Jinsi ya Kufanya Mengi Zaidi Katika Wakati Mchache Zaidi
‘Wakati ulienda wapi?’ Ni mara nyingi kadiri gani wewe umejikuta ukijiuliza swali hilo? Ikiwa wewe ni kama watu walio wengi, labda huliuliza mara nyingi zaidi ya uwezavyo kukumbuka.
Mambo yanayofuata yatokeza madokezo kulingana na maoni ya mwanamke, lakini kwa kuwa wanawake na wanaume wana kiasi kile kile cha wakati kila juma, swali ni hili, ‘Mimi nawezaje kupata manufaa nyingi zaidi kutokana na wakati nilio nao?’ ni moja ambalo wanaume na wanawake pia wangependa kujibu.
Panga Mambo ya Kufanywa Kwanza
Kwa kuwa kila utendaji wa maisha huchukua wakati, kuna mambo fulani ambayo kiasili hutangulia mengine kwa umaana. Kwa kielelezo, katika asubuhi baridi ya kipupwe, hakuna jambo ambalo mama angetaka kufanya kuliko kukaa muda mrefu zaidi katika kitanda chake chenye ujoto. Lakini saa yatoa ishara kwamba ni wakati wa kutayarisha kiamsha-kinywa na kuaga mume wake kwenda kazini na watoto kwenda shuleni.
Pia ni lazima upange yaliyo ya kufanywa kwanza ikiwa mambo ya nyumba yako yataenda ifaavyo. Kuna wakati wa kwenda dukani kununua chakula na wakati wa kukipika; wakati wa kusafisha nyumba na wakati wa kufua nguo; wakati wa kustarehe na wakati wa kujifunza; wakati wa kuangalia masomo ya nyumbani ya watoto na kazi za nyumbani—na kadha wa kadha.
Je! wewe hufanya kazi nje ya nyumbani? Ikiwa ndivyo, kukiwa na kazi zaidi za kufanya, wakati huwa wa thamani kubwa hata zaidi. Huwezi kuthubutu kuuharibu, wala huwezi sikuzote kuahirisha mambo kwa ajili ya siku nyingine. Ndiyo sababu wanawake wengi hukiri kwamba ratiba yahitajiwa kabisa ili kazi yao iweze kufanyika.
“Bila ratiba ya kila siku,” asema Josephine, mama ya watoto sita wa kuanzia umri wa miaka 2 hadi 15, “singeweza kamwe kutimiza miradi yangu ya kila siku.” Sandra, aliye na watoto watatu, hufanya kazi nje ya nyumbani muda wa saa 25 kwa juma, naye huafiki hivi: “Kwa kweli, kama singekuwa na ratiba, nafikiri ningerukwa na akili.”
Zaidi ya hilo, bila shaka chenye kuamua ni mambo gani utafanya kwanza ni kadiri ambavyo wewe huuthamini wakati wenyewe. Hivyo ndivyo mambo ya Lola huamuliwa. Si kwamba tu yeye ana mume wa kutunza bali pia hutumia kuanzia saa 90 hadi 100 kwa mwezi kwenye kazi yake ya elimu ya Biblia. Yeye ataarifu hivi: “Wakati ni wa maana sana kwangu. Mimi nahisi yafaa kabisa kutokawiza watu wakiningojea. Na wakati wale ambao huenda ikawa ni wazembe waonapo kwamba mimi huthamini sana wakati, wao huelekea kuustahi zaidi wakati wangu.”
Zipange Kazi Kitengenezo
Kwa nini wanawake fulani huelekea kutotimiza kamwe kazi yao? Au kwa nini baadhi yao hulalamika sikuzote juu ya kukosa wakati? Je! sababu moja ingeweza kuwa kwamba wao hushindwa kupanga kazi yao kitengenezo? Katika vizazi vilivyopita iliwachukua wanawake siku nzima kufua na siku ya pili kupiga pasi, hali kila siku walinunua vitu dukani na kupika. Hata hivyo, katika nchi zilizo nyingi leo, mwanamke aweza kusafisha nyumba, afue nguo na kuzikausha, na kupika wakati ule ule ikiwa amepanga mambo kitengenezo. Vifaa vya ki-siku-hizi vimewaweka huru wanawake kufanya kazi nje ya nyumbani na bado watunze mahitaji ya familia.
Lakini namna gani wakati utumiwao mbali na nyumbani? Sehemu kubwa ya wakati huo, mbali na ule unaotumiwa hasa kufanya kazi, hutumiwa kusafiri kwenda na kutoka kazini, kungoja katika ofisi za madaktari na matabibu wa meno na kwingineko. Je! mwingi wa wakati huu ungeweza kutumiwa? Kwa kielelezo, je! wewe hufuma sweta, kupiga krocheti, kushona, au kushonelea umaridadi katika vitambaa? Je! ungeweza kuratibu baadhi ya majaliwa haya kwenye nyakati na mahali pa jinsi hiyo? Wanawake wengi husoma, hutayarisha orodha ya vitu vya kununua, au huandika barua. Kwa uhakika, wakati ule mwingine uketipo ili utazame televisheni, kwa nini usifanye ushonaji fulani au ufanyize vitu fulani kwa ajili ya familia? Huenda wao wakavithamini kuliko vile vya kununuliwa dukani, nawe utakuwa na uthibitisho wenye kuonekana wazi kwamba wewe huharibu wakati!
Hata hivyo, kuna upande mwingine wa jambo hili. Mtu apaswa kuepuka kufuatilia mipango mno kwa kujaribu kutumia kila dakika. Waweza kuwa mtumwa wa wakati, na hiyo itakunyang’anya shangwe. Kuna nyakati ambapo mtu hutaka kuketi kwa utulivu na kufikiria mambo ambayo amefanya. Dakika hizo zaweza kuwa zenye thamani kweli kweli!
Kanuni iyo hiyo ingetumika wakati ambapo kuweka akiba ya pesa kwahusika. Usawaziko wahitajiwa. Huenda ukazunguka-zunguka mji mzima kutafuta kitu ambacho kitaokoa mapeni machache, kumbe utumie wakati na petroli nyingi zaidi kwa kufanya hivyo. Bila shaka, ikiwa matumizi ya pesa zako yahitaji kuchungwa sana, ni jambo la maana kuweka akiba. Basi labda ingesaidia kufanya ununuzi katika duka moja kuu. Wajua ni wapi bidhaa zilipo (na jambo hilo laokoa wakati wako), nawe wajua ni wakati gani bidhaa huuzwa kwa bei ya chini (jambo ambalo huokoa pesa zako).
Kuchagua Wakati Bora Zaidi
Kila mwanamke ana saa yake mwenyewe ya ndani. Baadhi yao hufanya kazi bora zaidi asubuhi; wengine hawafanyi vizuri mpaka alasiri. Ikiwa wewe ni mtu wa asubuhi, kwa vyovyote ratibu kazi zako ngumu wakati huo. Tumia nguvu zako wakati wa vipindi hivyo vya kilele. Ikiwa wewe hufanya kazi nje ya nyumbani, kwa nini usiongee na mwajiri wako? Itakufaidi wewe na yeye pia akikugawia kazi kulingana na hali. Kwa upande mwingine, ikiwa mwendo wako wa kazi asubuhi huwa wa kujikokota, weka kazi yako iliyo ya maana zaidi uifanye baadaye wakati ambapo wewe huifanya vizuri zaidi.
Mary ni mtu wa asubuhi. Yeye huuona wakati atumiao katika huduma yake kuwa sehemu iliyo ya maana zaidi ya siku yake. Hivyo basi alitafuta kazi ya nusu-siku yenye kufanywa alasiri. Hiyo humwezesha kutumia saa zake bora zaidi akiwa kwenye kazi yake ya kufundisha Biblia. Je! wewe ungeweza kupanga ratiba yako kwa njia kama hiyo?
Fanya Mambo kwa Mafaa Halisi
Ili ratiba iwe yenye kutumika, ni lazima isihusishe utendaji mwingi mno. Kujaribu kuwa Mama, Mke, au Mfanya Kazi Maalumu kwaweza kutamausha na kuvunja moyo. Ndivyo ilivyo hasa ikiwa una matatizo ya afya. Jifunze kufanya kazi ndani ya mipaka yako.
Dolly, ambaye ana ugonjwa wa daima, aeleza hivi: “Wakati wangu hutegemea hasa utendaji wa mume wangu. Yeye ni mhudumu anayesafiri. Kwa kuwa sisi twaishi katika nyumba ndogo ya kuhamishwa-hamishwa, amalizapo kazi yake, ndipo mimi hufanya yangu. Ugonjwa wangu hunizuia nisifanye yale yote nipendayo kufanya. Lakini niwezapo, huduma yangu ndiyo hufanywa kwanza. Mambo mengine nyumbani huachwa bila kufanywa siku hiyo.”
Uwe Mwenye Kubadilikana
Mtihani wa umadhubuti wa mwanamke ni jinsi awezavyo kuhimili mkazo. Akiweza kubaki mtulivu wakati wa shida kubwa, atatimiza mengi sana kuliko kama akivurugika kabisa kihisia-moyo.
Sandra aliigundua siri ya kudhibiti mkazo. Asema hivi: “Wakati dharura zitokeapo kisha mimi nahisi nimesongwa na mambo pande zote, mimi hustarehe tu. Najua hilo lasikika kuwa ajabu, lakini huwa na matokeo. Nikiisha kujidhibiti, hapo ndipo naweza kuamua ni jambo gani lapasa kufanywa kwanza. Nisipostarehe, siwezi kupanga mambo yafaayo kufanywa kwanza. Haya yakiisha kupangwa ndipo mimi huharakisha utendaji wangu ili kutimiza dharura ile na kutimiza mambo. Kwa kielelezo, wakati mmoja wageni fulani waliwasili mapema kwa saa kadhaa kuja kwenye mlomkuu. Badala ya kubabaika, mimi nilipika tu huku nikipiga gumzo nao kwa kadiri ambayo ningeweza. Wote walistarehe na kuona shangwe.”
Tafuta Msaada
Wakati mmoja mtu fulani alisema kwamba afisa mtekelezaji aliye bora zaidi ni yule ambaye huwa na wasaidiaji wengi walio hodari. Je! wewe huhusisha msaada wa wengine kazini? Wakati wafanya kazi wenzi wajuapo kwamba msaada wao wathaminiwa, wao hujitolea kuutoa kwa utayari zaidi. Ndivyo ilivyo nyumbani. Kwa tukio baya, wanawake fulani ni watunzaji nyumba na wapishi wenye kutaka kufanya mambo kwa uangalifu mno hivi kwamba wao huvunja moyo kusaidiwa. Na maoni hayo hayo yangeweza kuwa ndiyo sababu ambayo wake na mama fulani huwa na mzigo mkubwa mno wa kazi hali washiriki wa familia yao huketi kitako tu wakionekana hawana hangaiko.
Sasa namna gani wewe? Wakati uhitajipo msaada, je! wewe hutia moyo kuupokea? Je! wewe huomba msaada, au wewe huudai? “Tafadhali ungependa” yasikika kuwa maneno yenye uvutio kuliko “Mimi nataka wewe u-”—uwe unasema na watoto wako au na mume wako.
Mwanamke mmoja, akimpongeza mume wake kwa msaada ambao yeye humpa, asema hivi: “Kwa jambo hilo yeye ni mzuri kweli kweli. Mimi niwapo mgonjwa, huniambia niende kitandani, naye hupika mlomkuu; yeye na watoto hujibwaga kazini wote pamoja na kusaidia kazi za nyumbani. Mimi nathamini hilo kweli kweli!”
Ni vizuri kama nini familia kuwa na maoni ya jinsi hiyo! Lakini mhusika mkuu katika hali hii ni mama. Yeye aweza kuzoeza watoto wake wang’amue thamani ya wakati na kusitawisha maoni chanya kuelekea kazi. Kwa kawaida watoto wa jinsi hiyo watataka kusaidia kwa sababu wao hupata shangwe kutokana na kuchangia mradi wa familia nzima kwa ujumla.
Lakini ni wazi kwamba watu fulani wataharibu wakati hata kama wengine waseme au wafanye nini. Hatuwezi kuwabadili; twaweza tu kujifanyia maendeleo. Twaweza kuazimia kutumia wakati kwa mafaa halisi, kupanga mambo kitengenezo zaidi, kupanga mambo yafaayo kufanywa kwanza, na kupata msaada uhitajiwapo.
[Picha katika ukurasa wa 15]
Ni lazima mambo ya kufanywa kwanza yapangwe ikiwa mambo ya nyumba yako yataenda ifaavyo