Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w90 10/15 kur. 22-25
  • “Kusimama Imara Kama Kundi Moja la Kondoo” Katika Chad

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • “Kusimama Imara Kama Kundi Moja la Kondoo” Katika Chad
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
  • Vichwa vidogo
  • Katika N’Djamena
  • Katika Barabara ya Kwenda Pala
  • Kile Kikundi Chenye Bidii Huko Kélo
  • Koumra, Doba, na Bongor
  • Wenye Mwungamano Ingawa Wako Mbali
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
w90 10/15 kur. 22-25

“Kusimama Imara Kama Kundi Moja la Kondoo” Katika Chad

Kama Wakristo wenzao kuzunguka ulimwengu, Mashahidi wa Yehova katika Chad wathamini makusanyiko ya kila mwaka ambayo hupangwa ili wajengwe kiroho. Huu ni usimulizi wa safari moja ya kwenda kwenye mfululizo wa siku za pekee za kusanyiko zilizofanywa katika sehemu ya kusini ya nchi hii ya Afrika ya kati, iliyobanika katikati ya bara.

Kwa sababu ya umbali na magumu ya usafiri, kwa kawaida makusanyiko katika Chad hufanywa katika vikundi vidogo, wakati wayo ukiamuliwa na hali ya hewa. Kuanzia Juni hadi Septemba, msimu wa mvua hufanya usafiri uwe mgumu na usiwezekane katika maeneo fulani. Siku za kusanyiko la pekee hufanywa baada ya zile mvua nzito kupita. Sikukuu za mwisho wa mwaka hufaa kwa mkusanyiko wa wilaya ulio mkubwa zaidi. Na kabla mvua hazijaanza tena katika Juni, yale makusanyiko ya mzunguko ya siku mbili hufanywa.

ILIKUWA alasiri ya Jumapili yenye joto la kunatisha jasho mwilini. Jumba la Ufalme huko N’Djamena, mji mkuu wa Chad, lilijaa watu 184. Kujapokuwa na joto, wao walikuwa wakiisikiliza kwa makini hotuba iliyo kuu, “Kusimama Imara Kama Kundi Moja la Kondoo.” Asubuhi hiyo walifurahi kushuhudia watu watatu wakifananisha wakfu wao kwa Yehova Mungu kwa ubatizo wa maji. Hili lilikuwa la kwanza la makusanyiko ya pekee sita ambayo mwangalizi mwenye kusafiri wa huko na mimi tulipendelewa kutumikia.

Kichwa cha mfululizo huo, “Kusimama Imara kama Kundi Moja la Kondoo,” kilithaminiwa kihususa na wale Mashahidi 267 katika Chad. Wao huishi mbali na Wakristo wenzao katika mabara mengine. Na bado, kupokea kwao chakula kile kile cha kiroho na kutunzwa kwa njia ile ile huwatia moyo waendelee kufanya kazi kwa mwungamano pamoja na ndugu zao ulimwenguni pote. Shauri lenye mafaa la programu hii liliwaimarisha pia wasimame imara dhidi ya uvutano wenye hila wa ulimwengu wa Shetani na pepo za mnyanyaso au upinzani.

Katika N’Djamena

Kundi la kwanza la Mashahidi wa Yehova katika Chad lilifanyizwa katika N’Djamena katika 1964. Sasa lina wahubiri zaidi ya 90 wa habari njema za Ufalme. Ilikuwa furaha kutazama nje kwenye hadhirina na kuona wengi ambao wamekuwa wakitumikia kwa uaminifu tangu siku za mapema za kazi katika Chad. Ndugu mmoja alikuwa na wake watatu alipojifunza kwanza juu ya ukweli wa Biblia. Muda si muda akauona uhitaji wa kupatanisha maisha yake na viwango vya Biblia. Alifunga ndoa kisheria na mke wake wa kwanza na kujitenga na wale wengine, ingawa alifanya mipango ya kuwatunza. Alibatizwa katika 1973 na amekuwa mtendaji katika kazi tangu wakati huo.

Mzee mmoja aliyeshiriki katika programu alikuwa amepita chini ya mtihani mkali wa imani. Katika 1975 serikali ya wakati huo ilishurutisha kushiriki katika desturi fulani zenye msingi wa ibada ya wafu; mtu yeyote asiyezifuata angeweza kuuawa. Ndugu huyo aliposimama imara asiridhiane imani yake, wenye mamlaka walianza kumtafuta. Ni badiliko tu katika serikali wakati huo wa maana lililomponyosha.

Katika Barabara ya Kwenda Pala

Baada ya N’Djamena, safari ya kwenda kusini kutumikia makusanyiko matano yaliyobaki ilianza. Tulikuwa tumeifuata njia hiyo mara nyingi lakini katika msimu wa ukavu tu. Sasa, mwishoni-mwishoni mwa Septemba kwenye umalizio wa msimu wa mvua, kila kitu kilikuwa cha kijani-kibichi na kusitawi sana. Ulikuwa wakati wa kuonewa shangwe kusafiri. Tulipita shamba baada ya shamba la mtama. Masuke juu ya yale mabua marefu yenye kufuliza kando ya barabara yalikuwa sasa yakiiva. Muda si muda yangevunwa, yakaushwe, na kuwekwa akibani katika ghala za ardhi zenye umbo la pia zilizotapakaa mashambani. Mtama ndicho chakula kikuu kwa Wachad walio wengi. Hutwangwa katika kinu kikubwa cha mti kwa mchi ambao mara nyingi huwa na kimo cha kumzidi mwenye kuutumia. Halafu unga ule huchanganywa na maji yanayochemka na kufinyangwa kuwa donge la kuliwa pamoja na mchuzi utayarishwao kwa okra au karanga.

Tuliona mashamba mengi zaidi na zaidi ya pamba tuliposafiri mbali zaidi kusini. Kwa sababu ardhi ni tambarare katika sehemu hii ya nchi, mashamba yenye kuchanua yalionekana kana kwamba yafika kwenye upeo wa macho. Muda si muda familia nzima-nzima zingekuwa nje katika mashamba zikichuma pamba kwa mkono. Pamba ndilo zao kubwa zaidi la uchumi katika Chad, kukiwa na tani 133,000 zenye kuvunjwa katika 1988. Kufikia jioni, tulikuwa tukipita Ziwa Léré. Hapa nchi ina vilima-vilima na yavutia sana, hususa wakati huu wa mwaka. Kwa kuwa huko wakati ufaao kabisa, tuliweza kununua samaki-kapi aliyekaangwa pale pale kando ya barabara. Ulikuwa mlo ambao mkaribishaji-wageni yeyote angeona fahari kuupakua.

Jambo moja lifanyalo usafiri uwe mgumu zaidi msimu huu ni kwamba kukinyesha, vipingamizi huwekwa barabarani kuzuia mtiririko wa magari. Kwa nini? Ili kuzihifadhi barabara. Kwa hiyo mioyo yetu ilishuka tulipoona anga kule mbele ikigeuka ghafula kuwa nyeusi tititi. Kwa uhakika hatukupendezwa kupiga kambi kwenye mvua kando ya baraba-ra. Lakini la maana zaidi, tungechelewa kwenye siku ifuatayo ya kusanyiko la pekee. Kwa kufurahisha, sehemu iliyo nzito zaidi ya mvua hii iliyochelewa haikugonga barabarani. Hata ingawa tulilazimika kungoja kwa muda kwenye vipingamizi kadhaa, baadaye sana usiku huo tuliwasili salama salimini katika Pala, mji wenye watu karibu 32,000. Lo, ni mazuri yaliyoje yaliyotungojea! Ile anga isiyo na mwezi baada ya mvua ilitupa sisi mwono wa kutazamisha wa nyota na wa lile fungu la nyota za Njia ya Kimaziwa, mwono wa kuvutisha pumzi ambao wanamajiji walio wengi hawapati kamwe kuuona. Hiyo ilitukumbusha sababu ya sisi kusimama imara—kumheshimu Muumba Mwadhamu wa ulimwengu wote mzima ulio wa ajabu.

Makundi madogo mawili na kikundi kilicho peke yacho yalikusanyika huko Pala. Ndugu vijana watatu walikuwa wametembea zaidi ya kilometa 100 kuja kwenye kusanyiko hili. Kwa kuwa makusanyiko kusini ni madogo na kuna wazee wachache, sehemu za programu zilirekodiwa kwenye kusanyiko katika N’Djamena na kufunguliwa zisikilizwe upya. Hiyo yahakikishia programu ya hali ya juu hata kukiwa na idadi ndogo katika hudhurio. Tulifurahi kuwa na mtaka-ubatizo mmoja.

Kile Kikundi Chenye Bidii Huko Kélo

Halafu, kulikuwako safari fupi ya kwenda Kélo, ambako 194 walikuwapo kwa ajili ya programu Jumapili. Familia nyingi zenye watoto wachanga zilikuwa zimetembea zaidi ya kilometa 30 kuhudhuria. Watu wawili waliojiweka wakfu karibuni wangebatizwa. Wakati wa msimu wa ukavu, ubatizo huwa tatizo mara nyingi kusanyiko lisipofanywa karibu na mto; kwa sababu hiyo, watu kadhaa walilazimika kubatizwa katika pipa. Lakini kuwa kwetu huko mwishoni mwa ule msimu wa mvua kulirahisisha mambo. Hata hivyo, ilihitajiwa kabisa kuendesha gari kilometa zaidi ya 20 kufika mahali pafaapo.

Mmoja wa wataka-ubatizo alikuwa msichana mchanga ambaye imani yake ilikuwa imetahiniwa vikali. Familia yake ilikuwa imemwahidi kufunga ndoa na mwanamume asiyependezwa na kujifunza Biblia. Zaidi ya hilo, mwanamume huyo alipendelea kuungamanishwa kwa desturi za kikabila kuliko kwa ndoa ya kisheria. Kwa sababu mwanamume huyo alikuwa na nia ya kulipa mahari kubwa, familia yake ilimsonga sana. Hata alilazimika kuhamia mahali pengine kwa muda ili auepuke mwungano usio wa kimaandiko ambao familia yake ilitaka. Alisimama imara kupitia yote haya na akafanya maendeleo mazuri. Tangu ubatizo wake, upinzani wa familia umekoma. Twamshukuru Yehova kwamba tuna watu waaminifu jinsi hiyo miongoni mwetu.

Akina ndugu hapa wana sababu nyingine za kumshukuru Yehova. Chad ilipatwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe yenye uchungu mwingi halafu, katika 1984, njaa kali. Mzee wa huko akumbuka kwamba wakati mmoja wa njaa hiyo, alitazama kuzunguka Jumba la Ufalme akashangaa kama wowote wa waliopo wangekuwa hai bado baada ya miezi michache. Hata hivyo, tengenezo la Yehova liliandaa msaada kwa namna ya chakula, likipunguza shida yao. Uthamini wao kwa jambo hilo waonyeshwa sasa katika utumishi wao wa bidii. Kuna roho imara ya upainia katika Kélo. Wakati wa Oktoba 1989, zaidi ya theluthi moja ya wahubiri wa Ufalme walipanga mambo yao ili waweze kushiriki wakati wote katika kazi ya kuhubiri.

Waliyojionea kuhusiana na njaa hiyo yaliwafundisha kwamba ni lazima wao pia wawe wakarimu. Mwaka uliopita mzee mmoja katika kundi aligonjweka ghafula akafa. Aliacha familia yenye watoto tisa, aliye mchanga zaidi akiwa na umri wa miezi michache tu. Mke wake alikabili msongo wa familia ili kushiriki katika desturi za kuomboleza zilizohusisha ibada ya wafu. Akina ndugu walimpa tegemezo lililohitajiwa, hivi kwamba akaweza kukinza msongo mkali. Halafu kundi likafanya kazi pamoja kuwajengea nyumba yeye na watoto wale wachanga zaidi, kuongezea na kusaidia kwa vitu vya kimwili kwa njia nyingine mbalimbali. Hiyo ilitokeza ushahidi mzuri sana kwenye mji huo, ikionyesha tokeo lenye kufurahisha la Ukristo wenye matendo.—Matendo 20:35.

Koumra, Doba, na Bongor

Kituo chetu kilichofuata kilikuwa Koumra. Barabara za changarawe zilirahisisha sana ile safari ya kilometa 300. Njiani, tulipita katika jiji la Moundou, kitovu cha viwanda chenye watu zaidi ya mia moja elfu. Watu 71 walihudhuria katika Koumra. Ndugu kijana asiyekuwa amepata kamwe masomo rasmi ya shuleni alihutubu kutoka jukwaani. Alieleza jinsi programu ya kujifunza kusoma na kuandika iliyofunzwa kwenye Jumba la Ufalme ilivyomsaidia na kumpa uhakika uliohitajiwa. Sasa yeye huongoza mafunzo katika Biblia pamoja na watu wengine wanne.

Baada ya siku ya kusanyiko la pekee katika Koumra, tulirudi kuelekea N’Djamena, tukawe na kituo chetu kifuatacho kule Doba kwa ajili ya kusanyiko la tano katika mfululizo wetu. Baadhi ya wale wenye kuhudhuria walinaswa katika mvua iliyochelewa wakalazimika kukaa usiku kucha kando ya barabara. Na bado, kila mmoja aliwasili kwa wakati ufaao kwa ajili ya mwanzo wa programu kule Doba. Watu 51 walikuwapo, na mtu mmoja akajitoa kwa ubatizo.

Kituo cha mwisho kilikuwa katika Bongor. Hili ni eneo lenye kukuza mpunga, nasi tulistaajabu jinsi eneo lilivyokuwa tambarare. Hudhurio kule Bongor lilileta jumla ya wale walioisikia programu katika Chadi iwe 630. Na wawili zaidi walipozamishwa, jumla ya watu waliobatizwa ilikuwa tisa.

Kurudi kwetu N’Djamena kulimaliza safari ya kilometa karibu 1,200. Ilikuwa furaha kushirikiana na watumishi wa Mungu ambao wamesimama imara kwa miaka mingi, na pia kukutana na wapya wengi wanaofanya maendeleo ya ajabu. Bidii yao kwa ajili ya huduma ilitia moyo kihususa. Wakati wa Oktoba  1989, kulikuwa na kilele kipya cha wahubiri 267 katika Chad, ongezeko la asilimia 20 zaidi ya mwaka uliotangulia.

Wenye Mwungamano Ingawa Wako Mbali

Kusafiri kupitia nchini kulitufanya tuthamini ni wito wa ushindani kama nini kueneza habari njema katika bara ambako lugha zaidi ya 200 husemwa. Ingawa Kifaransa na Kiarabu ndizo lugha rasmi za Chad, kwenye kila moja ya siku za makusanyiko ya pekee, ilikuwa lazima programu itafsiriwe kutoka Kifaransa kuingiza katika lugha tofauti. Hata hivyo, wengi waliokuja mahali pa kusanyiko hawakusema lugha ya jimbo hilo, hivyo basi lilikuwa lingali ni tatizo kuwasaidia waielewe programu.

Katika mahali pote tulipozuru, ndugu na dada zetu walitutendea ukaribishaji-wageni. Kwa ujumla milo ilikuwa mtama au ugali wa unga-mchele na mchuzi wenye vikolezo uliotajwa mapema kidogo. Nyakati fulani msichana mchanga alileta chakula kikiwa juu sinia iliyofunikwa kitambaa cha rangi nyangavu. Sinia hiyo ilisawazishwa kwa uzuri juu ya kichwa chake, na ikawa lazima mtu avutiwe na mwendo wake wa madaha mema.

Idadi ya wakaaji wa Chad ya kaskazini ni Waislamu hasa; sana-sana watu kusini ni Wakatoliki, Waprotestanti, au waabudu-maumbile. Serikali huunga mkono sera ya uhuru wa dini, nasi tuna furaha kuweza kukutana pamoja kwa uhuru.

Programu ya siku ya kusanyiko la pekee ilisaidia kile kikosi kidogo cha Mashahidi katika Chad wathamini kwamba ingawa wao wako mbali kijiografia kutoka kwenye ndugu zao katika sehemu nyingine za ulimwengu, wameungamana nao kikweli katika kundi moja la kondoo. Hiyo iliwawezesha ‘kusimama imara katika roho moja’ japo misongo na upinzani uwapatao.—Wafilipi 1:27.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki