Wapiga Mbiu ya Ufalme Waripoti
Yehova Aandaa Msaada
JUZIJUZI, Mashahidi wa Yehova katika Afrika Kusini walipokea habari juu ya hali mbaya mno ya ndugu zao wa kiroho katika nchi iliyo karibu ambapo kazi yao ya kuhubiri imepigwa marufuku. Iliripotiwa kwao kwamba kwa sababu ya ukavu mkali, ndugu zao walikuwa wakiendelea kuishi kwa kula mizizi fulani. Pia walikosa nguo zenye kufaa, jambo ambalo liliwafanya Mashahidi wengine wasitake kushiriki katika huduma ya shambani.
Mara moja ndugu katika Afrika Kusini waliitikia. Mwito ulitolewa kwenye makundi ya eneo la Johannesburg juu ya uhitaji wa nguo. Haipati siku nyingi, tani 3 za nguo zilikuwa zimechangwa. Vitu hivyo kisha vikapangwa na wafanya kazi wenye kujitoa. Mipango ikafanywa kupeleka tani 3 za maharagwe, tani 1 ya mafuta, tani 1 ya sabuni, na tani 17 za unga wa mahindi. Kampuni iliyotoa unga wa mahindi iliposikia juu ya hali mbaya ya Mashahidi katika bara lililopatwa na hali ya ukavu, ilichanga zaidi ya tani moja ya chakula hicho kilichohitajika sana.
Siku ya Jumatatu, Aprili 16, 1990, lori yenye mzigo wa tani 25 ya maandalizi ya kusaidia iliondoka Afrika Kusini kwenda safari ndefu ya kilometa 5,500. Lakini sasa ruhusa kutoka kwa mamlaka ilihitajiwa ili kupeleka maandalizi hayo kupitia nchi yao yenye vita.
Mamlaka kwenye nyumba ya balozi walisema kwamba ingawa Mashahidi wa Yehova hawakukubaliwa katika nchi yao, walijua vizuri kwamba walikuwa huko. Hakungekuwa katazo lolote la kupeleka maandalizi kwa ndugu zetu. Ruhusa ilitolewa. Hati zilizohitajiwa zilitolewa, na siku ya Ijumaa, Aprili 20, Mashahidi walivuka mpaka bila tatizo lolote. Hata hivyo, walikabili vizuizi-barabara 30, ambapo mara nyingi walihitajiwa kuonyesha hati zao. Ni hapo walipong’amua jinsi hati hizo zilikuwa za lazima.
Baada ya wao kusafiri kilometa 140 katika nchi hiyo, kuendelea kwao kulizuiwa na mto mkubwa ulioghariki. Daraja la kwanza lilikuwa limeharibiwa, na lile la muundo wa muda lililokuwa limewekwa mahali palo halikufaa kutumiwa na lori kubwa. Hata hivyo, walipata kwamba gari dogo lililofuata msafara huo lingeweza kuvuka salama daraja lililojaa maji. Iliamuliwa wagawanyike wawe vikundi viwili. Kambi ilifanywa kwenye mto uliojaa maji kwa kikundi kimoja, huku kikundi kile kingine kikiendelea njiani kukutana na ndugu kilometa 260 hivi mbele zaidi kaskazini. Walifurahi jinsi gani kukutana hatimaye na akina ndugu! Hawakuweza kuacha kutabasamu, kukumbatiana, na kusalimiana kwa mikono. Upesi lori za mahali hapo zilikuwa njiani kukutana na kikundi kile kingine cha akina ndugu waliokuwa wakingojea kwenye mto. Hapo, misaada ilihamishwa kutoka lori hiyo kubwa kwenye zile ndogo mbili.
Ripoti ambazo zimepokewa zinaonyesha shukrani yenye kina kirefu kwa uandalizi wa Yehova wa msaada wa kimwili. Hata hivyo, ijapokuwa hali yao mbaya ya kimwili, kilio cha akina ndugu kwa ajili ya chakula cha kiroho kilikuwa kikubwa hata zaidi. Kundi moja lilikuwa na Mnara wa Mlinzi mmoja tu, ambao ulipasa kunakiliwa kwa ajili ya kila familia. Shukrani ni kwa Yehova, mipango inaendelea sasa ili kuandaa mtiririko thabiti wa chakula cha kiroho kwa ndugu katika nchi hiyo.y