Je, Kuna Yeyote Anayejali Kikweli?
“Machozi yao waliodhulumiwa” yamekuwa mengi sana. Hayo ni machozi ya watu wanaofanyiwa “madhalimu” mengi sana ulimwenguni pote. Mara nyingi wale wanaodhulumiwa huona kwamba “hawana mfariji”—kwamba hakuna yeyote anayewajali kikweli.—Mhubiri 4:1.
LICHA ya machozi hayo mengi, wengine hawaathiriwi na kuteseka kwa wanadamu wenzao. Wao hupuuza kimakusudi maumivu ya watu wengine, kama vile kasisi na Mlawi walivyofanya katika kielezi cha Yesu Kristo cha mtu aliyeshambuliwa, akapokonywa, akaachwa nusura kufa. (Luka 10:30-32) Maadamu hali yao na ya familia yao ni nzuri kwa kadiri fulani, wao hawajali wengine. Hivyo, ni kama kusema, “Nani anayejali?”
Hilo halipaswi kutushangaza. Mtume Paulo alitabiri kwamba katika “siku za mwisho” watu wengi wangekosa “shauku ya kiasili.” (2 Timotheo 3:1, 3) Mchunguzi mmoja alisikitikia mitazamo ya kutojali ambayo imesitawi. Alisema kwamba, “kanuni mpya ya ubinafsi inachukua mahali pa itikadi na mapokeo ya zamani ya watu wa Ireland ya kujali na kushirikiana.” Ulimwenguni pote, watu wana ubinafsi na hawajali sana hali mbaya ya wengine.
Uhitaji wa Kuwa na Mtu Anayejali
Bila shaka, kuna uhitaji wa kuwa na mtu anayejali. Kwa mfano, fikiria mwanamume mpweke nchini Ujerumani “aliyekutwa ameketi mbele ya televisheni yake—miaka mitano baada ya kufa wakati wa Krismasi.” “Mkiwa [huyu] mlemavu, aliyekuwa ametalikiwa,” ambaye alitiwa uchungu na mambo yaliyompata maishani, alikumbukwa tu baada ya akaunti ya benki ya kulipia kodi yake ya nyumba kuisha. Hakuna aliyemjali kikweli.
Fikiria pia, wale watu hoi wanaoonewa na makabaila wenye nguvu na pupa. Katika eneo moja, takriban watu 200,000 (robo ya idadi ya watu) “walikufa kwa sababu ya kugandamizwa na kwa sababu ya njaa kuu” baada ya mashamba yao kunyakuliwa kijeuri. Au fikiria watoto walioona ukatili usioaminika. Ripoti moja ilisema hivi: “Idadi ya watoto katika [nchi moja] waliojionea ukatili mwingi—uuaji, mapigo, ubakaji, ambao wakati mwingine ulifanywa na wabalehe wenzao, ni kubwa mno.” Waweza kuelewa ni kwa nini mhasiriwa wa ukosefu huo wa haki aweza kuuliza kwa machozi, “Je, kuna yeyote anayenijali kikweli?”
Kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa, watu bilioni 1.3 katika nchi zinazoendelea wanalazimika kujiruzuku kwa kiasi cha fedha kinachopungua dola moja ya Marekani kila siku. Lazima wajiulize ikiwa kuna yeyote anayejali. Hali kadhalika maelfu ya wakimbizi ambao, kama isemavyo ripoti katika The Irish Times, “wanakabili uamuzi mgumu na usiopendeza wa kukaa katika kambi duni za wakimbizi au katika nchi isiyowataka au kujaribu kurudi katika nchi yao ambayo bado imesambaratika [au, imeharibiwa] na vita au mgawanyiko wa kikabila.” Ripoti hiyohiyo ilitia ndani zoezi hili lenye kuvunja moyo: “Funga macho yako, hesabu moja hadi tatu, mtoto mmoja tayari amekufa. Ni mmoja kati ya watoto 35,000 watakaokufa leo kutokana na utapiamlo au maradhi yanayoweza kuzuiwa.” Si ajabu kwamba wengi hupaza kilio kwa msononeko na uchungu!—Linganisha Ayubu 7:11.
Je, kwa kweli hali ilikusudiwa iwe hivyo? Kwa kweli je, kuna mtu yeyote ambaye licha ya kuwa mwenye kujali ana uwezo pia wa kukomesha kuteseka na kuondolea watu uchungu wote ambao umewapata?
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 2]
Cover and page 32: Reuters/Nikola Solic/Archive Photos
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
A. Boulat/Sipa Press