Meteora—Ile Miamba Mikubwa Sana
ILE miamba mikubwa sana ya Meteora katika wilaya ya Thessaly ya Ugiriki ya Kati, ni ya kustaajabisha kweli kweli! Na ule uwanda mkubwa wa Thessaly wenyewe umejawa na maajabu ya kiasili. Uzuri wao na rutuba iliyomo ni mambo yanayosifika sana. Mtu anapoukaribia uwanda huo kutoka mashariki, anapita katika kibonde cha kuvutia ajabu cha Tempe, kilicho kama lango, chini ya uvuli wa mlima Olympus ulio mkubwa sana, mahali ambapo kulingana ya hadithi za kimapokeo walikaa miungu 12 wa Kigiriki. Kwenye sehemu ya chini ya mlima huo unatiririka Mto Pinios, na kwenye mwisho wa mbali wa magharibi ya uwanda huo ndipo ilipo ile miamba mikubwa ya Meteora.
Miamba-miamba hiyo mikubwa sana inaleta mshangao mwingi, inavutia watu, inatia hofu, furaha, na kizunguzungu. Mingine ya miamba hiyo inafikia kimo cha meta 600. Ni mirefu kama minara iliochongwa na hakika miamba hiyo inatoa ushahidi mwingi sana wa kwamba Muumba ni mwenye nguvu mwingi.
Kulingana na wataalamu wanaochunguza historia ya ardhi, kufanyika kwa miamba ya Meteora kulitukia kule nyuma zamani sana katika vipindi vinavyotimika tu kwa kutazama hali za ardhi, wakati ambao Uwanda wa Thessaly wote ulipokuwa sakafu ya bahari iliyofinywa kutoka pande zote za kandokando hata sakafu hiyo ikaacha kuwa tambarare na kuwa na vilima-vilima. Wachunguzi wengine wanauweka wakati unaodhaniwa ndipo miamba ya Meteora ilipofanyika kuwa ni maelfu machache tu ya miaka iliyopita, nao wanasema kilichoisababisha ni matetemeko ya ardhi na mmong’onyoko wa ardhi ulioletwa na maji. Hata hivyo, wote wanakubali kwamba kilichoichongoa miamba hiyo mikubwa sana ni maji yenye kufanya kazi kwa nguvu nyingi ajabu. Bila shaka, mtu anaweza kuuliza chanzo cha maji hayo kilikuwa nini.
Gharika Katika Hadithi za Mapokeo
Hadithi ya kale ya Kigiriki inalitaja eneo hilo. Kulingana na mashahiri ya Pindar na maandishi ya Apollodorus, wakati Deucalion wa kihadithi tu alipokuwa mfalme wa Phthia katika Thessaly, Zeus mfalme wa miungu ya Olympia alikata shauri kuangamiza wanadamu wasio na woga wa kimungu na wakorofi kwa kutumia gharika. Ili kuepuka hasira kuu ya miungu, Deucalion alipanga safina ikajengwa. Humo ndani akaingiza vyakula na vitu vilivyohitajiwa. Mara tu baada ya yeye kuingia katika safina pamoja na Pyrrha mke wake, gharika kubwa sana ilibubujika, ikafurika katika sehemu kubwa ya Ugiriki, na kuzamisha “karibu wanadamu wote.” Wakati wa gharika hiyo, ndipo inapodhaniwa kuwa milima ya Thessaly ilifanyika. Kwa michana na mausiku tisa, safina ya Deucalion ilipita-pita juu ya mawimbi ya maji mpaka ikashuka na kutua juu ya Mlima Parnassus, katika Thessaly.
Baada ya kutoka safinani, Deucalion alimtole dhabihu Fixius Zeus. Mungu Zeus aliwaamuru Deucalion na Pyrrha watupe mawe nyuma yao Mawe yaliyotupwa na Deucalion yakawa wanaume hali yale yaliyotupwa na Pyrrha yakawa wanawake. Hakika hiyo ni namna iliyopotoshwa ya kumbukumbu la Biblia linalohusu Gharika ya kweli iliyotukia siku za Noa!—Mwanzo 6:1–8:22.
Makao ya Watawa wa Meteora
Mwamba Mkuu wa Meteora una kimo cha meta 613 juu ya sakafu ya mto Pineos. Juu ya mahali palipo tambarare pa mwinuko huo lipo kao la watawa la Metamorphosis, nalo ndilo kubwa zaidi ya yale makao sita ya watawa yanayoendeshwa sasa. Si kazi rahisi kupanda kule juu kwa kutumia barabara iliyotandazwa na kutumia ngazi zilizochongwa katika mawe.
Katika makao ya watawa ya Meteora, sasa kuna maktaba zenye hati nyingi sana, nyingi zilipatikana zikiwa zimefichwa katika mahali kama kuta na paa au chini ya godoro.
Mambo yalio katika hati hizo sana-sana ni ya kidini na ya kipadre. Lakini pia kuna hati zenye mambo ya kihistoria, ya uandishi wa vitabu, ya kifalsafa, na ya kisayansi. Kurasa za hati hizo ni za ngozi au za karatasi, nazo ni za tangu karne ya 9 mpaka 19. Kati yazo kuna Kodeksi 591 ya ngozi, iliyo ya tarehe 861-62 W. K. Hiyo ndiyo hati ya zamani katika Ugiriki, ina kurasa 423, na ina hotuba zenye kufasiri maana ya Injili ya Mathayo.
Pia kuna maandishi yaliyohifadhiwa yenye mambo rasmi kama vile kurasa zilizopakwa rangi ya dhahabu, mambo hayo yakiwa yanahusu wafalme na wazee wa ukoo wakati wa Milki ya Kiroma ya Mashariki. Jumla ya maandishi hayo yaliyohifadhiwa ni karibu 3,000. Lakini hati za Biblia ni chache, kwa maana wanakili wa kule Meteora hawajajitia sana katika kazi ya namna hiyo.
Makao ya watawa hayo yamejawa na sanamu za kidini zinazoonyesha watu wa kihadithi tu na pia watu halisi, na pia matukio yanayoshuhudia kwamba watawa hao wana imani za kidini. Kwa mfano, picha moja inayohusu Kuja kwa Pili inaonyesha watenda dhambi wakitupwa ndani ya vinywa vya madubwana mabaya sana. Mahali pengine, katika hekalu ya Yohana Mbatizaji, na picha yenye mambo ya kuchongwa yanayoonyeshwa mpanda-farasi ambaye mbele yake amesimama Venus.
Hapo ndipo inapoishia ziara yetu ya Meteora. Hata tufikiri nini juu ya vitu vilivyofanywa na wanadamu vinavyopatikana kule sasa, tunavutwa na uzuri wa ajabu wa miamba-miamba hiyo mikubwa sana iliyo katika Thessaly.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 30]
Embassy of Greece photo