Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 11/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Tatizo la Maji
  • Tahadhari Juu ya Kikombe cha Kahawa Ofisini
  • Watoto Hupendelea Vichangamshi Sahili
  • Hatari ya Uchafuzi wa Hewa kwa Madereva
  • Kustarehesha Ng’ombe
  • Watoto Wahispania na Televisheni
  • Mwanzo wa Mapema Zaidi wa Historia ya China
  • Minukio Yenye Kushangaza
  • Kuchomwa na Jua Kivulini
  • Semina Juu ya Damu Katika Bulgaria
  • Kampeni ya Pekee Nchini Bulgaria Yafanikiwa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2010
  • Kupatwa kwa Jua na Ule Uvutio wa Astronomia
    Amkeni!—1995
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—2002
  • Uhuru wa Kidini Katika Bulgaria
    Amkeni!—1992
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 11/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Tatizo la Maji

“Iwapo hatua fulani haichukuliwi, thuluthi mbili za jamii ya binadamu zitapatwa na kiu kabla ya mwaka 2025,” latangaza gazeti la Kifaransa L’Express. Gazeti la habari Le Figaro laelezea hivi: “Robo moja ya idadi ya watu duniani sasa haiwezi kupata maji ya kunywa kwa njia ya moja kwa moja.” Ili kushughulikia tatizo la maji, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni [UNESCO] lilifanya mkutano wa kimataifa huko Paris, Machi 1998. Zaidi ya wajumbe 200 kutoka nchi 84, kutia ndani rais wa Ufaransa, walizungumzia njia za kuhifadhi maji yaliyo duniani. Moja ya matatizo yaliyokaziwa ni kwamba mara nyingi maji hutumiwa vibaya kwa sababu ya mifumo isiyofaa ya kunyunyizia mashamba maji na mabomba ya maji yaliyotoboka. Rais wa Ufaransa Jacques Chirac alikazia kwamba maji ni sehemu ya urithi wa pamoja wa mwanadamu, na hivyo yahitaji kusimamiwa vizuri ulimwenguni kote.

Tahadhari Juu ya Kikombe cha Kahawa Ofisini

“Visumbufu vidogo—kutia na vingine vyenye kuogopesha kama vile E. coli—vinaongezeka kwa wingi sana, kwa sababu katika ofisi nyingi watu hawasafishi vikombe vyao kwa uangalifu au kuua viini kwenye sinki za kuoshea vyombo na sehemu za kutayarishia vyakula,” laripoti The Toronto Star. Watafiti Charles Gerba na Ralph Meer walichunguza vikombe na vifaa vya kutayarishia kahawa katika ofisi 12. Asilimia zipatazo 40 za vikombe na asilimia 20 za sponji zilizopatikana kwenye sinki za kuoshea vyombo katika ofisi, zilikuwa na bakteria ya aina ya coliform, E. coli ambayo mara nyingi yaweza kuwa hatari. “Huo kwa kawaida ni wonyesho wa hali ya uchafu,” asema Gerba. Ripoti hiyo yamalizia hivi: “Isipokuwa kuwe na mashine ya kusafisha vyombo, vikombe vyapasa kusafishwa kwa maji moto yenye sabuni, kisha kuua viini kwa kutumia madawa ya kuua viini yaliyochanganywa na maji. Vitambaa na spongi zapaswa kusafishwa kwa ukawaida.”

Watoto Hupendelea Vichangamshi Sahili

Wawezaje kuwa mama mzuri machoni pa watoto wako? Katika uchunguzi wa Taasisi ya Whirlpool uliofanyiwa watoto Wamarekani 1,000 wenye umri wa miaka 6 kufikia 17, wengi zaidi walipendelea kufanya mambo sahili yaliyo ya kawaida pamoja na mama zao, yaani “kuwa tu pamoja.” Utendaji waliopendelea zaidi wakiwa na mama zao ulikuwa ni “kula mlo wa jioni pamoja.” Utendaji wa pili ulikuwa “kwenda kutembea pamoja” na “kununua vitu pamoja.” Utendaji wa tatu uliofuatia kwa ukaribu ulikuwa “kuketi na kuzungumza pamoja.” Chaguo la kwanza la watoto hao la namna ya kuwashukuru mama zao, lilikuwa pia sahili. Asilimia 70 walisema kwamba mara nyingi zaidi wao huwapa mama yao “kumbatio na busu.” Machaguo yaliyofuata waliyoyapendelea ni kusema, “Nakupenda” na “Asante.”

Hatari ya Uchafuzi wa Hewa kwa Madereva

“Dereva aliye kwenye msongamano wa magari atapumua kwa mara tatu vichafuzi ambavyo mwendesha baiskeli au mtu anayetembea kwa miguu atapumua, na mara mbili zaidi ya mtu anayetumia basi kwa usafiri,” laripoti The Times la London. Uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya Ulaya ya Sera za Mazingira ulionyesha kwamba wenye magari waliokwama kwenye misongamano ya magari yanayosonga polepole katika barabara kuu, “hupumua gesi nyingi zenye sumu.” Mtetezi wa mambo ya mazingira Andrew Davis husema kwamba kinyume na kufikiri kwa kawaida, waendesha magari waweza kuhitaji zaidi kuvalia vizuizi vya usoni, kuliko mwendesha baiskeli ambaye huendeshea kandokando ya barabara.

Kustarehesha Ng’ombe

Magodoro yaliyojazwa vipande-vipande vya mpira kutoka kwa tairi zilizotengenezwa upya, yanatokea katika mabanda ya kufugia ng’ombe, laripoti The Globe and Mail la Kanada. Yafikiriwa kwamba magodoro yenye kimo cha sentimeta tano yaweza kuwapa ng’ombe maisha marefu ya utoaji maziwa. Kulingana na ripoti hiyo, “ng’ombe wa maziwa hutumia sehemu kubwa ya maisha yao kwenye sakafu ya saruji,” ambayo huwafanya “waumwe kwato na kujeruhiwa miguu.” Magodoro hayo hayapunguzi matatizo ya kwato na miguu tu bali pia husaidia kupunguza vishindo kwenye magoti yao wanapojibwaga chini ili kupumzika. Mtengenezaji wa Magodoro hayo asema kwamba wazo ni kuwafanya ng’ombe wajihisi kama vile wao hujihisi wanapolalia malisho yenye nyasinyasi.

Watoto Wahispania na Televisheni

Mtoto mtazama-televisheni wa kawaida katika Hispania anaweza kushuhudia mauaji 10,000 na vitendo vya ujeuri 100,000 afikiapo umri wa miaka kumi, kulingana na Carlos María Bru, wa Kamati ya Hazina ya Hispania ya Watoto ya Umoja wa Mataifa, laripoti Shirika la Habari la Europa. Isitoshe, Profesa Luis Miguel Martinez alisema kwamba zaidi ya robo tatu za watoto Wahispania wa kuanzia umri wa miaka 4 kufikia 12 hutazama televisheni kwa angalau muda wa saa mbili na nusu kwa siku, na karibu robo moja hutazama zaidi ya muda wa saa nne kila siku. Kwa wastani, ripoti hiyo yaonyesha, “watoto hutumia muda wa saa 937 kwa mwaka mmoja wakitazama televisheni, hiyo ikiwa zaidi ya muda wa saa 900 utumiwao shuleni kila mwaka.” Kulingana na Ricardo Pérez-Aznar, wa Idara ya Sayansi ya Upashanaji Habari katika Chuo Kikuu cha Complutensian, ujeuri unaoonyeshwa katika televisheni ni mmoja wa mchanganyiko wa sababu za kisaikolojia ambazo zaweza kusababisha ujeuri katika jamii.

Mwanzo wa Mapema Zaidi wa Historia ya China

Mwaka wa mapema zaidi wa historia ya China iliyorekodiwa kwa muda mrefu umedhaniwa kuwa 841 K.W.K., mwaka wa kwanza wa muhula wa Gong He, wa milki ya Zhou ya Magharibi. Hata hivyo, hivi majuzi rekodi yenye maandishi ya awali zaidi yaligunduliwa ambayo hutaja kupatwa kwa jua, laripoti China Today. Rekodi hiyo huhusianisha kupatwa huku kwa jua na mwaka wa kwanza wa Mfalme Yi wa milki ya Zhou. Wanasayansi na wanahistoria wamefikia mkataa wa kwamba kupatwa huku kwa jua kulitokea mwaka wa 899 K.W.K., hivyo kukisongeza nyuma mwanzo wa historia iliyorekodiwa wa China kwa zaidi ya nusu karne. “Hakujawa na katizo katika rekodi hii yenye maandishi muda wote huo kufikia karne ya 20,” chaandika kitabu Outline of the History of the Chinese People. Chaiita rekodi hii “moja ya michango mikubwa zaidi ya Wachina kwa historia ya ustaarabu wa wanadamu.”

Minukio Yenye Kushangaza

Watengenezaji divai wamejua kwa muda mrefu umuhimu wa harufu nzuri katika kutofautisha divai moja na nyingine. Sasa, kukiwa na lengo la kutengeneza divai nzuri zaidi, wanasayansi wanapanga zile kemikali 500 au zaidi ambazo zaweza kuchangia ile manukato ya divai. Wanasayansi wametumia msaada wa watu ambao wana pua zenye wepesi wa kunusa, laripoti gazeti New Scientist. Vikundi vya wanusaji wamelinganisha minukio hususa ya divai fulani na vitunguu, asali, mmea wa jamii ya yungiyungi, tumbaku, chokoleti, na tini zilizokaushwa. Kwa kushangaza, harufu nyinginezo zilihusianishwa na vitu vilivyotia ndani “soksi zenye ukungu, mayai yaliyooza na mpira unaochomeka.” Divai fulani iliyotengenezwa kwa hamira hutokeza harufu ambayo yaweza kufasiriwa kwa njia mbalimbali. Asema mtaalamu Jane Robichaud: “Inategemea kadiri mtu awezavyo kunusa harufu hiyo, iwe yaboresha divai au yaipa uvundo kama blanketi ya kuendeshea farasi.”

Kuchomwa na Jua Kivulini

Kujikinga na jua chini ya mti au mwavuli wa ufuoni huenda, usiandae kinga kamili kutokana na mnururisho wa urujuanimno, kulingana na uchunguzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kitiba ya Queensland, Australia. Kama ilivyoripotiwa katika The Canberra Times, mtu aliye kwenye kivuli kilicho wazi angali bado katika hatari ya kupatwa na mnunurisho wa urujuanimno uliotawanyika. Dakt. Peter Parsons, mwanabiokemia aliye pia mshiriki wa uchunguzi huo, aonya hivi: “Ikiwa kiwango cha juu zaidi kinachopendekezwa cha kupigwa na jua la moja kwa moja la adhuhuri ya kiangazi katika miji mikuu ya Australia ni dakika 10 hadi 12, basi watu wanaosimama au kulala kwenye kivuli watachomwa kwa kadiri fulani na [mnururisho wa urujuanimno B], unaosababisha mchomo wa jua kwa muda usiopungua saa moja.” Hata katika majira ya baridi kali na siku zenye mawingu mazito, kuna kiwango kikubwa cha mnururisho wa urujuanimno. Dakt. Parsons asema kwamba kwa kawaida, “kadiri ya ukubwa wa anga unaloweza kuona, ndivyo hatari inavyozidi kuwa kubwa.”

Semina Juu ya Damu Katika Bulgaria

Semina yenye kukazia uhifadhi wa damu wakati wa upasuaji na utumizi wa vibadala vya kutiwa damu mishipani, ilifanywa mwanzoni mwa mwaka huu katika Sofia, Bulgaria. Semina hiyo iliwapa madaktari kutoka kotekote Bulgaria fursa ya kushauriana na kikundi cha wataalamu juu ya damu kutoka nchi nane. Profesa Ivan Mladenov wa Sofia alielezea kwamba chini ya mfumo wa utawala uliotangulia, ‘mambo mengi hayakujulikana kuhusu kuambukizwa kwa damu, na virusi vinavyoenezwa na damu’ na kwamba, ‘maswali yaliyozushwa na wagonjwa yalionwa kuwa tabia mbaya ambayo ingesababisha kukataa kutibiwa.’ Itikio la waliohudhuria semina hiyo laonyesha ufahamu mwingi katika Bulgaria wa haki ya mgonjwa ya kujiamulia mambo kibinafsi, na idhini baada ya kuarifiwa, kama ilivyokubaliwa na Mahakama ya Ulaya ya Haki za Kibinadamu.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki