Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g91 4/8 kur. 10-12
  • Berlin—Wonyesho wa Jinsi Ulimwengu Wetu Ulivyo?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Berlin—Wonyesho wa Jinsi Ulimwengu Wetu Ulivyo?
  • Amkeni!—1991
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Vita ya Maneno Vyaanza
  • Ukuta wa “Amani” na wa “Aibu”
  • Amani na Usalama wa Kweli Ni Karibu
  • Yehova Alitutunza Chini ya Marufuku-Sehemu ya 2
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1992
  • Mambo Ambayo Ujerumani Iliyounganika Inakabili
    Amkeni!—2001
  • ‘Na Ukuta Ukaanguka kwa Kishindo’
    Amkeni!—1992
  • Mashahidi wa Yehova Katika Ulaya Mashariki
    Amkeni!—1992
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1991
g91 4/8 kur. 10-12

Berlin—Wonyesho wa Jinsi Ulimwengu Wetu Ulivyo?

Na mleta habari za Amkeni! katika Ujerumani

KATIKA Novemba 9, 1989, umati wenye furaha tele ulikwea Ukuta wa Berlin na wakazi wa Berlin ya Mashariki wasio na hesabu walivuka kwenda ng’ambo nyingine ya vituo vya upekuzi—jambo ambalo lilistaajabisha sana Wajerumani na watazamaji TV walio wengi kuuzunguka ulimwengu.

Tangu 1945 kwa njia fulani Berlin, imeonyesha ushindani ulioko kati ya zile mamlaka mbili kubwa, zinazowakilishwa kuwa “mfalme wa kaskazini” na “mfalme wa kusini.” (Danieli 11:36-45) Ushindani huo ulisitawije katika Berlin, na ni kwa nini mipaka ikafunguliwa sasa? Je! ulimwengu wetu uliogawanyika utabadilika pia?

Wakati wa Vita ya Ulimwengu ya 2 Soviet Union, United States, na Uingereza ziliungana katika kukabiliana na Ujerumani ya Nazi. Mataifa hayo yenye muungano yalidhani ushirikiano huo ungeendelea baada ya vita. Kwa hiyo, yakaafikiana kugawanya Ujerumani iliyoshindwa kuwa maeneo ya kukaliwa na majeshi yao na kuwa na shirika ya jiji yayo kuu, Berlin, ambayo ikaja kufurahia cheo cha kipekee. Kwa hiyo katika 1945 Ujerumani na Berlin zikagawanywa ili zidhibitiwe na usimamizi wa kijeshi wa Urusi, Amerika, Uingereza, na Ufaransa.

Upesi ikawa wazi kwamba mamlaka hizo ziliona na kufanya mambo kwa njia tofauti. Soviet Union ilitaka kuwe usimamizi wa Kikomunisti kwa Berlin yote, lakini mamlaka za Magharibi zilikazania mfumo wenye vyama vingi vya kisiasa katika visehemu vyazo. Katika uchaguzi wa Oktoba 1946, wanne kati ya kila wakazi watano wa Berlin walipiga kura ya kupinga Wakomunisti.

Katika 1948, wakati mamlaka za Magharibi zilipoamua kupendelea muundo mpya wa kiuchumi na kuwa na taifa moja la kidemokrasi katika maeneo yao yaliyokaliwa kijeshi katika Ujerumani ya Magharibi, Warusi waliondoka kwenye Baraza la Udhibiti la Mataifa Yenye Muungano. Ndivyo ulivyokoma usimamizi wa mamlaka nne zenye kuungana. Tumaini la kutawala Ujerumani kwa umoja kutoka Berlin likawa lenye maisha mafupi.

Vita ya Maneno Vyaanza

Berlin, iliyotiwa ndani ya eneo la Kirusi, ilidumisha hali yayo ya kusimamiwa na mamlaka nne. Kwa Warusi, waliodhibiti sehemu ya mashariki ya jiji hilo, kile kisehemu cha Magharibi kilichopachikwa humo kilikuwa ni “kiasili cha kigeni” kilicho hatari. Katika Juni 1948 walifanyiza ususiaji kamili wa barani dhidi ya sehemu za Magharibi kwa kusudi la kufunga njia za upitiaji za Berlin ya Magharibi ili kulazimisha Magharibi waachilie haki zao katika Berlin. Magharibi wangeitikiaje?

Katika Juni 26, 1948, usafirishaji kwa kutumia ndege ulio mkubwa zaidi katika historia ulianza. Kwa mwaka mmoja hivi, United States na Uingereza zilipanga safari za ndege 279,114, zikiwasilisha tani zipatazo milioni 2.3 za chakula, makaa ya mawe, na bidhaa nyingine kwenye jiji hilo. “Kizuizi cha Berlin kilikuwa ndicho kitangulizi cha Vita ya Maneno,” aeleza Norman Gelb katika kitabu chake The Berlin Wall. “Wakati uo huo, itikio kuelekea ususiaji huo ulithibitisha kwa mkazo uongozi wa Amerika katika Magharibi.”

Yeye aendelea hivi: “Kwa Moscow, ule uwezo wa Muungano wa Mataifa wa kukinza jitihada za Urusi za kuwafukuza kutoka kisehemu chao chenye utundu kilichopachikwa katikati ya eneo la Kikomunisti ulithibitisha usadikisho usiotikisika kwamba Magharibi walikuwa wameazimia kuangamiza mfumo wa Kirusi. Hakukuwa shaka jingine zaidi katika Kremlin kwamba, ili kuokoka, Soviet Union ingepaswa kuwa mamlaka kubwa ya kijeshi. Ung’ang’aniaji wa Berlin ulianzisha mvutano wa mamlaka zenye nguvu kubwa kati ya Urusi na Amerika ambao ukaja kuwa jambo kuu katika mambo ya kimataifa wakati wa nusu ya pili ya karne ya ishirini.”

Ususiaji huo ulipokoma, mamlaka za Magharibi ziliazimia kukaa katika Berlin, zikilinda hali yayo. Pengo kati ya Mashariki na Magharibi lilionekana lisiloweza kuzibika wakati, katika 1949, mataifa mawili ya Kijerumani yalipoanzishwa: Jamhuri ya Muungano ya Ujerumani (Magharibi) na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani (Mashariki). Sasa Berlin ilikuwa na usimamizi maradufu wa kiraia na mifumo miwili ya fedha. Wakati wa 1952 na 1953, taifa la Ujerumani ya Mashariki lilivunja uhusiano wa simu na kufunga miunganisho ya barabara na njia za kupitiwa na basi kati Berlin ya Mashariki na ya Magharibi.

Huku raia za Magharibi wakifurahia Wirtschaftswunder, mafanikio ya kiuchumi yenye kutolea wateja uchaguzi mkubwa wa bidhaa, walio wengi katika Mashariki waliachwa bila kuridhika. Jambo hilo lilionekana wazi katika Juni 1953, wakati wakazi wa Berlin ya Mashariki walipogoma, maandamano ya kupinga yalienea kwenye sehemu zote za Ujerumani ya Mashariki. Ongezeko liliongoza kwenye uasi wenye jeuri dhidi ya mfumo wa Kikomunisti. Serikali ya Ujerumani ya Mashariki iliomba vikosi vya Urusi msaada. Vifaru viligandamiza mchafuko huo.

Mamlaka za Magharibi hazikufanya lolote ila kutazama tu, zikitolea uhakikisho sehemu zazo za Berlin peke yazo. Matumaini ya kwamba mgawanyo wa Ujerumani ungekuwa wa muda tu yakavunjika. Mpaka kati ya maeneo yaliyokuwa hapo awali ya Urusi na Magharibi yakawa mstari wenye kugawanya Mashariki na Magharibi.

Ukuta wa “Amani” na wa “Aibu”

“Mfalme wa kusini” alifanya Berlin ya Magharibi kuwa “duka la wonyesho wa magharibi” lenye kuvutia, na watu kutoka Mashariki, ambao wangeweza kutembelea marafiki na watu wa ukoo kwa urahisi katika Berlin ya Magharibi, wakaona jinsi maisha yalivyokuwa tofauti huko. Katika 1960 karibu Wajerumani 200,000 walitoroka Mashariki kuingia Magharibi, walio wengi wakipitia Berlin ya Magharibi. “Mfalme wa kaskazini” angezuiaje “mvujo” huo? Asubuhi ya Agosti 13, 1961, walinzi wa Ujerumani ya Mashariki wenye silaha na wafanya kazi walijenga “uliokuja kuitwa upesi ama ‘Ukuta wa Aibu’ au ‘Ukuta wa Amani’—ikitegemea msimamo wako wa kisiasa,” kama anavyosema Norman Gelb. Mkomunisti mmoja wa Ulaya ya Mashariki alieleza hivi: “Sisi hatukuwa na jingine la kufanya. Tulikuwa tunapoteza wengi sana kati ya watu wetu walio bora zaidi.”

Si kwamba tu Ukuta wa Berlin ulikomesha mmiminiko wa wakimbizi bali pia uligawanya watu wa ukoo na marafiki. Miezi 28 baada ya ujenzi wao, wakazi wa Berlin ya Magharibi walipewa ruhusa ya kuona watu wa ukoo katika Berlin ya Mashariki kwa siku moja moja. Kufuatia maafikiano ya mamlaka nne, vizuizi vililegezwa zaidi katika miaka ya 1970, kwa simu na ziara kuruhusiwa kati ya Mashariki na Magharibi. Hata hivyo, karibu watu 80 walipoteza maisha zao wakijaribu kuvuka Ukuta wa Berlin.

Kabla ya Ukuta huo kubomolewa, Chansela Kohl alitaarifu hivi: “Sera ya Katibu Mkuu Gorbachev ya kuunda upya yaandamana, kwa mara ya kwanza tangu mwisho wa Vita ya Ulimwengu ya 2, na tumaini lenye kukubalika la kushinda pambano la Mashariki-Magharibi.” Hilo limejionyeshaje katika Berlin?

Mabadiliko katika milki ya “mfalme wa kaskazini” yaliruhusu maelfu ya Wajerumani wa Mashariki wakimbilie makao ya kibalozi ya Ujerumani ya Magharibi katika nchi kadhaa za Ulaya ya Mashariki katikati ya 1989. Makao ya kibalozi yalisongamana watu mno, hali ikawa isiyovumilika. Katika Septemba 1989 kulionekana tamasha ya mmiminiko wa wakimbizi waliochoka sana wakifunguliwa kutoka Mashariki na kuvikwa makoja walipowasili Magharibi. Shauku ilikuwa isiyozuilika, maono ya moyoni yakawa hayana mipaka.

Kuondoka huko kulichochea mijadala katika Ujerumani ya Mashariki. Ni nini kilichokuwa kisababishi cha mmiminiko huo? Mabadiliko makubwa-makubwa yalikataliwa, na katika Oktoba na Novemba 1989, Wajerumani wa Mashariki zaidi ya milioni moja, walifanya maandamano yenye amani katika Leipzig, Berlin ya Mashariki, na majiji mengine, wakipaaza sauti hivi: “Sisi akina yahe twataka haki zetu.” Serikali ya Ujerumani ya Mashariki ilikubali kushindwa na, baada ya miaka 28, ikafungua Ukuta wa Berlin na milango ya badiliko la kisiasa na kiuchumi. Ni kama gazeti Die Zeit la Kijerumani lilivyoeleza: “Katika 1989 historia ya ulimwengu ilitikiswa hadi kwenye misingi yayo, ikisukumwa zaidi na akina yahe kuliko na mamlaka.”

Kwa kuwa mipaka ilifunguliwa, wakazi wa Berlin “hawaishi tena kwenye kisiwa,” lasema gazeti la Kijerumani Süddeutsche Zeitung. Ubomoaji wa Ukuta huo ulianza katika 1990.

Amani na Usalama wa Kweli Ni Karibu

Kwa muda mrefu, Berlin ya Magharibi na Mashariki ilionekana kuwa wonyesho, si wa ulimwengu wetu uliogawanyika tu, bali pia wa matatizo yao. Kwa kielelezo, ingawa Wajerumani wa Mashariki wengi walifurahia faida fulani za kijamii, Mashariki walitatizwa na upungufu mbalimbali wa kiuchumi na uchafuzi ulioenea sana. Berlin ya Magharibi ilikabili matatizo yayo yenyewe, kama vile maasi ya wanafunzi, uharamia, na kashifa za kisiasa. Kwa hiyo, wala Magharibi wala Mashariki hazina mwongozo unaoweza kusuluhisha matatizo ya ainabinadamu ya tufe lote.—Mithali 14:12.

Hata mataifa yaweze kutimiza nini, jitihada za kibinadamu za kuunganisha ulimwengu wetu uliogawanyika haziwezi kuondoa ubinafsi au kufanya dunia iwe paradiso. Ni nguvu inayozidi uwezo wa kibinadamu tu ndiyo iwezayo kuleta umoja wa kweli na kuondoa hata magonjwa na kifo. Ufalme wa Mungu utatimiza kazi hiyo iliyo kubwa sana.—Mathayo 6:10; Ufunuo 21:1-5.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki