Collegiants—Funzo la Biblia Liliwafanya Wawe Tofauti
Je, umesikia juu ya Collegiants?
Kikundi hiki kidogo cha kidini cha Uholanzi cha karne ya 17 kilikuwa tofauti na makanisa mashuhuri ya wakati huo. Kilikuwaje tofauti, nasi twaweza kujifunza nini kutokana nacho? Ili tupate kujua, acheni turudi nyuma hadi wakati huo.
KATIKA mwaka wa 1587, Jacobus Arminius (au, Jacob Harmensen) aliwasili katika jiji la Amsterdam. Alipata kazi ya kuajiriwa bila shida kwa kuwa elimu na uzoefu wake wa kitaalamu ulivutia. Alihitimu katika Chuo Kikuu cha Leiden cha Uholanzi akiwa na umri wa miaka 21. Baada ya kuhitimu, alikaa Uswisi kwa miaka sita, akifundishwa theolojia na Théodore de Bèze, mwandamizi wa Mleta-Marekebisho Mprotestanti, John Calvin. Si ajabu kwamba Waprotestanti wa Amsterdam walifurahi kumweka rasmi Arminius, mwenye umri wa miaka 27, kuwa mmoja wa makasisi wao! Ingawa hivyo, miaka michache baadaye, washiriki wengi wa kanisa walijutia uchaguzi wao. Kwa nini?
Lile Suala la Kuamuliwa Kimbele Yatakayompata Mtu
Punde baada ya Arminius kuwa mmoja wa makasisi wao, uvutano ulizuka miongoni mwa Waprotestanti wa Amsterdam kuhusu fundisho la kuamuliwa kimbele yatakayompata mtu. Hilo lilipata kuwa fundisho muhimu kati ya mafundisho ya Calvin, lakini baadhi ya washiriki wa kanisa wakaonelea kwamba Mungu aliyeamua kimbele watu fulani wapate wokovu na kuhukumia wengine adhabu, ni mkali na hafuati haki. Wafuasi wa Calvin walitarajia Arminius, kwa kuwa alikuwa mwanafunzi wa Bèze, awasahihishe wabishi hao. Hata hivyo, badala yake, Arminius aliwaunga mkono wabishi hao na kuwatia hofu kuu wafuasi wa Calvin. Kufikia mwaka wa 1593, ubishi huo ulikuwa umechacha sana hivi kwamba uliwagawanya Waprotestanti wa jiji kuwa vikundi viwili—wale wenye kuliunga mkono fundisho hilo na wale wenye kulipinga, yaani, watu wenye maoni ya kadiri.
Katika muda wa miaka michache, ubishi huo uliokuwa wa mahali pamoja ulienea kuwa mgawanyiko wa kitaifa wa Kiprotestanti. Hatimaye, katika Novemba 1618, hali hiyo ikawa mbaya sana hivi kwamba, kulitokea mapambano ya kutambulisha mshindi katika ubishi huo. Wafuasi wa Calvin, wakiungwa mkono na jeshi na maoni ya umma, waliwaita wabishi hao (ambao wakati huo waliitwa Walalamishia) kwenye baraza la kitaifa, yaani, Sinodi ya Protestanti ya wilaya ya Dordrecht. Mkutano ulipomalizika, makasisi wote wa Walalamishi walitakiwa wachague: Ama kutia sahihi makubaliano ya kutohubiri tena kamwe, ama kuondoka nchini. Wengi walichagua kwenda uhamishoni. Wafuasi wa Calvin wenye maoni yenye kupita kiasi walichukua mahali pa makasisi wa Walalamishi walioondoka. Sinodi ilitumainia kwamba mafundisho ya Calvin yalikuwa yameshinda—au kitu kama hicho.
Chanzo na Ukuzi wa Collegiants
Kama vile ilivyokuwa kwingineko, kutaniko la Walalamishi katika kijiji cha Warmond, karibu na Leiden, lilipoteza kasisi wao. Hata hivyo, tofauti na ilivyokuwa kwingineko, kutaniko hilo lilikataa kasisi aliyeidhinishwa na sinodi achukue mahali pa huyo kasisi wao. Isitoshe, wakati kasisi mmoja wa Walalamishi alipohatarisha uhai wake kurudi Warmond mwaka wa 1620 kushughulikia kutaniko hilo, baadhi ya washiriki wa kutaniko walimkataa vilevile. Washiriki hao walikuwa wameanza kufanya mikutano yao ya kidini kisiri bila msaada wa kasisi yeyote. Baadaye, mikutano hiyo iliitwa colleges nao wahudhuriaji wakaitwa Collegiants.
Ingawa Collegiants walitokea kwa sababu ya hali wala sio kwa sababu ya kanuni za kidini, hali hiyo ilibadilika upesi. Mshiriki wa kutaniko, Gisjbert van der Kodde, alitoa hoja kwamba kwa kukutana bila usimamizi wa makasisi, kikundi hicho kilikuwa kikijipatanisha zaidi na Biblia na njia ya Wakristo wa mapema kuliko makanisa yaliyokuwa mashuhuri. Alisema kwamba jamii ya makasisi ilikuwa imebuniwa baada ya kifo cha mitume ili kutokeza kazi kwa ajili ya watu ambao hawakuwa tayari kujifunza kufanya kazi ya namna fulani.
Katika mwaka wa 1621, Van der Kodde na washiriki wengine wenye maoni sawa na yake walihamisha mikutano yao hadi kijiji jirani cha Rijnsburg.b Miaka kadhaa baadaye, wakati mnyanyaso wa kidini ulipokoma na watu wakawa wenye uvumilivu, sifa ya mikutano ya Collegiants ilienea kotekote nchini na kuvutia “watu wa tabaka zote,” kama vile mwanahistoria Siegfried Zilverberg alivyosema. Kulikuwapo Walalamishi, Wamenoni, Wasosini, na hata wanatheolojia. Wengine walikuwa wakulima. Nao wengine walikuwa washairi, wachapishaji, matabibu, na wachuuzi. Mwanafalsafa Spinoza (Benedictus de Spinoza) na mwalimu Johann Amos Comenius (au, Jan Komenský), na vilevile mchoraji maarufu, Rembrandt van Rin, waliunga mkono harakati hiyo. Mawazo tofauti ambayo watu hawa wenye kumcha Mungu walileta, yaliathiri usitawi wa itikadi za hao Collegiants.
Baada ya mwaka wa 1640 kikundi hiki chenye nguvu kilikua haraka. Katika majiji ya Rotterdam, Amsterdam, Leeuwarden, na majiji mengine, colleges ziliongezeka haraka. Profesa wa historia, Andrew C. Fix asema kwamba kati ya miaka ya 1650 na 1700, “Collegiants . . . walikua wakawa kimojawapo cha vikundi muhimu vya kidini vyenye uvutano zaidi katika Uholanzi ya karne ya kumi na saba.”
Itikadi za Collegiants
Kwa kuwa kusababu, uvumilivu, na uhuru wa kusema, yote yalikuwa sifa bainifu za harakati ya Collegiant, kila Collegiant alikuwa huru kushikilia itikadi tofauti. Hata hivyo, waliunganishwa pamoja na mambo ambayo wote walisadiki. Kwa kielelezo, Collegiants wote walithamini umuhimu wa funzo la Biblia la kibinafsi. Kila mshiriki, akaandika mmoja wa hao Collegiants, apaswa “kujichunguzia mwenyewe, na asije kumjua Mungu kutoka kwa mtu mwingine.” Walifanya hivyo. Kulingana na mwanahistoria wa karne ya 19, Jacobus C. van Slee, ujuzi zaidi wa Biblia ulipatikana miongoni mwa Collegiants kuliko vikundi vingine vya kidini vya wakati huo. Hata wapinzani waliwasifu Collegiants kwa uwezo wao wa kutumia Biblia kwa ustadi.
Hata hivyo, kadiri Collegiants walivyozidi kusoma Biblia, ndivyo walivyositawisha itikadi tofauti na zile za makanisa mashuhuri. Vyanzo vya tangu karne ya 17 hadi karne ya 20 vyafafanua baadhi ya itikadi zao:
Kanisa la Mapema. Katika mwaka wa 1644, Adam Boreel, mmoja wa Collegiants na pia mwanatheolojia, aliandika kwamba kanisa la mapema lilipoanza kushiriki katika siasa wakati wa Maliki Konstantino, lilivunja agano lake na Kristo na kupoteza upulizio wa roho takatifu. Aliongeza kusema kwamba, likiwa tokeo, mafundisho ya uwongo yaliongezeka na kuendelea hadi siku yake.
Yale Marekebisho Makubwa ya Kidini. Yale Marekebisho Makubwa ya Kidini ya karne ya 16 yaliyoongozwa na Luther, Calvin, na wengineo hayakurekebisha kanisa kwa kiwango kinachofaa. Badala yake, kulingana na Galenus Abrahamsz, ambaye alikuwa mmoja wa Collegiants na pia tabibu mashuhuri (1622-1706), hayo Marekebisho Makubwa ya Kidini yalifanya hali ya kidini iwe mbaya zaidi kwa kusababisha mizozo na chuki. Marekebisho ya kweli yapaswa kuubadili moyo, jambo ambalo Marekebisho Makubwa ya Kidini yalishindwa kufanya.
Kanisa na Makasisi. Makanisa mashuhuri ni yenye ufisadi, ya kilimwengu, na yasiyo na mamlaka ya kimungu. Uchaguzi mzuri zaidi ambao yeyote anayechukua dini kwa uzito angeweza kufanya ni kuacha kanisa lake ili asishiriki dhambi zake. Cheo cha ukasisi, Collegiants wakasema, ni kinyume cha Maandiko na “chenye kudhuru hali njema ya kiroho ya kutaniko la Kikristo.”
Ufalme na Paradiso. Mmoja wa waanzilishi wa college ya Amsterdam, Daniel de Breen (1594-1664), aliandika kwamba Ufalme wa Kristo haukuwa ufalme wa kiroho uliokaa moyoni mwa mtu. Mwalimu Jacob Ostens, mmoja wa Collegiants wa Rotterdam, alisema kwamba “wazee wa ukoo walitazamia kwa hamu ahadi za kidunia.” Vivyo hivyo, Collegiants walingojea wakati ambapo dunia ingegeuzwa kuwa paradiso.
Utatu. Baadhi ya Collegiants mashuhuri, walioathiriwa na itikadi za Wasosini, waliukataa Utatu.c Kwa mfano, Daniel Zwicker (1621-1678) aliandika kwamba fundisho lolote lisilopatana na sababu, kama vile Utatu, lilikuwa “jambo lisilowezekana na la uwongo.” Katika mwaka wa 1694 tafsiri ya Biblia iliyotafsiriwa na Collegiant aliyeitwa Reijnier Rooleeuw, ilichapishwa. Ilitafsiri sehemu ya mwisho ya Yohana 1:1 hivi: “Na neno alikuwa mungu” badala ya tafsiri ya kidesturi: “Na neno alikuwa Mungu.”d
Mikutano ya Kila Juma
Ingawa Collegiants wote hawakupatana kwa habari ya itikadi, colleges zao katika majiji mbalimbali zilifanya kazi kwa njia iliyofanana kabisa. Mwanahistoria Van Slee aripoti kwamba katika siku za mapema za harakati ya Collegiants, mikutano haikutayarishwa mapema. Collegiants walionelea kwamba kwa kutegemea maneno ya mtume Paulo kuhusu uhitaji wa “kutoa unabii,” washiriki wote wanaume wangeweza kuhutubia college hiyo kwa uhuru. (1 Wakorintho 14:1, 3, 26) Tokeo likawa kwamba, mara nyingi mikutano iliendelea hadi usiku sana na baadhi ya wahudhuriaji “walilala fofofo.”
Baadaye, mikutano ilipangwa vizuri zaidi. Collegiants walikutana Jumapili na pia jioni za katikati ya juma. Ili kumwezesha msemaji na kutaniko lijitayarishe mapema kwa ajili ya mikutano yote ya mwaka huo, programu iliyochapishwa iliorodhesha mistari ya Biblia ambayo ingechunguzwa na vilevile herufi za kwanza za jina la msemaji. Baada ya mkutano kufunguliwa kwa wimbo na sala, msemaji alifafanua mistari hiyo ya Biblia. Alipomaliza, aliomba wanaume watoe maelezo juu ya kichwa kilichokuwa kimetoka tu kuzungumziwa. Kisha msemaji wa pili alionyesha matumizi ya mistari hiyohiyo. Mikutano ilifungwa kwa wimbo na sala.
Collegiants wa jiji la Harlingen, katika jimbo la Friesland, walikuwa na njia yenye kuvutia ya kufuata wakati ulioratibiwa kwa ajili ya mikutano yao. Msemaji aliyezidisha wakati alipaswa kulipa faini ndogo.
Makusanyiko ya Kitaifa
Collegiants pia waliona uhitaji wa makusanyiko makubwa zaidi. Hivyo, kuanzia mwaka wa 1640, Collegiants kutoka nchini mwote walisafiri mara mbili kwa mwaka (wakati wa masika na wa kiangazi) kwenda Rijnsburg. Makusanyiko hayo, mwanahistoria Fix aandika, yaliwatolea nafasi ya “kufahamu mawazo, hisia, itikadi, na shughuli za ndugu zao waliotoka kila mahali.”
Baadhi ya Collegiants waliozuru walipanga vyumba vya wanakijiji ilhali wengine walikaa katika Groote Huis, au Jumba Kubwa, lenye vyumba 30 lililomilikiwa na hao Collegiants. Milo ya pamoja ya watu 60 hadi 70 iliandaliwa humo. Baada ya mlo, wageni wangeweza kutembea-tembea katika bustani kubwa ya jumba hilo ili kufurahia ‘kazi za Mungu, mazungumzo yenye utulivu, au kipindi kifupi cha kutafakari.’
Ingawa sio Collegiants wote walioona ubatizo kuwa jambo la lazima, wengi walibatizwa. Hivyo, ubatizo ukawa sehemu kuu ya makusanyiko makubwa. Mwanahistoria Van Slee asema kwamba kwa kawaida sherehe hiyo ilifanywa Jumamosi asubuhi. Wimbo na sala zilifuatiwa na hotuba juu ya uhitaji wa kuzamishwa. Ndipo msemaji alipowaomba watu wazima waliotaka kubatizwa kukiri imani yao, kama vile, “Naamini kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu aliye hai.” Baada ya hotuba kumalizwa kwa sala, wote waliokuwepo walitembea kwenda kwenye kidimbwi cha kubatizia na kushuhudia wanaume na wanawake waliopiga magoti ndani ya kidimbwi, hivi kwamba maji yalifika kwenye mabega. Kisha mbatizaji alikiinamisha mbele polepole kichwa cha mwamini mpya na kukiingiza ndani ya maji. Baada ya sherehe hiyo, wote walirudi kwenye viti vyao kwa ajili ya hotuba nyingine.
Jumamosi saa 11:00 alasiri, mkutano halisi ulianza kwa usomaji mfupi wa Biblia, wimbo, na sala. Ili kuhakikisha kwamba sikuzote kulikuwepo msemaji, colleges za Rotterdam, Leiden, Amsterdam, na Uholanzi Kaskazini, zilitoa wasemaji kwa zamu kwa ajili ya kila kusanyiko. Jumapili asubuhi iliwekwa kando kwa ajili ya kusherehekea Mlo wa Jioni wa Bwana. Baada ya hotuba, sala, na wimbo, wanaume, kisha wanawake,walishiriki mkate na divai. Hotuba zaidi zilifuata Jumapili jioni, na Jumatatu asubuhi wote walikusanyika kwa ajili ya hotuba ya kumalizia. Hotuba nyingi zilizotolewa kwenye mikusanyiko hiyo, asema Van Slee, zilihusu utendaji, zikikazia zaidi kutumia yale waliyojifunza kuliko kuyafafanua tu.
Kijiji cha Rijnsburg kilifurahia kuwa mwenyeji wa makusanyiko hayo. Mchunguzi mmoja wa karne ya 18 aliandika kwamba kuingia kwa wageni wengi waliotumia pesa kununulia vyakula na vinywaji, kulikiletea kijiji hicho mapato mazuri. Isitoshe, baada ya kila mkusanyiko, Collegiants walichangia maskini wa Rijnsburg kiasi fulani cha pesa. Bila shaka, kijiji hicho kilipata hasara mikutano hiyo ilipokomeshwa mwaka wa 1787. Baadaye, harakati ya Collegiant ikafifia. Kwa nini?
Kwa Nini Walififia
Kufikia mwisho wa karne ya 17, ubishi ulikuwa umezuka kuhusu fungu ambalo kusababu kulitimiza katika dini. Baadhi ya Collegiants walionelea kwamba kusababu kwa kibinadamu kulipasa kutangulizwa mbele ya ufunuo wa kimungu, lakini wengine hawakukubali hilo. Hatimaye, ubishi huo uligawanya harakati nzima ya Collegiants. Waliungana tena baada tu ya kifo cha watetezi wakuu wa pande hizo mbili za ubishi. Hata hivyo, baada ya mgawanyiko huo, harakati hiyo “haikupata tena kuwa jinsi ilivyokuwa,” asema mwanahistoria Fix.
Hali ya uvumilivu iliyoongezeka katika makanisa ya Kiprotestanti ya karne ya 18, pia ilichangia kufifia kwa Collegiants. Kadiri kanuni za kusababu na uvumilivu wa Collegiants zilivyozidi kukubaliwa na jamii kwa ujumla, ndivyo “ile nuru ya pekee, ambayo wakati mmoja Collegiantism ilitoa, ilivyozidi kufifia kwenye pambazuko jangavu la ile Enzi ya Kusababu.” Kufikia mwisho wa karne ya 18, Collegiants walio wengi wakawa sehemu ya Wamenoni na vikundi vingine vya kidini.
Kwa kuwa Collegiants hawakunuia kuwa na muungano wa fikira katika harakati yao, walikuwa na maoni mengi tofauti, idadi yake ikiwa karibu sawa na ya Collegiants wenyewe. Walitambua jambo hilo na hivyo, hawakudai kuwa “wameunganishwa kwa kufaa katika akili ileile na katika mstari uleule wa fikira,” kama mtume Paulo anavyowasihi Wakristo wawe. (1 Wakorintho 1:10) Hata hivyo, wakati huohuo, Collegiants walitazamia kwa hamu wakati ambapo itikadi za kimsingi za Ukristo, kama vile muungano wa fikira, zingekuwa mambo hakika.
Kwa kufikiria uhakika wa kwamba ujuzi wa kweli ulikuwa bado mdogo siku za Collegiants, wao waliweka kielelezo ambacho dini nyingi leo zinaweza kuiga. (Linganisha Danieli 12:4.) Kule kukazia kwao uhitaji wa funzo la Biblia kulipatana na shauri hili la mtume Paulo: “Hakikisheni mambo yote.” (1 Wathesalonike 5:21) Funzo la Biblia la kibinafsi lilimfahamisha Jacobus Arminius na wengine kwamba mafundisho fulani ya kidini na mazoea ambayo yamefundishwa kwa muda mrefu hayakutegemea Biblia hata kidogo. Walipong’amua jambo hilo, walikuwa na ujasiri wa kutofautiana na dini mashuhuri. Je, wewe ungefanya vivyo hivyo?
[Maelezo ya Chini]
a Katika mwaka wa 1610, wabishi hao walikuwa wamepeleka malalamishi rasmi (hati iliyoonyesha sababu za kupinga) kwa watawala wa Uholanzi. Baada ya kufanya hivyo waliitwa Walalamishi.
b Collegiants pia waliitwa Wakazi wa Rijnsburg, kwa sababu ya eneo hili.
c Ona Amkeni! la Februari 8, 1990, ukurasa wa 15, “Wasosini—Kwa Nini Walikataa Utatu?”
d Het Nieuwe Testament van onze Heer Jezus Christus, uit het Grieksch vertaald door Reijnier Rooleeuw, M.D. (Agano Jipya la Bwana Wetu Yesu Kristo, iliyotafsiriwa kutoka Kigiriki na Reijnier Rooleeuw, M.D.)
[Picha katika ukurasa wa 24]
Rembrandt van Rijn
[Picha katika ukurasa wa 26]
Kijiji cha Warmond ambacho ndicho chimbuko la “Collegiants,” na Mto De Vliet ambapo ubatizo ulifanyiwa
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 23]
Mandharinyuma: Courtesy of the American Bible Society Library, New York