Tinnitus—Je, Ni Kelele ya Kuishi Nayo?
BEETHOVEN, mwandikaji Mjerumani Goethe, na mchongaji Mwitalia Michelangelo—huenda wote walikuwa nayo. Huenda Wamisri wa kale nao walijua juu yayo, yaonekana wakiurejezea ugonjwa huo kuwa “sikio lililorogwa.” Leo ugonjwa huo unaitwa tinnitus, na yakadiriwa kwamba asilimia 15 ya watu wa ulimwengu wa Magharibi huupata kwa ukawaida au wanao daima. Karibu watu 5 kati ya kila watu 1,000 wanaugua ugonjwa huo kwa hali mbaya zaidi.
Ugonjwa huu wenye kuudhi ni nini hasa? Neno “tinnitus” latokana na neno la Kilatini tinnire, yaani “kulia kama kengele ndogo,” nalo hufafanuliwa kuwa “kelele masikioni isiyosababishwa na vitu vya nje.” Kulingana na The Merck Manual of Diagnosis and Therapy, hiyo yaweza kuwa “mvumo, mlio wa kengele, ngurumo, mbinja, au mlio mwembamba au yaweza kuhusisha kelele nyinginezo tata zaidi ambazo hubadilikana kwa muda fulani wa wakati. Kelele hiyo yaweza kuwa ya vipindi, yenye kuendelea, au yenye kupiga-piga.” Kiasi cha kelele hii chaweza kuanzia kiwango cha chini sana hadi kiwango cha juu sana chenye kuudhi. Na ni kelele ambayo wenye kuugua hawawezi kukomesha. Hivyo, hiyo kelele yenye kudumu yaweza kutokeza athari nyinginezo nyingi: taabu ya kihisia-moyo, matatizo ya kupata usingizi, maumivu, ugumu wa kukaza fikira, uchovu, matatizo ya kuwasiliana, na mshuko-moyo.
Ni Nini Ambacho Husababisha Huo Ugonjwa?
Baada ya tinnitus kuanza, mtu mwenye kuugua aweza kujiuliza kwa wasiwasi kuna kasoro gani. Huenda akaogopa kwamba amepatwa na mvujo wa damu katika ubongo, amepata tatizo fulani la akili, au kwamba ana uvimbe. Kwa uzuri, ni nadra sana tinnitus isababishwe na ugonjwa mbaya. Wengine wamepatwa na tinnitus baada ya kujeruhiwa kichwani. Na Profesa Alf Axelsson, wa Göteborg, Sweden, ambaye ni mtafiti na mtaalamu wa habari ya tinnitus, aliliambia Amkeni!: “Dawa nyinginezo, kama vile aspirin nyingi, zaweza kutokeza athari ya muda mfupi ya tinnitus.”
Lakini, tinnitus husababishwa hasa na tatizo fulani la sikio. Profesa Axelsson alieleza hivi: “Tatizo huwa katika sehemu ya sikio la ndani iitwayo koklea, yenye chembe za nywele za hisi zipatazo 15,000 zisizoweza kuonekana kwa macho. Baadhi yazo zikipatwa na madhara, hizo zaweza kupeleka na kupokea mkondo usiosawazika wa ishara za neva. Hiyo huonwa na mwenye kuugua kuwa kelele.”
Ni nini kisababishi cha madhara hayo ya sikio? Kulingana na Profesa Axelsson, kisababishi kimoja cha tinnitus ni kuwa katika mahali pa kelele za juu. Kwa mfano wale ambao huvaa hedifoni za stirio hujiumiza kwa kucheza muziki kwa sauti ya juu. Mojawapo madhara yawezayo kutokea ni tinnitus.
Bila shaka, ni vizuri kukumbuka maelezo ya Richard Hallam katika kitabu chake Living With Tinnitus: “Mwili si mahali pa ukimya kabisa na hivyo kadiri fulani ya ‘tinnitus’ ni jambo la kawaida. Kelele hutokana na miendo ya misuli, mifupa, damu na hewa. . . . Inafikiriwa kwamba katika hali za kila siku, kelele hizi za kichini-chini hufunikwa na kelele kubwa zaidi za mazingira yetu—na hivyo hazisikiki kabisa.” Kusoma makala hii huenda kumekufanya usikie kelele hizo za kichini-chini. Lakini, hizo hazisumbui watu wengi.
Hiyo Hutibiwaje?
Namna gani ikiwa ugonjwa huu unakusumbua sana? Jambo la kwanza unalopaswa kufanya ni kumwona daktari wako. Yeye atakusaidia kuona ikiwa tatizo linalotokeza dalili za ugonjwa wako laweza kutibiwa. Kwa kuhuzunisha, mara nyingi hakuna tiba kwa hiyo kelele. Lakini kuna mambo kadhaa yawezayo kufanywa ili kukusaidia kuishi na tinnitus:
▪ Upasuaji: Broshua Tinnitus, iliyotangazwa na Shirika la Tinnitus la Uingereza, yasema: “Nyakati nyingine tinnitus husababishwa na tatizo katika sikio la kati, na pindi kwa pindi husababishwa na kasoro katika mishipa ya damu au misuli iliyo katika sikio au karibu na sikio. Katika hali hizo zilizo nadra sana kuna uwezekano wa kuondoa tinnitus kabisa kwa kufanyiwa upasuaji.”
▪ Dawa: Ikiwa mwenye kuugua anapata ugumu wa kupata usingizi au ana hangaiko, mkazo, au ameshuka moyo, daktari aweza kumwagiza atumie dawa za kitulizo au za kuondoa mshuko-moyo ili kuondoa dalili hizo.
▪ Visaidizi vya Kusikia na “Vifunikaji”: Ikiwa kuna tatizo dogo la kutosikia vizuri, kisaidizi cha kusikia chaweza kusaidia sana. Pia kuna chombo kiitwacho kifunikaji, ambacho hufanana na kisaidizi cha kusikia. Hicho hutokeza sauti ya kichini-chini ili kufunika kelele za tinnitus. Lakini nyakati nyingine kucheza tu redio au kuwasha pepeo kwaweza kuwa na tokeo lilo hilo.
▪ Tiba Nyinginezo: Profesa Axelsson aliliambia Amkeni!: “Tiba ya msongo wa juu wa oksijeni pekee yaweza kuthibitika kuwa yenye msaada kwa wagonjwa fulani. Hiyo yatia ndani kuweka mwenye kuugua katika kizimba chenye msongo wa hewa, ambapo anapata oksijeni safi. Hilo laweza kuboresha kupona kwa sikio la ndani.” Na kwa kuwa kwa wagonjwa fulani dalili za tinnitus huonekana kuwa mbaya zaidi wanapokuwa na mkazo au wenye wasiwasi, madaktari fulani wamependekeza tiba mbalimbali za kutuliza.a Hata hivyo, kujifunza kutulia na kuepuka mkazo wa kimwili na kiakili kwa kadiri iwezekanavyo kwaweza kuwa kwenye msaada.
Kuishi na Huo Ugonjwa
Mpaka sasa, hakuna tiba ya tinnitus inayotazamiwa karibuni. Kwa hiyo tinnitus ni kelele ambayo huenda ni lazima ujifunze kuishi nayo. Chasema kitabu Living With Tinnitus: “Mimi na wenzangu sasa huamini kwa dhati kwamba itikio la kawaida kwa tinnitus ni kuendelea kuipuuza.”
Ndiyo, unaweza kufundisha ubongo wako kupuuza hiyo kelele, kuiona kuwa si kitu cha kutolea uangalifu. Je, waishi sehemu yenye kelele nyingi? Au, Je, wewe huwasha pepeo au kidhibiti-hewa? Mwanzoni kelele hizo huenda zilikuudhi, lakini baada ya muda ulizipuuza tu. Hata huenda ulijifunza kupata usingizi na kelele hizo! Vivyo hivyo, unaweza kujifunza kutotoa uangalifu mno kwa tinnitus.
Ugonjwa wa tinnitus ni mmojawapo magonjwa ambayo ni lazima yavumiliwe mpaka kufika kwa ulimwengu mpya wa Mungu unaokuja, ambamo “hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.” (Isaya 33:24) Kwa wakati huu, tinnitus yaweza kuwa tatizo la kufadhaisha, lakini si lazima iharibu au kutawala maisha yako. Uwe na hakika ya kwamba hii ni kelele unayoweza kuishi nayo!
[Maelezo ya Chini]
a Mkristo atataka kuhakikisha kwamba tiba kama hiyo haikiuki kanuni za Biblia. Kwa kielelezo, ona makala juu ya mazoezi ya autogenic (kujitibu mwenyewe) katika toleo la Amkeni! la Februari 22, 1984, la Kiingereza.
[Picha katika ukurasa wa 26]
Kupimwa na tabibu anayestahili kwaweza kuwa hatua ya kwanza ya kujifunza kuishi na “tinnitus”