Barabara ya Emmy Zehden—Hadithi ya Jina Hilo
KATIKA Mei 1992, barabara mojawapo katika jiji la Berlin, Ujerumani, iliitwa kwa jina la Emmy Zehden, mmoja wa Mashahidi wa Yehova.
Emmy alizaliwa 1900. Aliolewa na mfanyabiashara Myahudi Richard Zehden, ambaye alikufa katika kambi ya mateso ya Auschwitz wakati wa utawala wa Nazi. Richard na Emmy walikuwa na mtoto wa kambo, Horst Schmidt. Horst na vijana wengine wawili Mashahidi wa Yehova walilazimika kujificha walipoitwa katika utumishi wa kijeshi.
Emmy aliwaficha Horst na waandamani wake wawili. Hata hivyo, baadaye waligunduli wa. Wote wanne walihukumiwa kifo—wavulana hao watatu kwa kukataa utumishi wa kijeshi na Emmy kwa kuwaficha. Waandamani wawili wa Horst walikatwa vichwa. Emmy aliomba aachiliwe, lakini ombi hilo lilikataliwa. Alikatwa kichwa katika Plötzensee, Berlin Juni 9, 1944.a Horst Schmidt aliokoka mateso ya Nazi na baadaye alifunga ndoa na Shahidi ambaye alikuwa mwokokaji wa kambi ya mateso.
Katika Mei 7, 1992, barabara moja katika Berlin iliitwa kwa jina la Emmy Zehden. Katika hotuba iliyotolewa na ofisa mmoja wa Ujerumani, mwanamke huyo alisifiwa kwa moyo mkuu wake na alitajwa akiwa kielelezo cha ‘majeruhi wengi wa vita waliosahauliwa.’
[Maelezo ya Chini]
a Kulingana na hati rasmi zilizo katika wonyesho kwenye Ukumbusho wa Berlin-Plötzensee, Emmy Zehden alifishwa Juni 9, 1944.