Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 8/8 kur. 16-17
  • Vito vya Anga la Kiafrika

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Vito vya Anga la Kiafrika
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Vioo vya Chuma
  • Mwenye Bidii Lakini Si Mwenye Kuvutia
  • Viota Vinavyoning’inia
  • Ndege Ambaye Hubusu Maua
    Amkeni!—1999
  • Kumlea Mtoto Porini
    Amkeni!—2001
  • “Mkazi wa Msituni Mwenye Kuvutia Kuliko Wote”
    Amkeni!—2000
  • Mbayuwayu Mwenye Kuruka kwa Kasi
    Amkeni!—1999
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 8/8 kur. 16-17

Vito vya Anga la Kiafrika

Na mleta-habari wa Amkeni! katika Kenya

MBUGA ya Kiafrika ni kame na ni ya kikahawia, ikiwa imeunguzwa na jua kali la ikweta. Twapitia katikati ya miiba ya mtanda-mbogo na vichaka vyenye miiba.

Kwa ghafula twasimama. Uangalifu wetu umenaswa na mwako wa rangi zenye kuvutia. Ndege mdogo mwenye rangi zenye kumetameta kana kwamba jua limetiwa ndani ya manyoya yake madogo yuaja na kutua juu ya tawi la mchongoma unaochanua maua. Kito hiki chenye mabawa kinaitwa chozi.

Vioo vya Chuma

Kuna zaidi ya aina mia moja za chozi. Chozi wengi hupatikana katika Afrika ya kitropiki, lakini waweza kupatikana pia katika Asia, Australia, na hata katika visiwa vya Pasifiki. Wakiwa maridadi na wa namna mbalimbali, chozi huakisi jua kama vioo vidogo sana vya chuma, vikitokeza rangi nyingi zenye kung’aa: nyekundu, rangi za kimanjano, samawati, na za kijani kibichi na vilevile rangi za shaba.

Kwa kawaida chozi hulinganishwa na ndege-wavumi wa Amerika. Kama ndege-wavumi, chozi wana rangi nyingi sana na hula maji matamu ya maua. Hata hivyo, ni wakubwa kuliko ndege-wavumi na hawana ustadi wa kupuruka kama wenzao wa Amerika Kaskazini.

Kwa kawaida, chozi huzidua maji matamu ya maua kwa kutua juu ya maua yaliyochanua na kutumia mdomo wake mrefu na uliopindika ili kufikia sehemu ya ndani kabisa ya maua yanayochanua. Lakini ikiwa ua lenye umbo la neli ni refu mno kwa mdomo wa ndege, chozi aweza kutoboa sehemu ya chini ya ua na kufyonza maji yake yenye thamani. Pia chozi hula wadudu wanaowapata kwenye maua au majani yaliyo karibu.

Ndege wa kiume ni waimbaji hodari pia. Nyimbo zao hutofautiana kutoka sauti nyembamba ya tssp ya chozi wa aina fulani kufikia sauti tamu ya tsik-tsik-tsik-tsik-tsit tree-tree-turrrr inayotolewa na neli-kijani mwenye manyoya mekundu wa Afrika Mashariki. Mara nyingi nyimbo zao ndizo huonyesha mahali walipo katika vichaka vikubwa. Hata hivyo, mara wanapotambuliwa, huonekana kwa urahisi katika mbuga ya Kiafrika iliyo kame na yenye rangi ya kikahawia.

Mwenye Bidii Lakini Si Mwenye Kuvutia

Ingawa inapendeza kumtazama na kumsikiliza chozi wa kiume, wa kike ni mdogo zaidi na hana rangi ya kuvutia. Kwa hiyo mara nyingi watazamaji wa ndege na wapiga picha humpuuza. Kwa kweli, yeye hutambuliwa tu anapokuwa pamoja na chozi wa kiume. Lakini kile ambacho wa kike hukosa katika rangi, kwa hakika hujaziwa na bidii yake.

Kwa kawaida ndege wa kike ndiye hujenga kiota na kufanya kazi hasa ya kulea makinda. Afanyapo kazi za kiota, chozi wa kiume husimama kulinda, akiwa tayari kuwafukuza wadukizi wasiwe karibu na kiota.

Viota Vinavyoning’inia

Ingawa hivyo, viota vya chozi si maridadi. Huonekana kama vipande vidogo vya takataka ambazo zimekusanywa na upepo na kurundikwa kwenye mchongoma. Kikiwa kimefanana na soksi inayoning’inia, kiota cha chozi hutengenezwa kwa nyuzinyuzi za mimea zilizofumwa au kushonwa pamoja na kufungwa kwa tando za buibui. Sehemu ya nje ya kiota hurembwa kwa ustadi kwa vitawi vidogo, majani yaliyokauka, kuvu kidogo, na mara nyingi maganda mawili hivi yenye kuning’inia huongezewa.

Ndani, sakafu hutandazwa kwa mimea laini, nyasi nyororo, manyoya, na vitu vingine vinavyotaka uangalifu mkubwa. Mwingilio ni tundu dogo lililo upande mmoja, karibu na sehemu ya juu. Mara nyingi ndege wa kike huatamia akiwa peke yake. Aketipo ndani ya kiota chake kilicho na umbo la pea, mdomo wake mrefu uliopindika kwa kawaida waweza kuonekana ukijitokeza kutoka kwenye kiota. Hutaga yai moja au mawili, ambayo huangua katika muda wa siku 14 hivi. Makinda yatokapo kwenye kiota, hayo huwa na rangi ya mama yao. Hata hivyo, chozi wa kiume waanzapo kukomaa, hutokeza manyoya yenye kuvutia ambayo siku moja yatawatofautisha kuwa ndege wenye kung’aa kama jua.

Chozi ni kielelezo kingine tu cha maandalizi mengi na unamna-namna wa Mbuni mwenye akili. Umaridadi wao na tabia yao ya kisilika hutusukuma kumthamini hata zaidi Muumba wao. Hivyo chozi ni baadhi ya viumbe ambao Biblia huwaamuru hivi: “Msifuni BWANA kutoka nchi, . . . vitambaavyo na ndege wenye mbawa.” “Kila mwenye pumzi na amsifu BWANA.” (Zaburi 148:7, 10; 150:6) Vito hivi vya anga la Kiafrika vyapasa kutusukuma sote tumsifu Muumba mwenye upendo aliyevitokeza.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki