Kwa Nini Nyakati Hizi ni Mbaya Sana?
UKETIPO kusoma gazeti la habari au kutazama habari za televisheni au kusikiliza msambazo wa habari za redio, watarajia habari mbaya, sivyo? Labda hushangai kupata kujua kwamba vita inayoendelea ingali ikiendelea kwa mshindo mkubwa, au kwamba uhalifu wenye jeuri ungali ukienea pote, au kwamba njaa kuu ingali ikidhoofisha nguvu za nchi inayositawi.
Ikiwa unaishi umbali fulani kutoka mambo hayo, labda huhisi daima kusononeshwa kupita kiasi na ripoti hizo. Ingawa hivyo, ni nani awezaye kuwa na hisia-mwenzi kwa matungamano hayo yote yenye kuteseka? Hata hivyo, ni vigumu sana kubaki bila kuathiriwa tunapokabiliwa na njia ambayo kuteseka huathiri watu mmoja-mmoja. Yaani, ingawa ni jambo moja kusoma juu ya vita na kufikiria takwimu juu ya waliouawa, ni jambo tofauti kabisa kusoma juu ya Adnan mdogo, mvulana Mbosnia mwenye umri wa miaka tisa ambaye mamaye aliuawa wakati bomu lilipoharibu nyumba yao. Babaye Adnan alikufa alipopigwa risasi na mpiga-risasi stadi kutoka mafichoni, miezi michache tu baadaye walipokuwa wakitembea mtaani pamoja. Majuma machache baadaye, dadaye alitokwa damu hadi akafa machoni pake, akiwa mhasiriwa wa kombora la kutupwa katika uwanja wa shule. Madaktari waliotibu hali ya Adnan ya vurugu walipata kwamba huyo mvulana alikuwa sugu, bila hisia zote—hata udadisi. Hofu na kuona yaliyotukia hapo nyuma kulimkumba alipokuwa macho; majinamizi yalisumbua usingizi wake. Adnan si takwimu. Yeye ni mtoto anayeteseka; twasukumwa kuwa na hisia-mwenzi kwake.
Ndivyo ilivyo pia kwa habari ya matukio mengine mabaya ya ulimwengu. Ni jambo moja kusoma juu ya njaa kuu; ni tofauti kabisa kuona picha ya msichana mwenye umri wa miaka mitano mwenye tumbo lililofura na viungo vilivyokonda sana, aliye mhasiriwa wa njaa kali aliye karibu sana kufa njaa. Ni jambo moja kusoma juu ya takwimu za uhalifu; ni jambo tofauti kabisa kusikia juu ya mjane mzee-mzee akipigwa kinyama, akinyang’anywa mali, na kubakwa. Ni jambo moja kusoma juu ya kudhoofika kwa familia; ni jambo tofauti kabisa kupata kujua kwamba mama fulani alimnyima mtoto wake chakula kimakusudi, akamtenda vibaya sana.
Inaumiza kusoma juu ya mambo hayo. Lakini ni vibaya zaidi kama nini wakati mapigo hayo ya tufeni pote yanapotuathiri moja kwa moja! Upatwapo na maovu kibinafsi, hali ya tufeni pote ionyeshwayo na habari za ulimwengu yaweza kuwa kubwa mno. Yaogopesha kukabili jambo la hakika kwamba kuteseka kutokana na uhalifu, vita, njaa kuu, na ugonjwa kunaongezeka kwa kadiri isiyo na kifani katika historia ya kibinadamu. Matokeo ya kushughulika na mambo halisi ya karne hii ya 20 yaweza kwa kweli kuwa magumu kuelewa—bumbuazi, hofu, na mshuko-moyo ni mambo ya kawaida.
Watu wa dini nyingi wanatafuta majibu kwa maswali yenye kusumbua kama vile, Kwa nini mambo ni mabaya sana? Wanadamu wanaelekea wapi?
Kwa kuhuzunisha, mara nyingi dini leo hazitoi majibu yenye kuridhisha. Ulipoona kwa mara ya kwanza lile swali lililo kwenye jalada la gazeti hili, huenda ukawa uliitikia kwa kutia shaka—itikio lenye kueleweka. Mara nyingi dini za harakati ya kufuata kanuni za msingi za kidini hujaribu kuelewa katika Biblia mambo ambayo hayamo humo hata kidogo—siku na saa barabara ya kuangamia kwa ulimwengu huu. (Ona Mathayo 24:36.) Wachapishaji wa jarida hili hupendelea kuiacha Biblia ijieleze yenyewe. Huenda ukashangaa kupata kujua kwamba mazungumzo ya Biblia juu ya siku za mwisho ni yenye mambo hakika na yenye kiasi. Na Biblia haielezi tu ni kwa nini mambo ni mabaya sana. Inaandaa pia tumaini kwa wakati ujao, tumaini lenye kufariji kikweli. Twakualika uchunguze makala zifuatazo ili uone jinsi hilo lilivyo kweli.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
Jobard/Sipa Press