Kumshinda Shetani na Kazi Zake
“Basi, mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.”—YAKOBO 4:7.
1. ‘Mkono wa mwovu’ umeathirije binadamu leo?
AYUBU alisema hivi kwa usahihi: “Dunia imetiwa mkononi mwa waovu [“yule mwovu,” NW].” (Ayubu 9:24) Na sasa twakabili nyakati zilizo ngumu zaidi katika historia yote ya binadamu. Kwa nini? Kwa sababu hizi ndizo “siku za mwisho” za udhibiti wa roho waovu wa Shetani juu ya dunia. Si ajabu kwamba, kwa kuchochewa na Shetani, ‘watu wabaya na wadanganyi wanaendelea, na kuzidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika.’ (2 Timotheo 3:1, 13) Isitoshe, minyanyaso, matendo yasiyo ya haki, ukatili, uhalifu, magumu ya kiuchumi, magonjwa ya kudumu, maumivu ya uzee, kushuka moyo kihisia—hayo na mengine yaweza kutuvunja moyo sana.
2. Twaweza kukabilianaje na mashambulizi ya Shetani leo?
2 Mkinzani mkuu, Shetani Ibilisi, anafanya mashambulizi mengi sana kwa wanadamu na hasa kwa waabudu wa kweli wa Mungu. Kusudi lake ni kugeuza wote wanaoweza kuwa washika uaminifu wa maadili kutoka kwa Mungu na kuwafanya waangamizwe pamoja naye na malaika zake wa kishetani. Hata hivyo, twahakikishiwa kwamba tukivumilia katika uaminifu wa maadili, Ibilisi atatukimbia. Kama Yesu, twaweza ‘kujifunza kutii’ Mungu kupitia mateso yetu, na kwa fadhili Zake zisizostahiliwa, twaweza kupata uhai wa milele.—Waebrania 5:7, 8; Yakobo 4:7; 1 Petro 5:8-10.
3, 4. (a) Ni majaribu gani ya nje ambayo Paulo alilazimika kukabili? (b) Paulo alihangaikia nini akiwa mzee Mkristo?
3 Mtume Paulo pia alijaribiwa kwa njia nyingi. Akitaja ustahili wake akiwa mhudumu wa Kristo, yeye aliandika: “Mimi ni zaidi; katika taabu kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana; katika mapigo kupita kiasi; katika mauti mara nyingi. Kwa Wayahudi mara tano nalipata mapigo arobaini kasoro moja. Mara tatu nalipigwa kwa bakora; mara moja nalipigwa kwa mawe; mara tatu nalivunjikiwa jahazi; kuchwa kucha nimepata kukaa kilindini; katika kusafiri mara nyingi; hatari za mito; hatari za wanyang’anyi; hatari kwa taifa langu; hatari kwa mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za jangwani; hatari za baharini; hatari kwa ndugu za uongo; katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi.
4 “Baghairi ya mambo ya nje, yako yanijiayo kila siku, ndiyo maangalizi ya makanisa [“makutaniko,” NW] yote. Ni nani aliye dhaifu, nisiwe dhaifu nami? Ni nani aliyekwazwa nami nisichukiwe?” (2 Wakorintho 11:23-29) Hivyo, Paulo alishika uaminifu wa maadili alipokabili minyanyaso na majaribu yatokayo nje, na akiwa mzee Mkristo, yeye alihangaikia sana kuimarisha ndugu na dada walio dhaifu kutanikoni, akiwasaidia kushika uaminifu wa maadili. Ni kielelezo chema kama nini kwa wazee Wakristo leo!
Uaminifu wa Maadili Chini ya Mnyanyaso
5. Jibu kwa mnyanyaso wa moja kwa moja ni nini?
5 Shetani hutumia mambo gani ili kuvunja uaminifu wa maadili? Kama ambavyo imeonyeshwa hapo juu, mojapo hila mbaya zaidi za Shetani ni mnyanyaso wa moja kwa moja, lakini kuna jibu. Waefeso 6:10, 11 (NW) yatushauri hivi: “Endeleeni kujipatia nguvu katika Bwana na katika uwezaji wa nguvu zake. Vaeni suti kamili ya silaha kutoka kwa Mungu ili mpate kuweza kusimama imara dhidi ya mbinu za [au, “matendo ya ujanja ya,” kielezi-chini] Ibilisi.”
6. Yaweza kuonyeshwaje kwamba Mashahidi wa Yehova ‘wameshinda kabisa’?
6 Mara nyingi katika siku hizi za mwisho, Mashahidi wa Yehova hulazimika kukabili majaribu. Hivyo, twaweza kusema pamoja na Paulo: “Katika mambo yote haya tunatokea tukiwa wenye kushinda kabisa kupitia yeye aliyetupenda.” (Warumi 8:37, NW) Hilo lathibitishwa na rekodi ya uaminifu wa maadili wa Mashahidi wa Yehova katika kambi za mateso za Ujerumani, Austria, Poland, na Yugoslavia katika kipindi cha utawala wa Nazi kati ya 1933 na 1945, wakidhulumiwa na Wakomunisti katika Ulaya Mashariki kati ya 1945 na 1989, na wakati wa minyanyaso ambayo imekumba sehemu fulani za Afrika na Amerika ya Latini katika nyakati za karibuni zaidi.
7. Ni vielelezo vipi vyenye kuchochea vinavyoripotiwa kutoka Ethiopia?
7 Mashahidi wa Yehova katika Ethiopia waliandaa kielelezo kizuri sana cha uaminifu wa maadili kati ya miaka 1974 na 1991. Mmoja wa watu wale waliowashika aliyekuwa mwenye kufikiri kisiasa alimweleza ndugu mmoja aliyekuwa gerezani hivi: “Ni afadhali kufungua simba kutoka kwa makao ya wanyama kuliko kuwaacha nyinyi huru tena!” Wanyanyasi hao wakatili waliwatesa watumishi wa Yehova, na baada ya miaka kadhaa mahakama ya rufani iliamuru wauawe. Mwili wa ndugu mmoja ulionyeshwa peupe uwe kielelezo cha kutoa onyo. Ndugu wengine waliokata rufani juu ya hukumu ya kifo waliachiliwa na mahakama moja isiyoshikilia mambo sana, na baadhi ya ‘washindi’ hao waaminifu walikuwa na sehemu katika programu ya “Ufundishaji wa Kimungu” Mkusanyiko wa Wilaya katika Addis Ababa mapema katika 1994.a—Yohana 16:33; linganisha 1 Wakorintho 4:9.
8. Shetani amejaribu kutumiaje vibaya ule “utakaso wa kikabila”?
8 Shetani ameshindwa kuvunja uaminifu wa maadili wa ndugu na dada hao waaminifu-washikamanifu kwa shambulio la moja kwa moja. Kwa hiyo, yeye hutumia mambo gani mengine ya ujanja? Ufunuo 12:12 wasema hivi juu ya siku za mwisho: “Ole wa nchi na bahari! kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.” Baada ya kushindwa kuangamiza watu wa Mungu walio waaminifu-washikamanifu kupitia minyanyaso, akiwa na hasira yeye hujaribu kuangamiza vikundi vyote vya watu, bila shaka akinuia kuangamiza watu wa Yehova pamoja na wengine wote. Kwa hiyo, ule uitwao utakaso wa kikabila umetekelezwa katika sehemu nyingi za ile iliyokuwa Yugoslavia, na majaribu ya kuangamiza makabila mazima yamefanywa katika Liberia, Burundi, na Rwanda.
9. Kwa nini mbinu za Shetani mara nyingi hushindwa? Toa vielelezo.
9 Lakini, mara nyingi mbinu za Shetani humgeukia, kwa kuwa mapigo ya kishetani huamsha watu wenye mioyo minyoofu watambue kwamba tumaini lao la pekee linategemea Ufalme wa Mungu, unaotangazwa kwa bidii na Mashahidi wa Yehova. (Mathayo 12:21) Kwa kweli, watu wenye kupendezwa humiminika kwa Ufalme! Kwa kielelezo, katika Bosnia na Herzegovina zilizojaa mizozo, katika sherehe ya Ukumbusho wa kifo cha Yesu katika Machi 26, 1994, watu 1,307 walihudhuria, wakiwa 291 zaidi ya mwaka uliopita. Kulikuwa na vilele katika Sarajevo (414), Zenica (223), Tuzla (339), Banja Luka (225), na miji mingine. Katika Kroatia iliyo jirani, kulikuwa na kilele kipya cha watu 8,326. Ujeuri uliokuwa ukiendelea sehemu walizokuwa haukuzuia Mashahidi wa Yehova katika nchi hizo kutii amri ya ‘kuitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.’—1 Wakorintho 11:26.
Katika Rwanda Iliyokumbwa na Mzozo
10, 11. (a) Ni mambo yapi yametendeka katika Rwanda inayoitwa eti ya Kikristo? (b) Wamishonari waaminifu wamejielezaje?
10 Katika 1993, Rwanda, ikiwa na wahubiri wa Ufalme 2,080, ilikuwa na watu 4,075 waliohudhuria “Ufundishaji wa Kimungu” Mkusanyiko wa Wilaya, na watu 230 walibatizwa. Kati ya hao, 142 waliomba mara hiyo utumishi wa upainia-msaidizi. Mafunzo ya Biblia yaliyokuwa yakiongozwa yaliongezeka hadi 7,655 katika 1994—kwa wazi Shetani hakupenda jambo hilo! Ingawa wengi zaidi ya wakazi hudai kuwa Wakristo, mauaji makubwa kati ya makabila yalianzishwa. Gazeti L’Osservatore Romano la Vatikani lilikiri hivi: “Haya ni maangamizi ya moja kwa moja ya kabila zima, ambayo inasikitisha kwamba hata Wakatoliki wameshiriki.” Wanaume, wanawake, na watoto wanaokadiriwa kuwa nusu-milioni walikufa, na wengine wapatao milioni mbili walipoteza makao au kulazimishwa kutoroka. Wakidumisha msimamo wa kutokuwamo kwa Kikristo kusiko kwa jeuri, Mashahidi wa Yehova walijaribu kukaa pamoja. Mamia ya ndugu na dada zetu waliuawa. Lakini katika kutaniko moja lenye wahubiri 65 wa Ufalme, ambamo 13 waliuawa, hudhurio la mikutano liliongezeka hadi 170 kufikia Agosti 1994. Misaada kutoka kwa Mashahidi katika nchi nyinginezo ilikuwa miongoni mwa misaada ya kwanza kufika. Sala zetu zapanda juu kwa niaba ya wale waliookoka.—Warumi 12:12; 2 Wathesalonike 3:1, 2; Waebrania 10:23-25.
11 Kati ya maogofyo hayo yote, wamishonari watatu waliokuwa nchini Rwanda waliponyoka. Wao waandika: “Twatambua kwamba ndugu zetu ulimwenguni kote wamelazimika kukabili hali kama hizo au hata zilizo mbaya zaidi, na twajua kwamba hayo yote ni sehemu ya ishara ya siku za mwisho wa mfumo huu mwovu. Lakini, mmoja anapopatwa mwenyewe na hali hiyo, yeye hutambua zaidi uhalisi wa mambo na kumfanya athamini thamani ya uhai. Maandiko fulani yamekuwa na umaana mzito zaidi kwetu, nasi twatazamia wakati ambapo mambo yaliyopita hayatakumbukwa tena. Kwa wakati huu twataka kuwa wenye shughuli katika utumishi wa Yehova.”
Vijana Washikao Uaminifu wa Maadili
12, 13. (a) Ni mwendo upi wa uaminifu wa maadili uliochukuliwa na kijana mmoja? (b) Vijana wetu waweza kupata wapi kitia-moyo leo?
12 Yesu alionyesha kwamba wale ambao hukataliwa na washiriki wa familia kwa ajili ya ile kweli watathawabishwa “mara mia.” (Marko 10:29, 30) Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Entellia, msichana mwenye umri wa miaka kumi katika kaskazini mwa Afrika, aliyependa jina la Mungu—Yehova—mara tu alipolisikia. Yeye alijifunza pamoja na Mashahidi wa Yehova na kutembea dakika 90 kwenda na pia kurudi kutoka mikutanoni, ingawa familia yake iliyompinga mara nyingi walimfungia nje aliporudi. Akiwa na umri wa miaka 13, yeye alianza kuhubiri nyumba kwa nyumba, na upinzani wa familia ukazidi. Siku moja watu wa ukoo walimfunga mikono na miguu na kumfanya alale kwenye jua kali sana kwa muda wa saa saba, mara kwa mara wakimmwagia maji machafu. Walimpiga kikatili, wakaharibu jicho lake, na hatimaye kumfukuza nyumbani. Hata hivyo, alipata kazi katika hospitali moja na hatimaye akahitimu kuwa muuguzi. Alibatizwa akiwa na umri wa miaka 20 naye alijiandikisha mara hiyo kuwa painia-msaidizi. Wakivutiwa na uaminifu wa maadili wake, familia yake ilimkaribisha arudi nyumbani, na tisa kati yao wamekubali mafunzo ya Biblia nyumbani.
13 Entellia alipata kitia-moyo sana kutoka Zaburi 116, hasa mistari 1-4, ambayo amesoma tena na tena: “Nampenda BWANA kwa kuwa anaisikiliza sauti yangu na dua zangu. Kwa maana amenitegea sikio lake, kwa hiyo nitamwita siku zangu zote. Kamba za mauti zilinizunguka, shida za kuzimu zilinipata. Naliona taabu na huzuni; nikaliita jina la BWANA. Ee BWANA, nakuomba sana, uniokoe nafsi yangu.” Yehova hujibu sala kama hizo!
14. Mashahidi Wapoland wameonyeshaje uaminifu wa maadili wenye kutokeza sana?
14 Kama ilivyo katika siku ya Yesu, mara nyingi Shetani ametumia ushupavu wa kidini katika kuchochea mnyanyaso—lakini bila mafanikio. Jambo la kutokeza sana ni kile kielelezo cha ndugu zetu katika Poland, kama kifafanuliwavyo katika Kitabu-Mwaka cha Mashahidi wa Yehova 1994, Kiingereza. Hata vijana walihitajika kujithibitisha kuwa washika uaminifu wa maadili. Katika 1946, mmoja wa vijana kama hao alikuwa msichana mwenye umri wa miaka 15 aliyeambiwa hivi: “Fanya tu ishara ya Katoliki ya msalaba. Ama sivyo risasi inakungoja!” Akidumisha uaminifu wa maadili, alivurutwa ndani ya msitu, akanyanyaswa kikatili sana, na kupigwa risasi.—Linganisha Mathayo 4:9, 10.
Mambo Mengine ya Ujanja ya Shetani
15, 16. (a) Ni ipi sera ya Shetani inayotumiwa na roho waovu, nasi twaweza kumkinzaje? (b) Kwa nini hakuna haja kwa vijana wetu kujikwaa?
15 Sera ya Shetani inayotumiwa na roho waovu kwa kweli ni “tawala au angamiza”! Yeye ana silaha nyingi zenye ukatili anazotumia. Basi si ajabu kwamba mtume Paulo aonya hivi: “Kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.” (Waefeso 6:12, 13) Tamaa za kupata mali, vitumbuizo na propaganda zilizopotoka, muziki wa kishetani, mkazo wa marika shuleni, matumizi ya dawa za kulevya, na ulevi—yoyote ya mambo hayo yaweza kuharibu kabisa maisha zetu. Kwa hiyo, mtume Paulo aendelea kushauri hivi: ‘Zaidi ya yote mtwae ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.’—Waefeso 6:16.
16 Yaonekana hiyo yahitajika hasa leo kwa sababu ya muziki wenye kupita kiasi ambao Shetani anamwagia ulimwengu huu. Nyakati nyingine kuna uhusiano wa moja kwa moja na Ushetani. Ripoti moja kutoka kwa ofisi ya mkuu wa polisi katika Wilaya ya San Diego (Marekani) ilisema: “Tulikuwa na wonyesho wa muziki hapa ambapo beni ya muziki iliwafanya watoto 15,000 kuimba ‘Natas’—yaani, Satan [Shetani] ikitamkwa kinyume.” (Italiki ni zetu.) Ushetani umefafanuliwa kuwa shimo ardhini ambamo vijana wanaobalehe hujikwaa “kwa sababu wamekuwa wakitangatanga kwa kukata tamaa, wenye hasira na wapweke.” Enyi vijana mlio katika kutaniko la Kikristo, hakuna haja mjikwae! Yehova huwaandalia suti ya silaha ya kiroho ambayo vishale vya Shetani haviwezi kupenya.—Zaburi 16:8, 9.
17. Hali ya kushuka moyo kihisia yaweza kushindwaje?
17 Vishale vyenye kuwaka moto vya kishetani vimeundwa ili vitumie vibaya hisia-moyo. Kupitia mikazo ya maisha, kama ugonjwa wa kimwili au hali ya kushuka moyo sana, mkinzani wetu aweza kufanya wengine wahisi kwamba hawafai kitu. Mmoja aweza kuvunjika moyo kwa sababu hawezi kutumia muda wa saa nyingi katika utumishi wa Mungu au kwa sababu ya kukosa mikutano fulani ya kutaniko. Utunzi wenye upendo wa wazee na ndugu na dada wengine wenye mioyo ya fadhili waweza kusaidia katika kushinda masumbufu makali. Nyakati zote ukumbuke kwamba Yehova hupenda watumishi wake waaminifu. (1 Yohana 4:16, 19) Zaburi 55:22 yaeleza: “Umtwike BWANA mzigo wako naye atakutegemeza, hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele.”
18. Wengine hulazimika kukabili mbinu zipi za kishetani?
18 “Mbinu” za ujanja za Shetani karibuni zimeonekana katika njia nyingine tena. Katika baadhi ya nchi fulani watu wazima walio wengi wameshambuliwa na mawazo yanayowadokezea kwamba wakiwa watoto, wao walitendwa kikatili sana na vidhehebu vya kishetani. Mawazo hayo hutoka wapi? Wajapofanya utafiti mwingi sana, maoni ya wataalamu hutofautiana sana. Wengine huona mawazo kama hayo kuwa kumbukumbu halisi, wengine huyaona kuwa mambo ya kuwaziwa tu—labda yakiletwa na utibabu wa akili unaotiliwa shaka—na bado wengine huyaona kuwa aina ya ndoto inayosababishwa na kisa fulani kibaya cha utotoni.
19. (a) Ayubu alilazimika kukabili mawazo gani? (b) Wazee wawezaje kufuata kielelezo cha Elihu?
19 Ni jambo la kupendeza kwamba mtumishi wa Mungu Ayubu alilazimika kukabili “mawazo yenye usumbufu” ambayo Shetani aliwasilisha kupitia Elifazi na Sofari. (Ayubu 4:13-18, NW; 20:2, 3) Kwa hiyo Ayubu alipatwa na “uchungu,” uliomfanya aseme ‘maneno ya haraka’ kuhusu “vitisho” vinavyopata akili yake. (Ayubu 6:2-4; 30:15, 16) Elihu alimsikiliza Ayubu kwa ukimya na kumsaidia kwa moyo mweupe aone maoni yenye hekima sana ya Yehova kuhusu mambo. Vilevile leo, wazee wenye ufahamu huonyesha kwamba wao hujali waliopatwa na pigo kwa kutowaongezea “mkazo” watu kama hao. Badala ya kufanya hivyo, kama Elihu, wao huwasikiliza kwa saburi na kisha kutumia mafuta yenye kufariji ya Neno la Mungu. (Ayubu 33:1-3, 7, NW; Yakobo 5:13-15) Hivyo mtu yeyote ambaye hisia zake za moyoni husumbuliwa na masumbufu, yaliyo ya kweli au ya kuwaziwa, au ‘atishikaye katika ndoto na kwa maono’ kama Ayubu alivyokuwa, aweza kupata faraja ya Kimaandiko yenye kutuliza katika kutaniko.—Ayubu 7:14; Yakobo 4:7.
20. Wakristo wanaosononeka wanaweza kusaidiwaje kudumisha usawaziko wao wa kiroho?
20 Wakati huu Mkristo aweza kuwa na hakika kwamba, kwa njia moja au nyingine, ni Shetani anayasababisha mawazo hayo mabaya. Ikiwa kuna watu fulani kutanikoni watesekao kwa njia hiyo, basi wao ni wenye hekima ikiwa wayaona mawazo hayo ya akilini kuwa jaribu la moja kwa moja la Shetani kuharibu usawaziko wao wa kiroho. Wao wahitaji utegemezo wa Kimaandiko wenye saburi na ufahamu. Kwa kumwendea Yehova kwa sala na kwa kunufaika na uchungaji wa kiroho, wale wanaopatwa na msononeko watapata nguvu ipitayo iliyo ya kawaida. (Isaya 32:2; 2 Wakorintho 4:7, 8) Kwa hiyo wataweza kuvumilia kwa uaminifu na kukataa kuruhusu mawazo maovu yanayowaingilia yaathiri amani ya kutaniko. (Yakobo 3:17, 18) Ndiyo, wao wataweza kumpinga Ibilisi, wakionyesha roho ileile ambayo Yesu alionyesha aliposema hivi: “Nenda zako, Shetani.”—Mathayo 4:10; Yakobo 4:7.
21. Maandiko yanatuonyaje juu ya njia za ujanja za Shetani?
21 Twajua kwamba lengo la Shetani ni kufisidi akili zetu kwa njia fulani, kama mtume Paulo alivyoonya katika 2 Wakorintho 11:3: “Lakini nachelea [“naogopa,” NW]; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo.” Uharibifu wa sasa wa miili yote, au jamii ya kibinadamu iliyotenganishwa na Mungu, watukumbusha ule upotovu uliosababishwa na ile mivyauso yenye jeuri iliyoitwa “Waangushaji” katika siku ya Noa. (Mwanzo 6:4, 12, 13, NW, kielezi-chini; Luka 17:26) Basi haishangazi kwamba Shetani hutumia matendo ya ujanja na njia za werevu katika kutoa hasira yake, hasa dhidi ya watu wa Mungu.—1 Petro 5:8; Ufunuo 12:17.
22. Shetani akiwa ameondolewa, twaweza kutarajia baraka zipi?
22 Shetani hata hatajwi mwishoni mwa sura za kumalizia kitabu cha Biblia cha Ayubu. Mwito wake mwovu kwamba wanadamu hawawezi kudumisha uaminifu wa maadili kwa Mungu ulikuwa umethibitishwa kuwa uongo na uaminifu wa maadili wa Ayubu. Vilevile, katika wakati ujao ulio karibu ambapo “mkutano mkubwa” wa washika uaminifu wa maadili watakapotoka katika “dhiki ile iliyo kuu,” Shetani atatiwa katika abiso. Wanaume na wanawake wa imani, kutia Ayubu mwaminifu, watajiunga na ule “mkutano mkubwa,” wafurahie baraka za kiparadiso, hata zilizo tukufu zaidi ya zile Ayubu alithawabishwa nazo!—Ufunuo 7:9-17; 20:1-3, 11-13; Ayubu 14:13.
[Maelezo ya Chini]
a Ona Kitabu-Mwaka cha Mashahidi wa Yehova 1994, ukurasa 177.
Maswali ya Kupitia
◻ Ayubu, Yesu, na Paulo waliweka vielelezo gani vizuri vya uaminifu wa maadili?
◻ Washika uaminifu wa maadili wamekabilije Shetani?
◻ Vijana wawezaje kukinza mambo ya ujanja ya Shetani?
◻ Ni nini kiwezacho kufanywa ili kukabili mbinu za kishetani?
[Picha katika ukurasa wa 7]
Katika Ethiopia, Meswat na Yoalan sasa wamtumikia Yehova wakati wote kwa kufuata kielelezo cha baba yao, aliyeuawa
[Picha katika ukurasa wa 7]
Entellia, kijana mwenye uaminifu wa maadili katika kaskazini mwa Afrika