Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g 9/11 kur. 24-27
  • Watartari—Maisha Yao ya Kale, Sasa, na Wakati Ujao

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Watartari—Maisha Yao ya Kale, Sasa, na Wakati Ujao
  • Amkeni!—2011
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Maisha Yao ya Kale
  • Tatarstan na Mji Wake Mkuu, Kazan’
  • Wenyeji na Lugha Yao
  • Tamaduni za Kitaifa
  • Wanatarajia Nini Wakati Ujao?
  • Kitu Chenye Thamani Kuliko Kazi
    Amkeni!—2011
  • Ziara ya Kurudi Urusi
    Amkeni!—1995
  • Warusi Wathamini Sana Uhuru wa Kuabudu
    Amkeni!—2000
  • Moscow—Ukumbusho Wake wa Miaka 850
    Amkeni!—1997
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2011
g 9/11 kur. 24-27

Watartari​—Maisha Yao ya Kale, Sasa, na Wakati Ujao

TANGU utotoni nilisikia msemo: “Ukimkwaruza Mrusi utapata Mtartari.” Nilijiona kuwa Mrusi, lakini hivi karibuni watu wa familia yangu waliniambia kwamba babu yangu alikuwa Mtartari.a Ninapowaambia rafiki zangu jambo hilo, wengine wao husema kwamba wao pia wana asili ya Kitartari.

Nimefurahia sana kujifunza kuhusu watu maarufu wenye asili ya Kitartari na kuhusu mafanikio yao katika sanaa, michezo, na mambo mengine. Kwa mfano, Rudolf Nureyev aliyekuwa na uvutano mkubwa katika dansi, alizaliwa nchini Urusi na wazazi Watartari. Watartari milioni saba hivi wanaishi katika nchi zilizokuwa chini ya Muungano wa Sovieti. Acheni nieleze yale ambayo nimejifunza kuhusu Watartari.

Maisha Yao ya Kale

Kwa karne nyingi, Watartari wamehusianishwa na watu kutoka Mongolia na Uturuki. Katika karne ya 13, walishiriki katika vita vya kijeshi vilivyoongozwa na Genghis Khan, aliyekuwa kiongozi Mmongolia.b Milki yake ilienea sehemu kubwa sana inayoweza kulinganishwa na eneo lililokuwa la Muungano wa Sovieti. Katika mwaka wa 1236, mashujaa wake 150,000 hivi, walielekea Ulaya, sehemu inayoanzia magharibi ya Milima ya Ural. Walipofika huko, kwanza walivamia majiji ya Urusi.

Muda mfupi baada ya Wamongolia kuvamia Urusi, walianzisha jimbo lililomilikiwa na Wamongolia na Waturuki, ambalo upande wake wa magharibi uliitwa Golden Horde. Mji wake mkuu, Sarai Batu, ulikuwa kwenye sehemu ya chini ya Mto Volga. Jimbo hilo lilitia ndani sehemu fulani ya Siberia na Milima ya Ural, pamoja na safu za milima ya Carpathia na Caucasus iliyo nchini Ukrainia na Georgia. Majimbo ya Urusi yalilazimishwa kulilipa jimbo la Golden Horde ushuru. Katika karne ya 15, majimbo hayo yaligawanyika na kuwa wilaya mbalimbali, kama vile Krimea, Astrakhan, na Kazan’.

Tatarstan na Mji Wake Mkuu, Kazan’

Leo, karibu watu milioni nne kutoka mataifa mbalimbali wanaishi katika Jamhuri ya Tatarstan, iliyo katika eneo la mbali la mashariki mwa Urusi. Eneo lake lina ukubwa wa kilomita 68,000 hivi za mraba, na linasifiwa kuwa moja ya maeneo “yaliyoendelea zaidi kiuchumi katika Shirikisho la Urusi.” Tatarstan ndilo eneo linalotokeza mafuta na gesi kwa wingi zaidi nchini Urusi. Viwanda vyake hutengeneza ndege na magari, na jamhuri hiyo ina viwanja kadhaa vya ndege.

Kazan’ ni jiji la kisasa lenye wakazi milioni moja mahali ambapo Mto Volga na Mto Kazanka hukutania. Ni moja kati ya majiji mengi nchini Urusi yaliyo na mifumo ya reli za chini ya ardhi.c Kila kituo kimetengenezwa kwa njia ya pekee. Vingine vina muundo wa kisasa na vingine vimejengwa kwa njia inayoonyesha utamaduni wa watu wa nchi za Mashariki, ilhali vingine vimejengwa kwa njia inayoonyesha utamaduni wa Enzi za Kati. Kituo kimoja mjini Kazan’ kimepambwa kwa michoro 22 maridadi iliyotiwa nakshi inayoonyesha hekaya za kitamaduni za Watartari.

Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Kazan kilianzishwa mwaka wa 1804 na aliyekuwa Maliki wa Urusi Alexander wa Kwanza na kina moja ya maktaba kubwa zaidi nchini Urusi. Chuo hicho kina uvutano mkubwa kwani ni kituo cha elimu na tamaduni na ndicho kilichochangia kusitawi kwa vyuo vingine huko Tatarstan. Kati ya vichapo 5,000,000 vinavyopatikana humo mna hati 30,000 za zamani, ambazo baadhi yake ni za tangu karne ya tisa W.K.

Inafurahisha kutembea kwenye Barabara ya Bauman katikati mwa jiji. Eneo hilo limejaa maduka na mikahawa yenye kupendeza. Tulipotembelea eneo hilo hivi karibuni, mimi na mke wangu tulifurahia kupanda mashua kwenye Mto Volga baada ya kutalii mji huo.

Sehemu moja yenye kupendeza katika mji wa Kazan’ ni ngome maarufu ya kremlin. Ngome hiyo ya zamani, yenye majengo ya tangu karne ya 16, ndiyo ngome pekee ya Kitartari ambayo imedumu hadi leo nchini Urusi. Kwenye ukingo wa ukuta wa mawe wa Kremlin hiyo ya Kazan’ utaona Mnara wa Syuyumbeki, majengo ya serikali ya Tatarstan, msikiti, na kanisa la Othodoksi.

Katika mwaka wa 2000, Kremlin hiyo ya Kazan’ ilichaguliwa kuwa Eneo Linalostahili Kuhifadhiwa Ulimwenguni la UNESCO. Wakati wa usiku jengo la kremlin hupendeza sana. Hiyo ni kwa sababu ya taa zake zinazomulika na kung’aa mtoni.

Wenyeji na Lugha Yao

Kabila la Tartari ndilo lenye idadi kubwa zaidi ya watu kati ya makabila mengine yote nchini Urusi yenye asili ya Kituruki na inakadiriwa kuwa idadi yao inafika watu 5,500,000 hivi. Lakini idadi yao haijulikani kabisa katika nchi hiyo kubwa.

Kitartari ni moja kati ya lugha za Kituruki. Lugha hizo zinatia ndani Kiazerbaijani, Kibashkir, Kikazakh, Kikirghiz, Kinogai, Kituruki, Kiturkomani, Kituviniani, Kiuzbeki, na Kiyakuti. Baadhi ya lugha hizo zinafanana sana kiasi cha kwamba wanaposemezana wanaweza kuelewana.

Ulimwenguni kuna mamilioni ya watu ambao huzungumza lugha za Kituruki. Katika barabara za miji kotekote Tatarstan, watu huzungumza Kitartari na Kirusi, na pia lugha hizo hutumiwa katika magazeti, vitabu, redio, na televisheni. Majumba ya maonyesho huko Tatarstan huonyesha michezo ya kuigiza katika Kitartari kuhusu historia, utamaduni, na maisha ya kila siku ya Watartari.

Majina ya maduka na ya barabara katika jiji la Kazan’ na miji mingine yameandikwa katika Kirusi na Kitartari. Kirusi kina maneno mengi yenye asili ya Kitartari. Mnamo 1928, katika Muungano wa Sovieti, Kitartari kiliacha kutumia alfabeti za Kiarabu na kikaanza kuandikwa kwa kutumia alfabeti za Kilatini. Tangu 1939, Kitartari kimekuwa kikiandikwa kwa kutumia muundo wa Kisirili kinachofanana na kile cha Kirusi.

Tamaduni za Kitaifa

Zamani Watatari walikuwa wawindaji na wafugaji. Hata leo, chakula chao cha kitamaduni kinatia ndani milo mingi yenye nyama. Moja kati ya hiyo ni belesh, na kinapendwa sana na familia nyingi za Watartari. Kinatayarishwa kama sambusa kubwa iliyojazwa viazi, nyama, vitunguu, na vikolezo. Kinaokwa kwa saa mbili hivi. Kisha kinaletwa mezani na kukatwa mbele ya kila mtu kikiwa bado kinatoa moshi.

Huenda Sabantui ndiyo sikukuu ya kitaifa ya zamani zaidi ya Watartari na iliyo maarufu zaidi. Inategemea desturi za kipagani ambapo watu walisali pamoja na kutoa dhabihu kwa mungu-jua na roho za mababu waliokufa. Wahusika waliamini kwamba dhabihu hizo zingehakikisha kwamba uzao wao unaendelea, wanyama wao wanaendelea kuzaana, na mashamba yao yanaendelea kutoa mazao.

Watartari wanapenda farasi. Farasi ni sehemu muhimu katika utamaduni wao na waliwatumia sana zamani walipokuwa wakihamahama. Kazan’ ndio mji wenye kiwanja kizuri zaidi ulimwenguni cha maonyesho ya farasi, kilicho na mazizi 12 na kliniki ya kuwatibu wanyama. Hata kuna kidimbwi cha kuogelea kwa ajili ya farasi!

Wanatarajia Nini Wakati Ujao?

Kurani inasema hivi: “Na hakika tuliandika katika Zaburi, baada ya kuandika katika [Torati] ya kwamba ardhi (hii) watairithi waja wangu walio wema.” (Sura 21, Al-Anbiyā [Manabii], mstari 105). Ni wazi kuwa maneno hayo yalinukuliwa kutoka katika zaburi za Daudi ambazo zilirekodiwa katika Biblia zaidi ya miaka 1,500 mapema. Zaburi 37:29 inasema: “Waadilifu wenyewe wataimiliki dunia, nao watakaa milele juu yake.”

Watu hao waadilifu na wenye furaha, watatoka katika taifa na kabila gani? Unabii uliorekodiwa katika Injil (ambayo ni Injili ya Wakristo ya Agano Jipya) unasema hivi: “Umati mkubwa, ambao hakuna mtu aliyeweza kuuhesabu, kutoka mataifa yote na makabila na vikundi vya watu na lugha.” (Ufunuo 7:9) Utakuwa ni wakati ujao mzuri kama nini kuishi katika dunia iliyojaa ndugu kutoka mataifa mbalimbali!d

[Maelezo ya Chini]

a Watartari ni sehemu ya kabila kubwa lenye asili ya Kituruki linalopatikana hasa nchini Urusi.

b Ona habari “Wahama-Hamaji wa Asia Waliofanyiza Milki,” katika Amkeni! la Mei 2008.

c Majiji mengine ya Urusi yaliyo na mifumo ya reli za chini ya ardhi yanatia ndani Yekaterinburg, Moscow, Nizhniy Novgorod, Novosibirsk, St. Petersburg, na Samara.

d Habari zaidi kuhusu kusudi la Mungu inapatikana katika broshua Mwongozo wa Mungu—Njia Yetu ya Kwenda Paradiso iliyochapishwa na Mashahidi wa Yehova.

[Sanduku katika ukurasa wa 25]

JINA LA MUNGU KATIKA KITARTARI

Kitabu Dinnər Tarixb (Dini za Ulimwengu) kilichoandikwa na mwandishi Mtartari, M. Khuzhayev, kinasema kwamba Adamu aliumbwa na Yakhve Allah, au Yehova Mungu. Pia, katika Pentateuki ya Kitartari, yaani, vitabu vitano vya kwanza katika Biblia za kisasa, kuna maelezo ya chini kwenye Mwanzo 2:4 yanayosema hivi kuhusu jina la Mungu: “Kuna uwezekano kwamba jina hili lilitamkwa Yahveh na Waebrania wa kale.”

[Sanduku katika ukurasa wa 26]

MASHAHIDI WA YEHOVA HUKO TATARSTAN

Mashahidi wa Yehova nchini Urusi wamekuwa na madarasa ya kufundisha lugha ya Tartari kwa sababu wanatamani sana kuwaeleza watu habari njema za Ufalme wa Mungu. Mwanamke mmoja huko Tatarstan alisema hivi: “Niliguswa sana hadi nikatokwa na machozi nilipojifunza kumhusu Mungu katika lugha yangu ya mama.”

Mnamo 1973 kikundi kidogo cha Mashahidi wa Yehova Watartari kilianza kufanya mikutano ya kujifunza Biblia katika Kitartari. Katika miaka ya 1990 Mashahidi wa Yehova walianza kuchapisha vitabu vya Biblia katika Kitartari.e Kisha mnamo 2003, kutaniko la kwanza la Mashahidi wa Yehova katika Kitartari lilianzishwa huko Naberezhnye Chelny, katika Jamhuri ya Tatarstan. Leo, kuna makutaniko 8 ya Kitartari na vikundi vingine 20 vya lugha hiyo nchini Urusi.

Katika mwaka wa 2008, wajumbe kutoka Astrakhan, eneo la Mto Volga, kutoka Milima ya Ural, Siberia Magharibi, na kutoka kaskazini ya mbali walihudhuria kusanyiko la wilaya la Kitartari. Kufikia sasa huko Tatarstan kuna makutaniko na vikundi 36 vya Kitartari, Kirusi, na Lugha ya Ishara ya Kirusi, ambapo zaidi ya watu 2,300 wanashiriki kwa bidii katika kazi ya kuwafundisha watu kweli za Mungu.

[Maelezo ya Chini]

e Shirika la Watch Tower Bible and Tract Society limechapisha Biblia na vichapo vya Biblia katika lugha zaidi ya 560.

[Sanduku/​Picha katika ukurasa wa 27]

ALIYEKUWA MWANARIADHA SASA NI MCHUNGAJI

Pyotr Markov alizaliwa katika kijiji cha Tatarstan mnamo 1948. Kwa miaka 30 alikuwa maarufu kutokana na uwezo wake wa kupigana mieleka na kuinua uzani. Wakati mmoja aliinua uzani wa kilo 32 mara 130. Sasa, tangu awe mmoja wa Mashahidi wa Yehova, anajulikana sana kwa kuzungumza na watu kuhusu Mungu katika Kitartari na Kirusi na pia kuwafundisha jinsi ya kukabiliana na matatizo maishani.

Hivyo, Pyotr anamwiga Muumba mwenye kujali, ambaye Isaya 40:11 inasema hivi kumhusu: “Atalichunga kundi lake mwenyewe kama mchungaji. Atawakusanya pamoja wana-kondoo kwa mkono wake; naye atawabeba katika kifua chake. Wale wanaonyonya atawaongoza kwa uangalifu.”

[Picha]

Pyotr, sasa anatumika akiwa mchungaji wa kiroho

[Ramani katika ukurasa wa 24]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

URUSI

MILIMA YA URAL

MOSCOW

St. Petersburg

JAMHURI YA TATARSTAN

Kazan’

Mto Volga

[Picha katika ukurasa wa 25]

Kremlin ya Kazan’ katika Mto Kazanka

[Hisani]

© Michel Setboun/CORBIS

[Picha katika ukurasa wa 26]

“Belesh” ni chakula kinachopendwa sana na familia nyingi za Kitartari

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki