Hukumu ya Kimungu Yatekelezwa Juu ya Manabii wa Uongo wa Jumuiya ya Wakristo
1, 2. (a) Kutahiriwa kwa mambo mema yajayo pasipo msingi kunatuacha katika hali ya kupatwa na jaribu gani? (b) Ni ulizo gani kubwa zaidi linalohitaji kujibiwa sasa, nalo ni jambo gani ambalo limelisukuma mbele?
KWA KAWAIDA sisi sote hupenda kusikia unabii au matabiri ya mambo mema yanayokuja karibuni, katika wakati wa muda wa maisha zetu. Jambo hilo hutuweka katika hali ya kupatwa na jaribu kubwa. Huenda tukataka kukubali matabiri fulani kuwa ya kweli kwa sababu tunayapenda, lakini si kwa sababu yana msingi imara au yana chanzo chenye mamlaka. Jambo hilo huenda likatuchochea kutenda kitendo ambacho chaweza kutudhuru. Sana sana hivyo ndivyo ilivyo ikiwa wakati wetu ujao wa milele unahusika. Hivyo ndivyo ilivyo SASA! Sababu gani ndivyo ilivyo sasa?
2 Sababu ni kwamba ulizo la maana sana linalohitaji kujibiwa linawaelekea wanadamu wote sasa. Ulizo hilo ni, Ni nani atakayetawala ulimwengu? Jambo ambalo limelisukuma mbele ulizo hili la maana sana si yale mashindano yasiyo na mwisho kati ya mataifa ya kibepari yaliyo huru kujitafutia utajiri wao wenyewe na yale ya Kikomunisti yanayopendelea mambo ya kijamii. Badala yake, tangazo ambalo mashahidi Wakristo wa Yehova wamekuwa wakifanya kuhusu ufalme Wake kupitia kwa Kristo ndilo jambo la hakika ambalo limefanya hivyo. Ufalme huo una haki ya kutawala tangu Majira ya Mataifa yalipokoma katika mwaka 1914.
3. (a) Kwa hiyo watu wamekuwa na wajibu wa kuchukua msimamo wao kuhusiana na ulizo gani? (b) Sababu gani Mataifa yapaswa kumtolea Yehova enzi zao kuu?
3 Watu waliosikia tangazo hilo la Ufalme katika lugha zapata 190 ulimwenguni pote wamekuwa na wajibu wa kuchukua msimamo wao. Je! sasa wao watauunga mkono utawala wenye haki wa Yehova kupitia kwa Kristo au hapana? Dunia hii tunayoishi ndani yake ni mali ya Muumba wake, si yetu sisi viumbe. Kulingana na hesabu ya wakati katika kitabu cha Muumba, Biblia, wakati alioruhusu kutawaliwa kwa ulimwengu na mataifa ya kidunia, kutia na yale ya Jumuiya ya Wakristo, ulikoma karibu na mwanzo mwa vuli ya mwaka 1914. Yeye alionyeshaje kwamba hayo Majira ya Mataifa yalikuwa yamekoma? Kwa kuutwaa “uweza [wake] ulio mkuu,” na kuanza kutawala kama Mfalme na kumshirikisha Mwanawe wa kimbinguni, Yesu Kristo, katika serikali yake ya kimbinguni. (Ufu. 11:15-18) Kwa hiyo sasa Mwanawe atawala. (Eze. 21:25-27) Huu ndio wakati wa Mataifa kumtolea Yehova enzi zao kuu.
4, 5. (a) Ni hatari gani iliyoielekea Mashariki ya Kati huko nyuma katika mwaka 614 K.W.K.? (b) Kufikia wakati huo ni jambo gani lililokuwa limevipata vyombo vitakatifu vya hekalu la Yerusalemu, nao utabiri wa Hanania kuhusu vyombo hivyo ungetimizwa kwa njia gani peke yake?
4 Huko nyuma katika mwaka 614 K.W.K. hali ya mambo inayolingana na hiyo ilitokea katika Ufalme wa Yuda. Wakati huo kulikuwako hatari ya ulimwengu! Kutoka wapi? Kutokana na kile ambacho Mungu aliita ‘jamaa zote za kaskazini.’ Hiyo ilimaansiha Mamlaka ya Ulimwengu ya Babeli, ambayo ingeshambulia Mashariki ya Kati ikifuata njia ya kaskazini. (Yer. 1:13-15; 25:9, 26) Tayari Mashariki ya Kati ilikuwa chini ya utawala wa Mfalme Nebukadreza wa Babeli. Sana sana hiyo ilikuwa hivyo tangu mwaka 620 K.W.K., wakati Yehoyakimu wa Yerusalemu alipata kuwa mfalme kibaraka kwa Babeli. Ndugu yake Sedekia akaja kuwa mfalme kibaraka wa mwisho wa mji huo mtakatifu, Nebukadreza alipomweka katika kiti cha enzi baada ya kumwapisha. Wakati Nebukadreza alipoondoka Yerusalemu kurudi kwake, alimpeleka uhamishoni mfalme aliyeondolewa Yehoyakini pamoja na wakuu wengine wa Yuda. Vilevile alichukua vyombo vitakatifu kutoka katika hekalu la Yehova na kuviweka katika nyumba za miungu wa uongo huko Babeli. Vyombo hivyo vitakatifu pamoja na vitu vingine vya thamani vilivyotwaliwa kutoka Yerusalemu vingekaa muda gani huko Babeli? Ulizo hilo lilipata kushindaniwa vikali sana katika mwaka wa nne wa utawala wa Sedekia.
5 Nabii wa uongo aitwaye Hanania mwana wa Azuri alijitanguliza na kudai kusema katika jina la Yehova akataja, “miaka miwili mizima.” Ingekuwa hivyo tu ikiwa Babeli ingeangushwa na Misri kuwa mamlaka ya ulimwengu kwa mara nyingine tena. Kwa kutabiri hivyo juu ya Babeli, Hanania alikuwa akiwatia moyo wale waliopendelea uasi wa mataifa yote juu ya Nebukadreza wa Babeli. Hivyo jambo hili lilikuwa kinyume cha amri na shauri la Yehova kama vile lilivyokuwa limekwisha tangazwa na Yeremia.
6. Kulingana na Yeremia 28:8, 9, unabii wa Hanania ulitofautianaje na ule wa manabii waliomtangulia Yeremia mwenyewe?
6 Kwa kuwa Hanania alikuwa akitoa matumaini ya uongo juu ya nchi ya Yuda, Yeremia alimalizia maneno yake ya jibu mbele ya makuhani na watu wote katika hekalu kwa kusema: “Manabii waliokuwako kabla ya zamani zangu, na zamani zako, walitabiri juu ya nchi nyingi, na juu ya falme kubwa, habari ya vita, na ya mabaya, na ya tauni. Nabii atabiriye habari za amani, neno la nabii yule litakapotokea, ndipo nabii yule atakapojulikana, kuwa [Yehova] amemtuma kweli kweli.”—Yer. 28:1-9.
7. Yesu Kristo alitabiri matukio gani kuhusu wakati wetu tangu mwaka 1914, nalo ni ulizo gani kuhusu wasema-kweli ambalo limetokea leo?
7 Nabii aliye mkuu zaidi wa Yehova, Yesu Kristo, alitabiri juu ya vita, njaa, magonjwa ya kipuku, matetemeko ya ardhi na misiba mingine ambayo ingetokea katika wakati wetu tangu mwaka 1914, hayo yote yakifikia upeo wake katika “dhiki kubwa” isiyo na mfano wake katika historia yote iliyotangulia ya wanadamu. (Mt. 24:4-22) Leo mashahidi wa Yehova wameonyesha namna unabii wa Yesu umeendelea kutimia hatua kwa hatua tangu mwaka 1914. Yeye hakutabiri juu ya amani yo yote yenye kuendelea ya ulimwengu huu katika wakati ulio karibu, katika kizazi hiki. Hivyo, basi, ni nani waliotumwa na Yehova na ambao husema katika jina lake, wakuu wa dini za Jumuiya ya Wakristo ambao hutabiri kinyume, au jamii ya Yeremia ya leo? Matukio ya wakati ujao yatawatambulisha wasema-kweli.
8. Ni tendo gani la kitamasha lililochukuliwa na Hanania baada ya jibu la Yeremia, nao ni unabii gani kuhusu wakati alioutoa?
8 Lazima nabii wa uongo Hanania awe alikuwa na uhakika juu ya kufaulu kwa uasi wa mataifa yote juu ya “mtumishi” wa Yehova, kwa kuwa sasa alitenda kitendo cha kitamasha:
‘Akaitwaa hiyo nira iliyokuwa juu ya shingo ya Yeremia, akaivunja. Naye Hanania akanena mbele ya watu wote, akisema, [Yehova] asema hivi, Hivyo ndivyo nitakavyoivunja nira ya Nebukadreza, mfalme wa Babeli, kabla haujatimia muda wa miaka miwili mizima, na kuiondoa shingoni mwa mataifa yote.”—Yer. 28:10, 11.
9. Yehova alimwambia Yeremia aseme nini sasa kuhusu nira, na kwa sababu gani?
9 Walakini, je! unabii kama huo ungetimia ati kwa sababu tu umenenwa katika jina la Yehova? Hapana! Yehova hangefanya vile Hanania alivyokuwa ametabiri na wakati uo huo atimize unabii wa Yeremia uliokuwa kinyume cha huo. Kwa hiyo, uasi wa mataifa yote juu ya “mtumishi” wa Yehova usingefaulu! “Enenda,” Yehova akamwambia Yeremia baadaye, “ukamwambie Hanania, ukisema, [Yehova] asema hivi, Umezivunja nira za mti; lakini badala yake utafanya nira za chuma. Maana [Yehova] wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nimetia nira ya chuma juu ya shingo ya mataifa haya yote, ili wamtumikie Nebukadreza, mfalme wa Babeli; na watamtumikia; nami nimempa wanyama wa nchi pia.” (Yer. 28:12-14) Kwa hiyo, hakuna mpango wa hila uliochochewa na Hanania ambao ungefaulu. Na zaidi, ili Yehova apate kumpa Nebukadreza “wanyama wa nchi pia,” Yehova angempa nchi za mataifa hayo yote yenye kufanya mpango wa hila.
KIONGOZI WA UASI WA KIDINI APATA YAMPASAYO
10. Ni tendo gani ambalo jamii ya Yeremia imeruhusiwa kuchukua juu ya viongozi wa kidini ambao kama Hanania, wanaunga mkono mpango wa hila wa mataifa yote juu ya Yehova?
10 Leo manabii-viongozi wa dini za Jumuiya ya Wakristo wanaunga mkono waziwazi ule mpango wa hila wa mataifa yote juu ya ufalme wa Yehova kupitia kwa Kristo wake. Mashahidi wa Yehova hawana mamlaka ya kutangaza hukumu ya kifo juu ya ye yote wao. Walakini wanaweza kuchukua usemi wa Yehova na kuutumia juu ya manabii wa uongo wa viongozi hawa, ambao kama jamii ndio waliofananishwa na Hanania. Hivyo, ebu basi sasa na tusome juu ya tendo la kiunabii la Yeremia:
“Kisha nabii Yeremia akamwambia nabii Hanania, Sikia sasa, Ee Hanania; [Yehova] hakukutuma; lakini unawatumainisha watu hawa maneno ya uongo. Basi [Yehova] asema hivi, Tazama, nakutuma uende zako toka juu ya uso wa nchi; mwaka huu utakufa, kwa sababu umenena maneno ya uasi juu ya [Yehova].”—Yer. 28:15, 16.
11. (a) Hanania aliishi kwa muda gani zaidi? (b) Viongozi wa dini za Jumuiya ya Wakristo vilevile wana hatia gani, na kwa hiyo lazima jamii ya Yeremia ionyeshe nini?
11 Hanania, wakili wa uasi wa mataifa yote yenye kufanya mpango wa hila juu ya Yehova, aliishi yapata miezi miwili zaidi. “Basi nabii Hanania akafa, mwaka uo huo [614 K.W.K.], mwezi wa saba.” (Yer. 28:17, 1) Kwa msaada wa tamasha hii ya kiunabii ya nyakati za zamani, namna gani juu ya manabii wa uongo wa viongozi wa dini za Jumuiya ya Wakristo leo? Wao wanawaunga mkono watawala wa kisiasa katika kukataa kutia shingo zao chini ya nira ya Mtumishi-Mfalme wa Yehova, aliye mkuu zaidi ya Nebukadreza wa nyakati za zamani. Jamii ya Yeremia haiwezi kukubaliana na viongozi wa kidini katika jambo hili. Lazima waendelee kuonyesha msiba ambao katika huo viongozi hawa wanawaongoza watu.
12. Kwa ajili ya Wayahudi ambao tayari walikuwa uhamishoni Babeli, ni ujumbe gani ambao Yeremia alipata kutoka kwa Yehova kuhusu manabii wa uongo Ahabu na Sedekia?
12 Katika siku hizo za zamani zilizokuwa na msukosuko wa kisiasa katika Mashariki ya Kati, hata wale Wayahudi waliokuwa uhamishoni huko Babeli walikuwa na manabii wa uongo miongoni mwao. Kwa hao manabii wa uongo waliokuwa wakisitawisha matumaini ya uongo kati ya Wayahudi hao wahamishwa waliokuwa katika nchi ya Nebukadreza, Mungu alituma ujumbe huu kupitia kwa Yeremia:
“Basi, lisikieni neno la [Yehova], ninyi nyote mliochukuliwa mateka, niliowapeleka toka Yerusalemu mpaka Babeli.
“[Yehova] wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, katika habari za Ahabu, mwana wa Kolaya, na katika habari za Sedekia, mwana wa Maaseya, wawatabiriao ninyi maneno ya uongo kwa jina langu; Tazama, nitawatia katika mikono ya Nebukadreza, mfalme wa Babeli, naye atawaua mbele ya macho yenu. Tena katika habari zao laana itatumiwa na wafungwa wote wa Yuda, walioko Babeli, [Yehova] akufanye ukiwa kama Sedekia, na kama Ahabu, ambao mfalme wa Babeli aliwaoka motoni; kwa sababu wametenda upumbavu katika Israeli, nao wamezini na wake za jirani zao, nao wamenena maneno ya uongo kwa jina langu, nisiyowaamuru; nami ndimi nijuaye, nami ni shahidi, asema [Yehova].”—Yer. 29:20-23.
Bila shaka “mtumishi” wa Yehova, Nebukadreza, alikuwa na sababu nzuri za kisiasa za kuwaoka Sedekia na Ahabu motoni, kwa kuwa, walikuwa wakitenda kinyume cha shauri la Yehova na cha faida za milki ya Babeli.
13. Je! Wayahudi hao wahamishwa wangetazamia ukombozi wa mapema, na kwa hiyo barua ya Yeremia iliwaambia wafanye nini?
13 Maneno hayo yaliyotajwa hapo juu yalikuwa sehemu ya barua ambayo Yeremia aliwapelekea toka Yerusalemu wazee, makuhani, manabii, na watu walio kuwa uhamishoni mbali huko Babeli, kwa mikono ya Elasa mwana wa Shafani na Gemaria mwana wa Hilkia, wakati Mfalme Sedekia wa Yerusalemu alipowatuma wajumbe hawa wawili kwa Mfalme Nebukadreza wa Babeli. (Yer. 29:1-3) Katika barua hiyo ya Yeremia, Yehova aliwaambia wahamishwa hawa wasitazamie ukombozi wo wote wa mapema kutoka Babeli, bali wathibitike huko waoe wazae na kuongezeka. Mahali pa kujaribu kuasi, “kautakieni amani mji ule, ambao [mimi, Yehova] nimewafanya mateka, mkauombee kwa [Yehova]; kwa maana katika amani yake mji huo ninyi mtapata amani. . . . Maana [Yehova] asema hivi, Babeli utakapotimiziwa miaka sabini, nitawajilia ninyi, na kulitimiza neno langu jema kwenu, kwa kuwarudisha mahali hapa.”—Yer. 29:4-10.
14. Kama vile nabii huyo wa zamani, jamii ya Yeremia inawaonya kwa upole Wakristo walio wakf na kubatizwa wafanye nini po pote walipo?
14 Kwa kufuata sana mfano wa Yeremia, jamii ya Yeremia ya leo wanawaonya kwa upole mashahidi wote wa Yehova walio wakf na kubatizwa wawe wananchi watiifu na wenye amani katika nchi ambamo, kusema kwa njia ya kiroho, wao ni “wapitaji na wasafiri.” (1 Pet. 2:11-15) Kwa utii wao wa kadiri kwa “mamlaka zilizo kuu,” wanakuwa vilevile na amani pamoja na Mungu.—Rum. 13:1-4, NW.
15. Shemaye nabii wa uongo huko Babeli alikuwa amefanya nini naye alitoa lalamiko gani kwa “msimamizi mkuu” wa hekalu la Yerusalemu?
15 Hata kabla Yeremia hajaitunga barua yake na kuipeleka, nabii wa uongo ambaye wakati huo alikuwa uhamishoni huko Babeli, yaani, Shemaya Mnehelami, alikuwa amekwisha kumpelekea barua Sefania mwana wa Maaseya, “msimamizi mkuu” wa hekalu la Yerusalemu. Kwa hiyo, Yehova alitaja jambo hili katika barua ambayo Yeremia alipelekea mateka wa Babeli akaendelea kusema hivi:
“Na katika habari za Shemaya, Mnehelami, utanena, ukisema, [Yehova] wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, ya kwamba, Kwa kuwa kwa jina lako mwenyewe umewapelekea barua watu wote walioko Yerusalemu, na Sefania, mwana wa Maaseya, kuhani, na makuhani wote, kusema [Yehova] amekufanya kuhani badala ya Yehoyada, kuhani, ili mpate kuwa watumishi katika nyumba ya [Yehova], kwa kila mtu aliye na wazimu, na kwa kila mtu ajifanyaye kuwa nabii, umtie katika mkatale na pingu. Mbona, basi, hukumkemea Yeremia wa Anathothi, ajifanyaye kuwa nabii kwenu, ambaye ametuma watu kwetu katika Babeli, kusema, Uhamisho huu ni wa siku nyingi; jengeni nyumba, mkakae ndani yake; pandeni bustani, mkale matunda yake.”—Yer. 29:24-28; linganisha Yeremia 29:4-6.
16. Msimamizi mkuu” huyo wa hekalu alifanya nini na barua iliyotoka kwa Shemaya, naye Yeremia aliambiwa atabiri nini kuhusu Shemayu?
16 Walakini, alipoipokea barua ya Shemaya, kuhani Sefania akiwa “msimamizi mkuu” wa hekalu, hakumtia Yeremia katika mkatale na pingu. Kwanza alisoma ile barua masikioni mwa Yeremia. (Yer. 29:29) Vipi sasa?
“Ndipo neno la [Yehova] likamjia Yeremia, kusema, Uwapelekee habari watu wote waliohamishwa, kusema, [Yehova] asema hivi, katika habari za Shemaya, Mnehelami; Kwa sababu Shemaya amewatabiria ninyi, lakini sikumtuma mimi, naye amewatumainisha neno la uongo; basi, [Yehova] asema hivi, Tazama, nitamwadhibu Shemaya Mnehelami, na wazao wake; hatakuwa na mtu atakayekaa katika watu hawa, wala hatayaona mema nitakayowataendea watu wangu, asema [Yehova]; kwa sababu amenena maneno ya uasi juu ya [Yehova].”—Yer. 29:30-32.
17. Ni kwa sababu gani uasi uliochochewa na Shemaya juu ya Babeli ulikuwa vilevile uasi juu ya Yehova?
17 Kwa yale ambayo Shemaya alitabiri na kuandika, yeye alikuwa akichochea uasi kwa upande wa Mfalme Sedekia wa Yerusalemu akiungwa mkono na Farao wa Misri, ambayo daima ilikuwa ikipinga Mamlaka ya Ulimwengu ya Babeli. Walakini uasi kama huo ungekuwa kuasi zaidi ya Babeli tu. Ungekuwa vilevile juu ya Yehova aliyekuwa wakati huo akimtumia mfalme wa Babeli kama “mtumishi” wake. Kwa hiyo Yehova ndiye aliyekuwa Bwana wa kimbinguni wa mfalme wa Babeli. Kwa hiyo, kuiasi Babeli kungekuwa zaidi sana kumwasi Yehova.
MNGOJEE YEHOVA KATIKA KUTOKUWAMO KWA KIKRISTO
18. Shemaya alikuwa akijitangulizaje mbele za Yehova, kukawa na matokeo gani kwake mwenyewe na uzao wake?
18 Shemaya aliyekuwako Babeli hakutaka kumngojea Yehova alete ukombozi kwa ajili ya Wayahudi waliohamishwa, ambao yeye alikuwa mmoja wao. Yeye hakuuamini unabii wa mapema wa Isaya 44:28 mpaka 48:4 kuhusu Koreshi Mwajemi, ambaye angeiangusha Babeli na kuwarudisha Wayahudi waliohamishwa mpaka nchi ya kwao. Hivyo, Shemaya alitaka kujitanguliza mbele ya Yehova. Yeye alipanga kujifanyia wokovu wake mwenyewe na wa wahamishwa wenzake katika njia yake mwenyewe. Yeye alipendelea mwendo ambao ungetia “nira ya chuma” shingoni mwa Mfalme kibaraka wa Yuda kutoka kwa mfalme wa Babeli. (Yer. 28:13, 14) Kwa hiyo, Shemaya mwasi hangepata ukombozi wo wote. Uzao wake ungekatiliwa mbali, usiweze kushiriki sehemu yo yote katika kurudishwa kwa Israeli!
19. Ni mwendo gani ambao umefuatwa na mfano wa kisasa wa Shemaya tangu mwaka 1914?
19 Sisi leo tutafanya vema tukitii shauri lililotolewa katika barua ya Yeremia katika Yeremia 29:8, 9. Kwa kufanya hivyo sisi hatutakuwa tukifuata mfano wa kisasa wa huyo mtaka uasi juu ya mpango wa Yehova, Shemaya Mnehelami. Viongozi wa dini za Jumuiya ya Wakristo, ambao hawakuwasikiliza jamii ya Yeremia tangu yakome Majira ya Mataifa katika mwaka 1914, sasa wamejionyesha wenyewe kuwa kama “tini mbovu, zisizoweza kuliwa, kwa kuwa ni mbovu sana.” Fikira za viongozi wa kidini zimevutwa kwenye sehemu mbalimbali za ile “ishara” iliyotabiriwa na Yesu Kristo na ambayo imekuwa ikitimizwa tangu mwaka 1914, ndio kusema, “upanga” wa vita, hata vita vya duniani pote, vilevile “njaa” yenye kuangamiza sana pamoja na “tauni” zisizozuilika na ‘kutawanywa’ kwa idadi za watu wasio na msaada, hata katika Jumuiya ya Wakristo ambayo hudai kuwa ya Kikristo. (Yer. 29:16-19; Mt. 24:4-20) Hata hivyo viongozi hao wa kidini wanaonyesha kwamba hawaamini maana ya “ishara” ambayo imefafanuliwa kulingana na Maandiko, na kwa hiyo hawayahimizi mataifa yamtolee enzi zao kuu Mtumishi-Mfalme wa Yehova, Yesu Kristo anayetawala sasa, na ambaye, tangu mwaka 1914, anashiriki pamoja na Baba yake wa kimbinguni katika “ufalme wa dunia,” kitu kilicho bora zaidi kuliko Milki ya Babeli ya Nebukadreza. Kinyume chake, viongozi hao wa kidini wanakubali mipango ya wanadamu na kuunga mkono Umoja wa Mataifa, wala si utawala wa Mungu.
20. Ni adhabu gani inayostahili ambayo hutekelezwa juu ya wale wanaoasi utawala, na kwa hiyo sisi tutapataje wokovu wa milele?
20 Leo, kati ya mataifa ya kilimwengu, uasi juu ya utawala uliowekwa kulingana na katiba unaleta adhabu ya kifo kwa wenye kuasi. Vivyo hivyo, uasi usio wa kikristo juu ya Yehova na Mtumishi-Mfalme wake wawaletea uharibifu wale viongozi wa kidini wanaoitwa ati “Wakristo” ambao ‘husema maneno ya uasi juu ya Yehova.’ (Yer. 29:32) Uharibifu wao ulifananishwa na ule ulioletwa juu ya Shemaya nabii wa uongo pamoja na wanawe ambao hawakuona hata kidogo “mema” ambayo Yehova alikusudia kuwafanyia watu watiifu kati ya watu wake waliokuwa uhamishoni. Hivyo si juu yetu kujifanyia wokovu wa mapema kwa njia za wanadamu. Kupata kwetu wokovu milele kunategemea kumngojea Yehova kwa subira na kwa kumtumaini alete wokovu kupitia kwa “mtumishi” aliye mkuu zaidi kuliko Koreshi Mwajemi, yaani Yesu Kristo.
21. Ni mwendo gani uliotabiriwa na Yehova katika Yeremia 29:12-14 kuhusu wahamishwa watiifu tunaopaswa kuiga leo?
21 Kujaribu kwetu kujitanguliza mbele ya Yehova hakutaleta ukombozi tunaoutamani sana. Mahali pa kumpa Yehova kisogo na kukosa kumfikiria, tutafanya vema tukiiga wale waliouona wokovu wa Yehova wakarudishwa katika nchi yao katika wakati wake uliowekwa. Mwendo wao unaofaa kuigwa Yehova aliutabiri katika maneno haya: “Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikia. Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote. Nami nitaonekana kwenu, asema [Yehova].”—Yer. 29:12-14.
22. Kwa sababu ya “mwaka wa nia njema” wa Yehova inatupasa tuchukue hatua juu ya tumaini gani ajili ya wakati ujao?
22 Sasa tuko karibu na mwisho wa “mwaka wa nia njema upande wa Yehova.” (Isa. 61:2, NW) Hivyo, kwa upande wetu, maneno yake bado yatumika: “Nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema [Yehova], ni mawazo ya amani, wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho [“wakati ujao,” NW]—.” (Yer. 29:11) “Wakati ujao” ambao Yehova anawaza juu yetu ndio wenye kutamanika sana, ikiwa tutatii enzi yake kuu ya ulimwengu wote, ni ule wa uzima wa milele pamoja na amani, fanaka na furaha kupitia kwa Mfalme-Mtumishi wake, Yesu Kristo. Hilo ndilo tumaini ambalo Yehova ameweka mbele yetu. Kwa kulithamini kabisa, acheni tutende kulingana nalo.—Kutoka The Watchtower Nov. 1, 1979.