Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g 12/07 kur. 26-27
  • Mfalme Aliyetimiza Mengi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mfalme Aliyetimiza Mengi
  • Amkeni!—2007
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kubuni Mfumo wa Kuandika
  • Jina la Mungu Lajulishwa Katika Kiswahili
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2012
  • Je, Unazungumza Ile “Lugha Safi” kwa Ufasaha?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2008
  • Lugha ya Watu Wote
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
  • Namna Lugha Moja Itakavyoleta Umoja kwa Wanadamu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2007
g 12/07 kur. 26-27

Mfalme Aliyetimiza Mengi

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KAMERUN

IBRAHIM NJOYA, alikuwa mfalme wa 17 wa kabila la Bamum, kabila kubwa ambalo bado linapatikana katika nyanda za magharibi za Kamerun. Alikuwa mfalme kuanzia 1889 hadi 1933, kama inavyoonyeshwa katika orodha ya watawala waliotawala tangu karne ya 14. Wakati wa utawala wa Njoya, Wafaransa na Wajerumani walikuwa wakijaribu kufanya eneo hilo kuwa koloni lao.

Tangu ujana wake, Njoya alithibitika kuwa mwenye akili sana na mvumbuzi, na alishirikiana kwa ukaribu na watu wenye hekima na wavumbuzi waliokuwa na malengo kama yake. Jumba la kifalme lenye kupendeza alilojenga linaloonekana katika picha iliyo chini, linathibitisha ujuzi wake wa uchoraji-ramani. Pia inasemekana kwamba alivumbua kinu cha kusaga mahindi kama kilichoonyeshwa hapa. Lakini uvumbuzi wake wenye kutokeza zaidi ulikuwa kubuni mbinu mpya ya kuandika lugha ya Bamum.

Kubuni Mfumo wa Kuandika

Kufikia mwishoni mwa karne ya 19, historia ya watu wa Bamum ilikuwa ikipitishwa kwa mdomo kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Njoya alitambua kwamba kungekuwa na hatari ya mambo fulani kusahauliwa au kutiliwa chumvi. Alijifunza Kiarabu baada ya kusoma vitabu alivyopata kutoka kwa wafanyabiashara Waarabu waliopita katika milki yake. Huenda pia alijua maandishi ya mapema ya Vai, ambayo wakati huo yalikuwa yakitumiwa huko Liberia. Kwa hiyo, akaanza kubuni mfumo wa kuandika lugha ya Bamum.

Njoya alianza kwa kuchora mamia ya ishara, hasa za picha. Mfumo huo uliwalazimu watu kukariri maana ya kila ishara. Kadiri miaka ilivyopita, kwa msaada wa watumishi wake alirahisisha mfumo huo. Walipunguza idadi ya ishara zinazohitajika kwa kutumia silabi. Kwa kuunganisha ishara kadhaa au herufi za maandishi yake mapya, maneno hususa yaliundwa. Msomaji alihitajika kukariri herufi chache zaidi na jinsi zilivyotamkwa. Njoya alipomaliza mfumo wake mpya wa kuandika ulioitwa A-ka-u-ku, ulikuwa na herufi 70.

Njoya aliwahimiza watu watumie maandishi ya Bamum kwa kuagiza kwamba yafundishwe shuleni na yatumiwe katika ofisi zote za serikali. Aliagiza kwamba historia yenye kupendeza ya nasaba yake na ya nchi yake iandikwe kwa maandishi hayo mapya. Hivyo, kwa mara ya kwanza, watu wa Bamum wangeweza kusoma kuhusu utamaduni, sheria, na desturi zao. Pia Njoya aliagiza mbinu za kitiba ziandikwe kwa kutumia maandishi mapya ya Bamum. Zaidi ya hati 8,000 za awali bado zimehifadhiwa katika rekodi za jumba la kifalme.

Faida ya mfumo huo mpya wa kuandika ilionekana wazi muda mfupi baada ya wakoloni Wajerumani kuwasili mnamo 1902. Ingawa Njoya alifaidika kutokana na maendeleo ya kiuchumi, hakukubaliana nyakati zote na Wajerumani. Kwa hiyo, alitumia ugunduzi wake mpya, ambao Wajerumani hawakuwa wameufahamu. Maandishi ya Bamum yamedumu kwa muda gani?

Wakati wa Vita vya Kwanza vya Ulimwengu (1914-1918), Ujerumani ilipoteza udhibiti wake juu ya milki ya Njoya. Hatimaye, Ushirika wa Mataifa uliokuwa umeanzishwa karibuni ulipatia Ufaransa eneo la Bamum. Ingawa Njoya alikuwa tayari kupokea maoni mapya, alijivunia urithi wake na alitaka sana kuhifadhi na kuendeleza utamaduni wa watu wake. Hilo bila shaka lilimfanya aupinge utawala wa Ufaransa. Kama ilivyokuwa kwa machifu waliowapinga wakoloni, mnamo 1931 aling’olewa mamlakani na Wafaransa. Miaka miwili baadaye, Njoya alikufa akiwa uhamishoni.

Wafaransa walipiga marufuku matumizi ya maandishi ya Bamum katika shule, na kwa kuwa Njoya hakuwepo kuwatia watu moyo watumie maandishi hayo, watu wengi wa Bamum waliacha kuyatumia na wakayasahau. Wamishonari wa dini zinazodai kuwa za Kikristo walipowasili, walijifunza lugha ya Bamum na kuandika kitabu cha sarufi ambacho kingetumiwa shuleni. Tofauti na Njoya, walitumia herufi nyingi kutoka katika alfabeti ya Kiroma na matamshi yake.

Hivi karibuni, jitihada zimefanywa ili kuwachochea watu wapendezwe tena na maandishi ya Bamum. Sultani wa sasa, Ibrahim Mbombo Njoya, amefungua shule katika jumba la kifalme ambalo babu yake alijenga. Watoto wa shule wanajifunza tena mfumo huo wa kuandika ili usitoweke.

[Picha katika ukurasa wa 27]

Bamba linaloonyesha orodha ya wafalme wa Bamum kutoka karne ya 14 hadi leo, lililoandikwa upande wa kushoto kwa alfabeti za Kiroma na maandishi ya Kibamum upande wa kulia

[Picha katika ukurasa wa 26]

All photos: Courtesy and permission of Sultan Ibrahim Mbombo Njoya, Foumban, Cameroon

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki