Wahukumiwa Kutoka Kinywa Chao Wenyewe
WAKIWAKILISHA makanisa yote ya Ulaya yenye kudai kuwa ya Kikristo, wajumbe 638 walikutana Mei uliopita katika Basel, Uswisi, kwa ajili ya “Amani Pamoja na Haki” Kusanyiko la Kanisa Lote la Ulaya. Kwa kura ya asilimia 94.5, walichagua kufuata hati ya kukata maneno ambayo yaweza kuonwa kuwa hati ya makubaliano ya Jumuiya ya Wakristo wa Ulaya. Acheni hati hii ijibu maswali kadhaa ambayo sisi tungeweza kuyauliza kwa kufaa. (Tarakimu zilizo katika mibano ya mviringo zinamaanisha visehemu vya hati.)
Je! makanisa haya yanaabudu yule Mungu mmoja wa kweli, Yehova, na kudumisha mwungamano unaofaa wa Kikristo?
“Sisi tuna deni la uhai wetu kwa Mungu Muumba, yule Mungu mwenye utatu—Baba, Mwana na Roho Takatifu; ambaye kwa rehema yake amejifunua mwenyewe kwa jamii ya kibinadamu katika Yesu Kristo. Hata kama kunaendelea kuwa na tofauti za maungamo, sisi tunashiriki katika imani hii.”(21)
“Kutokana na ubatizo na itikio katika imani la kusikia neno la Mungu, tayari sisi Wakristo ni mmoja katika Kristo, hata ingawa bado sisi hatumo katika ushirika kamili. Tunatafuta kushinda tofauti ambazo zingali katika fundisho na zoea ili tufikie ushirika kamili.”(39)
“Tumeshindwa kushinda migawanyiko miongoni mwa makanisa na mara nyingi tukatumia vibaya mamlaka na uwezo tuliopewa ili kuimarisha miungamano mipungufu na isiyo ya kweli kama ubaguzi wa rangi, utukuzo wa ngono na wa taifa.”(43)
Je! wao wameishi kulingana na dai lao la kuwa wafuasi wa Mwana-Mfalme wa Amani?
“Sisi Wakristo tunaamini kwamba amani ya kweli itapewa kwa kutembea pamoja na Kristo, hata ingawa mara nyingi sisi tunasita-sita kumfuata mpaka mwisho. Kukataa kwake jeuri kunatokana na upendo huo ambao unatafuta hata kumpata adui ili amgeuze na kushinda uadui na pia jeuri. Upendo huu uko tayari kuteseka kwa njia ya kutenda. Unafunua wazi hali isiyo haki ya kitendo cha jeuri, unawatoza hesabu wale wanaotumia jeuri na unamvuta adui ndani ya uhusiano wa amani.”(32)
“Sisi tumesababisha vita na kushindwa kutumia nafasi zote za kujitahidi kuelekea usuluhisho na upatanisho; tumeachilia vita na mara nyingi tukavitetea kwa urahisi kuwa ni vya haki.” (43)
“Mitengano na ugomvi wa kidini imekuwa na matokeo makubwa juu ya historia ya Ulaya. Vita vingi vimekuwa vita vya kidini. Mamilioni ya wanaume na wanawake wameteswa na kuuawa kwa ajili ya imani zao.”(48)
Je! wamefuata mfano wa Yesu wa kusema ukweli, kutafuta uadilifu, na kuonyesha heshima kwa uhai na uumbaji wa Mungu?
“Makanisa na Wakristo wameshindwa katika mambo mengi na sikuzote wamekuwa hawajaishi kulingana na viwango vya wito wa Mungu hata kushindwa kutangaza ukweli wa Yesu Kristo . . . Kwa muda mrefu mno sisi tumekuwa vipofu kutokuona mimaanisho na madai ya Gospeli kwa habari ya haki, amani na ukamilifu wa uumbaji.”(42)
“Tumeshindwa kutoa ushahidi wa utunzaji wa Mungu kwa ajili ya viumbe vyote na kusitawisha mtindo-maisha unaoonyesha tunajielewa tukiwa sehemu ya uumbaji wa Mungu.”(43)
Je! wanakosa maarifa juu ya sababu ya matatizo ya ulimwengu?
“Ni nini visababishi vilivyo mzizi wa matisho tunayoelekeana nayo leo? . . . Visababishi halisi . . . vinapasa kutafutwa katikati kabisa ya aina ya kibinadamu, katika maoni na njia za kufikiri kwa binadamu.”(18, 19)
“Vipingamizi ambavyo mwishowe tunajikuta ndani yavyo vina mizizi katika uhakika wa kwamba njia za Mungu zimeachiliwa mbali.”(41)
Ijapokuwa kukiri hivyo, je! wanaukataa utawala wa binadamu na kuweka tumaini lao katika Ufalme wa Mungu ulioanzishwa?
“Matukio matatu ya maana na mazito yanahitaji uangalifu wa pekee: kufanyiwa maendeleo kwa mahusiano kati ya Mashariki na Magharibi katika ile shughuli yenye kuendelea ya Mkutano wa Usalama na Ushirikiano Katika Ulaya [CSCE]; mageuzo ya kidemokrasi katika Urusi na nchi nyingine za Ulaya ya Mashariki; mwendeleo wa kuunganika kwa Ulaya ya Magharibi (Kifungu Kimoja cha Sheria ya Ulaya, ambacho kitaanza kazi kikamili kuanzia 1993).”(51)
“Muundo wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa unapasa kufanywa uwe na matokeo zaidi. Wao wamethibitisha kwamba wanaweza kusaidia katika kutatua mapambano kati ya eneo na eneo, katika kutoa usaidizi kwa jitihada za ukuzi wa nchi nyingi, katika kushughulika na matatizo ya mazingira. Kwa hiyo, kuna uhitaji wa serikali za ulimwengu kuongeza tegemezo lao kwa Umoja wa Mataifa na kufanya tegemezo hili liwe kwa namna yenye kuonekana wazi.”(83)
Je! kuna wonyesho wowote kwamba hivi karibuni huenda wakabadili mwongozo wao wa kuhusika katika siasa?
“Zaidi ya hilo 1992 utatia alama mwaka wa 500 wa kuanza kwa kipindi cha mpanuko wa Ulaya kwa kuletea hasara vikundi vingine vya watu. Jambo hili linatuhitaji sisi tujitahidi kuleta uhusiano wa haki na wenye amani kati ya nchi zilizo katika Ulaya na pia kati ya Ulaya na sehemu nyinginezo wa ulimwengu hasa Mashariki ya Kati ambayo kwayo Ulaya inalaumika kwa mambo mengi ya kihistoria. Sisi tunaomba makanisa yetu yategemeze jitihada ya watu katika Amerika ya Kilatini, Afrika na Esia ya kutafuta haki ya kijamii, heshima ya kibinadamu na kuhifadhiwa kwa mazingira yao.”(84n)
Ni nini kanuni ya Biblia inayopasa kutumiwa katika kuzihukumu dini ambazo zilitunga hati hii ya mwisho?
Mathayo 12:37 inasema hivi: “Kwa maneno yako utahesabiwa haki [uadilifu, NW], na kwa maneno yako utahukumiwa.” (Ona pia Luka 19:22.) Jumuiya ya Wakristo wa Ulaya ikoje kulingana na hayo? Je! maneno yake yanaitangaza kuwa ina uadilifu, au inaihukumu? Kwa sababu ya maneno yaliyonakiliwa juu, je! kunaweza kuwa na shaka?
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 12]
Swiss National Tourist Office