunyauka kwa ini, maradhi ya moyo, mchochota wa mfuko wa tumbo, vidonda vya tumbo, na mchochota wa kongosho. Pia hayo yaweza kufanya mtu ashikwe kwa urahisi zaidi na maradhi ya kuambukizwa kama vile nimonia. Katika Marekani, kila mwaka “dola bilioni 10 hutumiwa kutibu watu ambao hawawezi kudhibiti unywaji,” kulingana na Dakt. Stanton Peele.
Mara nyingi kileo huathiri kijusi kilicho katika tumbo la uzazi. Kila mwaka makumi ya maelfu ya watoto Marekani pekee huzaliwa wakiwa na kasoro kwa sababu mama zao walikuwa wanywaji sana wakiwa waja-wazito. Baadhi ya vitoto hivyo hugunduliwa kuwa na ugonjwa wa kileo (FAS), na mara nyingi wana kasoro za kimwili na za kiakili. Gharama za wastani za kutibu kila mtoto mwenye FAS maishani mwake mwote imekadiriwa kuwa dola milioni 1.4.
Kwa kuwa kileo hupunguza uwezo wa mwili kuidhibiti misukumo, kunywa kupindukia mara nyingi huchangia mifoko ya jeuri, ambayo inaweza kutokeza majeraha yanayoweza kuhitaji matibabu. Pia kuna madhara mabaya sana yasababishwayo na wale ambao huendesha magari wakiwa wamelewa. Fikiria madhara yaliyompata Lindsey, msichana mwenye umri wa miaka minane ambaye aling’olewa kutoka kiti cha nyuma cha gari la mamake baada ya dereva mlevi kugongana nao. Lindsey alikaa hospitalini kwa majuma saba naye alihitaji kufanyiwa upasuaji kadhaa. Gharama zake za kitiba zilipita dola 300,000. Hata ni vizuri kwamba hakufa.
MATUMIZI MABAYA YA DAWA. Mtafiti mmoja akadiria kwamba gharama ya kila mwaka ya matumizi mabaya ya dawa Marekani kuwa dola bilioni 67. Joseph A. Califano, Jr., msimamizi wa Kitovu cha Uraibu wa Dawa na Kileo katika Chuo Kikuu cha Columbia cha New York, ataja gharama nyingine kubwa ya tatizo hilo: “Watoto wazaliwao na mama waliotumia dawa ya kulevya ya crack, ambao walikuwa nadra sana mwongo mmoja uliopita, sasa wamejaa wodi za gharama ya dola 2,000 kwa siku. . . . Inaweza kugharimu dola milioni moja kutibu kila mtoto afikiaye utu-uzima.” Kwa kuongezea, asema Califano, “mama waja-wazito wanaokataa kwenda kliniki na kukataa kuacha dawa za kulevya waligharimiwa kiasi kikubwa cha karibu dola bilioni tatu za msaada wa matibabu zilizotumiwa katika 1994 kwa matibabu ya wagonjwa waliolazwa hospitalini kwa matatizo yahusikayo na dawa za kulevya.”
Msiba wa hali hiyo wazidishwa tufikiriapo gharama za uhai ambao hauwezi kuhesabika. Mzozo wa ndoa, watoto waliopuuzwa, na fedha ambazo hazitoshi ni miongoni mwa matatizo yanayoathiri familia zilizovurugwa na dawa za kulevya.
NGONO ZA OVYOOVYO. Zaidi ya watu milioni 12 katika Marekani huambukizwa maradhi yanayopitishwa kingono (STD) kila mwaka, ikifanya Marekani iwe na kiwango cha juu zaidi cha watu wanaoambukizwa maradhi ya kingono kuliko nchi nyingineyo yote iliyoendelea. David Celentano, wa Johns Hopkins University School of Hygiene and Public Health, aliita jambo hilo “aibu ya kitaifa.” Gharama za moja kwa moja za maradhi hayo, bila kutia ndani UKIMWI, ni karibu dola bilioni kumi kila mwaka. Matineja hasa wamo hatarini. Na hiyo si ajabu! Kulingana na ripoti moja, kufikia wakati ambao wamefika kidato cha nne, asilimia ipatayo 70 kati yao tayari wamefanya ngono na karibu asilimia 40 kati yao wamefanya ngono na angalau watu wanne tofauti-tofauti.
UKIMWI wenyewe ni msiba wa kitiba. Mapema katika 1996 tiba yenye matokeo zaidi ya nyinginezo zote—vizuia protease ambavyo vimechanganywa na dawa za zamani—iligharimu kati ya dola 12,000 na dola 18,000 kwa mwaka kwa kila mtu. Lakini hiyo ni sehemu ndogo tu ya gharama yenyewe ya UKIMWI, ambayo hutia ndani hali ya kutofaa kwa mtu na vilevile kwa wale wanaoomba ruhusa kutoka kazini au shuleni ili kumtunza. Inakadiriwa kwamba kufikia mwaka wa 2000, virusi HIV na UKIMWI vitakuwa vimegharimu kati ya dola bilioni 356 na dola bilioni 514 ulimwenguni pote—hiyo ni sawa na kutumia uchumi wote wa ama Australia ama India.
UJEURI. Alipokuwa ofisa mkuu wa afya wa Marekani, Joycelyn Elders aliripoti kwamba gharama za kitiba za ujeuri zilikuwa dola bilioni 13.5 katika 1992. Rais wa Marekani Bill Clinton alionelea: “Sababu mojawapo inayofanya matibabu yawe ghali mno Marekani ni kwamba hospitali zetu na vyumba vyetu vya dharura vimejaa watu waliojeruhiwa kwa kukatwakatwa na kupigwa risasi.” Kwa sababu nzuri The Journal of the American Medical Association laita ujeuri katika Marekani kuwa “dharura ya afya ya umma.” Ripoti hiyo yaendelea kusema: “Ingawa ujeuri si maradhi ‘hasa,’ athari yake kwa afya ya mtu na umma ni kubwa mno kama vile tu magonjwa mengine ya kiakili—na labda hata zaidi.”
Ripoti moja iliyotolewa na hospitali 40 katika Colorado yasema kwamba wastani wa gharama ya kutibu kila mhasiriwa wa ujeuri katika miezi tisa ya kwanza ya 1993 ilikuwa dola 9,600. Zaidi ya nusu ya wale waliolazwa hospitalini hawakuwa na bima, na wengi wao hawakuweza kulipa gharama zao au hawakutaka kuzilipa. Hali kama hizo hutokeza kodi za juu zaidi, bima za juu zaidi, na gharama za juu za kutibiwa hospitalini. Shirika la Hospitali la Colorado laripoti: “Sote twalipa.”
Badiliko la Mtindo-Maisha
Kwa maoni ya kibinadamu, taraja la kurekebisha mitindo-maisha halionekani kuwa zuri. “Marekani si Bustani ya Edeni nasi hatutaweza kamwe kuacha kutumia vibaya kileo na dawa za kulevya,” yasema ripoti moja ya Chuo Kikuu cha Columbia. “Lakini kwa kadiri tuachavyo matumizi hayo mabaya, tutavuna mazuri kwa kuzaa watoto wenye afya, kupunguka kwa ujeuri na uhalifu, kodi za chini, gharama za chini za matibabu, faida za juu, wanafunzi wenye elimu bora na visa vichache zaidi vya UKIMWI.”
Mashahidi wa Yehova wamepata Biblia kuwa msaada mkubwa zaidi katika kutimiza mradi huo. Biblia si kitabu cha kivivi-hivi. Imepuliziwa na Muumba wa mwanadamu, Yehova Mungu. (2 Timotheo 3:16, 17) Yeye ndiye ‘akufundishaye ili upate faida, akuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata.’ (Isaya 48:17) Kanuni zilizowekwa katika Biblia ni zenye afya, na wale wafuatao shauri lake hupata manufaa kubwa.
Kwa mfano, zamani Esther alikuwa mvutaji sana wa sigareti.a Baada ya yeye kuanza kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova, mwalimu wake wa Biblia alimwalika atumie siku moja kuzuru makao makuu ya Mashahidi wa Yehova, katika Brooklyn, New York. Kwanza, Esther alisitasita. Akijua kwamba Mashahidi wa Yehova hawavuti sigareti, alifikiria jinsi ambavyo ataweza kuwa nao siku nzima. Basi Esther aliweka sigareti moja katika pochi yake, akisababu kwamba akihisi kuvuta sigareti, ataenda tu chooni. Kama tu alivyopanga, baada ya mojawapo ya ziara kadhaa Esther alienda chooni na kutoa sigareti yake. Lakini akaona jambo fulani. Chumba hicho kilikuwa safi sana, na hewa ilikuwa safi. “Singeweza kuchafua mahali hapo kwa kuvuta sigareti,” akumbuka Esther, “basi nikaipiga maji chooni. Na hiyo ikawa sigareti ya mwisho niliyopata kushika!”
Ulimwenguni kote, mamilioni ya watu kama Esther wanajifunza kuishi kwa kupatana na kanuni za Biblia. Wao hujinufaisha, nao huja kuwa wenye manufaa sana katika jumuiya wanamoishi. Jambo kubwa zaidi, wao humletea Muumba wao heshima, Yehova Mungu.—Linganisha Mithali 27:11.
Ingawa jitihada bora zaidi za mwanadamu haziwezi kutokeza “Bustani ya Edeni,” Biblia yasema Mungu atafanya hivyo. Petro wa Pili 3:13 lasema: “Ziko mbingu mpya na dunia mpya ambazo tunangojea kulingana na ahadi yake [Mungu], na katika hizo uadilifu utakaa.” (Linganisha Isaya 51:3.) Katika hiyo dunia mpya, matibabu hayatakuwa hangaiko, kwa kuwa wanadamu watafurahia maisha yenye afya kamili—jinsi ambavyo Mungu alikusudia iwe tangu mwanzoni. (Isaya 33:24) Je, ungependa kujua zaidi juu ya ahadi za Mungu? Mashahidi wa Yehova watafurahi kukusaidia.
[Maelezo ya Chini]
a Si jina lake halisi.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]
© 1985 P. F. Bentley/Black Star