Kutana na Jamaa Fulani Mwenye Kuwaka Moto
Na mleta habari za Amkeni! katika Italia
NYAKATI nyingine mimi hufikiri kwamba kwa kweli mimi si jamaa wa kawaida—mimi ni mwembamba, mkavu, na mwenye kusisimuka sana hivi kwamba mimi hutokeza cheche. Mimi hufoka sana hivi kwamba hunichukua nukta moja tu kunifanya niwake moto. Wengine wajua mambo hayo na hunitumia kwa faida yao. Hata hivyo, mwelekeo wangu wa kuwaka moto ni sehemu ya asili yangu. Kwa kweli, watu huelekea kuudhika nikikosa kuwaka moto. Lakini wao huwa na sababu—mimi ni mshale wa kiberiti.
Je! si kweli kwamba nyakati nyingine wewe hunitambui nawe huniangalia wakati tu ninapokosa kuwaka au wakati kisanduku cha kiberiti kinapokuwa kitupu? Hata hivyo, ningependa kuona ukijaribu kuwasha moto namna watu walivyofanya nyakati za kale, kufikicha vijiti viwili pamoja ili kuwasha rundo la majani makavu au kugongesha jiwe gumu dhidi ya chuma, jambo hilo likiwa na hatari ya kutia jeraha vidole vyako! Vyovyote vile ungeshukuru mshale wa kiberiti ulio wa hali ya chini.
Kubuni Mshale wa Kiberiti wa Kuwashia
Historia ya familia yangu imejawa na majaribio ya kuvumbua njia fulani inayofaa ya kuwashia moto. Hata katika karne ya 17, baada ya mwanakemia Mjerumani Hennig Brand kugundua fosforasi, ilifikiriwa juu ya uwezekano wa kuvumbua kitu fulani ambacho kingefanya iwe rahisi kuwasha moto. Ilichukua muda mrefu zaidi ya wanasayansi walivyotazamia.
Mwanzoni mwa karne ya 19, Mfaransa Jean Chancel alibuni nta yenye kushika moto upesi iliyofanyizwa kwa potasiamu kloreti, sukari, na nta ya Uarabu. Ili kuiwasha, kiasi kidogo kiliwekwa kwenye ncha ya kijiti kilichotiwa sulfur, na kugusishwa kwenye asbestos iliyochovywa ndani ya sulfuric acid. Hicho hakikuwa kitu cha kutembea-tembea nacho mfukoni!
Unaoelekea kuwa mshale wa kiberiti wa kwanza wa msuguano, au “nuru ya msuguano,” ulibuniwa katika 1826 na John Walker, mwanadawa Mwingereza. Mshale huo wa kiberiti ulikuja kujulikana baadaye kuwa Lucifer-match, au Lucifer. Kwa nini “Lucifer”? Kwa sababu hiyo ndiyo tafsiri ya Kilatini ya neno la Kigiriki linalotafsiriwa “mleta-nuru”—fosforasi! Na neno lilo hilo la Kigiriki hutumiwa kuwa “mleta nuru,” au “nyota ya mchana,” kwenye 2 Petro 1:19, NW! Hata katika lugha nyingine, kama vile Kihispania na Kireno, ningali naitwa fósforo!
Karibu na wakati uo huo ambao Walker alibuni mshale wake wa kiberiti, “Prometheans” (kutokana na Prometheus katika hekaya za Kigiriki, Jitu ambalo liliiba moto kutoka Olympus na kumpa binadamu) wakatokea. Wao walikuwa ni nusu ya uvumbuzi wa Chancel na nusu ya mshale wa kiberiti wa ki-siku-hizi. Potasiamu kloreti, sukari, na nta vilichanganywa na kufungwa katika kunjo la karatasi nyepesi. Kwenye ncha moja kulikuwako kifuko kidogo cha gilasi kilichojazwa asidi salfa. Gilasi hiyo inapovunjwa, asidi hiyo na ile nta yenye kushika moto upesi, na kusababisha mwako. Wakati wa safari zake kwenye Beagle kupitia Amerika ya Kusini, Charles Darwin aliwashtua watu sana katika Uruguay kwa kuvunja akitumia meno kifuko hicho cha gilasi cha Promethean, na kusababisha mwako. Hiyo haikuwa mishale ya kiberiti cha msuguano bali ilikuwa mishale ya kiberiti cha tendo la kemikali.
Karibu na wakati uo huo, mwanakemia Mwiitalia, Domenico Ghigliano, pia alikuwa anapendezwa na familia yangu. Baada ya majaribio kadhaa, alitayarisha nta yenye kushika moto upesi iliyofanyizwa kwa antimony sulfidear na viasili vingine ambavyo vilifanywa vigandamane kwenye ncha za vijiti vidogo. Viliposuguliwa kwenye sakafu isiyolainika, nta hiyo iliwaka moto mara moja.
Potasiamu kloreti na fosforasi nyeupe, ambazo wakati huo zilikuwa zimekuwa viungaji vikuu vya nta hiyo, zote mbili zilikuwa ni hatari na zenye sumu. Hatimaye, mahali pazo palichukuliwa na risasi dayoksaidi (au risasi nyekundu pamoja na manganizi dayoksaidi) na fosforasi nyekundu. Hilo pia lilisaidia kuondoa matatizo katika utengenezaji na matumizi yayo.
Kutoka Shina la Mti Hadi Kuwa Mshale wa Kiberiti
Leo mimi hutengenezwa kwa kitu gani? Mwili wangu mfupi, mwembamba, ulio mkavu hutengenezwa kwa mti fir, msunobari, poplar nyeupe. Kichwa changu hasa ni fosforasi salfaidi, kloreti, chuma au zinki oksaidi, gilasi iliyofanywa kuwa unga-unga, na mpira au nta.
Bila shaka, sisi mishale ya kiberiti ni familia yenye utofautiano mkubwa, na visanduku ambamo tunatiwa ndani vinatofautiana hata zaidi. Mimi ni ule mshale wa kiberiti wa kawaida unaotumiwa jikoni, lakini pia kuna cerino, au mshale wa kiberiti wa nta (ambaye kihalisi hutengenezwa Italia, kile kijiti cha mshale wa kiberiti kikiwa kimetengenezwa kwa karatasi yenye nta iliyoviringwa). Halafu kuna mshale wa kiberiti wa Kiswedi (hufanyizwa bila fosforasi kichwani na ni wa utaalamu mkubwa hivi kwamba huwaka wakati tu anaposuguliwa kwenye ukanda wa fosforasi wa kisanduku chake).
Kwa maneno rahisi, utengenezaji wetu umegawanywa kuwa hatua tatu: Kwanza kabisa, kuna matayarisho ya mwili wangu, kijiti cha mshale wa kiberiti; kisha kuna uchanganyaji wa nta isiyoshika moto upesi; na, mwishowe, muunganisho wa viasili hivyo viwili.
Wakati wa hatua ya kwanza, mashina ya mti huumbuliwa ganda yayo na kufanywa kuwa mamilioni ya vijiti vidogo vya mishale ya kiberiti vyenye umbo la mpitano wa mraba au mstatili. Kwa upande ule mwingine, ili kufanyiza mishale ya kiberiti ya nta, uzi mrefu wa karatasi iliyosongwa yenye nta huchovywa ndani ya rangi. Kisha hupunguzwa na kikatio kuwa na urefu wa sentimeta mbili hivi.
Nta yenyewe hutengenezwa kutoka kwa kemikali tofauti-tofauti, na vichwa vyenyewe vyaweza kutofautiana kutoka mshale mmoja wa kiberiti hadi ule mwingine. Ile hatua ya mwisho ni muunganisho wa sehemu hizo mbili. Sisi mishale ya kiberiti hulazwa kichwa kikielekea chini, na vichwa vyetu hupitwa juu na kizungukaji kilichofunikwa kwa nta. Kisha sisi huruhusiwa tukauke, na mwishowe tunatiwa ndani ya visanduku. Kile kiwambo ambacho si laini unachotuwasha kwacho ni utando wa nta iliyochanganywa na unga-unga wa gilasi iliyopakwa kwenye upande wa kisanduku cha kiberiti. Wakati mmoja utaratibu wote wa utengenezaji ulifanywa kwa mkono; sasa, bila shaka, mashine hutumiwa. Hizo hututengeneza kwa mamilioni.
Tahadhari—usituache mahali ambapo watoto waweza kutufikia. Wao ni wadadisi sana na hupenda kuiga watu wazima—unakuja kugutuka kwamba wanakwaruza kichwa changu kwenye upande wa kisanduku, na kwa sababu ya hali yangu ya kuwaka moto, mwako mdogo waweza kusababisha moto mkubwa. Kwa hiyo tafadhali uwe mwangalifu nami!