Mashariki Ikutanapo na Magharibi
“OH, MASHARIKI ni Mashariki, na Magharibi ni Magharibi, na hizo mbili hazitapata kamwe kukutana.” Maneno hayo ya mtunga-shairi Mwingereza Rudyard Kipling yatukumbusha juu ya zile tofauti kubwa sana za kitamaduni ambazo huigawanya ainabinadamu, ambazo huchangia zile chuki za kikabila, kirangi, na za kitaifa zinazolipuka kotekote kutuzunguka leo. Wengi huuliza hivi, Je! Mungu hawezi kufanya jambo fulani kuhusu hali hiyo? Ndiyo, yeye aweza! Na hata sasa anafanya jambo fulani! Mstari ufuatao wa shairi la Kipling ulirejezea hilo. Mashariki na Magharibi zingekuwa zimegawanyika kwa muda gani? Mshairi huyo alisema: “Hadi Dunia na Mbingu zisimamapo hivi karibuni kwenye Kiti cha Hukumu kikubwa cha Mungu.”
Mungu amemkabidhi Mwanae Yesu Kristo, daraka la kuhukumu. (Yohana 5:22-24, 30) Lakini kipindi hicho cha kuhukumu chaanza wakati gani? Ni nani wanaohukumiwa, na tokeo likiwa nini? Ni Yesu aliyeeleza katika unabii juu ya vita vya ulimwengu na misononeko ambayo ingefuata na iliyoanza kuipata ainabinadamu katika mwaka wa 1914. Alisema kwamba hiyo yatia alama “ishara” ya “kuwapo [kwake kusikoonekana] na ya umalizio wa mfumo wa mambo.”—Mathayo 24:3-8, New World Translation.
Kwenye upeo wa unabii huo mkuu, Yesu atambulisha wakati wetu uliopo kuwa wa hukumu, akisema hivi juu yake mwenyewe: “Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake; na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi; atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto.” Kitamathali, watu wote wa dunia wamekusanyika sasa mbele ya Hakimu na wana wajibu wa kutoa hesabu kwa njia wanayoitikia ujumbe wake wa wokovu. Hukumu inapotekelezwa hivi karibuni katika ile dhiki kuu, watu wasiotii walio mfano wa mbuzi “watakwenda zao kuingia katika adhabu ya [kukatiliwa mbali kwa, NW] milele, bali wenye haki [wale watiifu walio mfano wa kondoo] watakwenda katika uzima wa milele.”—Mathayo 25:31-33, 46; Ufunuo 16:14-16.
‘Kutoka Mashariki na Kutoka Magharibi’
Kwa kweli hukumu ya ulimwengu huu ilianza katika ile miaka yenye msukosuko ya Vita ya Ulimwengu 1. Wakati huo, makasisi wa Jumuiya ya Wakristo walitegemeza kwa moyo wote pande zilizokuwa zikipigana. Hilo liliwatambulisha kuwa sehemu ya ulimwengu huu mfisadi unaostahili “ghadhabu ya Mungu.” (Yohana 3:36) Lakini namna gani wale Wakristo wapendao amani waliozoea imani katika Mungu? Kuanzia mwaka wa 1919, hao walianza kukusanywa kwenye upande wa Mfalme, Kristo Yesu.
Wametoka pande zote za dunia, kwanza mabaki ya wale wapakwa 144,000, walioteuliwa muda wote wa karne za enzi ya Ukristo. Hao watakuwa “warithio pamoja na Kristo” katika Ufalme wake wa kimbingu. (Warumi 8:17) Nabii wa Mungu awaambia hao hivi: “Usiogope; maana mimi ni pamoja nawe; nitaleta wazao wako toka mashariki, nitakukusanya toka magharibi; nitaiambia kaskazi, Toa; nayo kusi, Usizuie; waleteni wana wangu kutoka mbali, na binti zangu kutoka miisho ya dunia. Kila mmoja aliyeitwa kwa jina langu, niliyemwumba kwa ajili ya utukufu wangu; mimi nimemwumba, naam, mimi nimemfanya.”—Isaya 43:5-7.
Lakini si hayo tu! Hasa tangu miaka ya 1930, umati mkubwa, unaojumlika sasa kuwa mamilioni, ulianza kukusanywa. Hao ndio “kondoo” ambao Yesu alirejezea kwenye Mathayo 25:31-46. Kama vile mabaki wapakwa waliowatangulia, hao wanakuwa na “imani” katika Yule atangazaye hivi: ‘Ninyi ni mashahidi wangu, nami ni Mungu.’ (Isaya 43:10-12) Kukusanywa kwa umati huo mkubwa kunaendelea pia ‘kutoka mashariki na magharibi, kutoka kaskazini na kusini, na kutoka miisho ya dunia.’
Kondoo hao wapendao amani wanaunganishwa imara katika udugu wa kimataifa. Wao husema zile lugha nyingi sana tofauti-tofauti za mabara 231 wanakoishi. Lakini wameunganika kiroho katika kujifunza “lugha iliyo safi” ya ujumbe wa Biblia juu ya Ufalme, “wapate kuliitia jina la BWANA [Yehova, NW], wamtumikie kwa nia moja.” (Sefania 3:9) Kuunganika kwao kwa imani, kusudi, na tendo huandaa ushuhuda mzuri ajabu kwamba kwa kweli Mashariki imekutana na Magharibi, na watu kutoka pande nyinginezo zote, kwa utumishi na sifa ya Bwana Mwenye Enzi Kuu Yehova.
Katika mabara mengine kukusanya huko kunatukia chini ya hali za ajabu, kama vile ripoti zifuatazo zitakavyoonyesha.