Kwa Nini Anga Ni Buluu?
Yale maeneo makubwa sana ya anga la juu yamefunikwa na giza. Tunachoita anga ni lile eneo linaloizunguka dunia, ile sehemu ya mbingu ionekanayo kwa jicho la kibinadamu. Kwa kutazama kwenye utando huo mkubwa, anga, wengi wameshangaa, ‘Ni kwa nini anga ni la buluu?’ Kwa nini si la urujuani, kijani-kibichi, kimanjano, rangi dhahabu-nyekundu, au jekundu—zile rangi nyingine za msingi za nuru?
Jua lina nuru ya miangaza yenye urefu mbalimbali, ambayo huonekana kuwa rangi tofauti za nuru yenye kuonekana. Ulio mrefu zaidi wa miangaza hiyo ya nuru ni nyekundu, na ulio mfupi zaidi ni buluu au urujuani. Molekyuli za gesi la eneo letu hutawanya nuru nyingi zaidi ya ile miangaza mifupi, buluu, kuliko ile miangaza mirefu zaidi, nyekundu. Kwa hiyo, anga lisilo na mawingu lina rangi ya buluu. Hewa inayozunguka dunia, ikiwa na visehemu visivyohesabika vyayo vidogo-vidogo vya vitu, kama vile vumbi, hutawanya nuru inayoonekana, kama kwamba inaangazwa kutoka kwa kioo.
Kwa upande ule mwingine, jua linapokuwa karibu na macho, nuru ya jua husafiri kupitia eneo kubwa zaidi ili kufikia jicho, na ile miangaza mirefu zaidi hupenya vizuri zaidi ya ile miangaza mifupi zaidi, hivyo kusababisha anga lionekane la rangi dhahabu-nyekundu iliyoshika na jekundu. Vitu katika hewa huongeza wekundu huo. Vivyo hivyo, wakati moshi au mawingu mazito yanapojaa angani, miangaza ya nuru ya rangi zote hutawanywa. Hilo husababisha anga lionekane la kijivu-jivu.
Wonyesho huo wenye kustaajabisha sana wa utumizi wa Mungu wa nuru katika mbingu zionekanazo hutukumbusha maneno ya mtunga zaburi: “Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, na anga laitangaza kazi ya mikono yake.”—Zaburi 19:1.