Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • jy sura 70 uku. 166-uku. 167 fu. 2
  • Yesu Amponya Mtu Aliyezaliwa Kipofu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Yesu Amponya Mtu Aliyezaliwa Kipofu
  • Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
  • Habari Zinazolingana
  • Kuponya Mwanamume Aliyezaliwa Akiwa Kipofu
    Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
  • Kuponya Mwanamume Aliyezaliwa Akiwa Kipofu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1988
  • Kutoitikadi kwa Mafarisayo kwa Sababu ya Ugumu wa Moyo
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1988
  • Mafarisayo Wakosa Kuamini kwa Kupenda
    Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi
Pata Habari Zaidi
Yesu—Njia, Kweli, na Uzima
jy sura 70 uku. 166-uku. 167 fu. 2
Baada ya kunawa katika dimbwi la Siloamu, kipofu anaanza kuona

SURA YA 70

Yesu Amponya Mtu Aliyezaliwa Kipofu

YOHANA 9:1-18

  • OMBAOMBA ALIYEZALIWA KIPOFU APONYWA

Bado Yesu yuko Yerusalemu siku ya Sabato. Yeye na wanafunzi wake wanapotembea jijini wanamwona mwanamume anayeombaomba ambaye amekuwa kipofu tangu kuzaliwa. Wanafunzi wanamuuliza Yesu: “Rabi, ni nani aliyetenda dhambi, ni mtu huyu au ni wazazi wake, hivi kwamba akazaliwa kipofu?”—Yohana 9:2.

Wanafunzi wanajua kwamba mtu huyo hana nafsi isiyoonekana ambayo iliishi kabla hajazaliwa. Hata hivyo, huenda wanajiuliza kama mtu anaweza kufanya dhambi akiwa katika tumbo la mama yake. Yesu anajibu hivi: “Mtu huyu hakutenda dhambi wala wazazi wake, bali ilikuwa hivyo ili kazi za Mungu zifunuliwe katika kisa chake.” (Yohana 9:3) Kwa hiyo, mtu huyu na wazazi wake hawakuwa na hatia ya kosa fulani au dhambi iliyofanya awe kipofu. Badala yake, kwa sababu ya dhambi ya Adamu, wanadamu hawazaliwi wakiwa wakamilifu na wanaweza kuwa na kasoro, kama vile upofu. Lakini upofu wa mtu huyo unampa Yesu nafasi ya kuonyesha kazi za Mungu, kama ambavyo amefanya pindi nyingine kwa kuwaponya watu magonjwa.

Yesu anakazia kwamba kazi hizo zinapaswa kufanywa haraka. “Lazima tufanye kazi za Yule aliyenituma kukiwa bado mchana,” anasema. “Usiku unakuja ambapo hakuna mtu atakayeweza kufanya kazi. Maadamu nimo ulimwenguni, mimi ndiye nuru ya ulimwengu.” (Yohana 9:4, 5) Naam, hivi karibuni kifo cha Yesu kitamwingiza katika giza la kaburi ambamo hataweza kufanya lolote. Kwa sasa, yeye ni chanzo cha nuru kwa ulimwengu.

Yesu anaweka tope kwenye macho ya mtu aliye kipofu

Lakini je, Yesu atamponya mtu huyo, ikiwa ndivyo, atafanyaje hivyo? Yesu anatema mate chini na kutengeneza tope kwa kutumia mate. Anampaka tope mtu huyo kwenye macho na kusema: “Nenda ukanawe katika dimbwi la Siloamu.” (Yohana 9:7) Mtu huyo anatii. Baada ya kunawa, anaanza kuona! Wazia shangwe yake anapoona kwa mara ya kwanza katika maisha yake!

Majirani na watu wengine waliomjua akiwa kipofu wanashangaa. “Je, huyu si yule mtu aliyekuwa akiketi akiombaomba?” wanauliza. Baadhi yao wanajibu: “Ni yeye.” Hata hivyo, wengine hawaamini nao wanasema: “Hapana, lakini anafanana naye.” Yule mtu anasema: “Ni mimi.”—Yohana 9:8, 9.

Basi wanamuuliza “Macho yako yalifunguliwaje?” Anajibu: “Mtu anayeitwa Yesu alifanyiza tope akanipaka kwenye macho kisha akaniambia, ‘Nenda mpaka Siloamu ukanawe.’ Basi nikaenda, nikanawa, nikaanza kuona.” Kisha wanauliza: “Yuko wapi mtu huyo?” Yule mtu anasema: “Sijui.”—Yohana 9:10-12.

Watu wanampeleka mtu huyo kwa Mafarisayo, ambao pia wanataka kujua jinsi alivyoanza kuona. Anawaambia: “Alinipaka tope kwenye macho yangu, nami nikanawa, sasa ninaona.” Mafarisayo wanapaswa kushangilia pamoja na mtu huyo aliyeponywa. Badala yake, baadhi yao wanamshutumu Yesu. Wanadai hivi: “Mtu huyo hatoki kwa Mungu, kwa sababu hashiki Sabato.” Nao wengine wanauliza: “Mtenda dhambi anawezaje kufanya ishara kama hizo?” (Yohana 9:15, 16) Basi kunakuwa na mgawanyiko kati yao.

Wakiwa na maoni yanayotofautiana, wanamgeukia mtu huyo ambaye sasa anaona na kumuuliza: “Unasemaje kumhusu kwa kuwa wewe ndiye uliyefunguliwa macho?” Hana shaka kumhusu Yesu naye anajibu: “Yeye ni nabii.”—Yohana 9:17.

Wayahudi wanakataa kuamini jambo hilo. Huenda wanafikiri kuna njama kati ya Yesu na mtu huyo ya kuwadanganya watu. Wanaamua kwamba njia moja ya kutatua jambo hilo ni kuwauliza wazazi wa mtu huyo kama kweli alizaliwa kipofu.

  • Ni nini kilichosababisha mtu huyo awe kipofu, bali si nini?

  • Baada ya mtu huyo kuponywa wale wanaomfahamu wanatendaje?

  • Kunakuwa na mgawanyiko gani kati ya Mafarisayo kuhusu kuponywa kwa mtu huyo?

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki