Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 7/22 kur. 3-4
  • Watu Wazee Wanaongezeka ulimwenguni

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Watu Wazee Wanaongezeka ulimwenguni
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • “Mojawapo ya Utimizo Mkubwa Zaidi wa Binadamu”
  • Kinachohitajika—Ni Badiliko la Maoni
  • Je, Unaweza Kuepuka Kuzeeka?
    Amkeni!—2006
  • Kwa Nini Sisi Huzeeka?
    Amkeni!—2006
  • Kutafuta-tafuta Maisha Marefu
    Amkeni!—1990
  • Kwa Nini Tunazeeka na Kufa?
    Amkeni!—1995
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 7/22 kur. 3-4

Watu Wazee Wanaongezeka ulimwenguni

MNAMO mwaka wa 1513, mvumbuzi Mhispania Juan Ponce de León alifikia ufuo mmoja kwenye sehemu ya pwani isiyojulikana huko Amerika Kaskazini. Ripoti moja yasema kwamba kwa kuwa eneo alilovumbua lilikuwa limefunikwa kwa maua, aliliita Florida, jina la Kihispania limaanishalo “-enye Maua Mengi.” Haikuwa vigumu kupata jina. Lakini kusudi la safari yake—la kutafuta chemchemi ya maji yenye uwezo wa kuwafanya watu wazee wawe vijana tena—halikuwezekana. Baada ya kutafuta kila sehemu ya nchi hiyo kwa miezi mingi, mvumbuzi huyo aliacha kutafuta chemchemi ya kihekaya ya kurudisha ujana kisha akaendelea na safari yake.

Ijapokuwa chemchemi za ujana bado hazipatikani leo kama katika nyakati za Ponce de León, yaonekana kwamba mwanadamu amegundua kile kilichoitwa na mwandikaji Betty Friedan “chemchemi ya uzee.” Alisema hivyo kwa sababu ya ongezeko kubwa la idadi ya watu wazee ulimwenguni pote. Watu wengi sana sasa wanafikia umri wa uzee hivi kwamba muundo wa watu ulimwenguni unabadilika. Kwa kweli, idadi ya watu wazee ulimwenguni inaongezeka.

“Mojawapo ya Utimizo Mkubwa Zaidi wa Binadamu”

Takwimu za watu hufunua mengi. Mwanzoni mwa karne hii, muda wa maisha unaotarajiwa wakati mtu anapozaliwa ulikuwa chini ya miaka 50 hata katika nchi tajiri zaidi. Leo, umeongezeka hadi zaidi ya miaka 75. Hali kadhalika, katika nchi zinazositawi kama China, Honduras, Indonesia, na Vietnam, muda wa maisha unaotarajiwa wakati wa kuzaliwa ni miaka 25 zaidi ya ulivyokuwa miongo minne tu iliyopita. Kila mwezi, watu milioni moja ulimwenguni pote wanafikia umri wa miaka 60. Kwa kushangaza, watu wenye umri wa miaka 80 na zaidi, wale ‘wazee wakongwe’ ndio kikundi kinachoongezeka haraka sana duniani leo wala si vijana.

“Kurefuka kwa muda ambao watu hutarajiwa kuishi,” asema mtaalamu wa takwimu za watu Eileen Crimmins katika gazeti Science, “kumekuwa mojawapo ya utimizo mkubwa zaidi wa binadamu.” Shirika la Umoja wa Mataifa linakubaliana naye, na ili kuvuta uangalifu kwa utimizo huu, limeteua mwaka wa 1999 kuwa Mwaka wa Kimataifa wa Watu Wazee.—Ona sanduku kwenye ukurasa wa 3.

Kinachohitajika—Ni Badiliko la Maoni

Ingawa hivyo, utimizo huu ni zaidi ya badiliko katika muda ambao mtu anatarajia kuishi. Unatia ndani pia badiliko katika maoni ya wanadamu juu ya kuzeeka. Ni kweli kwamba wazo la kuzeeka bado huwahangaisha watu wengi sana, na kuwatia hofu, kwa sababu kwa kawaida uzee huhusianishwa na mwili dhaifu na kupungua kwa uwezo wa kufikiri. Hata hivyo, watafiti wanaochunguza hali ya kuzeeka wanasisitiza kwamba kuzeeka na kuwa mgonjwa ni mambo mawili tofauti. Watu huzeeka kwa njia zinazotofautiana sana. Watafiti wanasema kwamba kuna tofauti kati ya umri wa mtu na kudhoofika kimwili. (Ona sanduku “Kuzeeka Ni Nini?”) Yaani, kuzeeka na kudhoofika kimwili si lazima kuambatane pamoja.

Kwa kweli, uzeekapo unaweza kuchukua hatua zinazoweza kuboresha hali yako ya maisha. Kwa kawaida, mambo haya hayatakufanya uwe kijana, lakini huenda yakakuwezesha kudumisha afya bora uzeekapo. Makala ifuatayo inazungumzia baadhi ya hatua hizi. Hata ikiwa kuzeeka hakukuhangaishi sasa, huenda ukataka kuendelea kuisoma, kwa kuwa punde si punde itakuhangaisha.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 3]

MWAKA WA KIMATAIFA WA WATU WAZEE

“Nikiwa nimetimia miaka 60 . . . , mimi sasa huhesabiwa katika takwimu nilizozitaja hapo awali,” akasema Katibu-Mkuu wa UM Kofi Annan hivi majuzi alipotangaza Mwaka wa Kimataifa wa Watu Wazee. Kuna watu wengi walio kama Bw. Annan. Watafiti wanasema kwamba mwanzoni mwa karne ya 21, katika nchi nyingi mtu 1 kati ya kila 5 atakuwa na umri wa miaka 60 au zaidi. Baadhi yao watahitaji kutunzwa, lakini wote watahitaji kupata njia ambazo wataweza kuhifadhi uhuru wao, staha yao, na utendaji wao. Ili kusaidia watunga-sera wakabiliane na magumu yanayoletwa na ‘badiliko la muundo wa idadi ya watu’ na ili kutambua zaidi “thamani ya watu wazee katika jamii,” Mkutano Mkuu wa UM uliamua katika mwaka wa 1992 kwamba mwaka wa 1999 utakuwa Mwaka wa Kimataifa wa Watu Wazee. Kichwa cha mwaka huu wa pekee ni, “Kuelekea Kuwa na Jamii ya Watu wa Umri Wote.”

[Picha]

Kofi Annan

[Hisani]

UN photo

UN/DPI photo by Milton Grant

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 4]

KUZEEKA NI NINI?

“Njia ya kutabiri matukio ya wakati ujao haitegemeki inapohusu kuzeeka,” asema mtafiti mmoja. “Hakuna yeyote anayeelewa vizuri kuzeeka,” akataarifu mwingine. Ijapokuwa hivyo, wanasayansi wanaochunguza kuzeeka wamejaribu kufafanua hali hiyo. Kwa ufupi, wanasema kwamba kuzeeka ni miaka aliyoishi mtu. Lakini kuzeeka ni zaidi ya kupita kwa miaka. Kwa kawaida hakuna mtu anayesema juu ya mtoto kuzeeka kwa sababu kuzeeka hudokeza kudhoofika kwa uwezo wa mtu. Kuzeeka ni madhara yanayompata mtu kwa sababu ya kusonga kwa miaka. Watu fulani huonekana wakiwa vijana zaidi ya umri wao. Kwa mfano, hili hudokezwa mtu fulani anapoambiwa kwamba “anaonekana kijana.” Ili kutofautisha baina ya kuzeeka kwa umri na kuzeeka kimwili, kwa kawaida watafiti hufafanua kuzeeka kimwili (kuzeeka kunakoandamana na kudhoofika kimwili) kuwa kukonga.

Profesa wa zuolojia Steven N. Austad anaeleza kukonga kuwa “kudhoofika polepole kwa karibu kila utendaji wa kimwili muda usongapo.” Naye Dakt. Richard L. Sprott, wa Taasisi ya Kitaifa Inayochunguza Kuzeeka, asema kwamba kuzeeka “ni kudhoofika polepole kwa zile sehemu za mifumo yetu zinazotuwezesha tukabiliane kwa utayari na mikazo.” Ingawa hivyo, wataalamu wengi hukubali kwamba kupata ufafanuzi dhahiri wa kuzeeka bado ni tatizo. Mwanabiolojia wa Molekyuli Dakt. John Medina aeleza sababu: “Toka utosini hadi wayo, toka protini hadi chembe za DNA, toka kuzaliwa hadi kifo, kuna mambo mengi sana yasiyoelezeka yanayotukia na kumfanya mwanadamu mwenye chembe zipatazo trilioni 60 azeeke.” Si ajabu kwamba watafiti wengi wanakata kauli kwamba kuzeeka ni “tatizo gumu sana kuelewa kupita matatizo yote ya kibiolojia”!

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki