Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g90 10/8 kur. 17-19
  • Nifanye Nini Wazazi Wangu Wakipigana?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Nifanye Nini Wazazi Wangu Wakipigana?
  • Amkeni!—1990
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Jambo la Kutofanya
  • Kuokoka Mgogoro Mkubwa wa Familia
  • Nifanye Nini Wazazi Wangu Wanapogombana?
    Maswali Ambayo Vijana Huuliza—Majibu Yafanyayo Kazi, Buku la 2
  • Nifanye nini wazazi wangu wanapobishana?
    Amkeni!—2007
  • Kwa Nini Mama na Baba Hupigana Sikuzote?
    Amkeni!—1990
  • Ninawezaje Kuwafahamu Wazazi Wangu Vizuri Zaidi?
    Amkeni!—2009
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1990
g90 10/8 kur. 17-19

Vijana Wauliza . . .

Nifanye Nini Wazazi Wangu Wakipigana?

WAKATI watu wawili upendao zaidi ya mtu mwingine yeyote ulimwenguni ‘wanapoumana na kulana’ kwa maneno yenye kuumiza, maisha yaweza kuwa jinamizi la kila siku. (Wagalatia 5:15) Ni kweli kwamba hata ndoa zilizo bora kabisa zitapatwa na “dhiki” fulani. (1 Wakorintho 7:28) Lakini mzozano wa wazazi uwapo usiomalizika, wenye ukorofi, au hata wenye jeuri, kuna kasoro nzito.

Basi, si ajabu kwamba vijana fulani hujihangaisha sana wakijaribu kutengeneza ndoa ya wazazi wao. “Mimi hata nimejiingiza katikati ya pigano na kujaribu kumwondoa baba yangu chumbani ili waache kupigana,” akasema mvulana mmoja tineja. Wengine hujiondoa mahali hapo kwa kimya cha kuvurugika akili. “Mimi hujaribu kukaa mbali nao wakati wawapo na mapigano haya, ili jambo hilo lisinishushe moyo,” akasema msichana mmoja mchanga. “Lakini ndipo mimi huhisi hatia kwa sababu sikujaribu kusaidia.”

Kwa hiyo yakupasa ufanye nini hasa wakati pigano kali la kifamilia lifokapo?

Jambo la Kutofanya

Usiwatendee kwa Kukosa Heshima: Ni rahisi kukata tamaa kabisa kuhusu wazazi wanaogombana. Ingawaje, wao ndio wapaswao kukuwekea wewe kielelezo—si wewe uwawekee wao. Ingawa hivyo, kutendea mzazi kimadharau yaelekea kutaongezea tu mivutano ya familia. La maana zaidi, Yehova Mungu huamuru vijana wastahi na kutii wazazi wao, hata wakati wao wafanyapo iwe vigumu kutenda hivyo.—Kutoka 20:12; linganisha Mithali 30:17.

Usijiunge na Upande Wowote: “Nyakati fulani wazazi wangu wanapobishana,” akasema msichana mmoja tineja, “mmoja wao ataniuliza mimi naonaje. Hiyo hunitia wasiwasi sana.” Bila shaka, wakati suala fulani likuhusupo wewe moja kwa moja, huenda ikafaa kutoa jibu pole lenye staha.—Mithali 15:1.

Au huenda ikawa kwamba mmoja wa wazazi wako ni Mkristo na yule mwingine si mwamini. Huenda magumu ya kidini yakatokea ambamo huenda wewe ukapata yahitajika kabisa kusimama upande wa uadilifu pamoja na mzazi anayemhofu Mungu. (Mathayo 10:34-37) Hata hivyo, wapaswa kufanya hivyo “kwa upole na staha ya kina kirefu” ili siku moja mzazi asiyeamini apate kuvutwa upande ufaao.—1 Petro 3:15, NW.

Lakini iwapo ni wazi kwamba mtetano fulani ni gombano lao, kwa kawaida huwa ni jambo la hekima kubaki bila kuwamo.a Mithali 26:17 huonya hivi: “Mtu apitaye na kujisumbua kwa ugomvi usio wake; ni kama mtu ashikaye mbwa kwa masikio yake.” Ukijiunga na upande wowote, wajasiria kuamsha uchungu wa ndani—na labda kutenga urafiki wa—mmoja wa wazazi wako.

Kijana aungaye mkono upande wowote wa ugomvi wa wazazi anajaribu pia ‘kushughulikia hali ambayo kwa kweli imetatanika mno kutoweza kueleweka.’ Ndivyo mshauri wa familia Mitchell Rosen alivyosema katika gazeti ’Teen. Magombano ya ndoa, yeye akasema, “huhusisha ndani mambo kadhaa, wala si shauri la kukata maneno moja kwa moja tu kwamba mama ndiye yuko sawa, baba ndiye mwenye kosa.” Mara nyingi, kwenye kiini cha ugomvi huwa kuna maudhia na machungu ya ndani ambayo yamerundamana kwa kipindi cha miaka. Basi Baba au Mama alalamikapo kwa sababu mlo wa jioni umechelewa dakika kadhaa au kwa sababu ogeo la bafu liliachwa likiwa chafu, huenda kukawa na mengi zaidi ya yale yenye kuonekana kwa macho.

Biblia huhimiza hivi: “Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote.” (Warumi 12:18) Kwa hiyo jaribu kubaki bila kuwamo. Ingawa hivyo, namna gani wazazi wako wakikukaza ujiunge na upande fulani? “Azuiaye maneno yake ni mwenye maarifa; na mwenye roho ya utulivu ana busara.” (Mithali 17:27) Ndiyo, jizuie kutoa sauti—au kwa ubaya hata zaidi, kupiga kelele—juu ya maoni yako. Labda waweza kuomba radhi kwa njia yenye neema kwa kusema jambo kama hili, ‘Mama na Baba, mimi nawapenda nyote wawili. Lakini tafadhali msiniombe nijiunge na upande wowote. Hili ni jambo mpaswalo kutatua kati yenu wenyewe.’

Usijiunge katika Mzozano: Sauti mbili zenye makelele zina ubaya wa kutosha. Mbona uongeze sauti ya tatu kwenye jibizano hilo? Mithali 15:18 husema hivi: “Mtu wa hasira huchochea ugomvi; bali asiye mwepesi wa hasira hutuliza mashindano.” Wewe liepuke tu pambano hilo. Na ukihisi kwamba pigano li karibu kufoka, kumbuka maneno ya Mithali 17:14, NW: “Mwanzo wa ushindani ni kama mtu anayefungulia maji; kwa hiyo kabla ugomvi haujabubujika, wewe jiondokee.”

Labda waweza kuomba radhi uende chumbani mwako ukasome, ujifunze, au upige muziki. Au huenda ukawa ni wakati mzuri wa kuzuru rafiki. Kutafuta jambo la kufanya lililo na matokeo mazuri hukuondoa mahali pa ushindani na kukusaidia kuondoa akili yako kwenye mambo hayo.

Usijaribu Kuwa Mshauri wa Ndoa: Kama vile mithali moja iwekavyo wazo hilo: “Mashindano ni kama mapingo ya ngome.” (Mithali 18:19) Mara nyingi wazazi wenye kugombana wamejenga pingamizi la kuoneana uchungu wa ndani ambalo ni kama “mapingo ya ngome.” Je! wewe una maarifa ama ujuzi wa maishani ili uwasaidie kubomoa pingamizi hilo? Haielekei hivyo.

Kufanya kimbelembele cha kujihusisha katika matata ya ndoa ya wazazi wako huenda kukayaharibu zaidi. Yasema hivi Mithali 13:10: “Kiburi huleta mashindano tu [kwa kimbelembele mtu husababisha mng’ang’ano tu, NW]; bali hekima hukaa nao wanaoshauriana.” Ndiyo, yaelekea kwamba wazazi wako waweza kutatua magumu yao vizuri zaidi kwa kushauriana pamoja wakiwa faraghani.—Linganisha Mithali 25:9.

Zaidi ya hilo, daraka la mpatanishi wa familia lingeweza kuwa kazi yenye kudai mengi kuliko vile wewe wang’amua. Katika kitabu chake Teen Troubles, Carolyn McClenahan Wesson hueleza juu ya msichana mchanga jina lake Cora aliyejaribu kuwa mshauri wa ndoa. Tokeo likawa nini? Ndoa ya wazazi wake ilipata nafuu, lakini Cora akapatwa na matatizo ya tumboni. Carolyn Wesson amalizia hivi: “Acha wazazi wako washughulikie matatizo yao. Kushughulikia ubalehe wako kwakutosha wewe.”

Usigonganishe Wazazi: Vijana fulani hupanga kujifaidi kutokana na mgogoro wa kinyumbani. Mama asemapo, “La!” wao huchokora hisia-moyo za Baba na kumbana aseme “Ndiyo.” Huenda werevu wa kufanya wazazi watende jambo fulani kukampa mtu uhuru fulani, lakini baadaye jambo hilo hurefusha magombano ya familia. Kijana ambaye huheshimu wazazi wake kikweli hatageukia kugonganisha mamlaka kwa njia hiyo.

Usifanye Hali Iharibike Zaidi: Tabia ya uvivu au ya ukali-ukali, kufura-fura shuleni, kuacha viwango vya masomo vishuke—mambo hayo huongezea tu matatizo yako. Jitwalie daraka la kuelekeza vitendo vyako, na usiache ukengeufu wa wazazi wako uwe udhuru wa kuwa na mwenendo wenye fujo. Jitokeze uwe mwenye msaada na ushirikiano.

Kuokoka Mgogoro Mkubwa wa Familia

Ni wazi kwamba huwezi kubadili wazazi wako. Hata hivyo, waweza kujaribu kuwatolea uvutio wenye kuleta mema. Jaribu kutazamia mema na kuwa mchangamfu kwa kadiri uwezavyo. Kumbuka kwamba, upendo “huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.” (1 Wakorintho 13:7) Usiache kamwe kusali ili mambo yapate nafuu. (Wafilipi 4:6, 7) Mshauri wa familia Clayton Barbeau apendekeza zaidi hivi: “Wajulishe [wazazi wako] wakiwa kila mmoja peke yake kwamba wewe wapenda kila mmoja wao.” Hiyo pekee huenda ikalegeza mivutano ya familia.

Waweza pia kujaribu kuhimiza wazazi wako wapate msaada. Hupaswi kufanya hivyo katika bishano kali. Mithali 25:11 husema juu ya ‘neno linenwalo wakati wa kufaa.’ Yaelekea hiyo ingekuwa ni wakati mambo yametulia na wazazi wako wana tabia-moyo ya uitikivu mwingi zaidi. (Ikiwa mzazi mmoja hukasirika upesi hasa, jaribu kumfikia yule ambaye aonekana kuwa na mbetuko wa kuzungumza mambo kwa kiasi.)

Anza kwa kuwahakikishia kwamba wawapenda. Halafu waeleze kwa utulivu jinsi mtetano hukuathiri wewe. Hiyo haitakuwa rahisi. Katika kitabu chake Trouble at Home, Sara Gilbert hukiri kwamba majaribio kama hayo huenda yakajibizwa hivi, “Shika lako mwenyewe—usiingilie yasiyokuhusu!” Hata hivyo, mwanamke huyo ashauri kwamba “wewe wahitaji kuelewesha wazi kwamba linakuhusu.” Waeleze jinsi kupigana kwao hukuogopesha sana, hukufadhaisha, au hukutia kasirani. Ingawa hutaki kuingilia maisha zao, kupigana kwao huvuruga sana maisha yako! Dokeza kwamba wazazi wako watafute msaada—labda kwa kufikia mzee Mkristo mwenye kutumainiwa.b

Kwa kukabiliwa usoni na matokeo ya ugomvi wao wa ndoa, huenda wazazi wako wakaguswa moyo waangalie kwa uzito kutatua matatizo yao—na labda hata waache kupigana.

[Maelezo ya Chini]

a Hatumaanishi hali ambazo baba mwenye matusi hutisha washiriki wa familia kwa jeuri. Katika visa hivyo, washiriki wa familia huenda wakalazimika kupata msaada wa nje ili wajilinde na madhara ya kimwili.

b Ikithibitika kwamba wazazi wako hawana kiasi wala nia ya kusikiliza, huenda likawa jambo la hekima kuongewa kwa usiri na Mkristo mkomavu. Yeye, awe ni mwanamume au mwanamke, hataweza kuingilia ndoa ya wazazi wako lakini aweza kutoa msaada wa kihisia-moyo na ushauri mwema wenye kuitikiwa.

[Picha katika ukurasa wa 18]

Je! vijana waweza kupatanisha mabishano ya wazazi kwa matokeo mazuri?

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki