Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 10/8 kur. 11-14
  • Magendo—Tatizo la Ulaya Katika Miaka ya 1990

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Magendo—Tatizo la Ulaya Katika Miaka ya 1990
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Hazina za Sanaa Zaagizwa Kisiri
  • Sumu—Aina Tofauti ya Magendo
  • Sigareti za Magendo
  • Biashara ya Binadamu
  • Jambo Lenye Kutia Woga Zaidi ya Yote
  • Magendo—Biashara Itakayoisha Karibuni
  • Pigano Linaloshindwa Kudhibiti Uhalifu
    Amkeni!—1998
  • Tisho la Nyuklia Halijaisha
    Amkeni!—1999
  • Tisho la Nyukilia—Je! Limekwisha Hatimaye?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • ‘Na Ukuta Ukaanguka kwa Kishindo’
    Amkeni!—1992
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 10/8 kur. 11-14

Magendo—Tatizo la Ulaya Katika Miaka ya 1990

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UJERUMANI

Mashua yenye kwenda kwa kasi yakimbia kutoka pwani ya Afrika Kaskazini, kuelekea Gibraltar; msafara wa magari waondoka Poland, ukielekea upande wa magharibi; lori ya Bulgaria yaelekea Ulaya kaskazini; ndege yasafiri kutoka Moscow hadi Munich. Ni nini kinachounganisha namna hizi za usafiri? Kila moja imetumiwa kwa magendo.

MAGENDO ni kuingizwa kwa vitu nchini au kutolewa kwa vitu nje ya nchi au eneo kisiri, ili kuepa ama wenye mamlaka kwa sababu vitu hivyo si halali ama kuepuka kuvilipia kodi. Magendo—ama usafirishaji wa vitu haramu imefanywa katika Ulaya tangu angalau karne ya 14. Utendaji huu haramu umeenea sana hivi kwamba sanaa za jadi za nchi nyingi sasa zatia ndani hadithi za mapenzi za wafanya-magendo, ambao baadhi yao walikuja kuwa mashujaa waliopendwa sana.

Magendo si halali na mara nyingi sana hudhuru—ingawa nyakati fulani imetokeza mema. Kwa kielelezo, katika karne ya 16, nakala za sehemu ya tafsiri ya Biblia ya William Tyndale ziliingizwa Uingereza kisiri, ambapo zilikuwa zimepigwa marufuku. Isitoshe, majeshi ya Ujerumani yalipoteka Ufaransa katika mwaka wa 1940, wafanya-magendo—wakiwa na uzoefu wa kutumia barabara ndogo-ndogo na vijia vya Normandy—“walikuwa na ujuzi zaidi katika upinzani wa [Ufaransa],” laripoti GEO.

Sasa, miaka 50 baadaye, magendo imesitawi kwa haraka—lakini ikiwa tatizo badala ya baraka. Ulaya imekuwa “paradiso ya wafanya-magendo” kulingana na gazeti la habari la Ujerumani Süddeutsche Zeitung. Ni nini kimechangia jambo hili?

Sababu moja ni kwamba Muungano wa Ulaya umepanuka, mataifa wanachama yakiongezeka kutoka 6 hadi 15 kwa muda wa miaka 40.a Kuondolewa kwa vizuizi vya kusafiri kumerahisisha zaidi biashara ya kimataifa. Mkazi mmoja wa Ulaya alisema: “Miaka thelathini iliyopita, maofisa walikagua hati zako katika kila mpaka. Siku hizi, waweza kusafiri na kuvuka mipaka hiyohiyo bila hata kusimama.”

Isitoshe, Ulaya Mashariki imefungua mipaka yake. Mipaka fulani iliyokuwako, kama ule wa awali uliogawanya Ujerumani mara mbili, hauko tena. Mambo haya yote yamerahisisha sana biashara kati ya mataifa. Lakini ndivyo na magendo imekuwa rahisi. Na uhalifu uliopangwa umefanya haraka kujifaidi katika hali hii mpya. Magenge ya wahalifu yanakuwa wataalamu wa bidhaa za namna nyingi za magendo.

Hazina za Sanaa Zaagizwa Kisiri

Kwa miaka mingi kabla Ulaya Mashariki haijafungua mipaka yake, hazina za sanaa katika Urusi hazingeweza kufikia wakusanyaji wa Magharibi. Hata hivyo, sasa, hazina hizo “zinaporwa na muungano usio wa kawaida wa biashara za sanaa za Ulaya magharibi na magenge yenye kuua ya wafanya-magendo wa Urusi,” laripoti The European. Kwa kweli, “inaaminiwa na polisi kwamba magendo ya hazina za sanaa zilizoibwa [katika Ulaya] imekuwa utendaji wa kihalifu wenye faida kubwa zaidi ikifuatia tu ulanguzi wa dawa za kulevya, na biashara ya silaha haramu.”

Magendo ya sanaa ni biashara kubwa katika Urusi na kwingineko. Katika Italia, kwa muda wa miaka miwili, vitu vya sanaa vyenye thamani izidiyo dola milioni 500 viliibwa. Asilimia 60 ya sanaa zilizoibwa za Ulaya hufika London, ambako kuna wanunuzi. Kwa kweli, bidhaa nyingi hata “huibwa baada ya kuagizwa na mkusanyaji mfidhuli.” Haishangazi kwamba ni asilimia 15 tu ya bidhaa hizi hupatikana tena.

Sumu—Aina Tofauti ya Magendo

Kuhusu sanaa wahalifu hulipwa ili waingize vitu katika nchi kiharamu, ilhali katika vitu vingine wao hulipwa kutoa bidhaa nje ya nchi. Kielelezo kimoja ni mabaki ya sumu. Kwa nini mtu ang’ang’ane kutoa kisiri mabaki ya sumu nje ya nchi? Kwa sababu gharama ya kutupa mabaki ya sumu kwa njia halali imeongezeka sana katika nchi nyingi. Jambo hili pamoja na tisho la vizuizi vikali vya kimazingira hufanya liwe wazo lenye kupendeza kulipa wafanya-magendo ili kutupa mabaki ya sumu ya kiviwanda nje ya nchi.

Mabaki haya hufikia wapi? Uchunguzi uliofanywa na Shirika la Kupeleleza Uhalifu la Ujerumani waonyesha kwamba magenge hutoa kisiri mabaki ya sumu—kama vile betri za magari ambazo zimetumika, vimumunyishaji, rangi, dawa za kuua wadudu, na metali za sumu—kutoka Magharibi na kuvitupa katika nchi kama vile Poland, Rumania, na ule uliokuwa Muungano wa Sovieti. Vitu hivi vitatisha afya ya watu wa nchi hizo kwa miaka mingi ijayo.

Sigareti za Magendo

Vikundi fulani vya wahalifu hushughulikia kwa ustadi sigareti za magendo. Mathalani, sigareti zimesafirishwa kutoka Afrika Kaskazini hadi Peninsula ya Iberia katika mashua zenye kwenda kwa kasi au kutoka Poland hadi Ujerumani katika magari. Unahusisha kiasi kikubwa sana cha fedha. Biashara haramu ya sigareti zisizotozwa kodi yafanya Taifa la Ujerumani lipoteze mark zipatazo milioni elfu moja (dola milioni 674) kila mwaka.

Kulingana na Die Welt, katika barabara za Berlin, wauzaji wapatao 10,000 huuza sigareti za magendo zilizopunguzwa bei.

Biashara ya Binadamu

Shughuli nyingine maalumu ya uhalifu uliopangwa—ambayo ni ovu hasa—yahusisha binadamu. Bei ya kumsafirisha mtu kisiri hadi Ulaya Magharibi—labda katika lori kama ile iliyotajwa mwanzoni mwa makala hii—ni kubwa sana. Kwa kweli, shirika la International Centre for Migration Policy Development, katika Vienna, lakadiria kwamba biashara hii ya binadamu huchuma zaidi ya dola bilioni 1.1 kwa mwaka.

Kwa kuwa wahamiaji wengi haramu hutoka katika nchi maskini ni wachache wawezao kuwalipa kimbele wafanya-magendo. Hivyo, baada ya kuwasili Ulaya, wanalazimishwa kulipia deni hiyo kwa kuwafanyia kazi wafanya-magendo na magenge yao ya uhalifu. Kwa hiyo, wahamiaji hao wa kusikitikiwa wanajipata wamebanwa katika utumwa wa siku hizi usioisha, wakitendwa vibaya daima, wakionewa, wakiibiwa kimabavu, na kubakwa. Wengine huishia kufanyia kazi magenge ya kufanya magendo ya sigareti kama wafafanuliwavyo na gazeti la Ujerumani Die Welt; wengine huishia katika ukahaba.

Gharama ya nchi mpya inayowakaribisha haipimwi kwa kodi zilizopotea tu. Magenge yanayopingana huhusika katika vita ambayo ilielezwa na Süddeutsche Zeitung kuwa ya “unyama usiowazika.” Tarakimu zaonyesha: Katika ile iliyokuwa Ujerumani Mashariki, magenge yalihusika katika visa vya uuaji 74 kwa muda wa miaka minne.

Jambo Lenye Kutia Woga Zaidi ya Yote

“Kati ya matokeo yasiyotazamiwa ya kuporomoka kwa Muungano wa Sovieti,” likaandika gazeti la habari, “labda hakuna moja linaloogopesha zaidi kuliko magendo ya vifaa vya nyuklia.” Inadhaniwa kuwa vifaa vya mnururisho vimeibwa kisiri kutoka Urusi na kuingizwa Ujerumani, hivyo kufanya hali hiyo iwe “tatizo la ulimwengu, na hasa tatizo la Ujerumani.”

Mathalani, fikiria safari ya ndege kutoka Moscow iliyotajwa mwanzoni mwa makala hii. Alipowasili Munich, abiria mmoja alipatikana amebeba plutoni, kifaa chenye mnururisho, ndani ya sanduku lake. Kwa kuwa plutoni ni yenye sumu sana na yaweza kusababisha kansa, uchafuzi ungeangamiza kabisa Munich na wakazi wake.

Mapema katika mwaka wa 1996, mwanafizikia mmoja Mrusi alikamatwa na kuhukumiwa kwa kosa la kupeleka ng’ambo kisiri zaidi ya kilogramu moja ya kifaa chenye mnururisho ambacho, kulingana na Süddeutsche Zeitung, kilisemekana “kinatoshea kuunda bomu la nyuklia.” Mataifa ya Magharibi yamehangaika kwa haki. Kwenye mkutano huko Moscow, wanasiasa kutoka mataifa yanayoongoza kiviwanda walikubaliana juu ya mpango wa “kuzuia vifaa vya silaha za nyuklia visitolewe kisiri kutoka ule uliokuwa Muungano wa Sovieti na kupelekewa magaidi au ‘mataifa makaidi,’” likaandika The Times la London.

Wakifikiria hatari hizo, watu wengi wanajiuliza: Je, mikataba ya kimataifa yaweza kuzuia magendo? Hata ingawa serikali zaweza kufuatia haki na ziwe na makusudi mema, je, zinaweza kuzuia uhalifu uliopangwa? Je, magendo itaendelea kutoka kuwa tatizo la miaka ya 1990 hadi kuwa pigo la milenia mpya? Au je, kuna sababu ya kutumaini kwamba biashara ya wafanya-magendo itakoma?

Magendo—Biashara Itakayoisha Karibuni

Kuna sababu nzuri za kusadiki kwamba hivi karibuni magendo itaisha. Hii ni kwa sababu hali zinazofanya magendo iwezekane, na ipendeze watu fulani, zitaondolewa. Ni hali za aina gani?

Kwanza, mifumo ya kiuchumi ya leo yenye uonevu na isiyo adilifu imetokeza kugawanywa kwa mali kwa njia isiyo ya haki. Ilhali watu katika nchi fulani wanafurahia ufanisi, watu walio ng’ambo tu ya mpaka waweza kuishi katika umaskini au waweza kupatwa na upungufu. Hizi ndizo hali zinazofanya magendo iwe na faida. Lakini Muumba wetu ameahidi katika Maandiko Matakatifu kwamba karibuni ataleta mfumo wa mambo ambamo “uadilifu utakaa.” Mifumo ya kiuchumi yenye kuonea na isiyo adilifu itatoweka.—2 Petro 3:13.

Isitoshe, mipaka ya kitaifa itaondolewa, kwa kuwa chini ya serikali ya Mfalme wa kimbingu, Yesu Kristo, wanadamu watakuwa jamii moja. Kukiwa na udugu wa kimataifa kama huo duniani pote, hakutakuwako tena wahamiaji haramu. Na kwa kuwa hakuna mtu atakayeenda vitani, hatari ya kuchafuliwa na mnururisho kutoka kwa vita ya nyuklia haitakuwako. Katika mfumo mpya wa mambo, mwanadamu atajifunza kuheshimu mazingira.—Zaburi 46:8, 9.

Mambo makuu yanayochochea magendo katika siku hizi ni pupa, ukosefu wa haki, na kutowapenda wengine. Uhakika wa kwamba watu wengi wanaonyesha tabia kama hizo leo ni ishara ya kwamba tunaishi katika kipindi ambacho Biblia inakiita “siku za mwisho.” (2 Timotheo 3:1-5) Mfumo mpya wenye uadilifu utakaoletwa na Yehova wakaribia. Sote tuna sababu nzuri za kutazamia wakati ujao tukiwa na uhakika, si katika serikali za kibinadamu au mifumo ya kiuchumi, bali katika mfumo mpya wa Yehova.

[Maelezo ya Chini]

a Mataifa wanachama ya Muungano wa Ulaya ni Austria, Denmark, Finland, Hispania, Ireland, Italia, Luxembourg, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Ugiriki, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani, na Ureno.

[Sanduku katika ukurasa wa 13]

Bidhaa Nyingine za Magendo

Wanyama adimu: Mtu mmoja alikamatwa akisafirisha kobe adimu kutoka Serbia hadi Ujerumani. Alikiri kusafirisha kisiri wanyama hao 3,000 katika kipindi cha miaka mitano, akijipatia mark nusu milioni (dola 300,000). Biashara ya wanyama adimu inafanywa hasa na wahalifu walio wataalamu na inaongezeka. “Magendo imezidi,” akasema ofisa mmoja wa forodha. “Wakusanyaji fulani hulipa kiasi kikubwa sana cha fedha.”

Bidhaa zenye chapa bandia: Katika muda wa nusu-mwaka, maofisa wa forodha katika uwanja wa ndege wa Frankfurt, Ujerumani, walizuia zaidi ya bidhaa 50,000 zilizokuwa na chapa zinazojulikana vizuri sana. Bidhaa hizo—kama vile saa, programu za kompyuta, vifaa vya michezo, na miwani ya jua—zote zilikuwa miigizo.

Magari: Kampuni mashuhuri ya kukodisha magari katika Ulaya iliripoti ongezeko la asilimia 130 katika wizi wa magari katika kipindi cha miaka mitano. Gazeti moja la habari lafafanua njia za “wezi wa barabarani wa kisiku hizi.” Wanakodisha magari, wanaripoti kwamba yameibwa, na kisha kusafirisha magari hayo kisiri nje ya nchi.

Metali zenye thamani: Kobalti, nikeli, shaba, rutheni, na germani zote zapatikana—kwa bei nafuu—katika Estonia, ambalo limekuwa mojawapo ya majiji makuu ya magendo ulimwenguni.

Petroli na dizeli: Wafanya-magendo wenye kutumia mashua ili kusafirisha petroli na dizeli haramu ng’ambo ya Mto Danube kati ya Rumania na Serbia waliweza kujipatia dola zipatazo 2,500 kwa kazi ya usiku mmoja. Katika eneo hili mshahara wa kila mwezi ni dola 80 hivi!

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki