Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w02 1/1 kur. 4-7
  • Je, Inawezekana Kuwa na Jamii Isiyo na Ubaguzi?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Je, Inawezekana Kuwa na Jamii Isiyo na Ubaguzi?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2002
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Sote Tu Sawa Mbele za Mungu
  • Jamii Isiyo na Ubaguzi—Jinsi Gani?
  • Jamii Isiyo na Ubaguzi Leo
  • Usawa Hutokeza Jamii Yenye Watu Mbalimbali
  • Matatizo ya Ubaguzi wa Kijamii
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2002
  • Utafutaji wa Usawa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1985
  • Watu Wote ‘Ni sawa—Jinsi Gani?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1985
  • Baa la Sasa la Ukosefu wa Usawa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2002
w02 1/1 kur. 4-7

Je, Inawezekana Kuwa na Jamii Isiyo na Ubaguzi?

JOHN ADAMS, aliyekuwa rais wa pili wa Marekani alikuwa mmojawapo wa watu waliotia sahihi ile hati muhimu ya Azimio la Uhuru, ambayo ilitia ndani maneno haya: ‘Sisi tunaamini jambo hili kuwa kweli kabisa kwamba watu wote wameumbwa wakiwa na usawa.’ Hata hivyo, John Adams alikuwa na shaka kama watu kwa kweli wako na usawa, kwa kuwa aliandika hivi: ‘Mungu Mweza Yote amewaumba wanadamu wakiwa tofauti sana Kiakili na Kimwili hivi kwamba hakuna mpango au sera yoyote inayoweza kuwafanya wawe na usawa.’ Mwanahistoria Mwingereza, H. G. Wells, alikuwa na maoni tofauti. Yeye aliwazia jamii ya watu ambao wamefanywa wawe na usawa kwa msingi wa mambo haya matatu: dini safi ya ulimwenguni pote, elimu sawa kwa wote, na kutokuwepo kwa majeshi.

Kufikia sasa, hakujatokea jamii yenye usawa kama Wells alivyowazia. Kwa kweli, wanadamu hawana usawa, na ubaguzi wa kijamii umeenea sana. Je, ubaguzi huo umeinufaisha jamii kwa jumla? La. Ubaguzi wa kijamii hugawanya watu na kusababisha wivu, chuki, uchungu, na umwagikaji mwingi wa damu. Yale maoni yaliyokuweko Afrika, Australia, na Amerika Kaskazini zamani kwamba mtu mweupe ni bora kuliko mtu mweusi ilisababisha msiba mkubwa kwa watu weusi—kutia ndani kuangamizwa kabisa kwa wenyeji wa Australia (Aborigines) katika Eneo la Van Diemen (ambalo sasa linaitwa Tasmania). Huko Ulaya, yale Maangamizi ya Wayahudi yalisababishwa na kuwatenga Wayahudi kuwa watu wa hali ya chini. Utajiri wa watu wa cheo cha juu na kutoridhika miongoni mwa watu wa cheo cha kati na cha chini kulisababisha Mapinduzi ya Ufaransa ya karne ya 18 na Mapinduzi ya Bolshevik huko Urusi katika karne ya 20.

Mtu fulani wa zamani mwenye hekima aliandika: “Mtu anayo mamlaka juu ya mwenziwe kwa hasara yake.” (Mhubiri 8:9, chapa ya 1989) Maneno yake ni ya kweli hata iwe wale walio mamlakani ni watu mmoja-mmoja au ni vikundi vya watu. Wakati kikundi kimoja cha watu kinapojiinua juu ya wengine, kunatokea msiba na kuteseka.

Sote Tu Sawa Mbele za Mungu

Je, watu fulani walizaliwa wakiwa bora kuliko wengine? Si machoni pa Mungu. Biblia husema: “[Mungu] alifanya kutoka kwa mtu mmoja kila taifa la watu, ili wakae juu ya uso mzima wa dunia.” (Matendo 17:26) Isitoshe, Muumba ‘hapendelei nyuso za wakuu, wala hawajali matajiri kuliko maskini. Kwani wote ni kazi ya mikono yake.’ (Ayubu 34:19) Wanadamu wote ni jamii moja na wote huzaliwa wakiwa sawa mbele za Mungu.

Kumbuka pia kwamba mtu akifa hawezi kujidai kuwa bora kuliko wengine. Wamisri wa kale hawakuamini jambo hilo. Farao alipokufa, waliweka vitu vyenye thamani kwenye kaburi lake ili aweze kuvifurahia huku akiendelea kushikilia cheo chake cha juu katika maisha ya baada ya kifo. Je, alitumia vitu hivyo? La. Vingi vya vitu hivyo viliibwa na wezi wa makaburini, na vingine vingi ambavyo havikuibwa vinaweza kuonekana leo katika majumba ya makumbusho.

Farao hangeweza kutumia vitu hivyo vyenye thamani kwa sababu alikuwa amekufa. Kaburini, hakuna mtu wa cheo cha juu wala cha chini, hakuna tajiri wala maskini. Biblia husema: “Wenye hekima hufa; mpumbavu na mjinga hupotea pamoja, na kuwaachia wengine mali zao. Lakini mwanadamu hadumu katika heshima, bali amefanana na wanyama wapoteao.” (Zaburi 49:10, 12) Tuwe wafalme au watumwa, maneno haya yaliyopuliziwa yanatuhusu sote: “Wafu hawajui neno lo lote, wala hawana ijara tena . . . Hakuna kazi, wala shauri, wala maarifa, wala hekima, huko kuzimu uendako wewe.”—Mhubiri 9:5, 10.

Sote huzaliwa tukiwa sawa machoni pa Mungu, na sote tunakuwa sawa tunapokufa. Ni jambo lisilofaa namna gani kutukuza watu fulani kuwa bora kuliko wengine katika maisha haya mafupi!

Jamii Isiyo na Ubaguzi—Jinsi Gani?

Lakini, je, kuna matumaini yoyote kwamba siku moja kutakuwa na watu ambao hawataona ubaguzi wa kijamii kuwa jambo la maana? Naam, kuna matumaini. Yesu alipokuwa duniani miaka 2,000 hivi iliyopita, msingi uliwekwa kwa ajili ya jamii kama hiyo. Yesu alitoa uhai wake kuwa dhabihu ya fidia kwa ajili ya wanadamu wote wanaoamini ili “kila mtu anayedhihirisha imani katika yeye asipate kuangamizwa bali awe na uhai udumuo milele.”—Yohana 3:16.

Akionyesha kwamba wafuasi wake hawapaswi kujitukuza juu ya waamini wenzao, Yesu alisema: “Nyinyi, msiitwe Rabi, kwa maana mmoja ni mwalimu wenu, lakini nyinyi nyote ni akina ndugu. Zaidi ya hayo, msiite yeyote baba yenu duniani, kwa maana mmoja ni Baba yenu, Aliye wa kimbingu. Wala msiitwe ‘viongozi,’ kwa maana Kiongozi wenu ni mmoja, Kristo. Lakini aliye mkubwa zaidi sana miongoni mwenu lazima awe mhudumu wenu. Yeyote yule ajikwezaye mwenyewe atanyenyekezwa.” (Mathayo 23:8-12) Mbele ya macho ya Mungu, wanafunzi wote wa kweli wa Yesu wako na usawa katika imani.

Je, Wakristo wa mapema walijiona kuwa na usawa? Wale walioelewa mafundisho ya Yesu walijiona kuwa na usawa. Walijiona kuwa na usawa katika imani, wakionyesha hivyo kwa kuitana “ndugu.” (Filemoni 1, 7, 20) Hakuna mtu aliyehimizwa ajione kuwa bora kuliko wengine. Fikiria jinsi Petro alivyozungumza kwa unyenyekevu kujihusu katika barua yake ya pili: “Simoni Petro, mtumwa na mtume wa Yesu Kristo, kwa wale ambao wamepata imani, yenye kushikiliwa katika pendeleo lililo sawa na letu.” (2 Petro 1:1) Petro alikuwa amefunzwa na Yesu mwenyewe, na akiwa mtume, alikuwa na madaraka muhimu. Hata hivyo, alijiona kuwa mtumwa na alitambua kwamba Wakristo wengine walishikilia imani katika pendeleo lililo sawa naye.

Huenda wengine wakasema kwamba kabla ya Ukristo, Mungu aliwafanya Waisraeli kuwa taifa lake la pekee, jambo lililo kinyume cha kanuni ya usawa. (Kutoka 19:5, 6) Huenda wakadai kwamba hiyo ilionyesha kwamba Waisraeli walikuwa bora, lakini hivyo si kweli. Ni kweli kwamba Waisraeli wakiwa wazao wa Abrahamu, walikuwa na uhusiano wa pekee na Mungu naye aliwatumia kujulisha watu ufunuo wake. (Waroma 3:1, 2) Lakini kusudi la Mungu halikuwa kuwatukuza. Badala yake, alitaka ‘mataifa yote ya dunia yajibarikie.’—Mwanzo 22:18; Wagalatia 3:8.

Hatimaye, Waisraeli wengi walishindwa kuiga imani ya babu yao Abrahamu. Walikosa imani na kumkataa Yesu kuwa Mesiya. Kwa sababu hiyo, Mungu aliwakataa. (Mathayo 21:43) Hata hivyo, wale waliokuwa wanyenyekevu walipata baraka zilizoahidiwa. Kutaniko la Kikristo lilianzishwa Pentekoste 33 W.K. Tengenezo hilo la Wakristo waliotiwa mafuta na roho takatifu liliitwa “Israeli wa Mungu,” na ndilo lingetumiwa kuleta baraka hizo.—Wagalatia 6:16.

Washiriki fulani wa kutaniko hilo walihitaji kufundishwa kuhusu usawa. Kwa mfano, mwanafunzi Yakobo aliwashauri wale waliowaheshimu zaidi Wakristo matajiri kuliko maskini. (Yakobo 2:1-4) Haikufaa kufanya hivyo. Mtume Paulo alionyesha kwamba Wakristo Wayahudi hawakuwa bora kuliko Wakristo wasio Wayahudi, nao Wakristo wanaume hawakuwa bora kuliko Wakristo wanawake. Aliandika hivi: “Kwa kweli, nyinyi nyote ni wana wa Mungu kupitia imani yenu katika Kristo Yesu. Kwa maana nyinyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hakuna Myahudi wala Mgiriki, hakuna mtumwa wala mtu huru, hakuna wa kiume wala wa kike; kwa maana nyinyi nyote ni mtu mmoja katika muungano na Kristo Yesu.”—Wagalatia 3:26-28.

Jamii Isiyo na Ubaguzi Leo

Mashahidi wa Yehova leo hujitahidi kuishi kulingana na kanuni za Maandiko. Wanajua kwamba ubaguzi wa kijamii hauna maana machoni pa Mungu. Hivyo, wao hawana jamii ya makasisi na ya watu wa kawaida, nao hawatenganishwi kulingana na rangi ya ngozi yao wala utajiri. Ingawa huenda ikawa baadhi yao ni matajiri, wao hawazingatii “wonyesho wa mtu wa kujivunia njia yake ya kutegemeza maisha,” kwa kuwa wanajua mambo hayo ni ya muda tu. (1 Yohana 2:15-17) Badala yake, wote wameunganishwa na ibada yao kwa Mwenye Enzi Kuu ya Ulimwengu Wote, Yehova Mungu.

Kila mmoja wao hukubali daraka la kushiriki katika kazi ya kuwahubiria wanadamu wenzake habari njema za Ufalme. Kama Yesu, wao huheshimu wanaoonewa na kupuuzwa kwa kuwatembelea nyumbani kwao na kujitolea kuwafunza Neno la Mungu. Wale wa hali ya chini hufanya kazi bega kwa bega na wale wanaoonekana kuwa wa cheo cha juu. Sifa za kiroho ndizo muhimu kuliko cheo cha mtu katika jamii. Kama ilivyokuwa katika karne ya kwanza, wote ni ndugu na dada katika imani.

Usawa Hutokeza Jamii Yenye Watu Mbalimbali

Bila shaka, usawa haumaanishi kwamba watu watafanana kabisa. Katika tengenezo la Kikristo kuna wanaume, wanawake, wazee, na vijana wanaotoka katika jamii, lugha, mataifa, na uchumi mbalimbali. Kila mmoja ana uwezo tofauti wa kiakili na wa kimwili. Lakini tofauti hizo hazifanyi baadhi yao kuwa bora kuliko wengine au wengine kuwa duni. Badala yake, tofauti hizo hutokeza jamii yenye watu mbalimbali, yenye kupendeza. Wakristo hao hutambua kwamba vipawa vyovyote walivyo navyo ni zawadi kutoka kwa Mungu na havipaswi kuwafanya wajione kuwa bora.

Ubaguzi wa kijamii husababishwa na mwanadamu anapojaribu kujitawala mwenyewe badala ya kufuata mwongozo wa Mungu. Karibuni, Ufalme wa Mungu utaanza kuitawala dunia, na matokeo yatakuwa kwamba ubaguzi wa kijamii ambao husababishwa na mwanadamu utaondolewa, pamoja na mambo mengine ambayo yamesababisha kuteseka wakati uliopita. Kisha ‘wapole watairithi nchi’ kihalisi. (Zaburi 37:11) Hakuna atakayekuwa na sababu yoyote ya kujiona kuwa bora. Ubaguzi wa kijamii hautaruhusiwa kugawanya udugu wa ulimwenguni pote wa wanadamu.

[Maelezo ya Picha katika ukurasa wa 5]

Muumba ‘hapendelei nyuso za wakuu, wala hawajali matajiri kuliko maskini. Kwani wote ni kazi ya mikono yake.’—Ayubu 34:19.

[Maelezo ya Picha katika ukurasa wa 6]

Mashahidi wa Yehova huwaheshimu majirani wao

[Maelezo ya Picha katika ukurasa wa 7]

Sifa za kiroho ndizo muhimu miongoni mwa Wakristo wa kweli

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki