Utafutaji wa Usalama
USALAMA. Viongozi wa ulimwengu hufanya mashauriano ya kuupata. Viongozi wa kidini husali waupate. Na bado, kwa akina yahe barabarani, usalama waonekana kuwa ndoto isiyoweza kutimizwa. Kwa kielelezo, mchukue Ron aliyekuwa akitembea kwenda kazini katika Johannesburg, jiji kubwa kabisa la Afrika Kusini.
“Walikuwako wanaume watano wenye kunizunguka, mmoja akiwa ameweka kisu kooni pangu na mwingine akiwa na kingine mgongoni pangu. Kwa muda wa sekunde chache wakawa wamepekua mifuko yangu. Nilihisi nikiwa kama kuku aliyeng’olewa manyoya. Watu wenye kupita hapo walinipuuza tu.” Ron hakukinza naye akaachwa bila kuumizwa.
Watu wengi huona ni jambo lenye mkazo mwingi kutembea katika barabara za jiji lolote kubwa. ‘Nawezaje kuepuka kushambuliwa?’ wao hukerwa na wazo hilo akilini. Hufanya haraka kumaliza ununuzi wao ili waweze kurudia usalama wa nyumbani kwao. Lakini nyumbani ni salama kadiri gani? “Uwezekano wa mtu fulani kuvamia nyumba yako aingilie haki zako, anyakue sehemu fulani au kiasi chote cha mali zako na kutoweka bila kugunduliwa unaongezeka mno kila mwaka,” chataarifu kitabu Total Home Security.
Tokeo ni kwamba, wenye nyumba huangika ilani zenye kuonya wadukizi kwamba mahali hapo pana mbwa wakali sana au kwamba huwa panatunzwa na washika-doria wenye silaha. Katika ujirani mwingi wenye nyumba huungana katika jitihada ya kupambana na uhalifu. “Kuna mipango zaidi ya 60,000 katika Uingereza pekee, yenye kuhusisha nyumba 750,000,” lataarifu jarida Security Focus. “Uhalifu ukiwa waongezeka, limekuwa jambo la kizamani majirani kutokuwa na uhusiano wa kirafiki,” akasema wakili mmoja wa bima katika Afrika.
Washiriki wa mipango ya kulinda ujirani huangaliana hali njema na kupelekea polisi ripoti juu ya utendaji wowote wenye shuku.a Lakini barua ya upashaji habari ilimweleza hivi mshiriki mmoja wa kikundi ambaye nyumba yake ilivunjwa: “La kusikitisha ni kwamba mpango huu si uhakikisho kamili wa kwamba wewe hutavunjiwa nyumba tena. Hakuna mpango wowote wa usalama uwezao kufanya dai hilo. . . . Ni lazima bado uhakikishe kwamba milango yako imetiwa kufuli, kwamba una king’ora cha kuzuia uvunjaji nyumba na kwamba umechukua tahadhari za usalama za kadiri ifaayo.”
Ingawa mipango ya kulinda ujirani imekuwa na matokeo fulani, ni jambo la kutilika shaka kama yaweza kupunguza kadiri ya uhalifu wa jumla. “Mipunguo ya uhalifu ambayo hudaiwa kutukia katika eneo dogo huwa ni ‘mafanikio’ ikiwa tu ni uhalifu kidogo au hakuna wowote ‘unaohamia’ maeneo jirani,” aeleza Shapland na Vagg katika Policing by the Public. Hivyo, katika majiji fulani ambako vikundi vya kulinda ujirani vimeripoti mafanikio ya kutokeza, kumekuwako ongezeko kubwa ajabu la uhalifu katika maeneo mengine ya majiji hayo hayo ambako ni vigumu kutengeneza mipango ya jinsi hiyo.
“Kuna maeneo fulani ambako kulinda ujirani hakufanikiwi kadiri hiyo,” akiri sekretari wa mpango wa nchini pote unaohusisha washiriki zaidi ya 20,000. Mwanamke huyo alikuwa akirejezea viwanja vikubwa “nje ya mji ambako majirani hawawezi kuonana na ambako doria haifanyi kazi.” Kwa kielelezo, mume na mke walihama kutoka jiji moja la Kiamerika kwenda kwenye kiwanja cha hektari 20 karibu na kijiji kidogo. Mnamo miaka michache, nyumba ilivunjwa ikaingiwa mara mbili. Mke alitamka hisia za wakaaji wengi wa mashambani: “Mimi hujaribu kukaa bila wasiwasi kama kawaida, lakini naogopa. . . . Sihisi kamwe nikiwa salama.” Katika nchi zenye kukumbwa na hitilafiano la kisiasa, wakaaji wa mashambani hukabili jeuri ya ziada na mara nyingi hubanwa waunge mkono upande fulani.
Si ajabu kwamba wengi hutamani sana ‘siku zile nzuri za zamani.’ “Karibu na mwanzo wa karne hii,” chataarifu kitabu The Growth of Crime, “kulikuwako . . . imani ya ujumla kwamba [uhalifu] ungekuwa wa hali ya upungufu zaidi.” Lakini badala ya hivyo ikawaje? Watungaji Sir Leon Radzinowicz na Joan King waeleza hivi: “Katika miaka ishirini ya kwanza ya karne hii, hata wakati wa vita ya ulimwengu ya kwanza, kadiri za uhalifu zilibaki bila kubadilika sana, zikilingana na idadi ya watu. Wakati wa ule mshuko wa thamani ya pesa baada ya vita ndipo elekeo la mfululizo lilipoonekana wazi. Muda wote wa miaka ya msukosuko wa kiuchumi, ukosefu wa kazi na vita kubwa nyingine, [uhalifu] ulipiga hatua bila kuzuilika . . . Jambo moja uonalo moja kwa moja utazamapo uhalifu ulimwenguni ni ongezeko lenye kuenea na kufuliza kila mahali.”
Ingawa huku “kuongezeka kwa kutokutii sheria” hakukutarajiwa na wengi, kwa kweli kulitabiriwa. Maafa makubwa ambayo yamekumba ainabinadamu tangu mwanzo wa vita ya ulimwengu ya kwanza katika 1914 yalionyeshwa zamani katika Biblia. Yesu alitabiri kwamba mfumo mbovu wa mwanadamu ulikuwa ukikaribia mwisho: “Taifa litainuka dhidi ya taifa na ufalme dhidi ya ufalme, na kutakuwako upungufu wa chakula na matetemeko ya dunia mahali hapa na mahali hapa. Na kwa sababu ya kuongezeka kwa kutokutii sheria upendo wa hesabu iliyo kubwa zaidi utapoa.”—Mathayo 24:3, 7, 12, NW; ona pia Luka 21:10, 11.
“Mambo hayo yaanzapo kutokea,” Yesu akaongezea, “changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia.” Hivyo, wewe una sababu ya kutazamia mazuri. Utafutaji wa mwanadamu wa usalama wa duniani pote uko karibu kutoshelezwa.—Luka 21:28-32.
[Maelezo ya Chini]
a Waombwapo wawe washiriki wa doria za ulinzi, Wakristo hupendezwa kufuata mwongozo wa kanuni zilizo kwenye Isaya 2:2-4 na Yohana 17:16.—Ona Mnara wa Mlinzi, Desemba 15, 1983, kurasa 16-19.