Utafutaji wa Amani na Usalama
Watu walio wengi wana tamaa ya kiasili ya amani na utulivu, lakini tamaa hiyo imevurugwa muda wa sehemu kubwa ya historia ya kibinadamu. Hata hivyo, miaka ya majuzi kumekuwako matimizo ya kustaajabisha katika jitihada ya binadamu kutafuta amani, kama ionyeshavyo orodha inayofuata.
1985: (Oktoba) Umoja wa Mataifa waadhimisha mwaka wa 40 wa siku ya kuzaliwa kwao na yapiga mbiu 1986 uwe Mwaka wa Amani ya Kimataifa.
(Novemba) Mkutano wa mataifa makubwa ulio wa kwanza katika muda wa miaka sita Gorbachev na Reagan wakutanapo; Reagan asema juu ya “mwanzo mpya kabisa.”
1986: (Januari) Gorbachev atoa wito wa kupiga marufuku silaha zote za nyukilia kufikia mwaka 2000.
(Septemba) Mkutano Juu ya Hatua za Kusitawisha Uhakika na Usalama na Kuondoa Silaha Katika Ulaya (mataifa 35, kutia na United States, Kanada, Urusi, na Ulaya yote isipokuwa Albania) watia sahihi mkataba wa kupunguza hatari ya kutokea vita ya kiaksidenti.
(Oktoba) Mkutano kati ya Reagan na Gorbachev katika Iceland wakosa kutimilika, ingawa Gorbachev asema walikuwa kwenye ukingo wa kufanya “maamuzi makubwa, yenye kufanyiza historia.”
1987: (Januari) Mwongozo wa glasnost (kusema wazi) waonekana kuwa ukielekeza kwenye enzi mpya katika Urusi.
(Machi) Ziara ya kwanza ya waziri mkuu Mwingereza kwenda Mosko katika muda wa miaka 12.
(Desemba) Gorbachev na Reagan watia sahihi mapatano ya INF (Intermediate-range Nuclear Forces [Makombora ya Nyukilia ya Masafa ya Kati]) ili kukomesha makombora ya nyukilia ya masafa ya kati.
1988: (Machi) Nikaragua na wapambani wenye kupinga Ukomunisti watia sahihi mapatano ya kukomesha vita, wakianza masikilizano ya kufikia suluhisho la daima.
(Aprili) Urusi yatangaza kuondoa vikosi kutoka Afghanistan kufikia Februari 1989; Ethiopia na Somalia zakubaliana kumaliza pigano.
(Mei) Vietnam yatangaza kuondoa askari 50,000 katika Kampuchea kabla ya mwisho wa mwaka, na waliosalia kufikia 1990.
(Juni) Waziri Mkuu wa Australia Bob Hawke asema hivi juu ya mkutano kati ya Gorbachev na Reagan katika Moscow: “Kwa mara ya kwanza katika kipindi kizima cha baada ya vita, kuna ishara halisi za kuibuka kwa ulimwengu uwezao kuishi kwa kujengana katika amani.”
(Julai) Iran yatangaza kupokewa kwa azimio la UM lenye wito wa kukomesha pigano katika vita ya miaka minane baina ya Iran na Iraq.
(Agosti) United States yakubali kulipa haki za UM ambazo zilikuwa zimezuiliwa, mwendo uliokwisha chukuliwa na Warusi, hivyo wakisaidia kumaliza tataniko la kifedha la UM na kulipatia tena msimamo.
(Septemba) Vikosi vya magaidi wa Morocco na Polisario vyapokea mpango wa UM kumaliza miaka 13 ya vita katika Sahara ya Magharibi.
(Oktoba) Vikosi vya kutunza amani vya UM vyatuzwa Tuzo la Nobeli la Amani; Libya na Chad zamaliza rasmi hali ya vita yenye kuwako kwa muda mrefu.
(Desemba) Kwenye UM, Gorbachev atangaza hatua kubwa ya upande mmoja ya kupunguza vikosi vya Urusi katika muda wa miaka miwili na kuondolewa kwa vikosi vifaru Czechoslovakia, Hungari, na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujeremani; Afrika Kusini, Namibia, na Kyuba zaafikiana kutekeleza azimio la UM siku ya Aprili 1, 1989, zikitoa uhuru wa Namibia na kumaliza miaka 22 ya vita; nusu ya askari 50,000 Wakyuba katika Angola kuondolewa kufikia Novemba 1, na waliosalia kufikia Julai 1, 1991; United States yakubali kuongea na Shirika la Ukombozi wa Palestina baada ya Yasser Arafat kuhakikishia kabisa haki ya Israeli “kuwako katika amani na usalama.”
1989: (Januari) Mataifa 149 yenye kuhudhuria Mkutano wa Paris Kuhusu Silaha za Kikemikali zatoa wito hatua ya haraka sana ichukuliwe kupiga marufuku usitawishaji, utengenezaji, uwekaji akiba, na utumiaji wa silaha za kikemikali.
(Februari) Costa Rica, Honduras, El Salvador, Nikaragua, na Guatemala zatia sahihi mwafaka wa kuhifadhi amani katika Amerika ya Kati; kikundi kilicho kikubwa zaidi cha uasi Kolombia, FARC (Majeshi Yenye Silaha ya Mapinduzi Kolombia), chatangaza kukomesha pigano, kikitokeza matumaini ya kwamba miaka 35 ya vita vya magaidi huenda yakaribia kuja kwenye ukomo.
(Machi) Mawaziri wa nchi za kigeni kutoka mataifa 35 waanza maongezi katika Vienna juu ya CFE (Masikilizano Kuhusu Majeshi Yenye Silaha za Kawaida Katika Ulaya), yakikusudiwa kupunguza majeshi katika Ulaya.
(Aprili) Vietnam yatangaza kuondoa kabisa askari katika Kampuchea kufikia Septemba 30.
(Mei) Hungari yaanza kuondoa kizuizi chayo cha seng’enge ya miaka 40 katika mpaka wa Austria; kwenye mkutano wa kwanza wa viongozi Warusi na Wachina katika muda wa miaka zaidi ya 30, Warusi watangaza kupunguzwa kwa majeshi ya Esia; Warusi waanza hatua ya upande mmoja kuondoa askari wao na silaha katika Ulaya ya Mashariki.
(Juni) Wito wa Bush wa kupunguza sana askari, vifaru, mizinga, na ndege za vita katika Ulaya kufikia 1992 waongoza gazetihabari kusema hivi: “Kwa kweli huenda hiyo ikafungua mlango wa mipunguzo ya silaha iliyo mikubwa zaidi tangu mwisho wa Vita ya Ulimwengu 2.”
(Agosti) Mataifa matano ya Amerika ya Kati yaafikiana juu ya mpango wa kumaliza vitendo vya uhasama katika Nikaragua.
Hata hivyo, kujapokuwa na matimizo hayo ya kuvutia, mabara mengi yangali mbali na kupata shangwe ya kuwa na amani. Watu wangali wanakufa katika Ailandi Kaskazini, Lebanoni, Sudan, Sri Lanka, Afghanistan, na Ufilipino—kutaja machache tu—kwa sababu ya tendo la kivita. Kwa sababu hiyo, ingawa watu wanahisi wakiwa na matazamio mazuri zaidi ya wakati uliotangulia kuhusu matazamio ya amani, hatupaswi kusahau kwamba mpanda farasi wa pili wa Apokalipsi, yule “farasi rangi-moto” wa vita, angali akiruka-ruka kupita duniani.—Ufunuo 6:3, 4, NW.