Mambo Ambayo Ujerumani Iliyounganika Inakabili
Na Mwandishi Wa Amkeni! Nchini Ujerumani
“MIMI na wazazi wangu tulipovuka mpaka wa Ujerumani Mashariki kuingia Berlin Magharibi, umati wa watu walisimama kwenye madaraja yaliyo juu ya barabara kuu ya magari yaendayo kasi wakipunga mikono na kushangilia,” Ronny akumbuka. “Tulizunguka eneo la maduka la Ku’damm mjini Berlin Magharibi, na mara tu watu walipotambua kwamba tulitoka Ujerumani Mashariki, walitununulia vinywaji. Kote kulikuwa ni vifijo na nderemo.” Jambo hilo lilitukia Novemba 10, 1989, siku moja baada ya kufunguliwa kwa Ukuta wa Berlin.
Furaha hiyo ilienea mbali zaidi ya Berlin, nayo ikafika kotekote Ujerumani Mashariki na Ujerumani Magharibi ambazo zilikuwa nchi mbili tofauti wakati huo. Kipindi cha Wende—ambacho charejezea kipindi muhimu cha mabadiliko au mapinduzi yasiyotumia silaha yaliyosababisha anguko la utawala wa kimabavu wa Taifa la Ujerumani Mashariki—kilishangaza watu wote. Miaka mingi baadaye, wengi bado huona Wende kuwa kipindi chenye furaha zaidi katika miaka 50 iliyopita. Bila shaka, nafasi ya furaha nyingi hiyo imechukuliwa na hali halisi ya maisha, na twaweza kuuliza, Maisha yamebadilikaje tangu kipindi cha Wende? Twaweza kujifunza nini kutokana na matukio tangu kipindi hicho?
Mwisho wa Vita Baridi
Kwa Wajerumani walio wengi kufunguliwa kwa Ukuta wa Berlin kulikuwa tulizo kubwa. Kulingana na ripoti mbalimbali watu elfu moja hivi waliuawa kwenye mpaka huo hatari uliotenganisha Mashariki na Magharibi. Mnamo Oktoba 1990, nchi mbili hizo za Ujerumani ziliunganishwa ziwe Taifa moja lenye watu milioni 80 hivi, liitwalo Jamhuri ya Muungano ya Ujerumani. Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani (GDR)—iliyokuwa Ujerumani Mashariki—ilikoma kuwapo miaka 41 tu baada ya kuanzishwa kwake. Eneo lililokuwa chini ya mamlaka ya GDR sasa limegawanywa kuwa majimbo sita, ambayo kwa kawaida hujulikana kama majimbo mapya ya muungano.
Ulimwengu ulishangazwa wakati Wende ilipoharakisha kuvunjika kwa utawala wa kikomunisti katika nchi nyingi, kukomeshwa kwa muungano wa ulinzi wa Mwafaka wa Warsaw na mwisho wa Vita Baridi. Vikosi vya mataifa makubwa—waliolinda mpaka wa ndani wa Ujerumani kwa muda wa miaka 40 hivi—waliondoka Ujerumani. Mambo hayo yalitukia pasipo utumizi wa silaha.
Baada ya kuunganika kwa Ujerumani, mabadiliko makubwa yaliathiri maisha, hasa katika majimbo mapya ya muungano. Kwa wengi mabadiliko hayo yalikuwa makubwa kuliko walivyotarajia.
Hatimaye Uhuru!
Watu wa GDR walitaka kipindi cha Wende kiwaletee hasa uhuru. Jambo hilo halishangazi, kwa kuwa Serikali hiyo ya kimabavu ilikuwa imezuia kupita kiasi uhuru wa raia. Katika siku za kabla ya Wende, ilikuwa vigumu sana kupata visa kwenda Berlin Magharibi au haikuwezekana. Kwa ghafula hali hiyo ilibadilika. Mwanamke mmoja alisema: “Wazia, twaweza kwenda Marekani!” Wengi waliokutana tena na watu wa ukoo na marafiki waliokuwa wameishi upande mwingine wa mpakani wana sababu ya kushukuru.
Uhuru hauruhusu tu wenyeji wa Ujerumani Mashariki kwenda magharibi, bali pia watu wa magharibi kwenda mashariki. Kwa hiyo, watalii waweza tena kutembea na kuona sehemu zenye kupendeza katika majimbo mapya ya muungano. Kwa mfano, watalii wanaweza kuzuru mji wa Wittenberg, ambapo Martin Luther alianzisha Marekebisho Makubwa ya Kidini, yaliyokuwa mwanzo wa dini ya Protestanti. Pia wanaweza kuzuru mji wa Meissen, ujulikanao kwa sababu ya vyombo vya kauri vinavyotengenezwa kwa mikono, na Weimar ambao ni mji walimoishi waandishi wawili mashuhuri wa Ujerumani waitwao Johann Wolfgang von Goethe na Friedrich von Schiller. Katika mwaka wa 1999, Weimar ulitangazwa kuwa Mji wa Utamaduni wa Ulaya, mji wa kwanza wa nchi za Kikomunisti kuheshimiwa hivyo.
Vipi uhuru wa kusema? Watu katika majimbo mapya ya muungano waweza kusema wazi bila kuogopa kusikilizwa na Stasi, au shirika la usalama la serikali. Na mtu mmoja-mmoja hufurahia kuchagua bila vizuizi vipindi vya televisheni na vitabu vya kusoma. Matthias akumbuka: “Nilipokuwa shuleni, tulinyang’anywa vitabu vyo vyote tulivyopata kutoka Magharibi.”
Namna gani Uhuru wa kuabudu? Nchini GDR, dini ilizuiwa, na raia 2 kati ya 3 hawakuwa na dini yoyote. Watu wote wa Ujerumani iliyounganika wamekuwa na uhuru wa kuabudu kwa muda wa zaidi ya miaka kumi, kipindi kirefu zaidi tangu Hitler alipoanza kugandamiza dini mwaka wa 1933. Hata hivyo, uhuru wa dini haumaanishi kwamba watu hupendezwa na dini. Kwa muda mrefu, makanisa makubwa yamekuwa yakilalamikia kupunguka kwa uvutano wake juu ya watu, na kipindi cha Wende kilizidisha hali hiyo. Kwa upande mwingine, Mashahidi wa Yehova, waliokuwa chini ya marufuku na kunyanyaswa na utawala wa kimabavu, wamepanua utendaji wao. Wakati wa miaka kumi iliyopita, Majumba ya Ufalme 123 na Majumba mawili ya Mkusanyiko yamejengwa na Mashahidi wa Yehova katika majimbo mapya ya muungano.
Ujenzi wa namna zote umefanywa kwa kadiri kubwa sana katika majimbo hayo mapya. Mji wa Berlin umerudishwa kuwa makao makuu ya taifa na unafanyiwa marekebisho makubwa. Kotekote katika majimbo mapya ya muungano, mambo ya msingi ya nchi yanarekebishwa yawe bora, na hayo yanatia ndani matumizi makubwa ya fedha kwa ajili ya barabara na reli. Mengi yamefanywa ili kusafisha mazingira na kufanya utunzaji wa afya na huduma ya jamii kufikia kiwango cha Magharibi. Wakazi wengi wa majimbo mapya ya muungano wanakubali kwamba sasa wana maisha ya hali ya juu zaidi.
“Maisha Yalipendeza”
Hata hivyo, wengine hukumbuka siku za kabla ya Wende na kuzitamani. “Maisha yalipendeza,” aeleza mwanamke mmoja. Maisha chini ya utawala wa kimabavu yalipendezaje? Watu kadhaa husema kwamba maisha yalikuwa ya kawaida na yenye usalama. Wengi walipenda uhusiano wa karibu pamoja na marafiki na majirani, wakahisi kwamba msaada uliweza kupatikana wakati wowote. Kulingana na Taasisi ya Uchunguzi wa Maoni ya Watu ya Allensbach, “utawala wa kimabavu hufanya raia zake kujihisi kuwa bora kimaadili na wenye usalama.” Mara utawala wa kimabavu wa GDR ulipokoma, ukaribu huo uliokuwa katikati ya watu ulitoweka pia.
Mfano mwingine: Katika miaka ya 1980 bei za bidhaa na huduma za kawaida zilikuwa za chini na kila mtu alikuwa na kazi. “Bei ya mkate mdogo ilikuwa pfennig tano za Ujerumani, lakini sasa bei imepanda kufikia angalau pfennig 50,” alalamika Brigitte. Wakati biashara huru ilipoanzishwa, biashara nyingi za serikali zilifilisika, na kusababisha ukosefu wa kazi. Ukosefu wa kazi katika sehemu iliyokuwa Ujerumani Mashariki ni maradufu ya sehemu ya magharibi.
Kufikia sasa, gharama ya kufanikisha muungano huo ni dola bilioni 800 hivi za Marekani. Na bado kuna mengi yanayohitaji kufanywa. Alipaye ni nani? Kodi maalum imetozwa kulipa sehemu ya gharama. Kwa hiyo, kipindi cha Wende kimegusa Wajerumani kihisia na pia kuwaathiri kifedha. Je, utumizi huo wa fedha na jitihada hizi zote zimekuwa zenye manufaa? Wengi huona muungano huo kuwa wenye manufaa, na jambo la kujionea fahari.
Twaweza Kujifunza Nini?
Kipindi cha Wende kimeonyesha kwamba kubadili serikali hakutoshelezi watu wote. Watu wengi—hata wale wanaoona kwamba kipindi cha Wende kilileta manufaa—wameona kwamba maisha katika jumuiya ya ubepari yenye mashindano yaweza kukatisha tamaa sawa na maisha chini ya utawala wa kimabavu. Bila shaka uhuru na ufanisi ni mambo mazuri. Lakini wakati uhuru na ufanisi unaposababisha maisha yasiyo na urafiki na huruma, furaha haidumu.
Ripoti ya karibuni kutoka Dessau, katika iliyokuwa Ujerumani Mashariki, yasema hivi: “Miaka kumi imepita tangu Ujerumani iungane; mabilioni ya dola zimetumiwa kwa kusudi la kutatua matatizo ya zamani.” Hata hivyo, kufikia leo wengi hawajafurahishwa na matokeo ya muungano huo.
Taasisi ya Allensbach yaripoti kwamba wengi hutumaini kwamba “mbali na uchumi huru na uchumi uliopangwa, kungekuwako njia ya tatu” ya kuongoza shughuli za wanadamu. Mashahidi wa Yehova wanalo tumaini hilohilo.
Wanaamini kwamba hakuna mfumo wa kisiasa wala wa kiuchumi uliotengenezwa na wanadamu, utatosheleza mahitaji ya wanadamu wote. Mashahidi huamini kwamba wanadamu watatoshelezwa mahitaji hayo kupitia tu Ufalme wa Muumba wa Kimesiya. Kulingana na Biblia, hivi karibuni, serikali hiyo ya mbinguni itaanzisha utawala wenye upendo na uadilifu juu ya dunia yote. Ufalme huo utaunganisha mataifa yote ya dunia na kuwezesha, si Wajerumani tu, bali wanadamu wote kukaa kwa amani. Ufalme huo utakuwa baraka iliyoje!—Danieli 2:44.
[Ramani katika ukurasa wa 23]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Bonn
Berlin
Wittenberg
Weimar
[Picha katika ukurasa wa 24]
Kubomolewa kwa Ukuta wa Berlin na kuondolewa kwa mpaka kulionwa na wengi kuwa tulizo
[Hisani]
Foto: Landesarchiv Berlin
[Picha katika ukurasa wa 24]
Kituo cha Ukaguzi cha Charlie, alama ya Berlin ya Vita Baridi, kabla na baada ya kukoma kwa vita hivyo
[Hisani]
Foto: Landesarchiv Berlin
[Picha katika ukurasa wa 25]
Berlin, ambao umerudishwa kuwa makao makuu ya taifa, unafanyiwa marekebisho
[Picha katika ukurasa wa 25]
Kufikia sasa Mashahidi wa Yehova wamejenga Majumba ya Ufalme 123 katika majimbo mapya ya muungano