Ulimwengu wa Kucheza Kamari
MASHINE za kutumbukiza pesa mara nyingi huitwa majambazi wenye mkono mmoja. Lakini tofauti na majambazi halisi, hazilazimishi mtu yeyote yule kutoa pesa; watu husimama kwa foleni kama kondoo wanyonywe na mashine hizo.
Kunazo mashine kama hizo karibu 420,000 katika Jamhuri ya Muungano ya Ujerumani, zikishughulikia unyonyaji wa karibu dola 900,000,000 kutoka kwa Wajerumani kila mwaka. Watu milioni tano huko hutumia saa moja kila juma wakimwaga pesa katika mashine hizo; Watu wapatao 80,000 hutumia zaidi ya saa tano kila juma kwenye mashine hizo.
Uhispania sasa inajivunia mashine za kutumbukiza pesa 750,000. Kucheza kamari kulikubaliwa kisheria huko mwaka wa 1977. Kufikia 1988, Wahispania tayari walikuwa wakitumia dola 25,000,000,000 kila mwaka katika namna yoyote ile ya kucheza kamari. Iliripotiwa kwamba Wahispania 200,000 ni wachezaji wazoevu wa kamari. Waitalia walicheza kamari kwa kiasi cha karibu dola 12,000,000,000 katika 1989—au karibu dola 210 kwa kila mtu, watoto wakitiwa ndani. Katika juma moja tu mapema mwaka 1990, Waitalia walitumia dola milioni 70 kuwekeana masharti kwa matokeo ya michezo ya mpira wa miguu.
Wacheza kamari katika United States hutumia zaidi ya dola 200,000,000,000 kila mwaka katika kucheza kamari inayokubalika kisheria pekee! Msimamizi wa kasino nyingi humo hivi majuzi alijigamba hivi: “Kucheza kamari ni biashara inayoendelea kwa kasi zaidi, ikiwa kubwa kama yale matumizi ya fedha ya kila mwaka [ya jeshi la U.S.].” Alilinganisha upendo wa Waamerika wa kucheza kamari na ile “tamaa ya kifalsafa” na utayari wa kujasiria zilizosukuma wavumbuzi na waweka mipaka katika historia ya taifa hilo. Lakini ndoto ya mcheza kamari ya kupata mali mara moja haiwezi kulinganishwa kabisa na miaka ya jasho na juhudi walizotumia wavumbuzi hao na wenyeji wa kwanza.
Mwanasosholojia Vicki Abt alisema hivi: “Michezo ya kamari hutoa wazo la kwamba zawadi haihusiani hata kidogo na juhudi zako.” Kuwaza kama huko kwaweza kuharibu kabisa maisha mazuri. Deni, umaskini, tabia zilizoharibika za kazi, familia zilizovunjika—hayo ndiyo mapato mabaya ya kucheza kamari. Kwa mamilioni, miongoni mwao kukiwa idadi inayoongezeka ya vijana, kucheza kamari hugeuka kuwa tamaa isiyoweza kudhibitiwa. Kwa kweli, Biblia inasema kweli inaposema kwamba “shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha.”—1 Timotheo 6:10.