Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w14 2/1 kur. 5-7
  • Msababishaji Mkuu wa Vita na Kuteseka

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Msababishaji Mkuu wa Vita na Kuteseka
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2014
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • ISHARA YA SIKU ZA MWISHO
  • KUZIVUNJA KAZI ZA IBILISI
  • Wapanda Farasi Wanne​—Jinsi Wanavyokuhusu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Toleo la Watu wote)—2017
  • Mpanda Farasi wa Ufalme Aendelea
    “Ufalme Wako Uje”
  • Kazi Tukufu Inayofuata Uendeshaji wa Wapanda-Farasi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1983
  • Vita Ambayo Itavimaliza Vita
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1988
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2014
w14 2/1 kur. 5-7

HABARI KUU | VITA VILIVYOUBADILI ULIMWENGU

Msababishaji Mkuu wa Vita na Kuteseka

Vita vya Kwanza vya Ulimwengu viliisha Novemba 11, 1918. Biashara zilifungwa, na watu wakashangilia kwa vifijo na nderemo barabarani. Lakini shangwe hiyo haikudumu. Tisho lingine hatari zaidi kuliko bunduki lilifuata punde tu baada ya vita vya ulimwengu.

Mnamo Juni 1918, wanajeshi waliokuwa vitani huko Ufaransa waliambukizwa ugonjwa wenye kuua unaojulikana kama homa ya Hispania. Punde si punde, homa hiyo ilithibitika kuwa hatari sana. Kwa mfano, kwa miezi michache tu iliua wanajeshi wengi wa Marekani nchini Ufaransa kuliko wale waliouawa vitani. Baada ya vita wanajeshi waliokuwa wameambukizwa walirudi makwao na hivyo kueneza ugonjwa huo haraka ulimwenguni pote.

Miaka iliyofuata baada ya vita ilikuwa na njaa na hali mbaya ya kiuchumi. Watu wengi barani Ulaya hawakuwa na chakula vita vilipokoma katika mwaka wa 1918. Kufikia mwaka wa 1923, pesa za Ujerumani hazikuwa na thamani yoyote. Miaka sita baadaye, uchumi ulimwenguni pote uliporomoka. Mwishowe, mwaka wa 1939, Vita vya Pili vya Ulimwengu vikaanza,​—na kwa njia fulani vilikuwa mwendelezo wa Vita vya Kwanza vya Ulimwengu. Ni nini kilichokuwa kikisababisha misiba hiyo iliyofuatana?

ISHARA YA SIKU ZA MWISHO

Unabii wa Biblia unatusaidia kujua kilichosababisha matukio fulani ya kihistoria, na hasa Vita vya Kwanza vya Ulimwengu. Yesu Kristo alitabiri wakati ambapo ‘taifa lingesimama kupigana na taifa’ na kungekuwa na upungufu wa chakula na tauni duniani kote. (Mathayo 24:3, 7; Luka 21:10, 11) Aliwaambia wanafunzi wake kwamba misiba hiyo ingekuwa sehemu ya ishara ya siku za mwisho. Habari zaidi zinapatikana katika kitabu cha Ufunuo, ambacho kinaonyesha kwamba matatizo yaliyo duniani yalisababishwa na vita vilivyotokea mbinguni.—Ona sanduku “Vita Duniani na Vita Mbinguni.”

Kitabu hicho pia kinataja wapanda-farasi wanne. Wapanda-farasi watatu wanafananisha misiba ileile ambayo Yesu alikuwa ametabiri, yaani, vita, njaa, na tauni. (​—Ona sanduku“Je, Kweli Wale Wapanda-Farasi Wanne Wako Mwendoni?”) Ni wazi kwamba vita vya kwanza vya ulimwengu vilianzisha matatizo ambayo bado yanaendelea mpaka leo. Biblia inafunua kwamba Shetani ndiye aliyeianzisha. (1 Yohana 5:19) Je, kuna yeyote anayeweza kumzuia?

Kitabu cha Ufunuo pia kinatuhakikishia kwamba Shetani ana “kipindi kifupi cha wakati.” (Ufunuo 12:12) Hiyo ndiyo sababu amejawa na hasira na anachochea uovu usio na kifani hapa duniani. Hata hivyo, matatizo tunayoona yanathibitisha kwamba muda wake unakaribia kwisha.

KUZIVUNJA KAZI ZA IBILISI

Kwa kweli Vita vya Kwanza vya Ulimwengu vilileta mabadiliko makubwa katika historia. Vilileta kipindi cha vita chenye maasi na kufanya watu wasiwaamini watawala. Pia, ni uthibitisho ulio wazi kwamba Shetani alikuwa amefukuzwa mbinguni. (Ufunuo 12:9) Mtawala huyo wa ulimwengu asiyeonekana alitenda kama dikteta mkatili ambaye anajua siku zake zimehesabiwa. Siku zake zitakwisha, matatizo ambayo yalisababishwa na Vita vya Kwanza vya Ulimwengu yatakoma.

Baada ya kuchunguza unabii wa Biblia, una sababu ya kuamini kwamba hivi karibuni Yesu Kristo, Mfalme wetu aliye mbinguni, ‘atazivunja kazi za Ibilisi.’ (1 Yohana 3:8) Tayari mamilioni ya watu wanasali Ufalme wa Mungu uje. Je, wewe husali hivyo? Kupitia Ufalme huo, watu waaminifu wataona mapenzi ya Mungu, bali si ya Shetani, yakitendeka duniani. (Mathayo 6:9, 10) Chini ya Ufalme wa Mungu, hakutakuwa tena na vita vya ulimwengu au vita vyovyote vile! (Zaburi 46:9) Jifunze kuhusu Ufalme huo ili uishi wakati ambapo kutakuwa na amani duniani!—Isaya 9:6, 7.

Vita Duniani na Vita Mbinguni

Karne 19 kabla ya Vita vya Kwanza vya Ulimwengu, Shetani alitaka kumpa Yesu “falme zote za ulimwengu.” (Mathayo 4:8, 9) Yesu alikataa kishawishi hicho, na baadaye akamtaja Ibilisi kuwa “mtawala wa ulimwengu.” (Yohana 14:30) Kwa kuongezea, mtume Yohana aliandika kwamba “ulimwengu mzima unakaa katika nguvu za yule mwovu.”​—1 Yohana 5:19.

Kwa kuwa Shetani Ibilisi ndiye mtawala wa ulimwengu, inapatana na akili kusema kwamba yeye ndiye aliyesababisha vita vya kwanza vya ulimwengu na matokeo yake. Kwa kweli, kitabu cha Ufunuo kinaonyesha kwamba Shetani ndiye aliyesababisha misiba ambayo imetokea duniani tangu mwaka wa 1914. Ufuatao ni mfuatano wa matukio yanayotajwa kwenye Ufunuo sura ya 12:

  • Mstari wa 7 Vita vinatokea mbinguni kati ya Mikaeli (Yesu Kristo) na yule joka mkubwa (Shetani).

  • Mstari wa 9 Ibilisi, “anayeipotosha dunia nzima inayokaliwa,” anatupwa duniani.

  • Mstari wa 12 “Ole wa dunia na wa bahari, kwa sababu Ibilisi ameshuka kwenu, akiwa na hasira kali, akijua kwamba ana kipindi kifupi cha wakati.”

Mfuatano wa matukio ya Biblia na matukio ya ulimwengu unaonyesha kwamba vita hivyo vya mbinguni vilipiganwa baada ya Ufalme wa Mungu kusimamishwa mbinguni mwaka wa 1914.a Kwa hiyo, vita vilitokea duniani na mbinguni katika mwaka huo muhimu.

a Ona sura ya 8 ya kitabu Biblia Inafundisha Nini Hasa? kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova.

Je, Kweli Wale Wapanda-Farasi Wanne Wako Mwendoni?

Farasi mweupe akiendeshwa na mfalme wa kimbingu

Mpandaji wa farasi mweupe ni mfalme mbinguni. Mfalme Yesu Kristo anamwendesha farasi huyo kwa kutetea uadilifu. (Zaburi 45:4) Jukumu lake la kwanza lilikuwa kumwondoa Shetani na mashetani wake kutoka mbinguni.​—Ufunuo 6:2; 12:9.

Farasi wa rangi ya moto na wanajeshi wakiwa vitani

Mpandaji wa farasi wa rangi ya moto amepewa mamlaka “ya kuondoa amani duniani.” (Ufunuo 6:4) Tangu mwaka wa 1914, vita vimewakumba wanadamu. Miaka 21 tu baada ya Vita vya Kwanza vya Ulimwengu, Vita vya Pili vya Ulimwengu vilianza na kuwaua watu wengi zaidi. Kadirio moja linasema kwamba Vita vya Pili vya Ulimwengu viliwaua watu milioni 60 hivi. Tangu mwaka wa 1945, kumekuwa na vita katika nchi mbalimbali lakini vilevile vimekuwa vya kikatili. Wanahistoria fulani wanakadiria kwamba watu zaidi ya milioni mia moja wamepoteza maisha yao vitani katika karne ya 20.

Farasi mweusi na watoto wengi wenye njaa

Mpandaji wa farasi mweusi ana mizani mkononi mwake inayofananisha njaa. (Ufunuo 6:5, 6) Wakati wa vita vya kwanza vya ulimwengu, majeshi ya Muungano yalizuia chakula kisiingizwe Ujerumani na hivyo kusababisha Wajerumani 750,000 hivi wafe njaa. Zaidi ya watu milioni mbili walikufa njaa nchini Urusi mwaka wa 1921, na nchi nyingine zilipatwa na msiba huohuo. Kwa ujumla, inakadiriwa kwamba watu milioni 70 walikufa njaa katika karne ya 20. Kila mwaka, ukosefu wa chakula chenye lishe bado husababisha vifo vya zaidi ya watoto milioni tatu walio chini ya umri wa miaka mitano.

Farasi wa kijivu na wagonjwa waliolazwa

Mpandaji wa farasi wa kijivu analeta kifo kwa pigo lenye kufisha. (Ufunuo 6:8) Homa ya Hispania ndio iliyokuwa tauni ya kwanza kuua watu wengi sana katika karne ya 20. Takwimu zinatofautiana, lakini kadirio moja linasema kwamba homa hiyo iliua watu milioni 50 hivi. “Ugonjwa huo wa kuambukiza ulikuwa mojawapo ya misiba mibaya sana katika historia,” kinasema kitabu kimoja (Man and Microbes). Kitabu hicho kinaendelea kusema kwamba “hata tauni ya majipu haikuua watu wengi na kwa haraka hivyo.” Ndui, malaria, na kifua kikuu ni magonjwa mengine ya kuambukiza ambayo yameua mamia ya mamilioni ya watu katika karne ya 20.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki