Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w90 9/15 kur. 30-31
  • Sababu Réunion Ina Majumba ya Ufalme Mengi Sana

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Sababu Réunion Ina Majumba ya Ufalme Mengi Sana
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
  • Vichwa vidogo
  • Kwa Nini Kuna Majumba ya Ufalme Mengi Sana?
  • Vipingamizi Vyashindwa
  • Sifa Yamwendea Yehova
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
w90 9/15 kur. 30-31

Sababu Réunion Ina Majumba ya Ufalme Mengi Sana

KARIBU kilometa 640 mashariki ya Madagascar, kisiwa kidogo cha Réunion huinuka kwa ghafula kutoka kwenye ile Bahari Kuu ya Hindi. Ingawa kina urefu wa kilometa karibu 60 kwa upana wa kilometa 50 tu, kisiwa hicho chajulikana kwa makuba ya kivolkeno na mionyesho ya kutoa-toa moto pindi kwa pindi. Kilele kilicho na kimo cha juu zaidi, kwenye meta 3,069 juu ya usawa wa bahari, ni ile volkeno Piton des Neiges (Kilele cha Matheluji) iliyokwisha nguvu zamani. Katika sehemu ya kusini-mashariki ya kisiwa hiki ipo ile volkeno yenye kimo cha meta 2,625 iliyo na utendaji wa kulipusha moto ambayo kwa kufaa ilipewa jina Piton de la Fournaise (Kilele cha Tanuri). Lo, huwa ni tamasha iliyoje wakati ilipukapo usiku! Barabara nyingi hujipinda-pinda kwa kupanda na kuteremka miinuko yenye magenge, zikiandaa miono yenye kufunga pumzi kwa mshangao wa kuona ule ambao umeitwa upendezi wa kuogofya sana wa Réunion.

Kwa Nini Kuna Majumba ya Ufalme Mengi Sana?

Hata hivyo, upendezi wa kweli wa Réunion umo katika njia ambayo wanakisiwa wengi huziitikia ‘habari njema za ufalme’ ambazo hupigiwa mbiu na Mashahidi wa Yehova. (Mathayo 24:14, NW) Kazi yao ya kuhubiri ilianza katika 1960, wakati wahudumu wawili wa wakati wote walipowasili kutoka Ufaransa. Sasa, miaka 30 baadaye, Mashahidi 1,665 ni wenye shughuli wakieneza ujumbe wa Ufalme miongoni mwa wale wakaaji 582,000—uwiano wa Shahidi 1 kwa kila watu 350 walio kisiwani.

Ukuzi wa jinsi hiyo umetaka ujenzi wa mahali pafaapo pa mikutano ili Mashahidi waweze kuendesha ibada yao na elimu ya kiroho. (Waebrania 10:24, 25) Tayari, 13 kati ya makundi 19 ya Réunion yamejenga Majumba ya Ufalme yao wenyewe. Kwa sababu ya tufani zitokeazo mara nyingi katika eneo hilo, haya ni majengo madhubuti ya mawe ambayo hutaka wakati mwingi sana—na gharama—kuyajenga. Kwa hiyo imewezekanaje kujenga majumba ya jinsi hiyo, madhali Mashahidi walio wengi katika kisiwa hiki hupata mishahara ya wastani na wana familia kubwa za kuruzuku? Kwa kutumia maneno ya Biblia, jibu ni kwamba ‘mkono wa Yehova si mfupi.’—Isaya 59:1, NW.

Vipingamizi Vyashindwa

Kwa kielelezo, fikiria jinsi Yehova alivyosukuma mioyo ya watu kusaidia ujenzi wa Jumba la Ufalme katika mji mdogo wa Saint Louis, ulio katika sehemu ya kusini-magharibi ya Réunion. Ramani za ujenzi zilipokubaliwa kwanza, Shahidi kijana alimwambia mwalimu wake wa somo la ujenzi wa mawe kwamba Jumba la Ufalme lingejengwa na wafanya kazi wa kujitolea. Si kwamba tu mwalimu alijitolea huduma zake mwenyewe bali pia alileta darasa lake lote kwenye ujenzi ili kusaidia kuchimba msingi. Baadaye, alisaidia kwa upaji wa vyuma vilivyohitajiwa kwa msingi.

Wakati wajitoleaji zaidi ya mia moja walipokusanyika pamoja wakati wa sikukuu moja ya watu wote ili kuweka zege juu ya eneo la meta karibu 190 za mraba, walishangaa kupata kwamba mji ulikuwa umefunga mifereji ya maji. Wangewezaje kutayarisha zege bila maji? Mmoja wa wafanya kazi aliyemjua mkuu wa idara ya moto aliamua kwamba angemweleza mwanamume huyo mwenye fadhili juu ya shida hiyo. Kitambo kidogo baadaye, lori la kuzima moto liliwasili kwenye ujenzi. Gari hilo lilikuwa na maji ya kuutosha mradi huo, na idara ya moto libaki hapo kwa siku nzima! Yaeleweka wazi kwamba wafanya kazi wote wa kujitolea waliguswa hisia ili watie moyo wao wote katika kazi hiyo.

Msaada wa Yehova ulionekana wazi katika njia ambayo vipingamizi vingine vilishindwa. Kwa kielelezo, kwenye hatua moja ya ujenzi, dari ilikuwa tayari kuwekewa taa 22 maalumu zilizokuwa zimeagizwa miezi minane mapema. Lakini kampuni hiyo ikawaarifu akina ndugu kwamba aina waliyotaka ilikuwa imekwisha acha kutengenezwa. Ni jambo gani lingeweza kufanywa? Je! ingekuwa lazima mwundo mzima na dari vibadilishwe? Sivyo, kwa maana katika wakati ufaao kabisa, akina ndugu walipata habari juu ya mwanakandarasi wa eneo hilo aliyekuwa na taa kama hizo kwa ajili ya mradi ambao haukufanyika.

“Una ngapi?” akaulizwa.

“Karibu 25,” yeye akajibu.

Bila kukawia tena, taa zilinunuliwa zikawekwa.

Mradi ulipoendelea mbele, mtu mmoja aliyekuwa ndipo tu ameanza kujifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova alivutiwa kwa kina kirefu na jengo zuri hilo.

“Niambieni,” yeye akauliza, “kuna chochote kingine mwahitaji?”

“Ndiyo,” ndugu mmoja akajibu. “Twahitaji vifaa vya kukuza sauti.”

Basi, mtu huyu aliyependezwa karibuni akatoa kitabu chake cha cheki na kutoa upaji uliokaribia kutosha kwa mfumo mpya kabisa wa vifaa vya kukuza sauti. Michango ya jinsi hiyo, pamoja na mkopo wa ukarimu kutoka makao makuu ya Watch Tower Society katika United States, ililisaidia kundi kumaliza hili Jumba la Ufalme lililo zuri.

Kuongezea uzuri wa yote hayo, Kundi la Saint-Louis lilifurahi sana kuwa na Ndugu  Carey W. Barber, mshiriki wa Baraza Linaloongoza la Mashahidi wa Yehova, kuja kuweka wakfu Jumba la Ufalme katika Desemba 1988. Ndugu Barber aliratibiwa aje kutoka makao makuu ya Sosaiti katika Brooklyn, New York, ili aweke wakfu tawi jipya katika kisiwa jirani cha Mauritius. Akina ndugu katika Saint-Louis waliposikia hilo, katika muda wa majuma matatu tu, walichanga pesa za kutosha kumlipia yeye na mshiriki wa Halmashauri ya Tawi la Mauritius nauli ya ndege ili wasafiri kutoka Mauritius hadi Réunion. Kwa sababu ya ukuzi tangu wakati huo, Kundi la St.-Louis limelazimika kugawanyika. Sasa, makundi mawili hushirikiana utumizi wa hilo Jumba la Ufalme jipya.

Sifa Yamwendea Yehova

Namna gani makundi yale mengine katika Réunion? Kwa sababu ya itikio zuri kwa kazi ya kuhubiri Ufalme, hudhurio la mikutano kwenye Majumba ya Ufalme limekuwa kuanzia asilimia 150 hadi 200 ya hesabu ya Mashahidi wa Yehova walio kisiwani. Kwa hiyo ni wazi ni kwa nini Majumba ya Ufalme mengi yahitajiwa katika Réunion. Kwa uhakika, matatu zaidi yamejengwa tangu lile moja lililo katika Saint-Louis, na hiyo imeleta hesabu ya jumla kuwa 13 kwa ajili ya yale makundi 19 yaliyo kisiwani.

Kwa yote hayo, sifa yamwendea Yehova, aliyetabiri hivi: “Mdogo atakuwa elfu, na mnyonge atakuwa taifa hodari; mimi, BWANA [Yehova, NW], nitayahimiza hayo wakati wake.” (Isaya 60:22) Kama ilivyo katika sehemu nyingine za dunia, unabii huo umetimia juu ya kisiwa hiki chenye upendezi.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki