Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g90 9/8 kur. 3-6
  • Kutafuta-tafuta Maisha Marefu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kutafuta-tafuta Maisha Marefu
  • Amkeni!—1990
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Maoni ya Kufanya Mambo Kisayansi
  • Matazamio Ni Nini?
  • Je! Sasa Kuna Maisha Marefu Zaidi, Yenye Furaha Zaidi?
  • Uwezalo Kufanya
  • Watu Wazee Wanaongezeka ulimwenguni
    Amkeni!—1999
  • Je, Unaweza Kuepuka Kuzeeka?
    Amkeni!—2006
  • Kwa Nini Sisi Huzeeka?
    Amkeni!—2006
  • Jitihada za Kurefusha Maisha
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Toleo la Watu Wote)—2019
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1990
g90 9/8 kur. 3-6

Kutafuta-tafuta Maisha Marefu

KUTAFUTA-TAFUTA maisha marefu zaidi kumekuwapo kwa muda unaokaribia kulingana na ule ambao uhai wenyewe umekuwapo. Kwa hiyo haishangazi kwamba historia, ya kale na ya ki-siku-hizi pia, ina hadithi na hekaya tele juu ya watu wenye kutafuta-tafuta siri ya maisha marefu.

Kwa kielelezo, historia yenye kusisimua mawazo ingetaka tuamini kwamba mvumbua nchi Mhispania Juan Ponce de León alikuwa akitafuta-tafuta chemchemi ya ujana aliposafiri kaskazini kutoka Puerto Riko katika mwaka 1513. Lakini marika wake wakataarifu kwamba alifunga safari hiyo ili akajipatie watumwa na bara jipya. Alichogundua hakikuwa chemchemi ya kurudisha ujana, bali ile ambayo sasa ndiyo Florida. Hata hivyo, hekaya hiyo ingali yaendelea.

Ukirudi kwenye wakati wa nyuma zaidi, usimulizi wa Kiakkadi wa matendo hodari ya Gilgamesh, ambao umetolewa kwenye mabamba ya udongo ya kabla ya karne ya 18 K.W.K., hueleza jinsi Gilgamesh alipagawa na hofu ya kufa baada ya Enkidu rafiki yake kufa. Hueleza safari zake na jitihada kali lakini zisizofua dafu za kufikia kutokufa.

Hivi majuzi zaidi, katika 1933, James Hilton katika riwaya yake Lost Horizon, alisimulia bara la kuwaziwa liitwalo Shangri-la. Wakaaji huko walionea shangwe maisha yanayokaribia kukamilika na kurefuka katika mazingira ya kiparadiso.

Hata leo, kuna wale ambao wamejitolea kufuatia mipango isiyo ya kawaida na ya kigeni-geni yenye ahadi ya kupata maisha marefu yaliyo nafuu. Hata hivyo, wengine huwa na maoni ya kishupavu zaidi. Wao huchukua hatua za kutafuta afya kwa kujikaza mno au hufuatilia sana kawaida za ulaji na mazoezi. Wao hutumaini kwamba hiyo itawasaidia waonekane wachanga zaidi na wahisi vizuri zaidi.

Hayo yote hukazia tamaa ya msingi ya kibinadamu ya kuishi maisha ndefu zaidi, zenye furaha zaidi.

Maoni ya Kufanya Mambo Kisayansi

Uchunguzi juu ya uzee na matatizo ya wazee umekuwa sayansi yenye kushughulikiwa kwa uzito. Wanasayansi wenye sifa huhisi kwamba wanakaribia sana kuvumbua kisababishi cha uzee. Baadhi yao hufikiri kwamba uzee umepangiliwa katika chembe za urithi. Wengine huhisi kwamba huo ni tokeo lililorundamana la magonjwa yenye kuharibu na matokeo yenye madhara kutokana na kuvunjika-vunjika kwa chembe za mwili. Bado wengine huhesabu kwamba uzee hutokana na hormoni au mfumo wa kinga za mwili. Wanasayansi huhisi kwamba kisababishi cha uzee kikiweza kujulikana wazi kabisa, basi labda chaweza kuondolewa mbali.

Katika kufuatia kutokufa, inakuwa vigumu zaidi na zaidi kupambanua tofauti yenye kutenganisha sayansi na sayansi iliyo ya kuwaziwa tu. Kielelezo kimoja cha jinsi hiyo ni uzalishi wa kuunganisha mwili mlinganifu wa kitu kwa kuunga chembe na kiasili cha urithi. Halafu, sehemu za mwili zipatwapo na maradhi au kukosa kufanya kazi, kiungo kipya chaweza kutolewa kwenye mwungo huo na kupandikizwa, kama vile sehemu iliyovunjika katika gari hubadilishwa kwa sehemu mpya ya kujazia. Wanasayansi fulani hudai kuwa kuna mambo mengi sana yasiyo na kikomo yawezayo kufanywa kwa kuunga chembe na kiasili cha urithi.

Halafu kuna ule utaratibu wa mbinu za krayoniki (ubaridishaji). Wenye kuuendeleza hueleza kwamba mtu afapo, mwili waweza kuhifadhiwa mpaka wakati ambapo ponyo lapatikana kwa kile kisichoponyeka leo. Halafu mwili waweza kuyeyushwa, uhuishwe tena, na kurudishiwa hali ya kwanza—yatumainiwa uwe na maisha marefu zaidi, yenye furaha zaidi.

Kwa sababu ya jitihada hizo na matumizi ya mamilioni yasiyohesabika ya dola za utafiti, tokeo limekuwa nini? Je! tumekaribia zaidi kujiweka huru na nira ya kifo kuliko maelfu ya mamilioni ya watu wale wote ambao wameishi na kufa kabla ya sisi?

Matazamio Ni Nini?

Ikiamuliwa kulingana na mipigo ya mbiu na matabiri yaliyofanywa na baadhi ya wale ambao wamejitia katika utafiti huo, ingeonekana kwamba karibuni sana kutakuwako maisha marefu kuliko yale ambayo tumezoea. Hivi hapa ni vielelezo vichache vilivyodondolewa miaka ya mwisho-mwisho wa 1960.

“Maarifa tupatayo kwa kutafuta-tafuta jinsi hiyo yatatupa sisi silaha ambazo twahitaji ili kupigana na yule adui wa mwisho—Kifo—tumpige hadi shina lake mwenyewe. Hiyo itafanya sisi tuweze kufikia hali ya kutokufa . . . Ingeweza kuwa hivyo katika wakati wetu.”—Alan E. Nourse, tabibu na mwandikaji.

“Tutalifutilia mbali kabisa tatizo la kuzeeka, hivi kwamba aksidenti tu ndizo zitakazokuwa kisababishi pekee cha kifo.”—Augustus B. Kinzel, ambaye wakati huo alikuwa msimamizi wa Taasisi ya Salk ya Mafunzo ya Kibayolojia.

“Kutokufa (katika maana ya kuwa na maisha yenye kurefuka kwa wakati usio dhahiri) kwaweza kupatikana kwa kutumia ustadi, si kwa ajili ya wazao wetu tu bali pia kwa ajili ya sisi wenyewe.”—Robert C. W. Ettinger katika The Prospect of Immortality.

Ingawa wakati huo si wachunguzi na watafiti wote wa hali ya kuzeeka walio na msisimuko huo, maoni ya ujumla ya wastadi yalionekana kuwa kwamba ufikapo mwanzo wa karne ya 21, kuzeeka kungedhibitiwa, na maisha yangerefushwa kwa kadiri kubwa.

Kwa kuwa sasa tuko karibu zaidi na mwanzo wa karne ya 21, mambo yakoje? Licha ya hali ya kutokufa, je! maisha marefu zaidi yaweza kupatikana? Fikiria maono haya.

“Wachunguzi wengi wa hali ya kuzeeka wataafikiana kwamba hizi ni nyakati zenye mvurugo mwingi sana kwetu. Sisi hatujui ni kitu gani hasa husababisha kuzeeka, wala hatuwezi kupima kadiri ya kuzeeka kulingana na utendaji fulani halisi wa kemikali mwilini.”—Journal of Gerontology, Septemba 1986.

“Hakuna mtu ajuaye vizuri kabisa utaratibu uletao uzee au kwa nini huo hufuata mwendo tofauti katika watu tofauti-tofauti. Wala hakuna mtu yeyote ajuaye jinsi ya kuongezea urefu wa maisha ya kibinadamu, kujapokuwako madai ya udanganyifu na yaliyo hatari nyakati fulani ambayo hufanywa na walaghai wasemao juu ya ‘kurefusha maisha’ na ya wengine ambao hufanya uchuuzi [wa kujinufaisha] kutokana na hofu na magonjwa ya wazee-wazee.”—FDA Consumer, jarida rasmi la Usimamizi wa United States wa Chakula na Dawa za Kulevya, Oktoba 1988.

Matabiri yaliyofanywa wakati uliopita juu ya kushinda kifo na kurefusha maisha kwa wakati usio dhahiri yaonekana wazi kuwa ya kusisimuka kupita kiasi. Kupata hali ya kutokufa kupitia sayansi kungali ndoto tu. Je! hiyo yamaanisha kwamba hakuna jambo liwezalo kufanywa ili kurefusha maisha au angalau kuyatia nafuu, mpaka kutakapotokea ugunduzi mkubwa katika sayansi au tekinolojia?

Je! Sasa Kuna Maisha Marefu Zaidi, Yenye Furaha Zaidi?

Ingawa watafiti hawajagundua siri ya maisha marefu, wamejifunza mengi juu ya uhai na ule utaratibu wa kuzeeka. Na baadhi ya habari ambazo zimepatikana jinsi hiyo zaweza kutumiwa kwa faida.

Kwa kielelezo, majaribio ya kuchunguza wanyama yamefunua kwamba “ulaji wa kiasi kidogo chenye kudhibitiwa waweza kurefusha viwango vya juu kabisa vya muda wa maisha kwa zaidi ya asilimia 50 na kukawiza kuzeeka sura na matatizo mengi makali yanayohusiana na uzee,” laripoti Times la London. Hiyo imeongoza kwenye uchunguzi juu ya kama yaweza kuwa hivyo hivyo kuhusu wanadamu.

Kwa hiyo, katika kitabu chake The 120-Year Diet (Ulaji wa Kuishi Miaka 120), Dakt. Roy Walford apendekeza kalori chache, mafuta machache, na ulaji mwingi wa vitu vyenye kujenga mwili pamoja na programu yenye mazoezi mazuri. Yeye atoa kielelezo cha watu wa Okinawa. Kwa kulinganishwa na ulaji wa Mjapani wa wastani, ulaji wao una kalori chache kwa karibu asilimia 40; hata hivyo wao “wana wanakarne [watu wa miaka 100] ambao hesabu yao ni mara 5 hadi 40 kama ile ya visiwa vingine vya Kijapani.”

Wenyeji wa jimbo la Caucasus katika Urusi ya magharibi ni kielelezo kingine cha maisha marefu ambacho hutajwa mara nyingi. Sula Benet, aliyeishi miongoni mwa wakaaji wa Caucasus, aliripoti katika kitabu chake How to Live to Be 100 (Jinsi ya Kuishi Kufikia Miaka 100) kwamba hesabu kubwa isivyo kawaida ya watu hao huishi maisha zenye afya na utendaji mwingi wakiwa wamekwishapita sana umri wa miaka 100, na kadhaa husemwa kuwa waliishi zaidi ya miaka 140. Mwanamke huyo aliandika kwamba “visababishi viwili hudumu kuwa vile vile katika ulaji wa wakaaji wa Caucasus: 1. Hakuna kula kupita kiasi . . . 2. Utwaaji mwingi kabisa wa vitamini za kiasili katika mboga zenye ubichi.” Kwa kuongezea, “si kwamba kazi yao huwaandalia mazoezi ya kimwili tu bali pia huwapa maarifa ya kwamba kwa kuifanya wanakuwa wakitoa mchango wa maana kwa jumuiya yao.”

Uwezalo Kufanya

Je! utatuzi ni kuhamia Okinawa au Caucasus au eneo fulani jingine ambako wenyeji huona shangwe ya maisha marefu zaidi? Labda sivyo. Lakini kuna mambo fulani ambayo wewe waweza kufanya. Waweza kuiga tabia nzuri za watu hao wenye kuishi muda mrefu na kufuata ushauri wa madaktari hodari, wanalishe, na wastadi wa afya.

Karibu hao wote hupendekeza maisha ya kiasi. Hiyo humaanisha si kufikiria kiasi tu cha chakula ulacho bali pia kuwa chonjo kula vyakula vyenye kujenga mwili na kuleta afya ambavyo waweza kuvipata. Pia yajulikana kwamba mazoezi ya ukawaida yana matokeo mazuri. Jitihada ya kiasi kufuata kanuni hizo na kukomesha tabia zenye madhara za jamii ya ki-siku-hizi, kama vile kuvuta sigareti na dawa za kulevya na utumizi mbaya wa kileo, yaweza kabisa kukufanya uhisi vizuri zaidi.

Ni wazi kwamba, kadiri tuutendeavyo mwili wetu vizuri zaidi, ndivyo tuwavyo wenye afya zaidi. Na kadiri tulivyo na afya zaidi, ndivyo tulivyo na fursa nzuri zaidi za kuishi muda mrefu zaidi. Hata hivyo, hata tufanye nini, muda wa maisha ya wastani wabaki ukiwa ile miaka 70 au 80 ya Kibiblia. (Zaburi 90:10) Je! kuna tumaini lolote kwamba muda huu wa maisha utapata kurefushwa, na ikiwa ndivyo, kwa urefu gani?

[Sanduku katika ukurasa wa 5]

WEWE UNA UMRI GANI?

Uwe unang’amua au sivyo, wewe una umri mkubwa kuliko vile huenda ukafikiri. Sayansi ya kibayolojia hutuambia kwamba wakati wa kuzaliwa, mifuko ya mayai ya mwanamke huwa tayari na mayai yote ambayo yeye atapata kuyazaa. Hiyo yamaanisha kwamba ikiwa mama yako alikuwa na umri wa miaka 30 wakati wewe ulipochukuliwa mimba, yai ambalo hatimaye lilikuja kuwa wewe lilikuwa tayari na umri wa miaka 30.

Labda hiyo haifanyi wewe uhisi ukiwa na umri mkubwa zaidi, lakini siku kwa siku, unakuwa mwenye umri mkubwa zaidi. Tuwe tu wachanga au wazee, sisi sote tunazeeka, na walio wengi kati yetu hupendezwa na kupunguza mwendo wa utaratibu huo—ikiwa si kuukomesha kikweli.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki