Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w94 8/1 kur. 2-5
  • Tisho la Nyukilia—Je! Limekwisha Hatimaye?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Tisho la Nyukilia—Je! Limekwisha Hatimaye?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Hatari za Kuongezeka kwa Nyukilia
  • Mabomu ya Kuuzwa
  • ‘Mabomu ya Amani Yaliyokawia Kulipuka’ na “Hatari kwa Uhai”
  • Wazitupe Takataka Wapi?
  • Ni Nani Wanaosababisha Tisho la Vita vya Nyuklia?
    Amkeni!—2004
  • Tisho la Nyuklia Halijaisha
    Amkeni!—1999
  • Je, Tisho la Nyuklia Limekwisha?
    Amkeni!—1999
  • Bado Kuna Tisho la Vita vya Nyuklia?
    Amkeni!—2004
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
w94 8/1 kur. 2-5

Tisho la Nyukilia—Je! Limekwisha Hatimaye?

“AMANI Duniani yaonekana yawezekana sasa kuliko wakati mwingine wowote tangu Vita ya Ulimwengu 2.” Tazamio hilo zuri la mwandikaji mmoja wa gazeti mwishoni mwa miaka ya 1980 lilitegemea jambo la kwamba mapatano muhimu ya kupunguza silaha na mabadiliko makubwa ya kisiasa ambayo hayakutarajiwa hatimaye yalimaliza ile Vita Baridi. Lakini, je, tisho la nyukilia, lililojitokeza sana katika makabiliano baina ya yale mataifa yenye nguvu zaidi, lilikwisha pia? Je! amani na salama ya kudumu ingepatikana haraka wakati huo?

Hatari za Kuongezeka kwa Nyukilia

Wakati wa ile Vita Baridi, mataifa yenye nguvu zaidi yakitegemea silaha za nyukilia ili kudumisha amani, yalikubali kuruhusu usitawishaji wa ujuzi wa nyukilia kwa minajili ya amani lakini yadhibiti hesabu ya mataifa ambayo yangeweza kutengeneza silaha za nyukilia. Mnamo 1970 Mkataba wa Kutoongezeka kwa Mataifa Yenye Nyukilia ulianza kutumika; baadaye ulithibitishwa na mataifa yapatayo 140. Lakini, mataifa yenye uwezo wa kutengeneza nyukilia, kama Argentina, Brazili, India, na Israeli, yamekataa kutia sahihi mkataba huo mpaka leo hii.

Hata hivyo, mnamo 1985, taifa jingine lenye uwezo wa kutokeza nyukilia, Korea Kaskazini, liliutia sahihi. Kwa hiyo, lilipotangaza kujiondoa kwenye mkataba huo katika Machi 12, 1993, kwa wazi ulimwengu ukawa na wasiwasi. Gazeti la habari la Ujerumani Der Spiegel lilisema: “Tangazo la kujiondoa kutoka kwa Mkataba wa Kutoongezeka kwa Mataifa Yenye Nyukilia hutokeza mwendo fulani: Sasa kuna tisho kwamba kutakuwa na shindano la kutengeneza silaha za nyukilia, kuanzia Asia, liwezalo kuwa hatari zaidi ya lile shindano la kutengeneza bomu baina ya yale mataifa yenye nguvu zaidi.”

Utaifa ukiendelea kutokeza mataifa mapya kwa mwendo wa kasi sana, labda hesabu ya mataifa yenye nyukilia itaongezeka. (Ona sanduku.) Mwandikaji wa gazeti Charles Krauthammer aonya hivi: “Mwisho wa tisho la Sovieti halimaanishi mwisho wa hatari ya nyukilia. Hatari kubwa ni kuongezeka kwa mataifa yenye nyukilia, na ongezeko hilo ndipo tu limeanza.”

Mabomu ya Kuuzwa

Mataifa ambayo yanatazamia kuwa na nyukilia yanatamani kupata umashuhuri na uwezo ambao silaha hizo hutokeza. Yasemekana kwamba nchi moja imenunua angalau makombora mawili yenye nyukilia kutoka Kazakhstan. Nchi hiyo ambayo zamani ilikuwa jamhuri ya Sovieti imeorodhesha makombora hayo kuwa “yamepotea.”

Mnamo Oktoba 1992 watu kadhaa walikamatwa Frankfurt, Ujerumani, wakiwa na gramu 200 za sizi (aina ya kemikali) inayonururisha sana, inayotosha kutia sumu maji yote yaliyo katika jiji. Juma moja baadaye, watu saba wenye kufanya magendo walikamatwa Munich wakiwa na kilogramu 2.2 za urani. Kugunduliwa kwa vikundi viwili vyenye kufanya magendo kwa muda wa majuma mawili kulishtua sana maofisa, kwa kuwa ni visa vitano tu kama hivyo vilivyokuwa vimeripotiwa ulimwenguni pote kwa mwaka mzima uliokuwa umepita.

Haijulikani kama watu hao walinuia kuuza vitu hivyo kwa vikundi vya maharamia au kwa serikali mbalimbali. Hata hivyo, uwezekano wa uharamia wa kinyukilia waongezeka. Dakt. David Lowry wa Kituo cha Habari cha Ulaya cha Ongezeko la Nyukilia aeleza juu ya hatari hiyo: “Mharamia ahitaji tu kupeleka sampuli ya urani ya hali ya juu sana kwa wenye mamlaka mashuhuri wa kuichunguza, akisema kwamba tuna urani nyingi sana na huu ni uthibitisho. Ni kama mtekaji nyara apelekapo sikio la mtekwa nyara.”

‘Mabomu ya Amani Yaliyokawia Kulipuka’ na “Hatari kwa Uhai”

Mwaka wa 1992 ulipoanza, mitambo 420 ya nyukilia ilikuwa ikitumiwa kwa makusudi yenye amani ya kutoa umeme; mingine 76 ilikuwa ikitengenezwa. Lakini kwa miaka iliyopita, aksidenti zitokazo katika mitambo ya nyukilia zimetokeza ongezeko la magonjwa, kuharibika kwa mimba, na kuzaliwa kwa watoto wenye kasoro. Ripoti moja yasema kwamba kufikia 1967 aksidenti katika kiwanda kimoja cha plutoni (aina ya madini) katika Sovieti zilisababisha mtoko wa unururishi kwa kiwango cha mara tatu kuliko unururishi uliotoka katika ule msiba wa Chernobyl.

Bila shaka, ni aksidenti hii ya baadaye katika Chernobyl, Ukrainia, mnamo Aprili 1986 ndiyo iliyotangazwa zaidi katika vyombo vya habari. Grigori Medwedew, aliyekuwa naibu wa mhandisi-mkuu katika kiwanda cha Chernobyl katika miaka ya 1970, aeleza kwamba “tungamo kubwa sana la unururishi wenye kudumu muda mrefu” lililorushwa angani “walinganishwa na mabomu kumi ya Hiroshima kwa habari ya madhara ya baadaye.”

Katika kitabu chake Tschernobylskaja chronika, Medwedew aorodhesha aksidenti mbaya 11 katika mitambo ya nyukilia katika ule uliokuwa Muungano wa Sovieti kufikia miaka ya katikati ya 1980 na nyinginezo 12 katika Marekani. Aksidenti za Marekani zilitia ndani moja yenye kushtua sana mnamo 1979 katika Three Mile Island. Kuhusiana na kisa hicho Medwedew asema: “Kilitokeza shaka kubwa ya kwanza juu ya nishati za nyukilia na kuondoa kabisa wazo la usalama wa viwanda vya nishati za nyukilia akilini mwa watu wengi—lakini si akilini mwa watu wote.”

Jambo hilo laonyesha sababu inayofanya aksidenti ziendelee kutokea. Katika kipindi cha 1992 ziliongezeka kwa karibu asilimia 20 katika Urusi. Baada ya mojayapo aksidenti hizo, mnamo Machi wa mwaka uo huo katika kituo cha nguvu za umeme cha Sosnovy Bore kule St. Petersburg, Urusi, viwango vya mnururisho viliongezeka kwa asilimia 50 katika kaskazini-mashariki mwa Uingereza navyo vikafikia maradufu ya kiwango kinachokubalika katika Estonia na kusini mwa Finland. Profesa John Urquhart wa Chuo Kikuu cha Newcastle akiri hivi: “Siwezi kuthibitisha kwamba ilikuwa ni Sosnovy Bore kilichoongeza [kiwango cha mnururisho]—lakini kama hakikuwa Sosnovy Bore, basi kilikuwa nini?”

Mamlaka fulani hudai kwamba mitambo kama ule wa Chernobyl ina kasoro fulani kwa namna ilivyotengenezwa na ni hatari sana kuendesha. Hata hivyo, zaidi ya mitambo 12 ingali inatumiwa kutokeza nguvu za umeme zinazohitajika sana. Waendeshaji fulani wa mitambo wamesemwa kuwa wanazima mifumo ya kudhibiti usalama ili kutokeza nguvu za umeme zaidi. Ripoti kama hizo huogofya nchi kama Ufaransa, inayotumia viwanda vya nyukilia kutokeza asilimia 70 ya umeme. Aksidenti nyingine kama ya “Chernobyl” ikitokea, huenda mitambo mingi katika Ufaransa ikalazimika kufungwa kabisa.

Kwa wazi hata mitambo “salama” hukosa usalama kwa sababu ya kukaa muda mrefu. Mapema katika 1993, wakati wa ukaguzi wa usalama unaofanywa kwa kawaida, mipasuko zaidi ya mia moja ilipatikana katika mabomba ya chuma-pua katika mtambo uliokuwa Brunsbüttel, mojapo mitambo ya kale zaidi katika Ujerumani. Mipasuko kama hiyo imepatikana katika mitambo iliyoko Ufaransa na Uswisi. Aksidenti mbaya ya kwanza katika kiwanda cha nyukilia cha Japani ilitokea 1991, ikisemwa kwamba aksidenti hiyo huenda ilisababishwa na uzee. Hilo lamaanisha kwamba yawezekana kwamba aksidenti kama hizo kutokea Marekani, ambako mitambo ya kibiashara ipatayo theluthi-mbili imekaa zaidi ya mwongo mmoja.

Aksidenti za mitambo ya nyukilia zaweza kutokea mahali popote na wakati wowote. Kuongezeka kwa mitambo husababisha kuongozeka kwa tisho; kadiri ya uzee wa mtambo hutokeza uwezekano mkubwa wa hatari kutokea. Si bila sababu kwamba gazeti moja liliiita mitambo hiyo mabomu yaliyokawia kulipuka na hatari za uhai za mnururisho.

Wazitupe Takataka Wapi?

Hivi majuzi watu walishangaa kupata mahali fulani pa mandari kando ya mto katika milima Alps ya Ufaransa pakiwa pamezingirwa ua na kulindwa na polisi. Gazeti la The European laeleza hivi: “Ukaguzi ulioamriwa ufanywe kwa ukawaida baada ya kifo cha mwanamke mmoja wa huko kilichotokana na sumu ya berili (aina ya kemikali) na kilichotokea miezi miwili iliyopita uligundua kwamba kulikuwapo viwango vya unururishi katika mahali hapo pa mandari kwa kadiri ya mara 100 kuliko maeneo jirani.”

Berili, aina ya madini mepesi inayofanyizwa kwa njia kadhaa, hutumiwa katika viwanda vya ndege, na inapokuwa imenururishwa, hiyo hutumiwa katika vituo vya nguvu za umeme za nyukilia. Inaonekana kwamba kiwanda fulani chenye kutengeneza berili kilikuwa kimetupa takataka zinazotokana na ule mfumo wa unururishi ulio hatari sana mahali hapo pa mandari au karibu na hapo. “Mavumbi ya berili, hata yasiponururishwa,” lasema The European, “ni mojapo takataka za viwanda zilizo na sumu zaidi ijulikanayo.”

Wakati uo huo, yasemekana kwamba vibebaji vipatavyo 17,000 vyenye takataka zenye unururishi vilitupwa majini kwa kipindi kizidicho miaka 30 katika pwani ya Novaya Zemlya, iliyotumiwa na Wasovieti kuwa mahali pa kujaribia nyukilia katika miaka ya mapema ya 1950. Kwa kuongezea, vipande vyenye mnururisho vya nyambizi (manowari ya chini ya maji) zenye nyukilia na visehemu vya angalau mitambo 12 vilitupwa katika maji hayo yaliyotumiwa yakiwa mahali pafaapo pa kutupia takataka.

Iwe zinatupwa kimakusudi au la, uchafuzi wa nyukilia ni hatari. Kuhusu nyambizi iliyozama katika pwani mwa Norway katika 1989, gazeti Time lilionya: “Mabaki hayo tayari yanavuja kemikali aina ya cesium-137, ambayo ni aina ya isotopu inayosababisha kansa. Kufikia sasa mvujo huo waonwa kuwa mdogo sana usiweze kuathiri viumbe vya majini au afya ya binadamu. Lakini nyambizi hiyo Komsomolets ilibeba pia makombora mawili yenye kilo 13 za plutoni ambazo nusu zazo tu zaweza kudumu kwa miaka 24,000 nazo zina sumu kali sana hivi kwamba kavumbi tu kanaweza kuua. Wastadi wa Urusi walionya kwamba plutoni ingeweza kumwagika majini na kuchafua eneo kubwa la bahari kuu haraka kufikia 1994.”

Bila shaka, kutupa takataka zenye mnururisho si tatizo linalopata Ufaransa na Urusi pekee. Marekani ina “milima mikubwa ya takataka zenye mnururisho na haina mahali pa kudumu pa kuziweka,” laripoti Time. Linasema kwamba mapipa milioni moja yenye kubeba vitu vilivyo hatari yamewekwa akiba kwa muda huku nyakati zote kukiwa na “hatari ya kupotea, kuibiwa na vilevile madhara katika mazingira kwa kutumiwa vibaya.”

Na kama kutoa kielezi cha hatari hiyo, tangi moja la takataka za nyukilia katika kile kilichokuwa hapo awali kiwanda cha kutengeneza silaha katika Tomsk, Siberia, lililipuka mnamo Aprili 1993, likitokeza ogofyo la kutukia kwa aksidenti nyingine kama ile ya Chernobyl.

Kwa wazi, matangazo yoyote ya amani na salama yaliyotegemea ule ulioonwa kuwa mwisho wa tisho la nyukilia hayana msingi mzuri. Lakini amani na salama iko karibu. Twajuaje?

[Sanduku katika ukurasa 4]

MATAIFA YENYE NYUKILIA

12 na Hesabu Inaongezeka

ZILIZOTANGAZWA au ZINA HAKIKA: Afrika Kusini, Belarus, China, India, Israeli, Kazakhstan, Marekani, Pakistan, Ufaransa, Uingereza, Ukrania, Urusi

YENYE UWEZO WA KUZITENGENEZA: Algeria, Argentina, Brazili, Iraki, Iran, Korea Kaskazini, Korea Kusini, Libya, Siria, Taiwan

[Picha katika ukurasa wa 5]

Hata matumizi yenye amani ya nishati ya nyukilia yaweza kuwa hatari

[Hisani]

Mandhari ya nyuma: Picha ya U.S. National Archives

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 2]

Jalada: Stockman/International Stock

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]

Picha ya U.S. National Archives

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki