Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g90 12/8 kur. 14-21
  • Uharibifu wa Ghafula!—Wamekabilianaje?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Uharibifu wa Ghafula!—Wamekabilianaje?
  • Amkeni!—1990
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Uharibifu wa Ghafula Zaidi
  • Kikumbusho Juu ya Mahitaji ya Msingi
  • Kukabiliana na Uharibifu wa Hugo
  • Kukabiliana na Tetemeko la Kalifornia
  • Kukua Pamoja Katika Upendo
    Mashahidi wa Yehova—Wapiga-Mbiu wa Ufalme wa Mungu
  • Upendo wa Kikristo Kati ya Misiba Katika Mexico
    Amkeni!—1996
  • Mambo Ambayo Kimbunga Andrew Hakingeweza Kuharibu
    Amkeni!—1993
  • Matendo ya Yehova ya Kuokoa Sasa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1990
g90 12/8 kur. 14-21

Uharibifu wa Ghafula!—Wamekabilianaje?

WAKATI Tufani Hugo ilipokumba Guadeloupe siku ya Jumamosi, Septemba 16, 1989, usiku ulionekana kama usioisha. Ukaitwa “USIKU WA JINAMIZI.” Halafu, Montserrat ilitiwa hofu kubwa na zile pepo zenye mwendo wa kilometa 230 kwa saa. Watu zaidi ya 20 walikufa katika visiwa hivyo vya Karibbea.

Ikiendelea na ushambulizi, Hugo iliparuza Visiwa vya Leeward vya St. Kitts na Nevis. Usiku uliofuata iliviharibu kinyama Visiwa Virgin vya St. Croix na St. Thomas. Uharibifu ulioachwa nyuma kule St. Croix ulikuwa usioaminika. Ikisonga mbele, karibu na adhuhuri ya Jumatatu tufani hiyo ilitandaza sehemu ya kaskazini-mashariki mwa Puerto Riko, hasa ikivikumba vibaya sana visiwa vidogo sana vya pwani, Vieques na Culebra.

Ikipata imara mpya juu ya maji, Hugo ilijikusanya pamoja kufanya shambulio jingine zaidi la wakati wa usiku. Karibu na usiku-kati wa Alhamisi, kwa kusongamanisha pepo zenye mwendo wa kilometa 220 kwa saa, ile dhoruba kubwa ilitandika pwani ya Karolina Kusini ya United States. Ilikata mparuzo wa uharibifu wa zaidi ya kilometa 160 kwa upana kuanzia kusini ya Charleston hadi upande mwingine wa Ufuo wa Myrtle. Pigo layo la uharibifu lilidumishwa kuingia bara kwa zaidi ya kilometa 320, likikatakata miti ya nguvu za umeme na kuangusha miti mikubwa sana ya oki hadi kule mbali Charlotte, Karolina Kaskazini.

Mamia ya maelfu walikimbia kutoka maeneo ya pwani na hivyo wakaokoka wakati pepo na mawimbi ya meta 5 yalipofagilia mbali nyumba nyingi na kuharibu mamia ya nyingine. Makumi ya maelfu ya nyumba na majengo mengine yaliharibiwa.

Ilikuwa lazima mtu aone uharibifu huo ndipo aweze kuamini kwamba ulitukia—mashua zikirundikwa pamoja kama vigari vya watoto kufikia idadi ya sita kwenda juu, mchanga ukirundikwa kufikia kina cha meta 1 barabarani, miti mikubwa sana juu ya nyumba mbalimbali, paa zikiwa na mashimo wazi kana kwamba zimetobolewa na mkono mkubwa. ‘Mwana wangu hufuga majimbi [majogoo] wa kuuza,’ akaripoti mwanamke mmoja. ‘Aliwafungilia wote kwenye miti ili wasipeperushwe, na sana-sana hawakupeperushwa. Lakini hawakubaki na hata unyoya mmoja.’

Hata hivyo, kwa sababu maonyo yalitiiwa, ni karibu watu 26 tu katika United States waliokufa wakati wa dhoruba hiyo, na wengi kidogo kuliko hao katika Karibbea. Kwa upande mwingine, hasara za kiuchumi ni kubwa sana, zikiwa maelfu mengi ya mamilioni ya dola. Sheria iliyotungwa na serikali ya United States kufuata dhoruba hiyo iliandaa msaada wa kwanza wa dharura ukiwa wa dola milioni elfu 1.1 kwa wahanga wa Hugo, kikiwa ndicho kiasi kikubwa zaidi ambacho kimepata kukubaliwa kusaidia wenye msiba. Hata hivyo, upesi rekodi hiyo ikapitwa kwa mbali.

Uharibifu wa Ghafula Zaidi

Siku ya Oktoba 17, mwezi mmoja baada ya Hugo kugusa bara, Kalifornia ya kaskazini ilitikiswa na tetemeko la dunia lenye kipimo cha 7.1 katika uzani wa Richter. Madaraja yalibomoka, majengo yakaanguka, na maelfu ama wakakimbia kutoka kwenye nyumba zao wakipiga mayowe au wakalemewa kabisa na hofu wakati nchi ilipowayawaya na kutikisika kwa sekunde 15 au zaidi. Nyumba zaidi ya mia moja elfu ziliharibiwa, na kuanzia mamia kadhaa hadi elfu moja zikaharibiwa kabisa. Juma moja baada ya tetemeko hilo, wakaaji wapatao kumi elfu wa Santa Cruz County walikuwa bado hawawezi kuendesha magari kwenda kwenye nyumba zao kwa sababu ya mibomoko-ardhi iliyozifunga barabara.

Kifo na uharibifu vingalikuwa vikubwa zaidi kama wajenzi wasingalifuatilia sheria zenye kuamrisha ujenzi wenye kukinza matetemeko. Kwa kielelezo, lile tetemeko la 1988 katika Armenia lilikuwa la nguvu chache zaidi lakini liliua watu 25,000. Hata hivyo, yaonekana ni wachache kuliko 70 waliokufa katika tetemeko la Kalifornia, wengi wao ikiwa ni wakati daraja lililo juu ya kisehemu chenye urefu wa kilometa moja na nusu cha barabara kuu ya Interstate 880 lilipoangukia motakaa kwenye daraja la chini kidogo.

Katika historia ya United States msiba wa kiasili haujapata kamwe kuwa wenye gharama kubwa hivyo. Juma lililofuata, sheria iliyotungwa na serikali iliandaa zaidi ya dola milioni elfu tatu za kusaidia. Hata hivyo, nyingi zaidi zitahitajiwa ili kujenga upya. Rais wa Mwungano wa Kalifornia wa Bima ya Kibinafsi alisema kadirio la kwamba tetemeko hilo lilileta hasara ya jumla ya dola milioni kumi elfu ‘lingekuwa la kiasi kizuri.’

Kikumbusho Juu ya Mahitaji ya Msingi

Mwanamume mmoja alikuwa katika ua wake katika kisehemu cha kukaa cha Charleston siku kadhaa baada ya Hugo kukumba. Mfanya kazi wa misaada alipokuwa akiendesha gari kupitia hapo, mwanamume huyo aliuliza hivi: “Una glasi ya maji?” Kwa muda fulani mfanya kazi huyo hata hakuwa amefikiria kwamba watu hawakuwa na maji ya kunywa!

Miaka zaidi ya 1,900 iliyopita, mtume Petro alielekeza kwenye uhitaji mmoja wa msingi wa wale walio katika hali hizo zenye kujaribu. “Mwisho wa mambo yote umekaribia,” akasema. “Zaidi ya yote iweni na juhudi nyingi katika kupendana.” (1 Petro 4:7, 8) Mwisho wa mfumo mzima wa mambo ya Kiyahudi ulikuwa karibu Petro alipoandika maneno hayo. Mwisho ulikuja miaka michache baadaye, katika 70 W.K., wakati majeshi ya Kiroma yalipofanya Yerusalemu ukiwa. Hata hivyo, Wakristo walikuwa wamepewa ishara mapema, nao waliitii wakakimbia milimani ng’ambo ya Mto Yordani karibu na mji wa Pella.—Luka 21:20-22.

Jaribu kuiwazia hali wakati ambapo labda ni maelfu ya Wakristo walikuwa wakiwasili katika eneo hilo la milima. Kwa wazi hawakuwa na nyumba wala mahitaji ya msingi bali walilazimika kujenga makao ya muda. Vitu vilikuwa haba na kulikuwa na magumu. (Mathayo 24:16-20) Wakati huo wenye majaribu walihitaji nini hususa? “Juhudi nyingi katika kupendana,” akasema Petro. Ndiyo, kusaidiana kukabili hali.

Je! roho hiyo ya usaidiano na upendo ilidhihirika baada ya uharibifu ya hivi majuzi iliyosababishwa na Hugo na lile tetemeko la dunia?

Kukabiliana na Uharibifu wa Hugo

Katika St. Croix, waokokaji wa Hugo walisalimiana kwa mikumbatiano ya shangwe na utulizo, wakiwa na furaha kuwa hai tu. Upesi jitihada kubwa za msaada zikawa zikifanywa, kuwaandalia wahanga makao na chakula. Hata hivyo, watu fulani walitafuta kujifaidi na msiba wa wahanga hao. Watafuta faida walitoza bei kubwa sana. Kwa kielelezo, mfuko wa barafu ambayo kwa kawaida ilikuwa ya senti 79 (za Amerika) uliuzwa kwa dola 10. Hata uporaji ulifanywa. Lakini kwa ujumla vitendo hivyo vya moyo mkavu vilifunikwa na vitendo vingi vya fadhili na huruma za kibinadamu. Zilizostahili kuangaliwa kihususa zilikuwa ripoti zilizohusu jitihada za kusaidia za Mashahidi wa Yehova.

Hata kabla Hugo haijakumba, wazee Wakristo waliwazuru wale wenye kuishi katika nyumba zisizo salama sana na kuwahimiza wahamie Majumba ya Ufalme yaliyojengwa kwa imara zaidi au katika nyumba zilizo salama zaidi za ndugu zao Wakristo. Jumba la Ufalme katika Summerville, Karolina Kusini, lilikuwa na watu zaidi ya 50 wenye kulala humo usiku wakati wa ile dhoruba!

Katika Guadeloupe matayarisho hayo yalithibitika kuwa yenye kuokoa uhai. Katika kisiwa hicho pekee, nyumba 117 za Mashahidi ziliharibiwa, hali nyumba karibu 300 za Mashahidi wengine zilihasiriwa vibaya sana. Kwa kuongezea, Majumba ya Ufalme 8 yalihasiriwa vibaya, hali mengine 14 yalihasiriwa kwa kadiri isiyo kubwa jinsi hiyo.

Ingawa Mashahidi kadhaa waliumizwa, hakuna waliouawa, ama katika Guadeloupe ama mahali pengine popote katika Karibbea. Hata hivyo, mwana aliye mtu mzima wa mmoja wa Mashahidi aliuawa wakati alipofyonzwa kihalisi na upepo ulioing’oa ghafula paa ya nyumba.

Ilipofika siku ya tatu baada ya dhoruba ndipo Mashahidi wenzao walipoweza mwishowe kupashana habari kwa simu na ndugu zao katika Guadeloupe. Hata hivyo, kwa wakati huo waangalizi wanaosafiri na wafanya kazi wa ofisi ya tawi katika kisiwa hicho walikutana kutengeneza uchunguzi wa mahitaji ya ndugu zao, yaani, Mashahidi wenzao.

Upesi maji, chakula, nguo, na mahitaji mengine ya lazima yakawa yakitolewa kwa ukarimu na wale wasioathiriwa kwa uzito sana. Maji yalipatikana kwenye ofisi ya tawi, na ilichangamsha moyo kuwaona akina ndugu wakileta vyombo vyote vilivyokuwako, kuvijaza, na kuvigawanya kwa wale wenye uhitaji. Mashahidi katika Martinique ni miongoni mwa waliokuwa wa kwanza kutoka nchi nyinginezo kuitikia mahitaji ya ndugu zao katika Guadeloupe.

Kwa kuwa Guadeloupe iko chini ya udhibiti wa Kifaransa, Mashahidi wa Yehova katika Ufaransa walisafirisha haraka kwa ndege shiti nzito za plastiki, kamba za nailoni, na mitungi-plastiki ya maji. Baada ya muda mfupi, kama tani 100 za metriki za vifaa vya ujenzi zikasafirishwa kwa meli hadi Guadeloupe na kugawanywa mara iyo hiyo.

Papo hapo, Mashahidi wa Yehova katika Puerto Riko walianza pia kutengeneza programu ya kusaidia. Kufikia mwisho-juma wa baada ya dhoruba ile, mamia ya maeneo yasiyoathiriwa ya kisiwa hicho yalikuwa yakiteremka kwenye miji iliyoachwa ukiwa ili kusaidia kutengeneza nyumba zilizoharibika. Pia, mashua mbili zilizojazwa chakula, vifaa, na karibu Mashahidi 40 ziling’oa nanga kwenda kwenye kile kisiwa kidogo cha Culebra. Baada ya muda mfupi kituo cha redio huko kikawa kikisifu kazi ya kujenga upya iliyokuwa ikifanywa. Mwisho-juma uliofuata Mashahidi 112, kwa kuandamwa na tani sita za vifaa vya ujenzi, waling’oa nanga kwenda kwenye kisiwa kidogo cha Vieques kwa ajili ya kazi kama hiyo ya kujenga upya.

Ilipofika Ijumaa, siku tano baada ya dhoruba ile, ndipo akina ndugu kutoka Puerto Riko walipoweza kukodi ndege ya mizigo na kupeleka chakula na dawa St. Croix. Mmoja wa ndugu hao aripoti hivi: “Kutoka angani kisiwa kizima kilionekana kama jaa la takataka. Vijiji vizima vilibomolewa na kupotwapotwa. Kotekote vilimani vilikuwako vipande vya mbao, metali, na utakataka; hakuna kijani-kibichi, visiki tu vya miti ya kahawia na nyasi zilizochomeka, zilizokaushwa na mifoko ya pepo zenye mwendo wa kufikia kilometa 320 kwa saa.”

Baada ya kuhakikisha kadiri ya hasara iliyotokea, Mashahidi walisafirisha kwa meli karibu tani 75 za vifaa vya ujenzi. Wakati wa Oktoba, karibu wajitoleaji mia moja kutoka Puerto Riko waliwasaidia ndugu katika St. Croix kujenga upya. Jumba la Ufalme moja lilitumika kuwa mahali pa kulala. Kila siku ilianza kwa mazungumzo ya andiko fulani la Biblia, kama vile ifanywavyo kwenye ofisi zote za matawi ya Mashahidi wa Yehova. Dada Wakristo wa huko waliwafulia, wakawasafishia, na kuwapikia akina ndugu.

Sheila Williams alikuwa ameweka akiba ya pesa kwa miaka mingi ili ajenge nyumba mpya, na alikuwa ndipo tu amehamia ndani wakati Hugo ilipoiharibu. Aliposikia kwamba ndugu zake Wakristo wangekuja kutoka Puerto Riko kusaidia wahanga, aliwaambia wafanya kazi wenzake. Lakini wao wakasema: “Hawatakufanyia lolote. Wewe ni mweusi, si Mhispania kama wao.” Walishangaa kama nini Sheila alipopata nyumba mpya kabisa baada ya muda mfupi!

Mtoto wa miaka mitano katika Michigan, U.S.A., akiisha kuona ripoti za habari juu ya ukiwa uliofanyika katika St. Croix, alitaka kuwasaidia wale waliopoteza mali zao. Aliomba ruhusa ya mama yake ili ampe vazi msichana mmoja mdogo ili ‘yeye aweze kuwa na sura nzuri aendapo kwenye Jumba la Ufalme.’

“Mimi nilishangaa,” akasema mama huyo, “alipochagua moja la mavazi yake yaliyo bora.” Vazi hilo lilipelekwa, na kama uwezavyo kuona katika ukurasa wa 18, mtoto mmoja katika St. Croix ana upendezo mwingi kuwa nacho.

Baada ya Hugo kukumba ikipita katika Karolina Kusini asubuhi ya Ijumaa, Septemba 22, halmashauri ya kusaidia ilifanyizwa mara ile ile. Wazee Wakristo katika kila moja la makundi mengi katika maeneo yaliyoathiriwa walipashwa habari, nao, kwa upande wao, wakatoa hesabu ya kila mshiriki wa kundi lao. Kwa kufurahisha, hakuna mtu aliyekuwa amejeruhiwa wala kuuawa, ingawa makao ya Mashahidi fulani yaliharibiwa na ya wengine yakahasiriwa vibaya. Jumba la Ufalme moja lilihasiriwa vibaya sana, na mengine pia yalipata hasara fulani.

Mambo yalionekana kutokuwa na matumaini hasa katika Charleston na maeneo yenye kuizunguka, maelfu ya miti ikiwa imeanguka, mamia ya paa zikiwa zinavuja, nyumba zikiwa zimeharibiwa au kutenganishwa vibaya, kukiwa hakuna maji ya kunywa, hakuna nguvu za umeme, hakuna friji, na hakuna petroli. Hata hivyo, hali ilibadilika haraka.

Ndugu wengi kutoka eneo la Charleston walikuwa wamekusanyika pamoja asubuhi ya Jumamosi, siku iliyofuata dhoruba, wakingojea msaada. Ron Edling, mwangalizi wa jiji, aeleza lililotukia wakati ambapo mwishowe neno lilipenya kusema kwamba Mashahidi wa kutoka maeneo ya kandokando walikuwa njiani kwenda huko. “Tulipoenda nje, tuliona mmoja wa miono ya kupendeza sana ambayo tumepata kuona. Kulikuwako msafara, na katika dirisha la mbele la lori lenye kuongoza na malori yenye kufuata ilikuwako ishara iliyosomeka ‘Wasaidiaji Kwenye Tufani wa MY.’

“Kulikuwako malori, magari, malori yenye kukokota trela, yakiwa na maelfu ya lita za maji. Yalileta misumeno ya umeme, na lita 1,100 za petroli ili kuitilia nguvu. Ulikuwa mwono ambao mimi sitasahau kamwe. Wakati huo niliwaza, ‘Huu ni mmoja wa nyakati nzuri kabisa ambazo nimejionea katika tengenezo la Mungu.’ Si kwamba ndugu hao walileta tu vifaa vyenye kuhitajiwa sana bali walileta tumaini pia. Nina uhakika kwamba wakati huo kila mtu aling’amua udugu mzuri sana tulio nao. Ingawa ingechukua kitambo kidogo, sisi tungejiondoa taabani.”

Mwisho-juma uliofuata wafanya kazi Mashahidi 400 wa kusaidia walikuwapo. Kwa ujumla wote, kazi ilifanywa katika paa au katika nyua za familia karibu 800, kutia na nyingi zisizo za Mashahidi. Kwenye kitovu kimoja cha kusaidia, akina ndugu walikuwa wakilisha karibu watu 3,000 kila siku. Kwa ujumla, Mashahidi walipokea na kugawanya kilo zaidi ya 230,800 za chakula na kilo 78,000 za nguo, bila kutaja vifaa vya ujenzi na vitu vingine vingi. Kufikia Jumapili, Oktoba 8, siku 16 tu baada ya Hugo kukumba, Majumba ya Ufalme yote yalitengenezwa kwa kadiri ya kwamba makundi yote yangeweza kurudia ratiba yayo ya ukawaida ya mikutano.

Kukabiliana na Tetemeko la Kalifornia

Sehemu yenye kulengwa katikati na lile tetemeko la dunia la Oktoba 17 ilikuwa kama kilometa 110 kusini ya San Francisco, karibu kilometa 16 kaskazini-mashariki mwa Santa Cruz. Katika eneo hili lenye idadi kubwa ya watu, ambapo mitetemo mifupi ya dunia hutukia kwa kawaida, mamilioni waliogofywa na ule ulioonekana kama msitikisiko usioisha wa sekunde 15 au zaidi.

“Jengo lilitikisika huku na huku,” akasema Ray Vaden, mzee mmoja Mkristo katika San Jose. “Nilishangaa kama lingebaki limesimama. Nilipotazama nje ya dirisha langu, niliweza kuona kwamba barabara zilisongamana magari wakati wa pirika-pirika ya kurudi nyumbani. Ilikuwa saa 11:04 ya jioni.

“Mwishowe tuliweza kuanza kupashana habari na akina ndugu katika kundi letu. Wale ambao hatukuweza kuwafikia kwa simu tulipanga kuwazuru katika nyumba zao. Hiyo ilichukua saa kadhaa kwa sababu ya msongamano wa magari. Kufikia saa 2:30 ya usiku tulipata habari kwamba hakuna yeyote aliyejeruhiwa, ingawa vitu vilivunjika ndani ya nyumba nyingi. Kesho yake tukapata habari kwamba nyumba za baadhi ya ndugu zetu katika eneo zilihasiriwa vibaya sana hivi kwamba wao wakalazimika kuhama. Walipokewa kwenye nyumba za Mashahidi wenzao.”

Karibu na Los Gatos, dada mmoja Mkristo alikuwa akioga katika sakafu ya pili ya nyumba yake ya ghorofa mbili wakati sakafu nzima ya kwanza ilipoanguka. Hivyo basi yeye akatoka katika hodhi la kuogea akiwa kwenye sakafu ya kwanza, na kwa kustaajabisha hakuumia. Kama angalikuwa katika sakafu ya kwanza, hakika angaliuawa.

Papo hapo, marafiki walitaka kujua wangeweza kuwafanyia nini wahanga. Siku ya Alhamisi, siku mbili baada ya tetemeko la dunia, halmashauri ya kuwatunza hawa iliwekwa. Siku ya Jumamosi, magari makubwa na motakaa nyinginezo zilipeleka mahema, mifuko ya kulalia, taa za mafuta na stovu, nguo, tochi, vyakula vya mikebeni, maji ya kunywa, na kadhalika, kwa wenye uhitaji. Asubuhi hiyo tu, dola 41,000 zilitolewa ziwe za mfuko wa kusaidia!

Lo, hiyo ilitofautianaje na maoni ambayo watu fulani wa ulimwengu walidhihirisha! Mwanamume mmoja alitambaa kumwendea mhanga mmoja wa kike aliyenaswa katika gari lake chini ya kisehemu kilichobomoka cha Interstate 880. Aliahidi kutomwumiza lakini ndipo akachukua pete zake, vito vya thamani, na kibeti, na kukimbia bila kumsaidia. Kwa ujumla ni watu zaidi ya 40 waliokufa katika anguko hilo la daraja la juu ya barabara, miongoni mwao akiwamo Mary Washington, mmoja wa Mashahidi wa Yehova.

Halmashauri ya Ujenzi ya Kijimbo ya Mashahidi wa Yehova ilianza upesi kukadiria hasara zilizotokea. Majumba ya Ufalme mawili yalihasirika kidogo. Hata hivyo, nyumba za Mashahidi kadhaa zilihasirika vibaya hivi kwamba zikahitajiwa kuharibiwa. Vikundi vya wafanya kazi viliweza kurudisha nyumba za trela kwenye misingi yazo na kutengeneza nyingi za nyumba za akina ndugu na kujenga upya nyinginezo. Mamia ya maelfu ya dola yametolewa kuendesha kazi hii.

Kadiri mwisho wa mfumo huu ukaribiavyo zaidi, kwa utimizo wa unabii wa Yesu, twaweza kutarajia matetemeko zaidi ya dunia na misiba mingine. (Mathayo 24:3-8) Bila shaka kutakuwako magumu makali kuliko hata yale yaliyowapata Wakristo wa mapema wakati Yerusalemu lilipoharibiwa. Unabii wa Biblia una kani kubwa hata zaidi katika siku yetu: “Mwisho wa mambo yote umekaribia.” Kwa hiyo, chahitajiwa nini? “Zaidi ya yote iweni na juhudi nyingi katika kupendana.” (1 Petro 4:7, 8) Hakika hutuchangamsha moyo kuona upendo huo ukionyeshwa miongoni mwa udugu wa Mashahidi wa Yehova!

[Ramani katika ukurasa wa 15]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

KALIFORNIA

Oakland

San Francisco

Los Gatos

Santa Cruz

[Ramani](Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

U.S.A.

Charleston

Bahari Kuu Atlantiki

Puerto Riko

Guadeloupe

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Kulia: Uharibifu wa Hugo katika pwani ya Karolina Kusini

[Hisani]

Maxie Roberts/Hisani ya THE STATE

Chini: Magari yamerundikana mbele ya shule moja ya sekondari

[Hisani]

Maxie Roberts/Hisani ya THE STATE

Chini: Wafanya kazi wa kusaidia wa Mashahidi wa Yehova wakisaidia kusafisha na kurudisha

[Picha katika ukurasa wa 18]

Kushoto: Mtoto mmoja wa St. Croix amevaa vazi lililopelekwa na mtoto wa miaka mitano katika Michigan aliyetaka kusaidia

Chini: Mashahidi wa Yehova katika Guadeloupe wakichagua chakula kilichotolewa

Kushoto chini: Sheila Williams pamoja na mfanya kazi wa kusaidia aliyesaidia kujenga upya nyumba yake iliyoharibiwa

[Picha katika ukurasa wa 21]

Juu: Daraja la juu la Interstate 880 liliangukia daraja la chini zaidi

Kushoto: Raim Manor katika sakafu ya pili ya nyumba yake, iliyoanguka kwenye sakafu ya kwanza

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki