Mwisho wa Enzi—Je, Ni Tumaini kwa Wakati Ujao?
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UJERUMANI
KATI ya 1987 na 1990, matetemeko ya dunia yafikayo kiwango cha 6.9 au zaidi kwenye kipimo cha Richter yalitikisa sehemu za Armenia, China, Ekuado, Filipino, Iran, na Marekani. Watu wapatao 70,000 walikufa na makumi ya maelfu waliachwa bila makao. Hasara ziligharimu mabilioni ya dola.
Lakini, hakuna yoyote kati ya matetemeko hayo yaliyoshtua watu wengi, au kutokeza pigo kubwa zaidi, kama tetemeko jingine lililopata ulimwengu wakati uo huo. Hilo lilikuwa tetemeko la kisiasa, tetemeko lililomaliza enzi moja. Kwa kufanya hivyo, tetemeko hilo lilibadili wakati ujao wa mamilioni ya watu.
Ni nini kilichosababisha tukio hilo lenye kutokeza sana? Nalo lingekuwa na matokeo gani?
Glasnost na Perestroika
Mikhail Gorbachev alitangazwa katibu-mkuu wa Chama cha Ukomunisti cha Muungano wa Sovieti mnamo Machi 11, 1985. Wananchi wa Sovieti, pamoja na wengi wa wachunguzi wa matukio ya ulimwengu hawakutarajia mabadiliko makubwa ya kisiasa wakati wa usimamizi wake.
Muda unaopungua mwaka mmoja baadaye, Arkady Shevchenko, ambaye zamani alikuwa mshauri wa kisiasa wa waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Sovieti, na ambaye vilevile kwa miaka mitano alikuwa katibu-mkuu mdogo wa Umoja wa Mataifa, alisema kwa ufahamu wa kihususa alipoandika: “Muungano wa Jamhuri za Kisoshalisti za Sovieti umetatanika. Matatizo makubwa ya kiuchumi na kijamii yasipotatuliwa karibuni ni lazima mfumo wa kiuchumi utaendelea kuzorota, na hivyo kuhatarisha, baadaye, hata kuwapo kwao wenyewe. . . . Hakika Gorbachev ameanzisha jambo jipya . . . Lakini tunangoja kuona iwapo uongozi wake utafungua enzi mpya kwa Muungano wa Jamhuri za Kisoshalisti za Sovieti. . . . Anakabiliwa na matatizo ambayo ni kama hayawezi kutatuliwa.”
Cheo cha Gorbachev sasa kilimpa mamlaka ya kisiasa aliyohitaji ili kuwapa jamii ya Wasovieti sera ambayo alikuwa tayari ameizungumzia 1971. Sera hiyo ilikuwa glasnost, neno limaanishalo “kuarifu umma” nayo ilikuwa na mwongozo wa unyoofu wa serikali juu ya matatizo ya Sovieti. Sera hiyo ilitaka jamii iliyo huru zaidi, ambamo wananchi wa Sovieti na vyombo vya habari wangekuwa na uhuru zaidi wa usemi. Hatimaye, glasnost ilifungulia njia uchambuzi wa umma dhidi ya serikali na baadhi ya hatua yayo.
Neno jingine ambalo Gorbachev alikuwa ametumia kwa muda mrefu lilikuwa “perestroika,” neno limaanishalo “marekebisho.” Katika insha iliyotangazwa 1982, yeye alisema juu ya “uhitaji wa kufanya marekebisho yafaayo ya kiakili” katika sekta ya kilimo.
Baada ya kuwa kiongozi wa Muungano wa Sovieti, Gorbachev akasadiki kwamba ilikuwa lazima kurekebisha usimamizi wa kiuchumi. Alijua kwamba ingekuwa vigumu kutimiza jambo hilo—labda hata halingewezekana ila tu kama mabadiliko ya kisiasa yangefanywa vilevile.
Bidii ya Gorbachev katika kutekeleza sera hizo za glasnost na perestroika haikumaanisha kwamba alikusudia kuharibu Ukomunisti. La hasha. Kitabu The Encyclopædia Britannica chaeleza: “Mradi wake ulikuwa kuanzisha mageuzi yanayoongozwa na serikali. Yeye hakutaka kudhoofisha mfumo wa Sovieti, yeye alitaka tu kuuboresha.”
Kuondolewa kwa vizuizi kwa sababu ya sera hizo kulitokeza hali ya wasiwasi miongoni mwa washiriki fulani wa uongozi wa Muungano wa Sovieti. Na ndivyo ilivyokuwa kwa viongozi wa baadhi ya nchi za Ulaya za kikomunisti. Ingawa wengi wao waliona uhitaji wa kurekebisha mambo ya uchumi, si wote waliokubali kwamba mabadiliko ya kisiasa yalikuwa ya lazima au yaliyotakikana.
Hata hivyo, Gorbachev aliwajulisha wenzake wa Ulaya Mashariki kwamba walikuwa huru kujaribu programu zao za perestroika. Wakati uo huo, Gorbachev akaonya Bulgaria—na kwa uhalisi nchi nyinginezo zote za kikomunisti za Ulaya—kwamba ingawa mabadiliko yalikuwa lazima, ni lazima kutahadhari ukuu wa Chama cha Ukomunisti usishushwe.
Mwanzo wa Kudhoofika
Uchambuzi dhidi ya Ukomunisti, katika Muungano wa Sovieti na vilevile katika nchi za Ulaya za kikomunisti, ulikuwa umeongezeka katika miaka iliyokuwa imepita. Kwa kielelezo, tangu miaka ya mapema ya 1980, gazeti la kila juma la Hungaria HVG (Heti Világgazdaság) lilikuwa likipinga vikali maoni ya kawaida ya Kikomunisti, ingawa lilikuwa limeepuka kuchambua moja kwa moja Chama cha Kikomunisti chenyewe.
Chama cha Solidarity, ambacho ndicho chama cha kwanza cha wafanyakazi kilichokuwa huru kuwapo katika nchi za Ulaya za kikomunisti, kilianzishwa Poland 1980. Hata hivyo, chanzo chayo chaweza kufuatiliwa nyuma hadi 1976, wakati ambapo kikundi cha waasi kilipoanzisha Kamati ya Kutetea Wafanyakazi. Kufikia mapema 1981, chama cha Solidarity kilikuwa na wanachama wapatao milioni kumi. Kilitaka mabadiliko ya kiuchumi na uchaguzi-huru, nyakati nyingine kikisisitiza madai yacho kwa kufanya migomo. Ikishindwa na tisho ambalo lingeweza kutukia la Sovieti kuingilia mambo, serikali ya Poland hatimaye ilivunja chama hicho, hata ingawa kiliendelea kutenda kichini-chini. Migomo iliyodai serikali ikitambue kuwa halali ilifanya kitambuliwe rasmi tena katika 1989. Uchaguzi-huru ulifanywa mnamo Juni, 1989, na wagombea viti wengi wa chama cha Solidarity walichaguliwa uchaguzini. Kufikia Agosti, kwa mara ya kwanza katika miaka 40, waziri mkuu asiye Mkomunisti alikuwa akitumikia katika Poland.
Sera za glasnost na perestroika, pamoja na matatizo yaliyokumba nchi za Kikomunisti, kwa wazi zilikuwa zikibadili nchi zote za kikomunisti za Ulaya.
Perestroika ya Kisiasa Yatokeza Mapinduzi
“Kufikia Julai 1987,” aandika Martin McCauley wa Chuo Kikuu cha London, “mambo yote yalitendeka jinsi Mikhail Gorbachev alivyotaka.” Hata baadaye kama Juni 1988, kwenye Mkutano wa 19 wa Chama cha Ukomunisti katika Moscow, yaripotiwa kwamba “wengi walimuunga mkono [Gorbachev] kwa programu zake, ingawa si kwa uchangamfu mara nyingine.” Lakini ilikuwa wazi kwamba alikuwa akipata magumu katika kurekebisha Chama cha Ukomunisti na serikali ya Sovieti.
Mnamo 1988, mabadiliko ya kikatiba yaliruhusu kuondolewa kwa Bunge Kuu la Sovieti lililokuwapo wakati huo, na mahali payo kuchukuliwa na Bunge la Muungano wa Jamhuri za Kisoshalisti za Sovieti la Wabunge wa Watu, ambalo lilikuwa na wabunge 2,250 waliochaguliwa mwaka mmoja baadaye katika uchaguzi-huru. Wabunge hao nao walichagua kutoka miongoni mwao bunge lenye kamati mbili, kila kamati ikiwa na washiriki 271. Boris Yeltsin akawa mshiriki mashuhuri wa bunge hilo. Upesi akaanza kutaja jinsi perestroika ilivyokosa kufanikiwa na kueleza mabadiliko ambayo alihisi ni ya lazima. Hivyo, hata ingawa Gorbachev alikuwa amepandishwa cheo katika 1988 kuwa rais, cheo ambacho alitaka kurekebisha kabisa na kuimarisha, alizidi kupata upinzani.
Kwa wakati uo huo, yale mataifa mawili makuu, Muungano wa Sovieti na Marekani, yalikuwa yakifanya maendeleo makubwa katika kupunguza majeshi na kuondoa tisho la nyuklia. Kila mwafaka uliofanywa ulitokeza tumaini jipya kwamba amani ya ulimwengu ingeweza kupatikana—hivi kwamba mwandikaji John Elson akasema hivi Septemba 1989: “Siku za mwisho za miaka ya 1980, kwa wafafanuzi wengi wa mambo, ni za kuaga silaha kwa njia fulani. Vita baridi yaonekana kama imekwisha; amani inaonekana inatokea katika sehemu nyingi za ulimwengu.”
Kisha Novemba 9, 1989 ikaja. Ingawa kihalisi Ukuta wa Berlin ulikuwa ungali umesimama, baada ya miaka ipatayo 28 ulifunguka na kwa ghafula ukakoma kuwa kizuizi cha mfano kati ya Mashariki na Magharibi. Taifa moja baada ya jingine la Ulaya Mashariki yaliacha utawala wa kisoshalisti kwa kufuatana. Katika kitabu chake Death of the Dark Hero—Eastern Europe, 1987-90, David Selbourne aliliita tukio hilo “mojayapo ya mapinduzi makubwa zaidi ya kihistoria: mapinduzi ya kidemokrasi, yenye kupinga kabisa usoshalisti, ambayo matokeo yayo yatadumu muda mrefu baada ya watu walioyatokeza, na wale walioyashuhudia, kutoweka.”
Mara yalipofikia upeo, mapinduzi hayo ya amani yalimalizika upesi. Bango moja lililoonekana Prague, Chekoslovakia, lilitaja hivi kwa ufupi: “Poland—[ukomunisti ulisalimu amri] Baada ya Miaka 10; Hungaria—Miezi 10; Ujerumani Mashariki—Majuma 10; Chekoslovakia—Siku 10. Na kisha baada ya juma moja la ogofyo kuu, Rumania—Muda wa Saa 10.”
Kumaliza Vita Baridi
Mtungaji wa vitabu Selbourne asema: “Mwendo wa ujumla wa kuanguka kwa Ulaya mashariki ulifuatana kwa njia ya kustaajabisha.” Kisha aongezea: “Kwa wazi kichocheo kilikuwa kutwaa mamlaka kwa Gorbachev katika Moscow mnamo Machi 1985 na kumaliza kwake ‘Sera ya Brezhnev’, jambo ambalo lilinyima tawala za Ulaya mashariki uhakikisho wa kupata msaada wa Sovieti na wa kuingiliwa mambo iwapo maasi ya wengi yangetokea.”
Gorbachev atajwa na The New Encyclopædia Britannica kuwa “mwanzilishi wa pekee kabisa wa mfululizo wa matukio mwishoni-mwishoni mwa 1989 na 1990 ambao ulibadili mfumo wa kisiasa wa Ulaya na kuanzisha kumalizika kwa Vita Baridi.”
Bila shaka, Gorbachev hangeweza kumaliza Vita Baridi akiwa peke yake. Akionyesha mambo ambayo yangetukia karibuni, waziri mkuu wa Uingereza Margaret Thatcher alisema hivi baada ya kukutana naye kwa mara ya kwanza: “Nampenda Bwa. Gorbachev. Tunaweza kushirikiana.” Na zaidi, uhusiano wa kibinafsi na wa kipekee kati ya Thatcher na rais wa Marekani Reagan ulimwezesha Thatcher amsadikishe Reagan kwamba ni jambo la hekima kushirikiana na Gorbachev. Gail Sheehy, mtungaji wa kitabu Gorbachev—The Making of the Man Who Shook the World, akata kauli hivi: “Thatcher angeweza kufurahi kuwa ‘katika maana halisi yeye alikuwa mdhamini wa uhusiano kati ya Reagan na Gorbachev.’”
Na kama vile mara nyingi imetukia katika historia, watu muhimu walikuwa mahali pafaapo kwa wakati ufaao ili kuleta mabadiliko ambayo labda hayangetokea.
Matarajio ya Wakati Ujao Yasiyo Maangavu
Hata wakati Mashariki na Magharibi ziliposhangilia kwamba Vita Baridi ilikuwa inakwisha, mawingu ya kutisha yalikuwa yakitokea sehemu nyingine. Ulimwengu haukufikiri sana katika 1988 uliposikia kutoka Afrika kwamba maelfu kadhaa ya watu katika Burundi walikuwa wamekufa katika jeuri mpya ya kikabila. Wala uangalifu haukuelekezwa kwa ripoti zilizokuwa zikitoka Yugoslavia mnamo Aprili 1989 kwamba jeuri mbaya zaidi ya kikabila tangu 1945 ilikuwa ikiendelea huko. Wakati uo huo, uhuru zaidi ulioonekana katika Muungano wa Sovieti ulikuwa ukitokeza ghasia nyingi za raia. Baadhi ya jamhuri hizo hata zilikuwa zikijaribu kupata uhuru.
Mnamo Agosti 1990, majeshi ya Iraki yaliingia Kuwait, yakiishinda kwa muda wa saa 12. Huku Wajerumani, muda unaopungua mwaka moja tangu kuanguka kwa Ukuta wa Berlin, walipokuwa wakisherehekea muungano wa Ujerumani, rais wa Iraki alikuwa akijigamba: “Kuwait ni mali ya Iraki, nasi hatutaiacha hata kama ni lazima tuipiganie kwa miaka 1,000.” Mnamo Novemba Umoja wa Mataifa ulichukua hatua na kutisha kuchukua hatua ya kijeshi Iraki isipoondoka Kuwait. Kwa mara nyingine tena ulimwengu ulikuwa ukingoni mwa msiba, na suala hasa lilikuwa udhibiti wa mafuta.
Basi, je, matumaini ya amani na usalama ambayo yalikuwa yameamshwa wakati wa mwisho wa Vita Baridi yangekwisha kabla ya kutimizwa? Soma kuhusu hilo katika makala ifuatayo “‘Utaratibu wa Ulimwengu Mpya’—Waanza Kihafifu.”
[Picha katika ukurasa wa 15]
Ukuta wa Berlin kwa ghafula ukakoma kuwa kizuizi cha mfano kati ya Mashariki na Magharibi
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 12]
Gorbachev (kushoto) na Reagan: Robert/Sipa Press