‘Na Ukuta Ukaanguka kwa Kishindo’
“NI NANI angaliweza kuamini?” “Mimi sikufikiri kamwe ningeona hayo maishani mwangu!” Ni nini kilichotokeza maneno hayo? Ni kuharibiwa kwa Ukuta wa Berlin usiopendwa na wengi pamoja na yote ambayo ulifananisha, kulikoanza katika Novemba 1989.a Waberlin wa Mashariki walimiminikia Berlin Magharibi, wengine ili waonje mapendezi ghali ya ubepari na wengine ili kuungana kama familia.
Mvunjiko huo wa handaki ulifungua milango ya furiko. Wengi walihisi kwamba Ulaya Mashariki haingekuwa kamwe kama vile ilivyokuwa pale mwanzoni.
Vita Baridi Yakomeshwa?
La maana zaidi kuliko anguko la ukuta wa Berlin ni anguko la ukuta wa kiitikadi uliotenganisha Mashariki na Magharibi. Kwa ghafula, hakuna Vita Baridi tena. Kama vile kanali David Hackworth wa Jeshi la U.S. aliyestaafu alivyoandika katika Newsweek: “Vita baridi imekoma. Hata wale wenye kuwachukia Wakomunisti sana wanakubali kwamba imekoma.”
Kulingana na gazeti la Kijerumani Stuttgarter Zeitung, hata NATO (Shirika la Mkataba wa Atlantiki Kaskazini), ilitambua mwisho wa Vita Baridi katika mkutano uliofanyiwa London katika Julai 1990. Chini ya kichwa “Patano la Atlantiki Lasema Kwaheri ya Mwisho kwa Enzi ya Vita-Baridi,” The German Tribune yanukuu gazeti la Stuttgart likisema: “Baada ya miaka 41 ya kukabiliana [na Urusi] viongozi 16 wa Nato waliandaa mbinu mpya na kuaga enzi ya vita baridi kwaheri ya mwisho. . . . Uhasama ungebadilishwa na ushirika. . . . Usalama na uthabiti. . . haungehakikishwa kamwe kwa njia za kijeshi hasa bali kwa sera ya usawaziko, mazungumzo, na ushirikiano wa Ulaya nzima.” Tamasha ya hitilafiano lenye kutisha amani imehama sasa kutoka Ulaya hadi Mashariki ya Kati.
Demokrasi Ina Bei Yake
Demokrasi, inayoitwa eti chaguo uhuru la watu, ndiyo siasa ya ki-siku-hizi yenye kupendwa na wengi. Na karibu kila mtu anaitaka. Lakini kuna bei ya kulipwa. Uhusiano wenye joto jingi zaidi kati ya Mashariki na Magharibi na demokrasi yake ya kibepari hauji kwa wepesi. Makala ya mhariri katika gazeti Asiaweek ilisema: “Nchi za lile lisiloweza tena kuitwa fungu la nchi za Urusi zimo katika tatizo kubwa la kiuchumi. . . Demokrasi huja kwa bei fulani. . . . Demokrasi ina mema mengi, lakini uthabiti mkamilifu si mojawapo.” Ni nani wanaolipa bei hiyo kwa ajili ya mabadiliko hayo ya jamii ya kidemokrasi, iliyo na uhuru zaidi kama inavyosemekana?
Mamilioni katika Polandi, Ujerumani mashariki, na kwingineko wanagundua kwamba ule mbadiliko wa kutoka kwenye uchumi unaodhibitiwa na serikali hadi kwenye mfumo wa soko huru huleta ukosefu wa kazi na taabu kubwa mwanzoni. Biashara zinapojaribu kuwa bora zaidi na kushindana, kufutwa kazi kunatokea. Sehemu nyingine za jamii zinaathiriwa kwa uzito pia—biashara za kijeshi na zana za kivita. Jinsi gani hivyo?
Woga na uhasama kati ya Mashariki na Magharibi unapotoweka, ndivyo na uhitaji wa majeshi mengi unavyodidimia. Mamia ya maelfu ya askari na familia zao watalazimika kuishi maisha ya kiraia pamoja na mikazo yayo yote. Kiasi cha fedha za serikali kwa ajili ya ulinzi huenda kikapunguzwa. Maagizo kwa viwanda vya kuundia silaha huenda yakapungua, na watengenezaji bidhaa huenda wakabadili aina ya bidhaa wanazotoa. Wafanyakazi huenda watalazimika kuhamia sehemu nyingine na kujifunza stadi mpya za kazi.
Mabadiliko haya yenye msukosuko na yenye kushangaza katika Ulaya Mashariki yamefanyiza hali mpya ya msingi ya kimataifa. Yote hayo yalitokeaje?
Maneno ya Maana, Mabadiliko ya Maana
Jambo la maana katika mabadiliko haya limekuwa ni ule mwelekeo mpya wa kutokuingilia ulioonyeshwa na Urusi. Katika wakati uliopita lile hangaisho kubwa la Urusi kuvamia Hungaria (1956) na Chekoslovakia (1968) liliwazuia wenye kutaka mabadiliko katika Ulaya Mashariki. Lakini lile ono la Polandi katika miaka ya 1980 la kutatizwa na chama cha Watetezi wa Mwungamano na mwendo wa polepole wa taifa kuelekea utawala wa kidemokrasi ulionyesha kwamba ile sera ya kwanza ya Urusi ya kuingilia mambo ya wengine kijeshi ilikuwa imebadilika. Ono la Polandi lilionyesha kwamba mipasuko katika nguzo ya Kikomunisti ilikuwapo na kwamba badiliko la polepole lenye amani lingeweza kupatikana, kwa bei fulani. Lakini ni nini kilichofanya haya yote yawezekane?
Kulingana na baadhi ya wafafanuzi wa kisiasa, la msingi katika mabadiliko yote katika Ulaya Mashariki imekuwa ni ile sera ya kujidukiza ya uongozi wa Urusi ulio chini ya uelekezi wa rais wa Urusi Mikhail Gorbachev. Katika Februari 1990 yeye alisema: “Chama cha Kikomunisti cha Urusi kilianzisha perestroika [kuunda upya jamii] na kikatokeza wazo na sera yayo. Mapinduzi makubwa yanayotia nyanja zote za maisha na sehemu zote za watu yameanzishwa kwa msingi huu nchini. . . . Mabadiliko ya haraka, yasiyo ya kawaida katika shauri na chanzo chake, yanatukia katika muundo wa perestroika.”
Kama vile Asiaweek lilivyoeleza: “Leo, ingawa kumekuwa na vizuizi fulani, kampeni ya [Gorbachev] ya glasnost (kutoa maoni waziwazi) na perestroika (kutengeneza upya) kumetia moyo wenye kutaka mabadiliko katika Hungaria, Polandi na kotekote katika Urusi.” Maneno haya mawili ya maana ya Kirusi, glasnost na perestroika, yameingia katika msamiati wa maneno ya ulimwengu tangu Gorbachev achukue mamlaka katika Urusi katika 1985. Maneno hayo yameonyesha mwelekeo mpya kuelekea serikali katika ulimwengu wa Kikomunisti.
Mfafanuzi wa kisiasa Philippe Marcovici, akiandika katika jarida la Kifaransa lisilopendelea mabadiliko Le Quotidien de Paris juu ya mabadiliko katika Chekoslovakia, alisema kwamba mabadiliko hayo yalikuwa yametokea “kwa msaada wa Moscow, kwa sababu jambo moja liko wazi: Warusi hawakuliacha tu litukie; walihakikisha kwamba Chekoslovakia, kama na demokrasi zile nyingine za watu, ingejiondoa kutoka kwenye kizuizi ambacho ilikuwa imefungiwa. . . . Katika Prague na Berlin Mashariki pia, maandamano makubwa yalileta mabadiliko; watu wenye kuandamana barabarani walilazimisha wenye mamlaka wajiuzulu kwa masharti na kuondoka.”
Matokeo yamekuwa kwamba, kama Mlima wa kisiasa St. Helen ukilipuka, demokrasi na uhuru zililipuka kwa nguvu katika ramani ya Ulaya yote ya Mashariki katika muda wa miezi michache—Polandi, Ujerumani Mashariki, Hungari, Chekoslovakia, Bulgaria, na Romania.
Muungano wa Ujerumani—Baraka au Laana?
Hilo ni swali ambalo wengi katika Ulaya wanajiuliza. Jerumani mbili zilianzisha umoja wa kifedha katika Julai 1990 na zikafikia umoja wa kisiasa katika Oktoba. Ingawa jambo hilo huwafanya mamilioni washangilie, pia huwafanya wengi katika Ulaya watetemeke. Hiyo inatia ndani wengine katika Ujerumani mashariki ambao huenda wakalazimika kupeana nyumba zao kwa wenyeji wa kwanza walio katika Ujerumani magharibi. Kujapokuwa na unyamavu ulioonyeshwa na viongozi wa Uingereza, gazeti moja la Uingereza lilikuwa na kichwa kikuu cha habari kilichosema: “Tutalazimika Tu Kutumaini Ujerumani Uliozaliwa-Upya.”
Ikiwa imeteseka chini ya mvamio mbaya sana na wenye gharama mikononi mwa Napoleon (1812) na Hitler (1941), Urusi mwishoni mwa Vita ya Ulimwengu ya 2 ilitaka ihakikishe usalama wake kwa kutumia maeneo mengine ya Ulaya Mashariki kama eneo salama la kuendeshea shughuli. Hivyo, bara la Urusi la nchi nane za Kikomunisti za Ulaya Mashariki lilifanyizwa miaka michache kabla ya 1945.b Sasa Urusi yahisi kuwa haitishwi sana na Ujerumani au United States, na imepunguza mamlaka yake juu ya nchi zake za kwanza ilizokuwa ikiongoza. Inaonekana kama kwamba lile Pazia la Chuma, lililotangazwa na Churchill katika 1946, limeyeyuka, likiruhusu mwangaza mpya kuingia.
Jinsi Mabadiliko Hayo Yanavyoweza Kukuathiri
Tayari tumeona baadhi ya matokeo ya kiuchumi katika mabadiliko hayo kwa nchi nyingi—kazi mpya, mazingira mapya, na ustadi mpya wa kazi kwa wengine. Kwa walio wengi kutakuwa na ukosefu wa kazi na taabu. Hayo ndiyo matokeo ya falsafa ya soko-huru la ulimwengu—kuokoka kwa wanaojiweza zaidi.
Kwa upande mwingine, badiliko hilo kuelekea demokrasi linaruhusu watu kutembea kwa uhuru zaidi. Na hiyo inamaanisha utalii wa kimataifa. Kama vile nchi nyingine (Hispania na Italia, kwa mfano) zimegundua katika miaka 30 iliyopita, utalii wa kutoka nchi za nje unaweza kuleta tofauti kubwa katika tatizo la baki baada ya malipo kwa serikali yoyote. Mamilioni katika Magharibi wanataka sana kuzuru miji ya kihistoria ya Ulaya Mashariki, miji ambayo majina yao hukumbusha vipindi vya utukuzo wa zamani za kale—Budapest, Prague, Bucharest, Warsaw, na Leipzig, kutaja michache. Watu wanataka pia waweze kuzuru Leningrad, Moscow, na Odessa, kwa uhuru. Vivyo hivyo, watu kutoka Ulaya Mashariki wanataka kuzuru Magharibi. Kwa kweli, utalii wa kimataifa huvunja vizuizi fulani vya chuki ya bila sababu na ujinga. Kama vile watalii wengi wamegundua, kushiriki pwani pamoja na waliokuwa eti maadui wako kwaweza kuufanya uhasama uishe.
Kuna jambo jingine kuhusu Ukuta huo ulioanguka ambalo huvutia mamilioni ya watu—ule uwezekano wa kushirikiana kwa uhuru pamoja na waamini wenzi wa kidini katika mataifa mengine. Ni kwa kadiri gani hilo litawezekana? Ni mabadiliko gani katika uwanja wa kidini yanayotokea katika Ulaya Mashariki? Makala inayofuata itafikiria swali hilo na mengine.
[Maelezo ya Chini]
a Ukuta wa Berlin, wenye urefu wa kilomita 47, unaotenganisha Berlin Mashariki na Magharibi, ulijengwa katika 1961 na Ujerumani Mashariki ili kuzuia kuhama kwa wakimbizi kuelekea Magharibi.
b Nchi hizo nane ni Chekoslovakia, Hungari, Romania, Bulgaria, Polandi, Ujerumani Mashariki, Albania, na Yugoslavia.
[Ramani katika ukurasa wa 5]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
UJERUMANI
Berlin
YUGOSLAVIA
HUNGARI
POLANDI
ROMANIA
CHEKOSLOVAKIA
ALBANIA
BULGARIA
URUSI