Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 6/8 kur. 13-15
  • Badiliko la Umbo Je, Kuona Ni Kuamini?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Badiliko la Umbo Je, Kuona Ni Kuamini?
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Je, Mambo Hayo Huungwa Mkono na Maandiko?
  • Kuona Hakuwi Kuamini Sikuzote
  • Badiliko la Kweli
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1985
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2001
  • Ufundishaji wa Kimungu Dhidi ya Mafundisho ya Mashetani
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2007
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 6/8 kur. 13-15

Badiliko la Umbo Je, Kuona Ni Kuamini?

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA JAMHURI YA AFRIKA YA KATI

MGANGA wa kienyeji alikuwa amekufa. Lakini wengi wa watu katika umati uliokusanyika nje ya nyumba yake, waliamini kwamba alikuwa amebadilika umbo tu. Kwa kuwa alipokufa, chatu mkubwa alionekana akitambaa kutoka mlangoni pa nyumba yake! Kwa watu wengine, hayo ni mambo tu yaliyotukia wakati mmoja. Lakini kwa wengine, chatu huyo alikuwa ithibati yenye kusadikisha ya kwamba yule mganga wa kienyeji alikuwa amebadilika na kuwa chatu—alikuwa amebadili umbo lake!

Katika sehemu nyingi za Afrika, watu wengi huamini kwamba binadamu anaweza kubadilika au kubadilishwa na kuwa mnyama. Mara nyingi wachawi huaminiwa kuwa na uwezo wa kutwaa umbo la chui au chatu. Hali kadhalika, watu wengi huhofu kwamba mchawi aweza kuwabadili wengine wawe wanyama. Katika Afrika magharibi, yaaminiwa kwamba walozi wanaweza kutuma roho za wanadamu kupitia ndege au wanyama wengine ili kudhuru. Katika Afrika ya kati, watu fulani hawawezi kumwua ndovu au nyoka, wakihofu kwamba huenda ikawa mmoja wa watu wa jamaa zao aliyekufa amebadilika na kuwa mmoja wa wanyama hao.

Ingawa huenda itikadi hizo zikaonekana kuwa za ajabu kwa wasomaji fulani, Waafrika wengi huhisi kwamba mabadiliko hayo ya umbo yamethibitishwa na watu fulani waliojionea kwa macho. Wao hudai kwamba zile hadithi nyingi zinazosimuliwa na watu wenye akili timamu kwa kweli si matukio ya kinasibu tu.

Pia kwa hakika itikadi kama hizo zaweza kupatikana ulimwenguni pote. Kwa kielelezo, huko Japani kuna itikadi ya kwamba mbweha, mbwa, na wibari waweza kukaa ndani ya wanadamu. Sanaa ya jadi ya Ulaya nayo ina hadithi za watu wanaobadilika usiku na kuwa watu-mbweha wauaji. Katika sehemu nyingine za ulimwengu, kuna hadithi juu ya simbamarara, nguruwe-mwitu, mamba, na hata paka ambao waweza kubadilisha-badilisha maumbo ya watu na wanyama.

Je, Mambo Hayo Huungwa Mkono na Maandiko?

Watu fulani hata hudai kwamba Maandiko yenyewe hukubali itikadi katika badiliko la umbo lisilo la kawaida. Masimulizi manne ya Biblia hutajwa mara nyingi kuwa ithibati ya jambo hilo. Katika simulizi la kwanza, Yesu alifukuza roho waovu kutoka kwa watu wawili, na baada ya roho waovu hao kufukuzwa, waliingia katika kundi la nguruwe. (Mathayo 8:28-33) Katika simulizi la pili, lililorekodiwa kwenye Hesabu 22:26-35, punda wa Balaamu alizungumza naye. Katika simulizi la tatu, pengine lijulikanalo zaidi kati ya masimulizi yote haya, nyoka alizungumza na Hawa katika shamba la Edeni.—Mwanzo 3:1-5.

Hata hivyo, kuyachunguza masimulizi hayo kwa makini hufunua kwamba kwa kweli hayo si mifano ya badiliko la umbo. Chukua kisa cha nguruwe wenye roho waovu. Biblia haisemi kwamba nguruwe hao walikuwa watu waliokuwa wamebadilika na kuwa wanyama. La, simulizi lasema kwamba kabla halijaingiliwa “kundi [hilo] la nguruwe wengi lilikuwa kwenye malisho.” (Mathayo 8:30) Roho waovu wa Shetani, wala si roho za wanadamu, waliwaingia nguruwe hao.

Namna gani punda wa Balaamu na nyoka katika Edeni? Katika kisa cha kwanza, Biblia yasema kihususa kwamba ‘BWANA alikifunua kinywa cha yule punda’ hivi kwamba angeweza kusema. (Hesabu 22:28) Punda hakuwa mwanadamu aliyebadilika umbo. Na kwa habari ya nyoka katika Edeni, Biblia yamtambulisha roho mwovu aitwaye Shetani Ibilisi kuwa “nyoka wa awali.” (Ufunuo 12:9) Shetani ndiye aliyenena kupitia nyoka na “[ku]mshawishi Hawa kwa ujanja wake.” (2 Wakorintho 11:3) Ndiyo, punda wa Balaamu na pia nyoka walikuwa wanyama—kabla ya kuzungumza, walipokuwa wakizungumza, na baada ya kuzungumza.

Simulizi la nne hutajwa mara nyingi kumhusu mfalme mwenye kiburi wa Babiloni, Nebukadneza. Biblia husema kwamba Mungu alimnyenyekeza Nebukadneza. “Moyo wake ukafanywa kuwa kama moyo wa mnyama, na makao yake yalikuwa pamoja na punda-mwitu; akalishwa majani kama ng’ombe, mwili wake ukalowa maji kwa umande wa mbinguni; hata alipojua ya kuwa Mungu Aliye juu ndiye anayetawala katika ufalme wa wanadamu.” (Danieli 5:21) Ile miaka saba ya kuwa kichaa, Nebukadneza alionekana na kutenda kama mnyama. Kulingana na Danieli 4:33, ‘nywele zake zilikua, zikawa kama manyoya ya tai, na kucha zake kama kucha za ndege.’ Hata hivyo, mfalme huyo hakumea manyoya wala kucha kamwe kihalisi. Aliendelea kuwa binadamu!

Wazo la badiliko la umbo lisilo la kawaida hupingana na mafundisho ya Biblia. Kwa sababu, Biblia huonyesha kwamba mwanadamu hana nafsi iliyo kando ambayo ingeweza kuishi ndani ya mnyama. Badala yake, mwanadamu mwenyewe ni “nafsi hai”! (Mwanzo 2:7) Pia, badiliko la umbo ni kinyume cha mpango wa kiasili wa mambo ambao ulianzishwa na Yehova Mungu. Wanyama waliumbwa ili wazae “kwa jinsi [“aina,” NW] zake.” (Mwanzo 1:24, 25) Kwa sababu ya mipaka ya kijeni ambayo Mungu aliweka, aina tofauti, au vikundi vikubwa-vikubwa vya wanyama haviwezi kujamiiana na kuzaa. Kuna pengo kubwa hata zaidi kati ya wanyama na mwanadamu, aliyeumbwa ‘kwa mfano wa Mungu.’ (Mwanzo 1:26) Bila shaka, Mungu hangedhihaki sheria zake mwenyewe kwa kuwapa wanadamu uwezo wa kujibadili na kuwa wanyama wasio na akili.

Ni kweli kwamba badiliko la umbo laweza kuonwa katika maumbile. Viwavi huwa vipepeo, navyo viluwiluwi huwa vyura. Hata hivyo, uchunguzi wa karibu huonyesha kwamba vielelezo hivyo vya badiliko la umbo havihusishi badiliko la “aina” bali ni hatua mbalimbali tu za ukuzi wa “aina” ileile. Hatua ya ukomavu ifikiwapo, watazaa “kwa jinsi zake.”

Kuona Hakuwi Kuamini Sikuzote

Basi, tuseme nini juu ya watu waliojionea kwa macho wanaodai kwamba walishuhudia badiliko la umbo lisilo la kawaida? Kwa wazi, hicho ni kielelezo kingine cha “utendaji wa Shetani pamoja na kila kazi yenye nguvu na ishara za uwongo na mambo ya ajabu na pamoja na kila udanganyo usio wa uadilifu kwa wale wanaoangamia.”—2 Wathesalonike 2:9, 10.

Sawa na wakandamizaji wote, roho waovu hutaka watu waamini kwamba wana uwezo zaidi ya walio nao kihalisi. Wao hufanya “ishara” zenye kusadikisha ambazo ni ujanja tu wa wevi na walaghai.

Hilo latukumbusha watu wachezeshao mchezo wa karata (kadi) katika sehemu nyingi za masoko katika Afrika. Wao huwashawishi wanawake fulani wapoteze fedha zao walizochuma kwa jasho katika mchezo wa karata wenye hila. Wanamwonyesha mwanamke kadi tatu—mbili nyekundu moja nyeusi—na kumwambia kwamba aweza kuongeza fedha zake maradufu kwa kuchagua tu ile kadi nyeusi. Anasitasita kucheza—mpaka anapomwona mtu mwingine aonekanaye akishinda kwenye mchezo huo rahisi. Hatambui hata kidogo kwamba yule eti mshindi anashiriki katika ulaghai huo. Aweka fedha zake, akikaza macho yake kwenye ile kadi nyeusi huku kadi zigeuzwapo na kuchanganywa. Lakini kwa aibu na mshtuko wake, kadi achaguayo ni nyekundu. Ametumia fedha za chakula cha familia—tokeo la tamaa yake mwenyewe na la ujanja wa mikono ya mjanja mwerevu! Ni kuchelewa mno, amepata kujua kwamba kuona hakuwi kuamini sikuzote.

Vivyo hivyo, Shetani na roho waovu wake hupendezwa kuwadanganya watu wafikiri kwamba wanadamu wanaweza kubadilika na kuwa wanyama. Shetani ni bingwa wa kudanganya. Kwa vyovyote, yeye ndiye aliyesema uwongo wa kwanza, akimwambia Hawa: “Hakika hamtakufa. . . . mtakuwa kama Mungu.” (Mwanzo 3:4, 5) Uwongo huo umetokeza mafundisho mbalimbali ambayo huwatia watu hofu, kama vile fundisho la kwamba nafsi haiwezi kufa, fundisho la moto wa helo, na fundisho la badiliko la umbo. Hivyo, katika Afrika watu hulipa fedha nyingi ili “wachanjwe” kwa sababu wanafikiri kwamba kufanya hivyo kwaweza kuwalinda wasibadilishwe kuwa mnyama. Kihalisi, watu hao ni watumwa wa “mafundisho ya roho waovu” nao wamezuiwa wasifanye mapenzi ya Mungu.—1 Timotheo 4:1; Yakobo 4:7.

Badiliko la Kweli

Huenda sikuzote umeamini au hata kuhofu badiliko la umbo. Ikiwa ndivyo, tii maneno haya ya Biblia kwenye Waroma 12:2. Katika andiko hilo, kwenye maandishi ya awali, namna ya neno la Kigiriki me·ta·mor·phoʹo latumiwa. Twasoma hivi: “mgeuzwe umbo [me·ta·mor·phouʹsthe] kwa kufanya upya akili yenu.” Hilo larejezea badiliko la umbo liwezalo kutokea—badiliko kabisa katika utu!

Wanaotaka kumpendeza Mungu lazima wafanye badiliko hilo, kwa kuwa Biblia huhimiza hivi: “Uvueni utu wa zamani pamoja na mazoea ya huo, na mjivike wenyewe utu mpya, ambao kupitia ujuzi sahihi unafanywa kuwa mpya kulingana na mfano wa Yule aliyeuumba.”—Wakolosai 3:9, 10.

Waweza kubadilikaje? Kwa kutwaa ujuzi sahihi kutoka katika Biblia. Huenda ujuzi huo ukakufanya uachane na mawazo na dhana ulizopenda sana. Lakini, kama vile Yesu alivyosema, “mtajua kweli, na kweli itawaweka nyinyi huru.” (Yohana 8:32) Ndiyo, waweza kuondolewa uwongo na hofu ya badiliko la umbo.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Kile ambacho macho yetu “huona” hakiwi jambo halisi sikuzote

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 13]

Mchawi: Courtesy Africana Museum, Johannesburg

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki