“Jenny Wren”—Ndege Mdogo, Mwenye Sauti Kubwa
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UINGEREZA
MAUA aina ya primrose yalitapakaa kwenye ukingo wa mto, nuru ya jua ilipopenyeza katikati ya miti, ikiremba uoto baada ya rasharasha kuisha. Nilipumzika kwenye mti uliokuwa umeanguka, nikiwatazama ndege wawili wadogo waliokwenda mbele na nyuma kwa haraka kwenye kangaga zilizokufa ambazo zilijitokeza juu ya mwamba uliokuwa juu ya kijito.
Nikawa mdadisi, nikaamka kupeleleza. Hapo nilipata nilichoshuku—kiota cha wren, kikiwa kimefumwa vizuri kwa kuvumwani na kufichwa miongoni mwa kamba za kangaga zilizoning’inia. Ndege huyo mchangamfu ana kimo cha sentimeta 10 kutoka kwenye ncha ya mdomo wake hadi kwenye mkia wake na kwa kawaida huonwa kuwa mmojawapo wa ndege wadogo zaidi wa Uingereza.a Kwa sababu hii, katika mwaka wa 1937 mfano wake ulichorwa kwa mara ya kwanza kwenye sarafu ndogo zaidi wakati huo katika Uingereza.
Majina Jenny wren, au kitty wren—ambayo yamepewa ndege wa jinsia zote mbili na watu wa mashambani wa Uingereza—yanajulikana sana Ulaya, Ulaya-Asia, na Marekani. Katika Uingereza, ndege huyu ndiye ambaye ametawanyika sana na ndiye apatikanaye kwa wingi sana kati ya ndege wenye kuzaana. Wimbo wake mtamu na wenye madoido umefananishwa na ule wa nightingale ulio na sauti ya juu sana hivi kwamba waweza kusikika kwa umbali unaozidi kilometa moja hivi! Lakini majira makali ya kipupwe huwaathiri vibaya na imejulikana kwamba majira hayo huua asilimia 75 ya ndege hao. Nyakati hizo mara nyingi wren hukusanyika pamoja ili kujipasha joto. Pindi moja zaidi ya wren 60 walipatikana ndani ya sanduku, wakiwa wamesongamana pamoja na katika tuta la manyoya.
Katika mwezi wa Aprili ndege wa kiume hujenga namna mbalimbali za viota vyenye umbo la kuba ambavyo vimefichwa kwa ustadi. Baada ya kujenga viota hivyo, ndege wa kiume atamwonyesha mwenzi wake viota vyote. Mwenzi wa kike atateua kiota kimoja na kukitandaza kwa manyoya. Mwishoni mwa mwezi wa Aprili, atakuwa ametaga mayai meupe matano au sita yenye madoa ya rangi nyekundu ya kikahawia. Ndege wa kike ataatamia mayai hayo akiwa peke yake kwa siku 14, kisha makinda yataondoka kwenye kiota baada ya angalau majuma mawili zaidi.
Ni kawaida kutaga mara mbili wakati wa kiangazi, na wakati ndege wa kike aatamiapo mayai ya pili, ndege wa kiume atatunza makinda ya kwanza, nyakati nyingine akiyachukua makinda hayo kwenye mojawapo ya viota vyake vingine. Ikiwa ni kiangazi kizuri, chenye wadudu wanaopatikana kwa wingi kwa ajili ya chakula, ndege wa kiume atachukua mwenzi wa pili na kumweka kwenye mojawapo ya viota vyake vingine.
Nikiwa nimeketi kwenye mti ulioanguka, ningeweza kuhisi joto la jua la mwezi wa Mei nilipokuwa nikitazama wren wakienda na kurudi. Niliona manyoya yao yenye rangi nyekundu ya kikahawia na mabawa yao yenye milia walipotua juu ya kitawi kilichokuwa karibu na mahali nilipoketi. Lakini, waliponigundua katika eneo lao, mikia yao midogo ilisimama, na wakaanza kutoa sauti zao. Hilo lilikuwa dokezo kwamba niondoke polepole.
[Maelezo ya Chini]
a Ndege wadogo zaidi wa Ulaya, ndege aitwaye resident goldcrest, ambaye kwa kawaida huitwa golden-crested kinglet, na ndege ambaye huzuru wakati wa majira ya kipupwe aitwaye firecrest ni wafupi zaidi kwa robo ya inchi moja lakini huonekana kwa nadra sana.