Kula Asali Kutokana na Mnyama Aliyekufa Zamani
■ Watu wengine wameshangazwa na kifungu kilichomo katika Waamuzi 14:8, 9, ambamo Samsoni anaelezwa kama akikomba asali kutoka kwa simba aliyekufa. Simba aliyekufa angewezaje kuwa mzinga wa nyuki? Hili ni ulizo lililoulizwa na msomaji wa Melbourne (Australia) Age, na jibu lilitokea katika gazeti hilo chini ya kichwa “Naturalist’s Diary.” Mwandikaji, H. A. Lindsay, alisema hivi:
“Maelezo peke yake niwezayo kutoa ni kwamba huu unaelekea kuwa uhakika wa wazi. Katika Palestina kulikuwako—na kungali kuna—upungufu wa miti yenye matundu ambamo nyuki-mwitu wanaweza kuanzisha jamii. Kwa sababu hiyo, wanatumia mianya ya miamba, matundu ya pembeni katika mapango, na hata matundu nchini.
“Katika majira ya ukavu ya jimbo hili, hasa katika kiangazi, mzoga wa mnyama mwenye ngozi ngumu, ukiachwa bila kuzikwa, karibuni unakuwa gofu lenye ngozi ngumu juu yake. Kwa kukosa mahali pazuri zaidi, nyuki-mwitu wanatumia shimo la kifua kama mahali pa mzinga.
“Hili si kisio, kwa sababu mimi naweza kutaja habari inayolingana na hiyo. Booborowie, Australia ya Kusini, ni uwanda mpana usio na miti wenye kujawa na mashamba ya kuchungia wanyama yenye mimea inayoitwa lucerne. Mmea huu wa kulishia wanyama unatoa asali nyingi sana wakati wa miezi ya kiangazi.
“Mwaka wa 1927 nilikuwa ninatembea juu ya kilima upande wa kusini wa mashamba ya lucerne nikaja kwenye mzoga wa farasi aliyekuwa amekufa miezi mingi iliyopita. Sasa alikuwa ngozi iliyokaushwa na jua iliyokaa juu ya gofu la mwili. Niliodhani kuwa wingi wa mainzi ya nyama ulikuwa wingi wa nyuki. . . . Nikaweza kufanya Samsoni alivyokuwa amefanya zaidi ya miaka 3000 iliyopita; nikala asali kadiri fulani kutoka mzinga uliokuwa umeanzishwa katika mzoga wa mnyama aliyekufa zamani.”—Novemba 21, 1960, ukurasa 17.