Nyakati Ngumu kwa Wazee-Wazee
MAMA ONIYAN, mwenye umri wa miaka 68, anaishi katika jiji moja kuu la Afrika Magharibi. Alipokuwa mchanga, alijiwazia akifurahia miaka yake ya uzeeni katika kustaafu kutulivu, akiwa amezingirwa na watoto na wajukuu wake. Badala ya hivyo, yeye hupisha siku zake akiuza maji baridi chini ya jua kali. Fedha kidogo anazochuma humsaidia kuendelea kuishi. Wana wake wawili wanaishi katika nchi nyingine iliyo mbali sana. Muda mrefu umepita tangu walipomtumia fedha zozote.
Nyakati zilizopita, wazee-wazee katika Afrika waliheshimiwa sana. Walistahiwa kwa sababu ya uzoefu na ujuzi wao, pamoja na hekima na utambuzi ambao hutokana nazo. Walisaidia kulea wajukuu. Wachanga walitafuta shauri lao na kibali chao. Watu waliishi kulingana na shauri hili la Biblia: “Mwondokeeni mtu mwenye mvi; heshimuni uso wa mtu mzee.”—Mambo ya Walawi 19:32.
Nyakati zimebadilika. Umaskini, infleshoni, ukosefu wa kazi za kuajiriwa, na watu wengi kuhamia majijini ni mambo ambayo yameacha wazee-wazee walio wengi wajitegemee. Mkurugenzi wa shirika la HelpAge Kenya, Camillus Were, asema hivi: “Utamaduni wa kutegemeza na kutunza wazee-wazee umezidi kudhoofika.”
Bila shaka, kudhoofika kwa vifungo vya familia si jambo linalotukia katika nchi za Afrika pekee. Likisema juu ya Japani, Guardian Weekly laripoti hivi: “Ujitoaji wa watoto ulikuwa msingi wa mfumo wa Kijapani wa viwango vilivyopitishwa na Dini ya Confucius, lakini haukuokoka kule kuhamia kwa watu majijini na kudhoofika kwa vifungo vya familia: leo, asilimia 85 ya Wajapani hufa katika hospitali mbalimbali au katika makao ya watu wazee.”
Kwa hali yoyote ile, wanaotaka kumpendeza Mungu kikweli hujitahidi kuwaheshimu wazazi wao. Wanatii shauri hili la Biblia: “Heshimu baba yako na mama yako . . . ili ipate kuwa vema kwako nawe upate kudumu muda mrefu juu ya dunia.” (Waefeso 6:2, 3) Ingawa sikuzote si rahisi kuheshimu na kutunza wazee-wazee, kwaweza kuleta thawabu nyingi.