Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w93 8/15 kur. 3-4
  • Kifungo cha Ndoa Kinachodhoofika

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kifungo cha Ndoa Kinachodhoofika
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
  • Habari Zinazolingana
  • Talaka Matokeo Yayo Mabaya
    Amkeni!—1992
  • Ndoa-Sababu Inayofanya Wengi Waivunje
    Amkeni!—1993
  • Talaka Biblia Inasema Nini Hasa?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1988
  • Ongezeko Kuu la Talaka
    Amkeni!—1992
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
w93 8/15 kur. 3-4

Kifungo cha Ndoa Kinachodhoofika

Mama mchanga alimkumbatia mtoto wake mchanga wa miezi miwili. Kisha, kwa kicha cha ghafula, akamwangusha chini. Mvulana huyo alikufa muda wa saa chache baadaye. “Nilimwangusha kimakusudi,” mama huyo akasema, “kwa sababu mume wangu hajali familia yake.” Badala ya kuongea jambo hilo pamoja na mume wake, alitoa hasira yake kwa yule mtoto mchanga asiye na hatia.

Akina mama wachache huchagua hatua hiyo yenye kupita kiasi, lakini wengi hushiriki hisia zake. Inazidi kuwa vigumu kwa waume na wake kufanikiwa katika ndoa yao. “Uwezekano wa kufanikiwa katika ndoa unapokuwa wa kiwango cha chini jinsi ulivyo katika United States leo,” lasema jarida Journal of Marriage and the Family, “kujifunga kwa nguvu, na kikamili katika wajibu wa ndoa . . . kunakuwa jambo la hatari sana hivi kwamba hakuna yeyote mwenye akili kamili ambaye angefanya hivyo.”

Katika nyakati hizi zenye msukosuko, ukosefu wa adili, kutopatana, madeni, kuzozana na wakwe, na ubinafsi hayo yote huchochea ugomvi wa nyumbani, ambao mara nyingi huongezeka kufikia hatua ya talaka. Hali ni mbaya sana katika Japani hivi kwamba hata Kanisa Katoliki, linalojulikana sana kwa msimamo walo thabiti dhidi ya talaka, limelazimika kufanyiza halmashauri ya pekee ili kuondoa ubaguzi dhidi ya washiriki waliotaliki na kufunga ndoa upya. Idadi yenye kuongezeka ya wahudhuriaji kanisa inaathiriwa na matatizo yanayohusiana na talaka.

Hata hivyo, idadi ya talaka hufunua sehemu ndogo tu ya tatizo lililo kubwa zaidi. Utafiti katika United States waonyesha kwamba ni kule kuzorota kwa ubora wa maisha ya ndoa yenyewe kunakosababisha ongezeko la talaka, kuliko tu ile mielekeo ya kijamii inayofanya talaka iwe rahisi zaidi. Kukiwa na juhudi kidogo zaidi na kutojifunga sana katika wajibu, maisha ya ndoa hukosa uvutio wayo. Wengi hudumisha sura ya kijuujuu tu ya kuwa mume na mke, lakini wananyimana haki za ndoa, na wanaongea pamoja mara chache sana. Wengine wanahisi kama vile mwanamke mmoja wa Mashariki aliyejinunulia kaburi lake mwenyewe, akisema, ‘Sitaki kuwa na mume wangu kaburini.’ Kwa kuwa hawezi kumtaliki mume wake sasa, anakusudia kumtaliki baada ya kifo. Kwa huzuni, ingawa watu kama hao hawajatalikana, maisha ya ndoa si chanzo cha furaha kwao.

Ndivyo ilivyokuwa na Isao. Alikuwa amemwoa mke wake kwa ajili ya msisimuko tu, kwa hiyo hakuhisi msukumo wa kubadili njia yake ya maisha yenye ubinafsi. Ingawa alikuwa na mshahara mzuri akiwa dereva wa malori ya kwenda safari za mbali, alitumia vibaya machumo yake yote kwa kula na kunywa, bila kuitunza familia yake. Likiwa tokeo, aligombana na mke wake daima. “Wakati wowote mambo yasipoenda vizuri kwangu,” akumbuka Isao, “ningeenda nyumbani na kuionyesha familia yangu kasirani yangu.” Kama vile volkeno yenye kulipuka daima, habari juu ya talaka ilitokea kila siku.

Wanaume na wanawake wengi wanavumilia ndoa mbaya. Watalikane, wasitalikane, hawapati furaha. Je! kuna njia ambayo wanaweza kufanikiwa katika ndoa yao? Ni nini liwezalo kufanywa ili kuimarisha kifungo chao cha ndoa?

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki