Wakaaji wa Nje ya Dunia Hii—Wako Wapi?
KULINGANA na mwandikaji wa sayansi Isaac Asimov, hilo ni “swali ambalo, kwa njia fulani, huharibu kila kitu” kwa wale waaminio kuna uhai katika sayari nyinginezo. Hapo kwanza liliulizwa katika 1950 na mwanafizikia wa kinyukilia Enrico Fermi, nalo lilikuwa nyongeza ya hoja iliyotokezwa hivi: Ikiwa uhai wenye akili umetokea katika sayari nyinginezo katika galaksi yetu, sasa kwapasa kuweko tamaduni nyingi zilizo mbele ya utamaduni wetu wenyewe kwa mamilioni ya miaka. Zapasa ziwe zilisitawisha usafiri wa kutoka nyota moja hadi nyota nyingine na kuenea kotekote katika galaksi yetu, huku ukifanyiza koloni na kupeleleza bila kipingamizi. Sasa basi ziko wapi?
Ingawa wanasayansi fulani wa SETI hukiri kwamba wanatatizwa na hicho “kitatanisho cha Fermi,” mara nyingi wao hukijibu kwa kuonyesha wazi jinsi ingekuwa vigumu kusafiri kati ya nyota na nyota. Hata kwa mwendo wa nuru, ulio wa kasi sana, ingeichukua meli-anga miaka mia moja elfu kuvuka galaksi yetu wenyewe tu. Huonwa kuwa jambo lisilowezekana kuupita mwendo huo.
Bunilizi (hadithi ya kubuni) ya sayansi yenye kuonyesha meli zikiruka kutoka nyota moja hadi nyingine kwa siku au saa chache ni msisimuko tu, wala si sayansi. Miendo iliyo kati ya nyota ni mikubwa sana kwa kadiri tusiyoweza kuwazia. Kwa uhakika, kama sisi tungeweza kujenga kiolezo cha galaksi yetu kikiwa kidogo sana hivi kwamba jua letu (ambalo ni kubwa sana kwa kadiri ya kuweza kumeza dunia milioni moja) lingepunguzwa liwe saizi ya chungwa, bado umbali ulio katika kiolezo hicho kati ya nyota na nyota ungekuwa na wastani wa kilometa zaidi ya elfu moja!
Ndiyo sababu wanasayansi wa SETI huegemea sana darubini za kiredio; wao huwazia kwamba kwa kuwa huenda tamaduni zenye maendeleo zisiweze kusafiri kati ya nyota na nyota, bado zingetafuta namna nyingine za uhai kwa njia zenye gharama ndogo na rahisi zaidi za kutumia mawimbi ya redio. Lakini kitatanisho cha Fermi kingali chawasumbua.
Mwanafizikia Mwamerika Freeman J. Dyson amekata kauli kwamba ikiwa tamaduni zenye maendeleo zimo katika galaksi yetu, kupata uthibitisho wa kwamba zipo kwapasa kuwe jambo rahisi kama kupata ishara za utamaduni wa kitekinolojia katika Kisiwa cha Manhattan katika Jiji la New York. Galaksi hiyo yapasa kuwa na miminiko ya ishara za kigeni na miradi yayo mikubwa ya uhandisi. Lakini hakuna yoyote imepatikana. Kwa uhakika, makala moja juu ya habari hiyo ilisema kwamba msemo wa “katafutwa, kakosekana” umekuwa kama wimbo wa kidini kwa wanaanga wa SETI.
Shaka Zaanza
Wanasayansi kadhaa wanaanza kung’amua kwamba wenzao wamefanya dhana nyingi mno za kutazamia mazuri katika kushughulikia suala hili. Wanasayansi hao hutokeza mawazo kuhusu tamaduni chache zaidi zenye maendeleo katika galaksi yetu. Baadhi yao wamesema kwamba kuna mmoja tu—sisi. Wengine wamesema kwamba kihisabati, kwapasa kuwa na chache zaidi ya moja—hata sisi hatupaswi kuwa hapa!
Si vigumu kuuona msingi wa kuwazia-wazia kwao. Ungeweza kufanyiwa muhtasari kwa maswali mawili: Ikiwa kuna hao wakaaji wa nje ya dunia hii, wangekuwa wanaishi wapi? Nao waliendaje huko?
‘Ala, si wangeishi juu ya sayari,’ huenda watu fulani wakajibu hivyo swali hilo la kwanza. Lakini kuna sayari moja tu katika mfumo wa jua ambayo haitatanishi uhai kabisa, ile moja ambayo sisi twaikaa. Lakini namna gani sayari zinazozunguka maelfu ya mamilioni ya nyota nyinginezo katika galaksi yetu? Je! haingeweza kuwa kwamba baadhi yazo zina uhai? Uhakika ni kwamba kufikia sasa wanasayansi hawajathibitisha kikamili kwamba kuna sayari hata moja nje ya mfumo wetu wa jua. Kwa nini?
Kwa sababu ni vigumu mno kuweza kuona moja. Kwa kuwa nyota ziko mbali sana na sayari hazitoi nuru yoyote yenye kutokana nazo zenyewe, kuweza kuona hata sayari kubwa sana, kama vile Jupiter, ni kama kujaribu kuona chembe ya vumbi yenye kuelea kuzunguka balbu ya taa yenye nguvu nyingi iliyoko umbali wa kilometa nyingi.
Hata kama sayari hizo ziko—na kuna uthibitisho fulani usio wa moja kwa moja ambao umerundamana kuonyesha kwamba ziko—bado hiyo haimaanishi kwamba hizo huzunguka aina ile ifaayo kabisa ya nyota katika ujirani wa galaksi ile ifaayo kabisa, katika umbali ule ufaao kabisa kutoka kwenye nyota hiyo, na kwamba hizo zenyewe ni za saizi na muundo ule ufaao kabisa ili kuendeleza uhai.
Msingi Wenye Kumong’onyoka
Ingawa hivyo, hata ikiwa kuna sayari nyingi zenye kutimiza yale matakwa magumu sana yaliyo ya lazima ili kuendeleza uhai kama tuujuavyo, swali hili labakia, Uhai ungetokeaje katika malimwengu hayo? Hiyo yatuleta kwenye msingi wenyewe wa imani ya kwamba kuna wahai katika malimwengu mengine—mageuzi.
Kwa wanasayansi wengi, laonekana kuwa jambo la kiakili kuamini kwamba kama uhai ungeweza kugeuka-geuka kutokana na mata isiyo na uhai katika sayari hii, hiyo ingeweza kuwa kweli katika nyinginezo pia. Kama vile mwandikaji mmoja alivyoweka wazo hilo: “Kufikiri kwa ujumla miongoni mwa wanabayolojia ni kwamba uhai utaanza wakati wowote upewapo mazingira ambamo waweza kuanza.” Lakini hapo ndipo mageuzi hukabiliana na kipingamizi kisichoshindika. Mageuzi hayawezi hata kueleza jinsi uhai ulivyoanza juu ya sayari hii.
Wanasayansi Fred Hoyle na Chandra Wickramasinghe hukadiria kwamba kutowezekana kwa enzaimu muhimu za uhai kufanyika kwa nasibu ni moja katika 1040,000 (1 ikifuatwa na sifuri 40,000). Wanasayansi Feinberg na Shapiro wachukua hatua zaidi. Katika kitabu chao Life Beyond Earth, wao huweka kutowezekana kwa vitu vilivyomo katika mchuzi wa uhai kuchukua hatua za kwanza za msingi kuelekea kuwa hai ni moja katika 10,1,000,000. Kama tungeandika tarakimu hiyo, gazeti hili lililo mkononi mwako lingekuwa na maki (unene) zaidi sana ya kurasa 300!
Je! wewe waziona hizo tarakimu kubwa mno kuwa ngumu kushikwa na akili? Neno “haiwezekani” ndilo rahisi zaidi kukumbukwa, nalo ni sahihi kabisa.a
Na bado, kwa kujawa na furaha wanaanga wa SETI hudhani kwamba ni lazima uhai uwe ulipata asili kwa nasibu kotekote katika ulimwengu wote mzima. Gene Bylinsky, katika kitabu chake Life in Darwin’s Universe, hukisia juu ya vipito mbalimbali ambavyo vingeweza kuwa vilifuatwa na mageuzi kuhusiana na malimwengu ya kigeni. Yeye hudokeza kwamba mawazo juu ya kuwako kwa pweza wakubwa, wanadamu wenye vifuko-tumbo vya kubebea watoto, na watu-popo wenye kufanyiza vyombo vya kimuziki si ya kutungwa tu. Wanasayansi mashuhuri wamesifu kitabu chake. Hata hivyo, wanasayansi wengine, kama vile Feinberg na Shapiro, huiona ile dosari ya wazi sana katika usababu wa jinsi hiyo. Wao huonyesha wazi “udhaifu ulio katika misingi ile mikubwa ya kufanyia majaribio” ya nadharia za wanasayansi juu ya jinsi uhai ulivyoanza duniani. Ingawa hivyo, wao husema kwamba wanasayansi hata hivyo “wametumia misingi hii kufanyiza mawazo ya kutazamia mambo makubwa kupita kiasi yaliyo kama minara yenye urefu unaofika mwisho wa [anga la] Ulimwengu Wote Mzima.”
Dini Ile Isiyofaa
Huenda wewe ukashangaa kwa kujiuliza, ‘Kwa nini wanasayansi wengi sana huchukua yasiyowezekana kana kwamba yawezekana?’ Jibu ni sahili na la kuhuzunisha kwa kiasi fulani. Watu huelekea kuamini kile watakacho kuamini. Wanasayansi, wajapofanya madai yao yote kwamba wao huchukua mambo kwa njia isiyo na upendeleo, hawaepushwi na kosa hili la kibinadamu.
Hoyle na Wickramasinghe wana maoni ya kwamba “nadharia ya kwamba uhai ulikusanywa na mtu mwenye akili” ina uyamkini “mkubwa sana” wa kuwa hivyo kuliko kwamba ulitokea wenyewe tu. “Kwa kweli,” wao huongezea kwamba, “nadharia ya jinsi hiyo iko wazi sana hivi kwamba mtu hushangaa ni kwa nini haikubaliwi kotekote kuwa yenye kujithibitisha wazi. Sababu zahusiana na hali ya kimawazo wala si ya kisayansi.” Ndiyo, wanasayansi wengi huwa hawataki kusikia wazo la kwamba kuna Muumba, hata ingawa uthibitisho waelekeza kidole upande huo. Katika kufanya hivyo, wamefanyiza dini yao wenyewe. Kama vile watungaji waliotangulia kutajwa waonavyo, nadharia ya Darwin huweka neno “Asili” (Maumbile) mahali pa neno “Mungu.”
Kwa hiyo kwa kujibu lile swali, “Je! kuna mtu yeyote huko nje?” sayansi haitoi misingi yoyote ya kuamini kuna uhai katika sayari nyinginezo. Kwa uhakika, kadiri miaka ipitavyo na ukimya kuendelea kutoka kwenye nyota, shughuli ya SETI ni aibisho lenye kuongezeka kwa wanasayansi wanaoamini mageuzi. Ikiwa namna mbalimbali za uhai hugeuka-geuka tayari kutokana na kisichokuwa uhai, mbona basi hatupati habari kutokana nazo katika huu ulimwengu wote mzima ulio mkubwa sana? Ziko wapi?
Kwa upande mwingine, ikiwa swali hilo lafaa kuulizwa katika dini, tutapataje jibu? Je! Mungu aliumba uhai katika malimwengu mengine?
[Maelezo ya Chini]
a Sehemu nyingine yote ya nadharia ya mageuzi imejawa hivyo hivyo na matatizo. Tafadhali ona kitabu Life—How Did It Get Here? By Evolution or by Creation? chenye kuchapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
[Sanduku katika ukurasa wa 8]
Je! Ni Wageni Wanaozuru Kutoka Kule Ng’ambo?
Watu wengi huamini kwamba binadamu anafanyiwa ziara, au amefanyiwa ziara wakati uliopita, na wakaaji wa nje ya dunia hii. Kwa ujumla wanasayansi hupuuza madai hayo; wao hutaja kwamba hakuna uthibitisho hakika katika visa vyote na hushikilia kwamba visa vingi zaidi vya kuona UFO (kitu kirukacho kisichotambulikana) vyaweza kuelezwa kwa ajabu za kiasili. Wao huelekea kupunguza uzito wa madai yanayohusu watu wenye kutwaliwa ghafula kwa kuonyesha kwamba mambo huonekana hivyo kwa sababu ya maeneo yasiyopata kupelelezwa ya akili ya kibinadamu au kwa sababu ya mahitaji ya kiakili na ya kidini.
Mwandikaji mmoja wa bunilizi (hadithi za kubuni) za sayansi aliandika hivi: “Hima ya kuchunguza na kuamini mambo hayo ni kama ya kidini hasa. Hapo zamani tulikuwa na miungu. Sasa sisi twataka kuhisi hatuko peke yetu, kwamba twalindwa na majeshi fulani ya kiulinzi.” Zaidi ya hilo, baadhi ya matukio ya UFO yahusiana zaidi na mafumbo ya roho kuliko sayansi.
Lakini wanasayansi wengi huamini kwa njia yao wenyewe katika “wageni wenye kuzuru.” Wao huona kutowezekana kwa uhai kuanza kwa nasibu hapa duniani, kwa hiyo hudai ni lazima uwe ulipeperukia huku kutoka angani. Baadhi yao husema kwamba watu wa kigeni walileta mbegu ya uhai kwenye sayari yetu kwa kupeleka roketi zenye kujazwa bakteria za kizamani. Mmoja hata amedokeza kwamba watu wa kigeni walizuru sayari yetu enzi zilizopita na kwamba uhai ulitokana na nasibu kutokana na takataka walizoacha nyuma! Wanasayansi fulani hukata mashauri kutokana na uthibitisho wa kwamba molekyuli sahili zenye uhai hupatikana kwa wingi katika anga. Lakini je! huo ni uthibitisho wa kweli kweli kwamba uhai ulifanyika kwa nasibu? Je! kuwako kwa duka la vyuma vya magari ni uthibitisho wa kwamba ni lazima gari lijijenge lenyewe humo?
[Picha katika ukurasa wa 7]
Hata kama kuna sayari nyinginezo zenye kukalika, je! kuna uthibitisho wowote kwamba uhai ungeweza kuanzia huko kwa nasibu?