Hifadhi ya Asili Yageuzwa Kuwa Mahali pa Mauaji ya Kiholela ya Vipepeo-Maliki
KATIKA safari ya uhamaji ya kustaajabisha sana, vipepeo-maliki ambao hupitisha kiangazi katika Kanada na kaskazini mwa Marekani, hutandaza mabawa yao ya rangi ya machungwa na nyeusi na kujipeperusha kutoka Kanada, wakivuka Marekani na kujikusanya katika eneo moja magharibi ya Mexico City. Huko, katika 1986 serikali ya Mexico ilitengeneza hifadhi tano za asili katika milima yenye kimo cha meta 3,400 iliyofunikwa kwa misunobari. Kulingana na hesabu iliyofanywa 1994, angalau vipepeo-maliki milioni 60 hupitisha majira ya kipupwe katika hifadhi hizo.
Misunobari hasa hupendwa na vipepeo kwa sababu miti hiyo hufanyiza mwavuli mzito ambao hulinda vipepeo hao na mvua ya baridi na barafu. Ni marufuku kukata miti katika hifadhi hizi, lakini marufuku hiyo haizuii ukataji miti bila ruhusa. Wanasayansi wanaoshughulikia vipepeo wana wasiwasi kwamba “ukataji miti ya misunobari katika hifadhi za Mexico, japo marufuku ya Serikali, unawafanya vipepeo-maliki kuathiriwa kwa urahisi na dhoruba na baridi kali. . . . Kupoteza miti na myavuli yayo hufanya vipepeo kuathiriwa kwa urahisi zaidi na mvua na barafu.” Ukataji miti huharibu mwavuli wenye kulinda. Kama Lincoln Brower, mzuolojia wa Chuo Kikuu cha Florida katika Gainesville, alivyosema kuhusu mwavuli wenye kulinda vipepeo-maliki: “Kadiri misitu hii inavyoharibiwa, ndivyo matundu yanavyozidi kuwapo katika mwavuli wenye kulinda.”
“Hali mbaya ya hewa na ukataji wa miti huangamiza vipepeo,” likasema The New York Times. Kisha liliripoti kuhusu kuanguka kwa theluji katika hifadhi hizo katika usiku wa Desemba 30, 1995: “Wasimamizi wa misitu wa serikali na wanazuolojia ambao walitembelea sehemu ya hifadhi hizo walisema kulikuwa na mafundo ya barafu yaliyojaa maelfu kwa maelfu ya vipepeo-maliki walioganda, na vipepeo wengi wakiwa wamefukiwa chini ya barafu.”
Picha iliyo juu kwenye ukurasa huu yathibitisha habari hiyo yenye msiba.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]
Jorge Nunez/Sipa Press